Na Dkt. Rose Shayo
NENO "siasa" kama litakavyotumika katika mada hii linahusu sayansi na mbinu ya utawala. Aidha, linaoanishwa na taaluma nzima ya uongozi katika vyombo au ngazi mbalimbali za utawala kuanzia ngazi ya familia, jumuiya, wilaya, mkoa hadi taifa. Uwanja wa siasa hujumlisha mifumo ya sheria, jamii, mazingira, vyombo vya habari, nguvu kazi pamoja na familia na kadhalika. Nguvu za kisiasa (political power) humaanisha uwezo wa kufanya maamuzi mbalimbali. Nguvu za kisiasa hutegemea sana idadi na uwezo wa wale walioko kwenye uwanja wa siasa.
Takwimu zilizopo zinaonesha kuwa uwanja wa siasa hapa Tanzania, na hata katika nchi nyingi za Kiafrika umetawaliwa na idadi kubwa ya wanaume ukilinganisha na wanawake. Hali hii imetokana na mfumo dume ambao umegawa majukumu katika jamii kulingana na jinsia. Katika mgawanyo huu wanawake wameegemea zaidi kwenye masuala yanayohusu malezi na utunzaji wa familia na kazi za nyumbani (private sphere). Wanaume nao wameelekezwa zaidi kwenye uwanja wa siasa (public sphere) na hata kuhesabiwa kama ndio viongozi wakuu. Kutokana na mgawanyo huu imekuwa vigumu kwa wanawake kuingia kwenye uwanja wa siasa na hasa katika ngazi mbalimbali za uongozi. Mgawanyo huu umedumu kwa miaka mingi na umepelekea kuzaa hali ya kutokuwepo na usawa kati ya wanawake na wanaume, utengwaji au kutengwa, unyanyasaji wa kijinsia (sexual disrimination).
Mbali na mfumo dume, kuna baadhi ya mambo mengine mengi yaliyochangia katika kutokuwepo na usawa katika uwiano wa wanawake na wanaume katika uwanja wa siasa hasa katika kipindi cha mfumo wa vyama vingi. Baadhi ya mambo hayo ni kama ifuatavyo: Mila na utamaduni, wanawake kutojiamini, utekekelezaji hafifu wa sera za kimataifa na kitaifa, ukosefu wa mazingira yanayovutia wanawake, ushirikiano mdogo kutoka kwa makundi makuu kama wanawake wenyewe, sera ambazo hazizingatii masuala ya kijinsia na kadhalika.
Katika sehemu hii tutajaribu kuchambua kwa kina hali halisi ya ushiriki wa wanawake katika siasa katika ngazi mbalimbali. Napenda ieleweke wazi kuwa ushiriki huu ni katika ngazi ya uongozi na utawala. Vinginevyo inabidi kuweka wazi kuwa ushiriki wa wanawake katika kazi za uzalishaji mali na nguvu kazi upo wazi an hauhitaji mjadala. Asilimia 85 ya wanawake wa Tanzania wanashiriki kikamilifu katika shughuli za uzalishaji mazao ya chakula na biashara. Asilimia 32 ya wafanyakazi wote serikali ni wanawake. Kuna wasiwasi kuwa idadi hii huenda imepungua kufuatia zoezi la upunguzwaji wa wafanyakazi (retrenchment programmes) ambao unatokana aidha na upunguzaji moja kwa moja wa wafanyakazi au ubinafsishaji wa vyombo na mashirika ya umma (Shayo, 1998).
Katika mada hii tutaangalia ushiriki wa wanawake katika maeneo mawili;
Ushiriki wa moja kwa moja kwenye vikundi rasmi na visivyo rasmi vya umma.
Uwakilishi katika vyombo mbalimbali.
Ushiriki wa wanawake kupitia vikundi rasmi
Katika sehemu hii tutachambua ushiriki wa wanawake
katika baadhi ya vyombo vya serikali ambavyo vinashughulika na kuandaa
sera na mipango ya maendeleo. Vikundi hivi ni pamoja na Bunge, Baraza la
Mawaziri, Serikali za Mitaa, Bodi za Mashirika na vyombo vinginevyo, vyama
vya siasa na vyama vya wafanyakazi, Tume ya Uchaguzi.
Bunge
Bunge la Tanzania ndiyo ngazi kubwa ambayo inahusika na kupitisha maamuzi makubwa yanayohusu mipango na matumizi ya rasilimali za nchi, sera za nchi na kadhalika. Wabunge hupatikana kwa namna mbili. Ama ya kwanza ni ile ya Wabunge ambao huchaguliwa kwa kura kutoka katika majimbo ya uchaguzi. Sheria ya Uchaguzi ya 1985 imeweka bayana kuwa wananchi wote (wanaume na wanawake) wenye sifa zinazohitajika wanaweza kugombea jimbo lolote wanalopenda. Aina ya pili ni ile ya Wabunge ambao huchaguliwa kupitia viti maalumu. Kwa mfano tangu mwaka 1980, Bunge lilipitisha uamuzi wa kutenga asilimia 10 ya viti vya Wabunge kwa ajili ya wanawake. Idadi hii imekuwa ikiongezwa mara kwa mara hadi kufikia asilimia 15. Katika uchaguzi ujao, tume ya Jaji Kisanga imependekeza viti maalum vya wanawake viongezwe hadi kufikia kati ya asilimia 20-30. Jedwali Na. 1, inaonesha ushiriki wa wanawake kati ya 1961-95:
Jedwali Namba 1: Ushiriki wa wanawake katika
Bunge 1961-1995) kwa asilimia)
Mwaka Asilimia ya w'ke Asilimia ya w'ume Jumla
1961-65 1.9 98.1 100.0
1965-70 4.0 96.0 100.0
1970-75 4.0 96.0 100.0
1975-80 7.3 92.6 100.0
1980-85 10.0 90.0 100.0
1985-90 10.0 90.0 100.0
1990-95 18.0 92.0 100.0Chanzo: Ripoti mbalimbali za serikali.
Kwa ujumla inaonekana wazi katika jedwali 1 kuwa katika kipindi chote cha miaka arubaini tangu nchi yetu ipate uhuru, ushiriki wa wanawake katika Bunge haujafikia asilimia 20. Hii inaonesha kuwa idadi hii ni ndogo sana. Ongezeko la uwakilishi wa wanawake bungeni limechangiwa kwa kiasi kikubwa na mpango wa "viti maalum". Uwakilishi wa moja kwa moja kutoka kwenye majimbo ya uchaguzi bado ni mdogo sana. Kwa mfano katika uchaguzi uliopita, ni wanawake wachache sana (watatu) walipata Ubunge kupitia majimbo ya uchaguzi. Uchambuzi wa kina unaonesha kuwa hawa ni baadhi ya wanawake wenye uzoefu mkubwa wa uongozi aidha serikalini au ndani ya chama chenyewe. Hata hivyo idadi ya wanawake wanaojitokeza kugombea Ubunge kupitia majimbo bado ni ndogo sana, kulinganisha na ya wanaume.
Ingawa takwimu hazikupatikana, inaelekea idadi kubwa ya wanawake huwania Ubunge kwa kupitia dirisha la viti "maalum" walivyotengewa na serikali tangu mwaka 1980. Kuna haja ya kuchambua idadi kamili na sifa za wanawake ambao hukosa kuchaguliwa ili kuangalia namna ya kuwatumia kwenye ngazi nyingine za uongozi.
Baraza la Mawaziri na Vyombo vinginevyo vya serikali
Baraza la Mawaziri ni chombo cha serikali ambacho kinahusika na kuandaa mipango ya kutekeleza sera na mipango ya nchi kama inavyopitishwa na Bunge. Mawaziri wanaoongoza wizara mbalimbali huchaguliwa na Rais wa Jamhuri ya Tanzania. Kabla ya mwaka 1995 mawaziri walichaguliwa bila kigezo maalum mbali ya kuwa na sifa na uwezo wa kutenda kazi zinazohusu wizara yenyewe.
Mnamo mwaka 1995, Bunge lilipitisha sheria kuwa mawaziri wote ni lazima wawe Wabunge. Moja kwa moja inaonekana kuwa uamuzi huu umeathiri moja kwa moja ushiriki wa wanawake katika Baraza la Mawaziri. Kama tulivyoonesha hapo awali idadi ya wanawake wabunge ni ndogo sana ukilinganisha na ile ya wanaume. Kwa ujumla ushiriki wa wanawake katika Baraza la Mawaziri umekuwa ni mdogo sana na idadi yao haijazidi wanne hata mara moja. Angalia jedwali namba mbili linaonesha hali halisi ya ushiriki wa wanawake katika Baraza la Mawaziri na vyombo vingine vya uongozi wakati wa mfumo wa chama kimoja. Hali haijabadilika sana hata katika kipindi cha mfumo wa vyama vingi.
Jedwali Na. 2: Idadi ya viongozi wanaume na
wanawake walioko sehemu mbalimbali Tanzania 1990.
Nafasi 1990 W/wake W/ume % ya w/wake
Mawaziri 5 15 25
Mawaziri wadogo 0 10 0
Makatibu wakuu 1 20 5
Wakuu wa Mikoa 0 25 0
Wakuu wa Wilaya 20 170 12
Wakuu wa Bodi 1 449 0.2
Wakurugenzi wakuu 0 40 0
Wakurugenzi (GM) 1 409 0.24
Mabalozi 1 56 2.7
Makamishna 1 24
Majaji 2 1.0Chanzo: Ripoti ya Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Wanawake na Watoto.
Vile vile katika nafasi ya mawaziri wadogo (Deputy Ministers) na Makatibu Wakuu (Permanet Secretaries) ushiriki wa wanawake umekuwa dhaifu sana. Wajumbe wanaoshika nyadhifa hizi pia huchaguliwa na Rais na serikali ya Muungano. Vigezo vinavyotumika kuteua wajumbe hawa hazipo wazi sana.
Itaendelea Ijumaa
|
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook |