Amsterdam
Kati ya wadachi milioni 15. 6, Waislamu ni nusu milioni, ambao ni ongezeko la mara kumi kulinganisha na walivyokuwa mwaka 1971.
"Hivi sasa Uislamu nchini Holland(Netherlands) si jambo geni, ni jambo la kawaida ambapo sehemu mbali mbali inaonekana misikiti na Waislamu wakijumuika humo kwa ajili ya swala", limeandika gazeti moja la kiislamu ulimwenguni litokalo kila mwezi.
Gazeti hilo limendika zaidi katika moja ya makala zake kuwa Serikali ya kidachi ya Holland haiingilii masuala ya dini ya jamii yoyote ile, inatekeleza demokrasia ambayo hutoa uhuru kwa kila mtu kushiriki mambo ya kijamii ikiwa ni pamoja na dini.
Nchi ya Holland ilifikiwa na Uislamu mnamo nusu ya karne iliyopita, watu wa mwanzo waliofanya tabligh hiyo walikuwa wahamiaji kutoka mataifa ya Waislamu yaliyokuwa chini ya himaya ya kidachi.
Mpaka mwaka 1949, himaya ya kidachi ilikuwa inajumuisha nchi kama Indonesia ambayo idadi kubwa ya wenyeji wake ni Waislamu.
Mnamo miaka ya sitini Holland ilikumbwa na tatizo la upungufu wa nguvu kazi kwa ajili ya viwanda vyake na mashamba lililohitajia ufumbuzi wa harakati kutoka nje ya nchi hiyo. Wafanyakazi kutoka nje ya nchi hiyo, waliajiriwa kukabiliana na hali hiyo. Wengi wa wafanyakazi hao walitoka nchi za Uturuki na Moroco.
Ingawa ilipofikia mwaka 1974, zoezi la kuagiza wafanyakazi toka nje lilisimamishwa, lakini halikuzuia wimbi la wahamiaji kutoka nchi hizo waliokuwa wakiwafuata ndugu na jamaa zao.
Aidha lilikuwepo wimbi la wahamiaji kutoka Surinam ambayo hadi mwaka 1975 ilikuwa haijapata uhuru. Wengi wa wahamiaji hao walikuwa Waislamu.
Idadi ya Waislamu hivi sasa nchini Holland ni asilimia nne ya raia wote wa nchi hiyo, wengi wao wakiwa ni wenye asili ya Uturuki ambao hawapungui 270,000, wakifuatiwa na Wamoroko wanaokaribia 225, 000 na Wasurinam wapatao 50,000.
Awali walikuwepo Waislamu waliohamia Holland kama wakimbiza kutoka nchi za Iran, Iraq, Somalia, Ethiopia, Misri, Afghanistan, uliokuwa muungano wa Sovieti na Bosnia.
Mpaka mwaka 1971, idadi ya Waislamu nchini Holland ilikuwa 54,000, mwaka 1975 idadi hiyo iliongezeka na kufikia 108,000, mwaka 1980 ikawa 225,000 na hadi kufikia mwaka 1997 ikawa 573,000.
Ibara ya 1 ya katiba ya Kidachi inaainisha haki za wakazi wote wa Holland. Imeeleza wazi wazi kuwa raia wote wana haki sawa. Imepiga marufuku aina zote za ukandamizaji kwa misingi ya dini, imani, siasa, jinsia au kabila.
Hii ikimaanisha kwamba Waislamu kama sehemu ya raia wa nchi hiyo, wana uhuru kamili wa kufuata na kutekeleza maamrisho ya dini yao kama ilivyo kwa Wakristo ambao ni asilimia kubwa ya wenyeji wa nchi hiyo iliyo barani ulaya.
Pamoja na uhuru huo bado raia wote wanawajibika kutekeleza wajibu wao kwa dola ikiwa ni pamoja na kulipa kodi na kupitia mkondo wa Elimu kama ulivyoandaliwa na Serikali. Hii ikiwa na maana kwamba watoto wote wenye umri wa miaka minne hadi 16 lazima wapelekwe shule za serikali au za binafsi ambazo hulazimika kufuata muhutasari wa Serikali.
Wageni wa nchi hiyo waliochukua uraia wanapata haki sawa na wenyeji ikiwa ni pamoja na kushiriki kupiga kura au kugombea nafasi yoyote ya uongozi wa kitaifa.
Katika serikali za mitaa kila mkazi wa Holland amepewa uhuru wa kushiriki. Imeripotiwa zaidi ya Waislamu 100 hivi sasa wanashika nafasi mbali mbali katika serikali za mitaa.
Kwa muijibu wa wakazi Waislamu waishio nchini humo, Holland ina uhuru kamili wa dini kwa mtu binafsi au jamii.
Serikali ya huko haingilii masuala ya dini, mambo yanayohusu dini hushughulikiwa na vyombo vilivyoundwa na wanadini husika kwa ridhaa yao kamili.
Kwa mujibu wa idara ya Takwimu za majengo ya nchi hiyo, Holland ina jumla ya misikiti 200 iliyojengwa sehemu mbali mbali za nchi hiyo. Waislamu wamepewa ruhusa ya kujenga misikiti kwa mujibu usanii(architecture) asilia wa Waislamu.
Aidha Waislamu wametengewa maeneo maalum ya kusalia wawapo makazini. Mavazi ya stara(Hijab) yanaruhusiwa kwa wanawake wa kiislamu wafanyao kazi na wanafunzi.
Hivi sasa vazi la Hijab ni la kawaida nchini Holland katika maofisi ya serikali, sekta binafsi na vyuo vikuu.
Kuhusu vyakula na hasa nyama, serikali ya nchi hiyo imetenga maeneo maalum kwa ajili ya machinjio ya wanyama kwa mujibu wa sheria ya kiislamu. Yapo machinjio ya kiislamu zaidi ya 500 nchi nzima.
Kuhusu masuala ya kijamii, serikali ya huko inahimiza mahusiano mema miongoni mwa raia licha ya kuwepo tofauti za kidini. Inafanya hivyo huku ikizingatia na kuheshimu miiko ya kila dini.
Serikali ya Holland hivi sasa ina mpango wa kuajiri washauri wa kiislamu katika magereza na kambi za wakimbi kwa ajili hiyo, inakusudia pia kuunda Tume ya ushauri wa mambo ya dini.
Ili kurekebisha tabia na kuwapa maadili ya kiroho wafungwa, serikali hiyo imeamua kubeba jukumu la kuwalipa mishahara viongozi wa dini wanaoendesha mahubiri magerezani.
Kama ilivyo hapa nchini, Waislamu na watu wa dini nyingine nchini Holland wamepewa uhuru wa kujenga mshule na vyuo kwa ajili ya vijana wao, lakini wanalazimika kufuata mitalaa ya kisekula.
Hivi sasa Waislamu nchini Holland wanamiliki "mashule ya kiislamu" yapatayo 30 chini ya udhibiti huo wa serikali. Tofauti iliyopo kati ya shule hizi na zile za serikali ni msisitizo wa kipindi cha dini na utekelezaji wa baadhi ya mafundisho ya kiislamu kama vile swala, mavazi ya stara na adabu nyingine ndogo ndogo.
Shule za Serikali nchini Holland zimeruhusiwa kuingiza somo la dini katika vipindi vya masomo ili kuwapa fursa wanafunzi Waislamu na wakristo kujifunza dini zao kupitia vipindi vya dini mashuleni.
Wanafunzi wasomao shule za serikali wamepewa hiyari ya kuchagua kituruki au kiarabu kuwa lugha yao ya pili.
Uislamu, lugha za kiarabu na kituruki vile vile vimepewa umuhimu katika elimu ya juu, wapo wahadhiri masomo wa hayo katika ngazi za vyuo vikuu.
Katika Chuo kikuu cha Amsterdam kuna idara ya Islamic Studies ambayo ilianzishwa na jumuiya moja ya kiislamu nchini humo.
|
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook |