Tanga wamshangaa Mufti wa BAKWATA

BAADHI ya wakazi wa Manispaa ya Tanga mji anaotoka Mufti wa BAKWATA Sheikh Hemed bin Jumaa wameeleza kushtushwa kwao na kauli za Mufti huyo alizozitoa huko Shinyanga kwa Masheikh wa BAKWATA Juni 19, mwaka huu.

Katika kikao chake na Masheikh hao, Sheikh Hemed alinukuliwa pamoja na mambo mengine aliwaasa Waislamu kuacha kukatazana kuipigia kura CCM.

Alieleza pia kuwa Waislamu hawana uwezo wa kuongoza nchi na kwamba BAKWATA ni chombo kilichoanzishwa na hayati Mwalimu Nyerere baada ya kuvivunja vyombo vilivyokuwa vimeanzishwa na Waislamu.

Baadhi ya wakazi hao wamesema, walikuwa wakidhani kuwa BAKWATA ni chombo cha Waislamu lakini Mufti Hemed amewazindua kuwa chombo hicho ni cha serikali.

"Hivi Nyerere alianzisha BAKWATA kwa maslahi ya serikali au ya Waislamu na kwanini avivunje vyombo vilivyoanzishwa na Waislamu wenyewe na kuanzisha anachotaka yeye wakati yeye ni Mkristo?" alihoji Bw. Hamza Ali.

Naye Bw. Musa Bakari amsema, haelewi mantiki ya Mufti Hemed kuzunguka nchi nzima kuwaasa Waislamu wasikatazane kuipigia kura CCM wakati BAKWATA si chombo cha siasa.

"Tuna hisia kwamba Mufti anaitumikia serikali kwa vile ameshatuambia kuwa BAKWATA anayoiongoza ilianzishwa na Nyerere", amesema.

Amesema, kitendo cha BAKWATA kujiegemeza mno na serikali kiasi cha kuwakataza watu wasikatazane kuipigia kura CCM kunawafanya wawe na imani kuwa chombo hicho si chao.

Akizungumzia kauli ya Mufti Hemed kwamba Waislamu hawana uwezo wa kuongoza nchi, Bw. Ramadhani Omar kutoka wilaya ya Pangani amesema, amekerwa na kauli hiyo ambayo alidai ni ya kashfa kwa Waislamu.

"Kwani Ali Hassan Mwinyi aliyekuwa Rais wa Awamu ya Pili hakuwa Muislamu?" alihoji Bw. Omar na kumtaka Mufti Hemed aeleze ni kwa mtazamo upi anaona kuwa Waislamu hawawezi kuongoza nchi.

Bw. Omar aliongeza kudai kuwa Mufti Hemed anataka kuleta suala la udini wakati kinachogombwa kwa CCM si kuwa na Rais Mkristo bali ni sera mbovu zinazowakandamiza wananchi.


Tume yashutumiwa kwa ubaguzi

TUME ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imetuhumiwa kufanya upendeleo wa kidini katika kufanya uteuzi wa wasimamzi wa uchaguzi mkuu utakaofanyika Oktoba 29, mwaka huu.

Tuhuma hizo zilitolewa mwishoni mwa wiki na Sheikh Ally Bassaleh alipokuwa akiwahutubia waumini wa Kiislamu mara baada ya swala ya Ijumaa ambayo iliswaliwa kwenye Msikiti wa Idrisa Kariakoo, Jijini Dar es Salaam.

Sheikh Basalleh alisema ni jambo la kushangaza kuona zaidi ya asilimia tisini ya majina ya wasimamizi walioteuliwa na NEC yakiwa ni ya Kikristo kana kwamba hakuna Waislamu wenye uwezo wa kusimamia uchaguzi huo.

"Tunaelezwa kuwa uchaguzi utakuwa wa huru na haki ilihali wasimamizi wanaoteuliwa wanatoka kwenye kundi moja. Je, hapa kutakuwa na uchaguzi wa haki kweli?" aliuliza Sheikh Bassaleh.

Alisema, Tume ilipaswa kuwateua wasimamizi wa uchaguzi kwa kuzingatia uwiano wa kidini kwa kuwa uchaguzi huo unashirikisha wananchi wa dini zote.

Alikumbusha kuwa pia hali inayojenga dhana serikali kutopenda kuwaona Waislamu kama watu walio na haki nchini kwa kutengwa tengwa na pale wanapodai haki hiyo kuonekana wakorofi na wachochezi.

Sheikh huyo amesema, Tume inapaswa kubatilisha mara moja uteuzi wa majina hayo na kuteua upya kulingana na uwiano wa kidini hata kwa kuwashirikisha viongozi wa kidini badala ya kuendelea kuteua kinyemela kwa manufaa ya kundi fulani.

--
JuuRUDI


Bonyeza hapa
kushriki mjadala au kutoa maoni juu ya habari hizi na masuala mengineyo ya Kiislamu kwenye Baraza ya Wasomaji

   Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu: Bonyeza hapa
Au
Andika barua  kwa: webmaster@islamtz.org


An-nuur Home | Ukurasa wa Mwanzo | Islam Tanzania
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook