Polisi watuhumiwa kuchochea mapigano, Wakristo na Waislamu


POLISI Jijini imetuhumiwa kuchochea mfarakano uliosababisha mapigano baina ya waumini makaburini Manzese Uzuri.

Mapigano hayo yalitokea Jumamosi baada ya waumini wa dini za Kiislamu na kikristu kutokukubaliana katika suala la mazishi ya mkristo eneo linalomilikwa na Msikiti.

Imeelezwa kuwa vurugu hilo lilitokea baada ya polisi kuamrisha wafiwa wamzike jamaa yao mahali hapo kinyume na ridhaa ya wahusika.

Gazeti hili lilizungumza na Waumini wa msikiti unaomiliki eneo hilo ambao karibu wote maelezo yao yamewalaumu polisi kwa kile walichodai kuwa uonevu wa dhahiri uliooneshwa na watendaji wa jeshi hilo dhidi ya Waislamu.

Wakizungumza huku wakiwa na hofu kubwa ya kukamatwa kufuatia msako ulioendeshwa baada ya tukio hilo, waumini hao wamesema wanasikitishwa na jinsi vyombo vya dola na vile vya habari vilivyoamua kuwa upande wa waumini wa kikristo katika kadhia hiyo.

Mzee mmoja wa makamo ambaye alikataa kutaja jina lake akizungumza na mwandishi nje ya msikiti huo alikanusha malezo yaliyotolewa na kamanda wa polisi kuwa mapigano yalitokea baada ya kuwepo mabishano makali baina ya Waislamu na wakristo.

Alisema pamoja na wakristo ambao alidai walionekana kudhamiria shari siku hiyo kumjeruhi kwa chepe mwenzao mmoja aliyekwenda kuhoji kwa nini walikuwa wakivunja makubaliano kwa kuendelea kuzika mahali hapo, wao hawakuchukua hatua ya kuanzisha mapambano bali walitoa taarifa kwa Mwenyekiti wa mtaa ambaye naye alifanya jitihada ya kuwaona wafiwa.

Kuhusu makubaliano kati ya waumini wa dini hizo, Mzee huyo alisema yalifanyika siku ya jumatano baada ya kutokea kifo cha mama mmoja mkristo aliyefahamika kwa jina la Catherine. Mazishi yake yalifanyika katika makaburi hayo baada ya mazungumzo kati ya wafiwa, waislamu,mwenyekiti wa mtaa na polisi.

Iliafikiwa kwa kuwa makaburi ya wakristo yamejaa maiti hiyo iwe ya mwisho kuzikwa mahali hapo.

AN-NUUR ilikutana na jamaa wa hayati bibi Catherine aliyejitambulisha kwa jina la Wilfred na alithibitisha kutokea kwa msiba huo na mazishi hayo kufanyika mahali hapo siku ya jumatano juni 28,chini ya sharti hilo.

Hata hivyo mzee huyo alieleza, siku ya jumamosi walionekana wakristo wakichimba kaburi eneo hilo hilo ili kumzika jamaa yao aliyefariki katika Hospitali ya Mwananyamala ambaye alifahamika kwa jina la Kishoka.

"Jamaa hao walionekana kujiandaa kwa lolote wakati wakichimba kaburi hilo, waumini wezetu waliokwenda kuwahoji walipigwa majembe na chepe na kujeruhiwa, tukalazimika kutoa adhana msikitini ili kujadili suala hilo", alisema mzee huyo.

Gazeti hili lilifika nyumba ya jamaa wa hayati huyo(jirani na bucha iitwayo "Sikuwahukumu") na kuhojiana na baadhi ya watu ambao walidai walimzika ndugu yao kwa ruhusa na usimamizi wa polisi.

Naye Mwenyekiti wa mtaa huo bwana Mgewe Kenyella akiongea na gazeti hili ofisini kwake alilifahamisha gazeti hili kuwa kiasili eneo linalogombewa ni la Waislamu la wakfu, lakini waliamua kuwakatia sehemu wakristo kwa ajili ya mazishi yao.

Hata hivyo Mwenyekiti huyo alisema eneo la wakristo lilijaa ambapo walitakiwa watafute sehemu nyingine ya kuzikia.

Akielezea chanzo cha mgogoro huo alisema januari 28, mwaka huu baadhi ya wakristo walikwenda msikitini kuomba wapewe sehemu ili wamuhifadhi jamaa yao ambaye alifariki mtaani hapo.

Baada ya majadiliano marefu Waislamu waliamua kutoa sehemu hiyo lakini kwa sharti kuwa maiti huyo awe wa mwisho kuzikwa mahali hapo.

Mwenyekiti huyo alisema iliendelea kufahamika hivyo na hapakuwa na mkiristo aliyekuwa akizikwa mahali hapo tangu maafikiano hayo ya januari 2000.

Lakini Bwana Kenyalla alisema ghafla juni 28, alipelekewa taarifa kuwa kulikuwa na mzozo baina ya Waislamu na Wakristo kuhusiana na sehemu ya kuzikia eneo hilo.

Alisema alilazimika kwenda kwenye eneo la tukio kushuhudia hali hiyo na kama Mwenyekiti wa mtaa aliitisha kikao akishirikiana na vyombo vya Dola na ikafikiwa maafikiano kuwa mazishi hayo yawe ya mwisho na maiti iruhusiwe izikwe mahali hapo.

"Lakini kabla hatujakaa kutafakari ufumbuzi wa kudumu wa suala hilo, siku ya jumamosi juni 1,nikaletewa taarifa kuwa kulikuwa na mzozo makaburini na baadhi ya watu wamejeruhiwa", alisema mwenyekiti huyo na kuongeza "tulifanya haraka kuwasiliana na vyombo vya Dola ambavyo viliwasili muda mfupi. Tuliitisha kikao baina ya uongozi wa serikali ya mtaa, polisi, Waislamu na wafiwa. Wafiwa hawakutaka kutafuta mahali pengine kwa madai kuwa maiti ilianza kutoa harufu. Viongozi wa Waislamu walionekana kukubali lakini walisema wasingeweza kutoa uamuzi wowote mpaka wakakutane na wenzao msikitini".

Aidha waumini wameeleza kuwa waliwataka polisi wawakamate kwanza wale wakristo walio wajeruhi waislamu kwa chepe.Hata hivyo polisi walikataa.Lakini hata kabla viongozi hawajaleta maoni ya waislamu,polisi waliwaruhusu wakristo waendelee na mazishi.Mmoja wa viongozi wa waislamu ameeleza kuwa alipojaribu kuwahoji polisi vipi wamekiuka makubaliano,amri ilitolewa akamatwe.

Mwenyekiti wa serikali ya mtaa ameeleza kuwa hayo yakitokea yeye alikuwa ashakwenda kutafuta sehemu nyingine ya kuzikia.

"Ili kuepusha balaa hilo mimi na Afisa wa manispaa,tuliona hayo makubwa, tukatoka hadi Kijitonyama kwa Ali maua tukapata sehemu kwa shilingi 3000 tukachimba kabisa lakini tuliporudi tukaambiwa jamaa washazika kwa kusimamiwa na polisi chini ya ukamanda wa Afisa upelezi mkoa bwana Said Mwema."

Taarifa kutoka eneo la tukio zinaeleza kuwa mapigano ya jumamosi yalianzishwa na bwana mmoja aliyefahamika kwa jina la Satana(mcheza kareti) ambaye imeelezwa baada ya Waislamu kufukia kaburi aliongoza kikosi ambacho kilifukua tena kaburi hilo huku kikikabiliana kwa mawe na Waislamu waliokuwa msikitini hapo.

Imeripotiwa kuwa baada ya polisi kuwaruhusu wakristo wazike,polisi wa kuzuia fujo F.F.U waliokuwa eneo hilo upande walikosimama wakristo waliamua kuwazunguka Waislamu na kuwafyatulia mabomu kadhaa ya machozi. Wengi wao waliamua kukimbilia msikitini.

Polisi hao waliuzingira msikiti na kuwakamata Waislamu ambao miongoni mwao walikuwemo akina mama zaidi ya 18.

Polisi ilizuia kuendeshwa kwa Swala katika masikiti huo tangu alasiri ya jumamosi hadi alasiri ya jumapili ambapo sheikh Juma Mbukuzi na baadhi ya waumini waliufungua tena baada ya mazungumzo na polisi.

Hazikuwepo taarifa za kukamatwa wakristo katika mapigano hayo yaliyodaiwa ya waislamu na wakristo.

Waislamu waliokamatwa na kufikishwa mahakamani jana kuhusiana na kadhia hiyo ni Imamu wa msikiti Ramadhani Pembe(52), Said Salum(21), Bakiri Haonga(19), Hussein Said(42), Abdul Mohammed, Ahmad Joackim(38), Twaha Kambanga(21) Mohammed Athuman(28), Ali Sultan na Said Nyoni(36).

Wanawake ni Arafa Msumi(28), Mwanaisha Ali(22), Fatuma Abdallah(22) na Zaituni Mohamed(38).

Watuhumiwa hao kasoro wawili walirudishwa rumande baada ya upande wa mashitaka kuiomba mahakama ifunge dhamana yao.

Kesi yao itatajwa tena julai 17, mwaka huu.


'Maimamu kuandaa maandamano Jijini'

KUNA uwezekano waislamu wakaandamana kupinga uteuzi wa wasimamizi wa uchaguzi uliofanywa na Tume mwezi Aprili mwaka huu.

Maandamanao hayo yameelezwa yanafuatia kimya cha serikali kuhusu malalamiko yao juu ya uteuzi huo.

Taarifa kutoka jumuiya mbali mbali za kiislamu zinafahamisha kupingwa kwa uteuzi huo ambao umedaiwa huenda una ajenda ya siri dhidi ya Waislamu katika uchaguzi huo.

Mwanajumuiya mmoja wa MSAUD akiongelea suala hilo amesema kwamba uteuzi hauna budi kupingwa kwa nguvu zote kwa kuwa unatishia umoja wa kitaifa uliopo nchini.

Amesema dalili ya kuhatarishwa kwa makusudi umoja huo zinaonekana katika uteuzi huo uliofanywa huku kukiwepo tuhuma kadhaa dhidi ya serikali kuhusiana na Waislamu.

Amezitaja tuhuma hizo kuwa ni pamoja na kupendelewa na vyombo vya dola kwa kuwa watendaji wengi serikalini ni Wakristo.

"Hili la uteuzi linaelekea mkondo huo huo unaohatarisha utaifa wa Watanzania", amedai mwanafunzi huyo anayechukua shahada ya kwanza ya ualimu.

Aidha alisema watu wanaolitakia mema taifa hawapaswi kuinyamazia hatari hiyo.

Wiki iliyopita Baraza kuu la jumuiya na Taasisi za kiislamu lilimpelekea waraka Mwenyekiti wa Tume hiyo Jaji Lewis Makame kutaka uteuzi huo utenguliwe.

Baraza kuu liliandika katika waraka huo kuwa uteuzi wa wasimamizi hao unaelekea kutekeleza ajenda ya kanisa ya kuwaweka madarakani viongozi wakatoliki.

Jumuiya zingine ikiwemo shura ya maimamu zimedai kuwa iwapo Tume haitatengua uteuzi huo serikali itakuwa imethibitisha madai ya Waislamu kuwa wanapuuzwa na wanabaguliwa.

Zimesema hiyo hiyo itakuwa imeziweka mashakani kauli za viongozi na hasa Rais Benjamin Mkapa kuwa Serikali yake haina ubaguzi wala upendeleo wa kidini.

Akiwahutubia waumini katika sherehe za Maulid Jijini wiki hii Katibu wa Kamati ya kutetea Haki za Waislamu, Ustaadh Ponda Isa Ponda amesema utawala bora ni ule unaojali na kuzingatia hisia na malalamiko ya raia wake.

"Vipi serikali ipuuze malalamiko ya kikatiba ya nusu ya raia wake halafu ijione ina utawala bora, alihoji Ustaadhi Ponda.

Nao maimamu wa misikiti ya wilaya za Kinondoni na Temeke wakizungumzia suala hilo kwa nyakati tofauti wamesema uteuzi huo haufai na umelenga kuendeleza kile kile ambacho Waislamu wamekuwa wakikipigia kelele.

Wamesema Tanzania inaelekea kujiua yenyewe kwa sumu ya upendeleo na ubaguzi wa kidini chini ya serikali ya CCM.

Wamewataka Waumini wao na wananchi wanaoitakia mema nchi walieleze hilo katika mikusanyiko yao na wamuandikie Mwenyekiti wa Tume hiyo kumuhadharisha juu ya matokeo ya uteuzi huo.

Aidha wamesema hatua ya mwisho wanayodhamiria kuichukua ni kuandaa maandamano ya amani kupinga uteuzi wa Wasimamizi hao.
--
JuuRUDI


Bonyeza hapa
kushriki mjadala au kutoa maoni juu ya habari hizi na masuala mengineyo ya Kiislamu kwenye Baraza ya Wasomaji

   Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu: Bonyeza hapa
Au
Andika barua  kwa: webmaster@islamtz.org


An-nuur Home | Ukurasa wa Mwanzo | Islam Tanzania
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook