Na Mohammed Dedesi
Wengi wamekumbwa na wimbi la upotoshaji wa chanzo cha mgogoro wa kisiasa wa Zanzibar uliokuwa ukifanywa na baadhi ya viongozi kwa makusudi kwa kukidhi maslahi yao. Wamekuwa wakidai eti mgogoro wa kisiasa wa Zanzibar unatokana na mazingira ya kabla ya mapinduzi ya mwaka 1964. Kwa sababu ya kutokuwa tayari kujihangaisha kufanya utafiti unaostahili kutafuta ushahidi wa wanayoambiwa, waandishi mbalimbali wamechukulia maelezo hayo kuwa ni sahihi. Hivyo ni muhimu sana kwa kuanzia tukaeleza, na kutoa ushahidi, wa kuwa mgogoro wa kisiasa wa Zanzibar umetokana na matukio ya uchaguzi mkuu wa mwaka 1995 na si kabla ya hapo abadani! Mgogoro huo katu haukuchangiwa na mazingira ya kisiasa yaliyokuwepo Zanzibar kabla ya mapinduzi ya 1964.
Kilichotokea na kinachoweza kusemwa kwa ushahidi kabisa ni kwamba sera za kibaguzi zilizotekelezwa na serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) baada ya mapinduzi hasa kwa kutoiendeleza Pemba zimechangia sana katika kuufanya upinzani uwe na nguvu baada ya kuruhusiwa vyama vingi mwaka 1992. Jengine lililoupa nguvu upinzani Zanzibar baada ya mwaka 1992 ni sifa ya viongozi wa upinzani hasa Maalim Seif Shariff Hamad katika kusawazisha makosa ya serikali ya Mapinduzi wakati alipokuwa Waziri wa Elimu wa SMZ na baadaye kuwa Waziri Kiongozi na kuonesha juhudi za kutoa haki na fursa sawa kwa wote. Jitihada zao hizi zilichangia sana katika kufukuzwa kwao katika uongozi wa Chama Cha Mapinduzi.
Kabla ya mapinduzi ya mwaka 1964, vyama vikubwa vilivyokuwa vikichuana katika chaguzi za vyama vingi zilizofanyika katika kipindi hicho vilikuwa ni Afro-Shirazi Party (ASP) na Zanzibar Nationalist Party (ZNP au Hizbu). Vyama vyote hivi vilipata misukosuko ya kusambaratika.
Kundi lililojitoa Hizbu liliunda Chama Cha kisiasa kilichojulikana kwa jina la Umma Party. Chama hiki kilishirikiana na ASP katika kufanya Mapinduzi ya 1964.
Kundi lililojitoa ASP liliitwa Zanzibar and Pemba People's Party (ZPPP). Wengi wa wafuasi wa chama hiki walikuwa wakaazi wa Pemba. Chama hichi baadaye kilijiunga na Hizbu na kuunda Serikali iliyopokea uhuru wa Zanzibar kutoka kwa Muingereza (aliyeitawala Zanzibar kabla ya hapo akishirikian na Sultani). Serikali ilidumu kwa mwezi mmoja na kufuatiwa na Mapinduzi ya Januari 1964. Inasadikika kwamba sera za kuikandamiza Pemba zilizotekelezwa na SMZ baada ya mapinduzi zilichangiwa na hasira za kuwa wafuasi wengi wa ZPPP ambao walijitoa kutoka ASP walikuwa ni Wapemba.
Na muhimu sana kuelewa kwamba hakuna hata kimoja kati ya vyama hivi vya siasa kilichokuwa cha kikabila. Vyama vyote vilikuwa na wafuasi na viongozi kutoka makabila yote yalioishi Zanzibar wakati huo. Pamoja na kuwa wengi wa wafuasi wa Chama kidogo cha ZPPP walikuwa ni Wapemba, lakini si sahihi kusema kwamba Wapemba wengi walikuwa ni wanachama wa chama hicho. Vyama vyote viwili vikubwa, ASP na Hizbu, vilikuwa na wanachama wengi Pemba na vilishinda viti katika uchaguzi. Kwa hiyo, U-Pemba na U-Unguja havihusiani na mgogoro wa kisiasa wa Zanzibar tunaouzungumzia hapa.
Kosa jingine kubwa linalohusishwa na mgogoro huu kimakosa ni kuuhusisha Uarabu katika matatizo yetu. Hili pia limeingizwa na viongozi wabaya wenye nia ya kuwapotosha wananchi kwa makusudi kwa kukidhi maslahi yao binafsi. Ukweli wanauelewa. Lengo lao ni kuwababaisha wananchi ili waendelee kutizamana kikabila na makosa ya viongozi hao yajifiche au yaonekane ni madogo (lesser evel) na hivyo wananchi wawafumbie macho na kuwavumilia ili waendeleze utawala unaoendelea kuiangamiza nchi.
Ajabu kubwa zaidi ni kukihusisha Chama cha CUF na chama cha Hizbu kilichokuweo kabla ya mapinduzi. Hii ni kwa sababu safu yote ya uongozi wa juu wa CUF ( au wazazi wao) walikuwa viongozi maarufu katika ASP. Na kwa kuheshimu hilo, siku waliokuwa viongozi hao wanafukuzwa katika CCM na Halmashauri Kuu ya Taifa ya chama hicho, Mheshimiwa Muhammed Mahmoud, Mjumbe na mzee wa chama tangu asili, alikiomba kikao hicho cha NEC kikae kimya kwa dakika moja kikimkumbuka Bwana Hamad Sharif Hamad, kaka yake Maalim Seif kwa mchango wake katika kupigania ukombozi wa Zanzibar katika Afro Shirazi Party. Hivi sivyo ilivyo katika CCM Zanzibar. Wengi wa viongozi wa juu walioko walihusika sana na chama kilichopinduliwa 1964 cha Hizbu (na ZPPP).
Chanzo cha mgogoro:
Mgogoro wa kisiasa wa Zanzibar umesababishwa na mambo mawili:
Usimamizi mbaya wa uchaguzi mkuu wa Zanzibar wa mwaka 1995 uliofanywa na Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar; na
Upotoshaji wa matokeo ya uchaguzi huo.
Vyama vyote viwili, CCM na CUF viliandika barua kwa Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (TUZ) kueleza kutoridhika kwao na uendeshaji wa uchaguzi na kuutangaza uchaguzi kwamba haukuwa huru na haki. Wote walifanya hivyo kabla ya matokeo kutangazwa, wakadai yasitangazwe, na kutamka rasmi kwamba hawatoyatambua yatakapotangazwa. Kwa mfano, CCM katika barua yao yenye kumbukumbu nambari CCM/AKZ/U.30/21 ya tarehe 25 Oktoba, 1995 iliyotiwa saini na Naibu Katibu Mkuu walisema:
"CCM ... is satisfied that the elections were not free and fair hence we do not accept the outcome of the results in these elections. Therefore we demand that the whole of the Zanzibar General Elections be nullified".
Katika kifungu cha mwisho cha barua hiyo, CCM walisema:
"We therefore insist that the results of the Presidential Election not be announced and that the whole alection be nullified and be done afresh in view of the so many irregularities that occurred."
Maneno yanayofanana yameandikwa na vyama vyote viwili kwa Tume ya Uchaguzi. Jee huu hautoshi kuwa ni ushahidi wa uchaguzi kusimamiwa vibaya?
Ni muhimu kuzingatia kwamba barua ya CCM iliandikwa siku moja baada ya Mkurugenzi wa Uchaguzi kuwaita viongozi wa vyama hivyo na kuvikabidhi matokeo yaliyoonesha mgombea wa CUF ameshinda kwa asilimia 51.4 mbele ya mshauri wa mambo ya uchaguzi Mama Judy Thompson kutoka Canada, na matokeo hayo kutangazwa na idhaa ya Televisheni ya DTV usiku ule ule, na gazeti la Majira siku ya pili yake. Barua ya CUF iliandikwa tarehe 24 Oktoba, 1995 kabla ya kupewa matokeo hayo na Mkurugenzi wa Uchaguzi.
Matokeo rasmi ya Uchaguzi yalitolewa na Mwenyekiti wa Tume siku ya tarehe 26 Oktoba, 1995 na kuonesha mgombea wa CCM ameshinda kwa asilimia 50.2.
Hii ndilo chimbuko la mgogoro wa kisiasa wa Zanzibar. Msingi wake mkubwa ni tume ya uchaguzi. Hii ndiyo Tume ambayo Serikali ya CCM inaing'ang'ania isimamie Uchaguzi Mkuu mwingine. Jee tunadhani lengo lao ni nini?
|
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook |