BAADA ya Wazungu kuhamia Amerika na Visiwa vya Magharibi (West Indies) usafirishaji wa watumwa uliendelea kwa muda wa miaka 350. Mamilioni ya Waafrika yalikusanywa kutoka sehemu mbali mbali za Bara na kuletwa Pwani ambapo walipakiwa kwenye mashua (meli ndogo) na kupelekwa huko waliko pelekwa! Pwani hizi ziliitwa Pwani za Watumwa (Slave Coast). Kwa kipindi cha karne moja tu (1680-1786) idadi ya watu huru waliokamatwa na kufanywa watumwa wa makoloni ya Kiingereza tu ilikuwa zaidi ya milioni 20 kufuatana na makadirio ya waandishi wa Kiingereza. Kwa kipindi cha mwaka mmoja tu (1790) watu 75,000 na zaidi walikuwa wamekamatwa na kuuzwa kwa Makoloni hayo ya Kiingereza. Meli zilizotumiwa kuwasafirishia Watumwa hao zilikuwa ndogo na chafu sana. Maskini Waafrika hawa walijazwa mpaka upenuni mwa meli hizi kama wanyama au mizigo na wengi wao walifungwa kwa minyororo iliyofungiwa kwenye vifungio maalu vya mbao. Hawakuweza kujisogeza pale walipofungwa kwa sababu minyororo hii ilikuwa mifupi sana kiasi cha inchi 18 tu hivi na mmoja alikuwa juu ya mwingine kama magunia. Walikuwa wakipewa chakula kibaya sana na kidogo mno na kila walipougua au kuumia hakuna yoyote aliyewajali kwa matibabu. Waandishi wengi wa Magharibi wanaeleza wenyewe kuwa karibu asilimia 20 (20%) ya watumwa waliteketea wakati wa safari kati ya Pwani za Afrika za Amerika. Pia inakadiriwa kuwa idadi ya watu waliofanywa watumwa na mataifa yote ya Kimagharibi inafikia milioni mia moja (100,000,000).
Hii ndio habari tunayoipata kutoka kwa watu wale
wale wanaoutangaza Uislamu vibaya usiku na mchana kuwa umekubalisha utumwa.
Biashara ya Utumwa na Kanisa
Mnamo mwaka 1517, Mmisionari maarufu Bishop Bartholome de Les Cacas, ambaye alikuwa rafiki wa Wahindi Wekundu alimshauri Mfalme wa Hispania kuwa Waafrika toka Afrika ya kati wangefaa sana kwa kazi ya utumwa kuliko wenyeji wa Amerika, ushauri huu ulikubaliwa na mfalme wa Hispania. Mfalme wa Hispania alitoa mkataba kwa raia wake mmoja unaomruhusu kusafirisha watumwa 4,000 kwa mwaka toka Afrika kuwapeleka visiwa vya Caribean na kwa mara ya kwanza utumwa ulianzishwa kati ya Afrika ya Wareno na Marekani ya Wahispania.
Wazungu walitajirika kutokana na nguvu kazi ya utumwa toka ng'ambo kuliko walivyofaidika kutokana na nguvu kazi huru katika nchi zao. Ombi la Bishop Batholeme delas cacas lilikuwa mamilioni ya Waafrika kutiwa utumwani. Mwanasheria P. Dcuntin mwandishi wa kitabu The Atlantic Slave Trade
amekadiria kati ya milioni 15-20. Mwanamapinduzi wa Kimarekani marehemu Malcomx alisema kuwa kiasi cha milioni 100 ya Waafrika walitiwa utumwani na kufikishwa Amerika wakiwa hai. Haijulikani idadi ya waliofia safarini.
John Hawkins alifanya safari tatu Afrika Magharibi katika miaka ya 1560, na kuchukua Waafrika ambao waliwauza kwa Wahispania Marekani. Aliporudi Uingereza baada ya safari kwanza, kwa sababu ya faida kubwa aliyopata, malkia Elizabeth wa kwanza alitamani kushiriki katika safari ya pili; na alitoa meli iitwayo Jesus (Yesu) kwa safari hiyo. Hawkins aliondoka na Jesus (meli) kuchukua watumwa Waafrika zaidi na aliporudi Uingereza alipata faida kiasi kwamba, Malkia Elizabeth alimpa nishani. Hawkins aliamua kuwa nembo ya cheo chake kuwa alama ya Mwafrika aliyefungwa minyororo.(1)
Maaskofu na wachungaji wa kanisa wa ngazi za chini, walikuwa na watumwa wao waliofanya kazi mashambani, kuwabeba machela mabwana zao, wachungaji walipelekwa huko na huko katika safari zao. (2)
Hayo yalifanyika sehemu nyingi za Afrika na kwingineko makanisa yalikokuwa yakijengwa enzi hizoza biashara ya utumwa. Na wale watumwa waliokamatwa Marekani walibatizwa kwa mpigo wakati wakipakiwa melini. Askofu alijengewa kiti maalum gatini kwa ajili ya kazi hiyo.(3)
Biashara ya Utumwa na Uislamu
Utumwa kabla ya kuja kwa Nabii Muhammad (s.a.w.) ulikuwa umeenea karibu katika sehemu zote za ulimwengu. Na utumwa huo haukukomea kwa watu wa rangi au kabila fulani tu bali ulisambaa na kuwakumba watu mbali mbali. Watumwa walipatikana kwa njia mbali mbali miongoni mwa hizo ni wale watumwa waliopatikana kutokana na mateka wa vita (Pows) au kwa kuvizia na kuvamia watu kwa mabavu na kuwatia minyororo (kidnapping) na hii ilikuwa ndio njia kuu ya kupatia watumwa na wakati mwingine watumwa walipatikana kutokana na kushindwa kulipa madeni.
Kwa ujumla watumwa waliteswa, walinyanyaswa na kuvuliwa utu wao. Sheria nyingi za zama hizo yaani karne ya saba (kwa Kalenda ya Kikristo) kama vile. sheria ya Warumi (Roman Law) ilimruhusu mtu kufanya apendalo kwa mtumwa wake. Mtumwa alihesabiwa kama bidhaa, chombo kama jembe au shoka. Na ndio maana mara nyingi mtu akimtesa au hata kumwua mtumwa wake hakuhesabiwa kuwa amefanya kosa lolote kisheria. Kwa mfano huko Urumi moja ya burudani mashuhuri zama hizo ilikuwa ni kushuhudia pambano baina ya watumwa wawili wenye majambia, na mshindi ni yule atakayefanikiwa kumfyeka na kumuulia mbali mwenzake. Hapo watazamaji hushangilia na kurejea nyumbani huku wakisimuliana pambano lilivyokuwa zuri. Au wakati mwingine mtumwa alilishwa vizuri sana kwa muda fulani halafu alipoonekana kuwa ana siha nzuri akatumbukizwa katika uwanja kama wa mpira lakini wenye kuta ndefu pande zote ili apambane na simba mwenye njaa kali sana. Zile kikirikakara na kuhangaika kwa mtumwa kutaka kujinusuru na kuliwa na simba ndio burudani yenyewe.
Hakika mazingira kama haya jukumu la Uislamu lilikuwa
zito sana. Uislamu uliwania siyotu kuwakomboa watu kimwili bali pia kubadili
mtazamo mzima wa watu kuwarejesha katika udugu na usawa wa binaadamu.
Ukombozi wa Kiroho na Kisaikolojia
Zaidi ya ukombozi wa kimwili, Uislamu umewaletea watu wote ukombozi wa kiroho na kisaikolojia. Jambo la kwanza la kuzingatia ni kuwa falsafa nzima ya Uislamu imejengwa juu ya msingi wa Tawhiid. Msingi ambao unawakataza watu wasiwe watumwa kwa kiumbe yeyote yule japo awe mfalme wa kutisha au hata jini. Badala yake watu wote wawe watumwa wa Mwenyezi Mungu ambaye ndiye Muumba wa viumbe wote. Msimamo huu ulijitokeza (unajitokeza) sana kwa Waislamu ambao hawakukubali kuwa watumwa wa mtu yoyote. Rabih ibn Amir alipokwenda kuwalingania Uislamu kwa wafalme wa Kikristo alipoulizwa juu ya madhumuni ya Uislamu alijibu kwamba, Uislamu una shabaha ya kuwaepusha watu na utumwa wa kuwaabudu binaadamu wenzao na badala yake kuwafanya wawe huru waja wa Mwenyezi Mungu (s.w.) peke yake. Ukweli huu umesisitizwa tena na tena katika Qur'an. Itakavyokuwa vyovyote binaadamu hata ajikweze vipi ni kiumbe tu na hana tofauti na binaadamu mwingine. Kinyume chake kila binaadamu ni ndugu wa mwenziwe kwani wote asili yao ni moja. Aidha katika kuwaandaa watu kiimani na kisaikolojia Uislamu umetoa mafundisho kadhaa ambayo lengo lake ni kusisitiza kuwa ubora wa mtu unatokana na imani na utii wake kwa Mwenyezi Mungu na si nasaba wala ukoo. Hivyo hata kama mtu atapata bahati mbaya ya kuvamiwa na kufanywa mtumwa, maadam ni muumin atakuwa bora mbele ya Mwenyezi Mungu (s.w.) kuliko hao waliomkamata. Mwenyezi Mungu anatuamrisha katika Qur'an kuwaoa au kuolewa na watumwa walioamini kuliko kufunga akdi na kafiri aliyehuru hata kama akitupendeza vipi:
Wala msiwaoe wanawake makafiri mpaka waamini. Na mjakazi mwenye kuamini ni bora kuliko muungwana kafiri, hata kama ingawa hakupendezeni. Wala msiwaoze wanaume makafiri (wanawake Waislamu) mpaka waamini. Na mtumwa mwenye kuamini ni bora kuliko muungwana kafiri, hata akikupendezeni. Hao (makafiri) wanaitia kwenye Moto! Na Mwenyezi Mungu anaitia kwenye Pepo na Msamaha kwa amri Yake. (2:221).
|
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook |