Maoni yetu

Polisi inajua uzito wa dhambi iliyofanya?


Kuua ni katika dhambi kubwa mbele ya Allah. Na wanaadamu wanakiri hivyo.

Lakini Allah anasema,kuwazuilia watu na dini yao na kuwazuilia watu kuingia msikitini ni dhambi kubwa zaidi ya kuua..

Allah anasema:Wanakuuliza(hukumu ya) kupigana vita katika miezi mitakatifu.Sema:"Kupigana vita katika (miezi) hiyo ni dhambi kubwa.Nakuwazuilia watu na dini ya Mwenyezi mungu,na kumkanusha (Mwenyezi mungu),na (kuwazuilia watu) msikiti huo mtakatifu,na kuwatoa watu waliomo,ni (dhambi) kubwa zaidi mbele ya Mwenyezi mungu.

Na kuwazuilia watu na dini yao ni mabaya zaidi kuliko kuua."(2:217).

Muislamu amezuiliwa kupigana vita katika miezi mitakatifu, lakini endapo atazuiliwa kumuabudu Mola wake,dhambi hiyo ni kubwa zaidi anaruhusiwa kupigana.

Halikadhalika watu wakizuiliwa kuingia msikitini wanaruhusiwa kupigana.

Haya ni mafundisho yaliyo wazi ya aya hii.

Kuwapiga watu bila ya haki si jambo lililoruhusiwa.Lakini Allah anasema:

"Napiganeni katika njia ya Mwenyezi mungu na wale wanaokupigeni,wala msipindukie mipaka (mkawapiga wasiokupigeni) kwani Mwenyezi Mungu hawapendi warukao mipaka"(2:190).

Waumini wa msikiti wa Manzese Uzuri makaburini wameikosa swala ya jamaa msikitini kwa vipindi vinne.

Tangu magharibi Jumamosi hadi Al'asri Jumapili juzi.

Waislamu walipigwa katika eneo la msikiti.Waliokuja kuswali swala ya Al'asri wakakamatwa,na makachero kubaki wakivinjari msikitini hapo.Hakuingia mtu kuswali mpaka Jumapili swala ya Al' asri alipofika sheikh Mbukuzi akiandamana na polisi ndipo msikiti ukafunguliwa.

Waumini kadhaa walikamatwa wakiwemo akina mama.Jana walifikishwa mahakamani na wamenyimwa dhamana.

Taarifa ya polisi imedai waislamu hao walihusika na ghasia zilizo zusha mapigano kati ya waislamu na wakristo.

Kama ni mapigano kati ya waislamu na wakristo ni kwanini wamekamatwa waislamu pekee, pengine hilo si muhumu kuhoji sasa hivi. Labda ni katika utaratibu wa kawaida tu. Inapokuwa kuteua wasimamizi na waratibu wa uchaguzi wawe wakristo,lakini inapotokea

kukamata watuhumiwa katika tukio kama hili basi iwe zamu ya waislamu kukamatwa peke yao!

Kabla ya polisi kufika katika eneo la tukio Waislamu watatu walikuwa wameshajeruhiwa na Wakristo kwa Majembe na chepe(rejea habari inayoongoza uk. Wa kwanza) Waislamu waliwataka Polisi wawakamateWakristo watuhumiwa kabla ya kufanya mjadala wowote.

Polisi hawakufanya hivyo, mabomu ya machozi na virungu vilielekezwa kwa Waislamu huku wakiwalinda Wakristo wazike.

Akinamama Waislamu waliokuja kuswali swala ya Al 'asri wakapokewa kwa virungu na kuwekwa ndani. Polisi wanadai wamehusika na ghasia.

Waliowakata Waislamu kwa Majembe, Polisi hawathubutu kuwagusa. Ni hadithi ileile ya mauaji ya Mwembe Chai.

Wakati majeruhi Waislamu waliokatwa na Majembe vichwani hatima ya hali zao haijulikani zitakuwaje, wahusika wanaendelea na shughuli zao kama kawaida japo wanajulikana. Bw.Imrani Amani(30) aliyekatwa na jembe kichwani jana hata kuzungumza ilikuwa shida.

Je,huu ndio urithi aliotuachia Mwalimu Nyerere hata CCM ikampa nishani ya kiongozi bora wa Karne!

Hii ndio Tanzania isiyo na ubaguzi wa kidini!

Hii ndio hali halisi ya Umoja na mshikamano ambao wanasiasa hawachoki kufoka kuwa wataulinda kwa nguvu zote!

Huu ndio mfumo na hali halisi ambayo kila anayeukosoa huambiwa anataka kuvuruga amani!

Hawa ndio Polisi walinzi wa raia na mali zao!

Lakini swala muhimu hapa ni je, Polisi wanajua uzito wa vitendo vyao? Pengine Polisi wamefanya hayo wakiwadhania Waislamu wa Manzese Uzuri aya kama hizi tulizozinukuu hawazijui. Au pengine wamewaona dhaifu sana wa Imani na nguvu kiasi kwamba hawawezi kufanya lolote.

Lakini tunadhani ingekuwa busara Polisi wakazingatia kuwa suala linapokuwa la Kanisa au Msikiti, haliishii kwa wanaoingia hapo pekee. Bali ni suala la Waumini wote wa dini husika. Na Qur an imesema:"Basi nawapigane katika njia ya Mwenyezi Mungu wale wanaouza maisha (yao) ya dunia kwa (kununua) ya Akhera.Na anaye pigana katika njia ya Mwenyezi Mungu,kisha akauawa au akashinda,tutampa ujira mkuu.

Na mna nini hampigani katika njia ya Mwenyezi Mungu na (katika kuwakoa) wale walio dhaifu katika wanaume na

Wanawake na Watoto ambao husema: "Tutoe katika mji huu ambao watu wake ni madhalim, na tujaalie tuwe na mlinzi anayetoka kwako, na tuwe na wa kutunusuru anayetoka kwako" (4:74-75)

Je, tuseme Polisi imeridhika kabisa kuwa hakuna Waumini wanaomtii Mola wao katika agizo lake la kuwasaidia walio dhaifu wanaopigwa mapanga kisha wao tena ndio wakawekwa ndani?

Yawezekana tathmini ya Polisi kwa kuzingatia matukio kama haya yaliyotangulia ikawa sahihi. Lakini sisi tunadhani isingekuwa busara kuwadhania watu ni wadhaifu wa imani kiasi hicho. Kwani imani ya Muumini si kitu kilichotuama. Ya kesho yaweza isiwe sawa na ya leo.

--
JuuRUDI


Bonyeza hapa
kushriki mjadala au kutoa maoni juu ya habari hizi na masuala mengineyo ya Kiislamu kwenye Baraza ya Wasomaji

   Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu: Bonyeza hapa
Au
Andika barua  kwa: webmaster@islamtz.org


An-nuur Home | Ukurasa wa Mwanzo | Islam Tanzania
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook