KATIKA mfululizo wa mbinu za kuhakikisha kuwa Uislamu unateketezwa makafiri wa Kikuraishi walitumia mbinu ya mateso kwa Mtume na waumini. Mateso haya yalikuwa ya aina tofauti kwa watu tofauti lakini aina kubwa ya mateso iliyohusu waumini wengi pamoja na Mtume mwenyewe ni kupigwa.
WANAHISTORIA ya Kiislamu wanaonesha kuwa makafiri wa Kikureish na wengine walithubutu kumpiga Mtume (s.a.w.) mara kadhaa katika kipindi cha Makka. Mtume (s.a.w.) alipigwa mara mbili kwenye Ka'aba. Mara ya kwanza ni pale alipoingia katika Ka'aba na kutangaza kuwepo kwa Mwenyezi Mungu mmoja. Kwa kufanya hivi Mtume alizuia zahama kubwa, makafiri wa Makka walimvamia kutoka kila upande na kumpiga. Ndipo Harith ibn Ab Hala alipokimbilia kumtetea Mtume (s.a.w.) lakini majambia yalimuelekea yeye na akafa shahidi wa kwanza katika utume wa Mtume (s.a.w.).
Mtume alipigwa mara ya pili katika uwanja huo huo wa Ka'aba. Siku moja wakuu wa makafiri wa kukureish walikaa katika Hijr walikuwa wanazungumza habari za Mtume (s.a.w.) mara Mtume (s.a.w.) akatokea. Mtume alikuwa anatufu alipofika usawa wa walipokaa walimshambulia. Hali ilikuwa hii kwa mara ya kwanza ya pili na ya tatu lakini katika hii mara ya tatu Mtume (s.a.w.) alisimama na kuwaambia:
Mnataka kumwua mtu kwa sababu anasema anamuamini Mungu mmoja? Wakamuacha na akaondoka.
Mara ya nne Mtume alipigwa hadi kuchuruzika damu mwili mzima alipokwenda Taif. Mtume alikwenda Taif kwa kueneza ujumbe wake. Wakuu wa Taif hawakutaka kusilimu na alipowalingania watu wa kawaida nao hawakutaka kusilimu. Pamoja na kukataa kwao Mtume aliendelea kuwalingania ndipo wakatoa amri Mtume apigwe mawe atakapoonekana.
Watu walipopata amri ile, waliwaelekeza watoto wahuni wa mjini wampige Mtume mawe mpaka aondoke.Bila ya huruma walimpopoa mtume mawe mpaka kumsindikiza nayo kwa umbali wa maili mbili. Zaidi bin Harith alijitahidi sana kumkinga Mtume kwa mwili wake lakini haikusaidia kitu kwani wote walibubujikwa damu mwili mzima kuanzia kichwani hadi miguuni.Wale watoto na wahuni wa mji walipoacha kuwapiga na kurudia zao, Mtume (s.a.w.) na Zaid walikaa kujipumzisha katika shamba la 'Utbah bin Rabi'ah. Utbah na ndugu yake walipomuona Mtume katika hali ile walimhurumia na wakamtuma mtumwa wao kuwaletea mtume vishada vya zabibu na vyakula vingine. Yule mtumwa alimuuliza Mtume (s.a.w.) juu ya safari yake na juu ya ujumbe wake. Yule mtumwa alisilimu baada ya kupata maelezo yale kutokana kwa Mtume (s.a.w.) na Bwana wake alijuta sana kwa nini alimtuma kwa Mtume (s.a.w.). Katika hali ile ya udhaifu Mtume (s.a.w.) alimuomba Mola wake dua ifuatayo:
"Ya Allah kwako nashitakia udhaifu wa nguvu zangu na udhalilifu wangu katika macho ya watu. Ewe mwingi wa Rehma na Huruma kuliko wote mwenye huruma; Wewe ndiye Bwana wa wanyonge wewe ndiye Mola wangu.
Ni kwa watu gani umenipeleka? Kwa adui asiye na huruma anayenikunjia uso au kwa mgeni uliyempa uwezo juu ya jambo langu hili? Sijali lolote kunitokezea isipokuwa naomba ulinzi wako. Naomba hifadhi ya nuru ya uso wako nuru iangazayo mbingu na kuondosha aina zote za giza na nuru iongozayo na kudhibiti mambo yote ya hapa duniani na Akhera. Naomba uninusuru na ghadhabu zako au kutokuwa radhi na mimi. Sina budi kuondosha au kutokuwa sababu ya kutokuwa radhi na mimi ili hatimaye uwe radhi na mimi. Hapana nguvu wala uwezo ila kutoka kwako" (Sahihi Muslim).
Mara baada ya dua yake alimjia Jibril (a.s.) na baada ya kumpa salaam alisema:
"Allah anajua yote yaliyotokea katika yako na watu hawa.ASnamtuma Malaika wa milima kuwa chini ya amri yako".
Mara tu baada ya Jibril (a.s.) kumaliza ujumbe ule malaika muhusika alisimama mbele ya mtume na kusema:
"Ewe Mtume wa Allah, niko chini ya utumishi wako (niko tayari kukutumikia utakavyonituma).Kama unataka naweza kuvigonganisha vilima viwili vilivyoutazama mji huu na watu wote ndani yake wahiliki au unaweza kuamua adhabuyoyote unayotaka wapate"
Mtume (s.a.w.) aliye rehema kwa viumbe alijibu:
Hata kama watu hawa hawakukubali Uislamu, ninategemea kwa Allah kuwa watatokea watu katika kizazi hiki watakaomuabudu Allah na kupigania dini yake"
Tukio hili la Taif, linatuonyesha jinsi Mtume (s.a.w.) alivyokuwa rehema kwa viumbe na mvumulivu katika kazi yake. Pamoja na kufanyiwa ukatili mkubwa kiasi kile na watu wa mji wa Taif, bado hakuwalaani au kuwataka waangamizwe, bali bado alikuwa na tamaa kuwa watatokea watu wazuri katika kizazi chao watakaokuwa Waislamu kuupigania inavyostahiki.
Kupigwa na mateso mbalimbali kulitofautiana kutoka mtu hadi mwingine kama ifuatavyo:
Abu Bakar (r.a.)
Mara tu Mtume (s.a.w.) alipodhiridha utume wake hadharani, Abu Bakr alikwenda kwenye Ka'abah akatoa khutuba juu ya Uislamu. Watu wote waliokuwa pale walimvamia na kuanza kumpiga. Baada ya kuanguka chini, Utbah bin Rabi'ah alimpiga kwa viatu mpaka akazimia. Hakupata fahamu mpaka jamaa zake wakampeleka nyumbani kwake, na alikaa kitandani kwa siku kadhaa. Siku moja wakati Mtume (s.a.w.) alipokuwa kwenye Ka'bah, Abu Jahl alikuja na kumtia shingani kamba ya nguo iliyosokotwa. Aliinyonga ile kamba na kuikaza ili kumniga Mtume mpaka afe. Abu Bakar (r.a.) alipona kitendo kile anafanyiwa Mtume, alienda mara moja kumuokoa kwa kumsukumiza Abu Jahl pembeni na kuitoa ile kamba shingoni mwa mtume, kisha akasema: "Mnataka kumuua mtu mzuri kama huyu ambaye ni Mtume wa Allah anayemtangaza Allah kwa sifa zake tukufu?" Kisha Abu Jahl na maadui wengine wa Uislamu walimgeukia Abu Bakar na kumpiga sana kikatili.
Bilal (r.a.)
Bilal alikuwa Mhabeshi na mtumwa wa Umayyah bin Khalaf, adui mkubwa wa uislamu. Ummayyah alikuwa akimpiga sana Bilal kisha alikuwa akimfunga kamba za mikono, miguu na shingoni na aliwaambia watoto wamburure njiani, mara nyingine alikuwa akimshindisha na kumlaza njaa, kisha siku ya pili yake alikuwa akimtoa nje na kumlaza chali uchi katika jua kali juu ya mchanga wa moto na kumuwekea jiwe kubwa la moto juu ya kifua chake na kumwambia, "Utasalia vivi hivi mpaka ufe au uache dini ya Muhammad". Bilal alikuwa akisema; Ahad, "Ahad "Yaani Naabudu Mungu mmoja tu. Alitaabishwa hivyo hivyo mpaka Abu Bakar alipomkomboa. Watumwa wengi walikuwa wakiteswa kwa ajili ya Uislamu wao.
Abu Fukayha (r.a.): Alikuwa kitaabishwa na kuteswa na mtoto wa Umayyah kwa namna ile ile alivyokuwa akitaabishwa Bilal.
Bibi Zinira (r.a.): Abu Jahl alikuwa akikiunguza chuma motoni kisha akimgandamiza nacho machoni mpaka akapofuka.
Khabbah Ibn - Ar att: Alikuwa akinyolewa nywele kisha akichomwa kwa bapa la chuma chyenye moto kichwani.
Ammar bin Yasir (a.s.): Baba yake na ndugu yake walikuwa wakipigwa kwa makuti ya mitende kila siku mpaka wakajaa madonda mwili mzima. Baba yake na ndugu yake waliuwawa katika mateso hayo na akabakia Ammar.
Mama yake Ammar (r.a.): Pamoja na mateso mengi aliuliwa kikatili mno. Alichomwa mkuki tumboni.
Amir bin Furahya (r.a.): Aliadhibiwa kikatili mno mpaka akarukwa na akili.
Bibi Luhayna (r.a.): Alikuwa akiadhibiwa kwa ukatili mno na 'Umar bin Khattab kabkla hajasilimu. Ummar alikuwa akimchapa bakora mpaka achoke.
Zubair Ibn Al-Uwwan: Baba yake mdogo alikuwa anamfunga ndani ya mkeka na kufukizwa moshi. Hii ni mifano michache tu ya mateso dhidi ya Mtume (s.a.w.) na Waislamu. Takribani Waislamu wote waliosilimu mwanzoni walionyeshwa mateso na makafiri na wengine waliteswa kwa mateso mabaya ambayo hayafai kutajwa hadharani. Mateso haya yalidumu kwa muda mrefu na kila kukicha makafiri walibuni mateso mapya.
Pamoja na mateso yote haya, kwake na kwa Waislamu, Mtume (s.a.w.) hakuwatukana maadui zake wala kuwalaani na wala hakumuomba Allah awalaani au awaangamize. Bali alikuwa ni mwenye kuvumilia na kusubiri na akawafunza Waislamu kufanya hivyo. Waislamu walivyozidi kuteswa na maadui zao ndivyo imani yao juu ya Allah na mtume ilivyozidi kuwa imara na ndivyo walivyozidi kuwa wavumilivu katika njia ya Allah. Nyoyo za Waislamu zilikuwa zimejawa na ule msimamo wa Mtume (s.a.w.) alioudhihirisha kwa makafiri wa Kiquraysh kupitia ami yake, "Sitaacha kazi hii hata kama wataliweka jua katika mkono wangu wa kulia na wakaweka mwezi katika mkono wangu wa kushoto. Ama Allah atanipa ushindi au nitakufa katika kazi hii." Mafundisho ya Qur'ani na mwenendo wa Mtume (s.a.w.) viliwavuta sana Waislamu na kuwafanya kuwa jasiri wasiokuwa na mfano.Walimpenda Allah, Mtume wake na Dini yake kuliko walivyozipenda nafsi zao. Walikuwa tayari kuteseka au kufa kwa ajili ya Allah, Mtume wake na dini yake.
Hatunabudi kufahamu kuwa Waislamu kupata mateso kwa ajili ya dini yao ni jambo la kawaida ambalo ameliandika Allah (s.w.). Mtu hawezi kuwa Muislamu wa kweli mpaka awe tayari kwa hali na mali kuipigania dini ya Allah. Wala haiwezi kuwepo jamii ya Kiislamu yenye kuendesha mambo yake yote katika kila kipengele cha maisha kwa kufuata barabara mwongozo wa Allah (s.w.) na mtume wake, bila ya Waislamu kushikamana kwa pamoja na kupigania Dini ya Allah kwa mali zao na nafsi zao.
Mbinu ya kuwa na majaribio ya Kuua.
Mbinu hii iliwahusu Waislamu wa ngazi zote na waliuliwa kwa namna zinazotofautiana. Harith ibn Abdala alikufa kwa kupigwa na makafiri wa Kikuraishi alipokuwa anamnusuru Mtume (s.a.w.) aliyekuwa anapigwa. Sumayya ndiye mama wa Ammar alikufa shahidi kwa kuchomwa mkuki na Abu Jahal. Yasiri alikuwa baba wa Ammar aliteswa hadi kufa.
Jitihada za kumuua Mtume (s.a.w.).
Ama kuhusu Mtume hawakuweza kumuua lakini walifanya jitihada mbalimbali za kumuua kama ifuatavyo:
Maquraysh walikasirika sana walipogundua kuwa takriban Waislamu wote wameshahamia Yathrib na walihofia kuwa wakimwacha Muhammad naye akahamia Yathrib, atajiimarisha na Uislamu utakita mizizi. Hata hivyo tetesi kuwa Mtume naye atahamia Yathrib zilishaenea miongoni mwa Maquraysh, ikabidi wakutane waaume la kufanya kabla jambo hilo halijatokea. Abu Jahl, adui mkubwa wa Uislamu aliitisha mkutano huo wa vijana 14 wa koo zote za Quraysh isipokuwa vijana wa Banu Hashim tu. Katika mkutano wao huo uliofanyika katika "Dar al-Nadwa", yalitolewa mapendekezo yafuatayo dhidi ya Muhammad (s.a.w.):
(1). Wamfunge Mtume peke yake katika chumba
(2). Wamzibe macho na wamfunge mikono barabara kisha wampandishe juu ya ngamia aliyeitiwa vitunga vya kuziba macho, aachwe ahangaike naye jangwani mpaka afe kwa kiu, njaa na jua kali.
(3). Mtu mmoja ampige panga ya shingo amuulie mbali.
(4). Wachaguliwe vijana watukufu kutoka katika kila tumbo la Quraysh, kisha kila mmoja apewe upanga mkali, wakusanyike, alfajiri moja makhsusi wamuue wote kwa pamoja, ili lawama ziangukie koo zote za Quraysh. Hapo Banu Hashim hatakuwa, na la kufanya ila kupokea diya tu.
Hizi ndizo njama za Maquraysh dhidi ya maisha ya Mtume (s.a.w.) ambazo pia zinabainishwa katika Qur'an:
"Na (kumbuka Ee Muhammad)! walipokufanyia hila wale waliokufuru ili wakufunge au wakuue au wakutoe (Makka kwa namna mbaya); na wakafanya hila (zao barabara). Na Mwenyezi Mungu akapindua hila hizo. Na Mwenyezi Mungu ni mbora wa kupindua hila (za watu wabaya)" (8:30).
Walikubaliana na ile rai ya nne, wachaguliwe vijana watukufu kutoka kila ukoo wa Maquraysh na wakaizunguka nyumba ya Mtume usiku ili akitoka alfajiri wamvamie wote kwa pamoja.
Katika mchana ule ambao usiku wake vijana wa kikuraysh waliazimia kumuua Mtume, alikuja Jibril akamueleza Mtume njama za Maquraysh dhidi yake na akampa amri ya kuhamia Yathrib katika usiku ule ule. Pale pale Mtume alimwendea Abu Bakar na kumfahamisha kuwa safari imeshawiva na atampitia usiku wa manane waende zao. Mtume (s.a.w.) na Abu Bakar walishaandaa safari kabla ya amri hii ya kuhama. Walishapanga njia watakayopita na pango watakamojificha katika siku za kutafutwa, pamoja na mipango mingine Abu Bakar alikwisha nunua ngamia wawili kwa ajili ya safari. Alimchukua Binti yake Asma, kwa siri siri mpaka kwenye pango la Thawr mahali watakapojificha ili awaletee chakula humo usiku; alimuamuru mchungaji wake wa mbuzi, Bwana Amr bin Furagha awe akiwaletea maji na maziwa kwenye hilo pango; alimuamuru mwanae mdogo, Abdallah, awaletee habari yoyote itakayowahusu watakapokuwa pangoni na alishamkodi bedui mmoja, Abdullah bin Uraiqit, kwa dinar 300 atakayewaongoza kwenda Yathrib kwa njia isiyotumiwa na yeyote.
Mtume baada ya kurejea kutoka kwa Abu Bakar alimwita Ally bin Talib, akamfahamisha habari ya safari yake na akamkabidhi amana zote za watu alizokuwa nazo ili azirudishe kwa wenyewe na wakamtaka alale kitandani mwake badala yake bila ya wasiwasi wowote.
Wakati wa kuondoka ulipofika, Mtume (s.a.w.) alitoka nje akawakuta maadui zake wamelala fofofo, akawanyunyizia mchanga vichwani mwao, huku akisoma Suratul Yassin, aya ya 1-9, kisha akaondoka zake salama salimini. Ieleweke hapa kuwa kilichomkinga Mtume (s.a.w.) hapa si Suratil Yaasin kama wengi wanavyoitakidi na wala Surat Yaasin sio kinga bali anayemkinga mja na shari yoyote ile ni Allah (s.w.). Bila shaka Mtume (s.a.w.) alisoma aya hizo ili kujikumbusha na kujiliwaza kutokana na ujumbe unaopatikana humo. Mtume (s.a.w.) hakuwa na wasiwasi wowote kwa kuwa alikuwa na yakini juu ya ulinzi wa Allah (s.w.).
Baada ya kutoka nyumbani kwake, Mtume (s.a.w.) alimpitia Abu Bakar wakaanza safari yao mpaka kwenye pango la mlima Thawr lililopo maili mbili kusini mwa Makkah.
Huku Makkah, Maquraish walipoona kuwa hila yao haikufanikiwa walikasirika sana wakawa wanakwenda huku na kule katika harakati za kumtafuta Mtume.Kabla hawajaenda mbali walipita kwa Abu Bakar naye hawakumkuta. Wakaamua kumkodi Bedui mmoja Abu Kurz Al-Khuzai, aliyekuwa hodari sana kutafuta nyayo za mwenye kutafutwa. Wakamfuata nyuma yake wakaikagua Makkah yote, Hatimaye aliweza kuitambua njia walioifuata Mtume (s.a.w.) na mwenzake, wakaanza kutafuta kwa hadhari kubwa hata wakapanda juu ya ule mlima wenye pango walimojificha Mtume. Walipofika juu, yule Bedui mfuata nyayo, aliwaashiria kwenye lile pango lililokuwa kiasi cha futi 40 hivi kutoka pale walipo. Abu Bakar alipowaona wamewakaribia kiasi kile alipatwa na wasiwasi kuwa labda wataonekana, Mtume alimtuliza na kumwambia:
"..... Usihuzunike, kwa yakini Mwenyezi Mungu pamoja nasi....." (9:40).
Vijana wa Kiquraysh walipotaka kuliendea lile pango, Umayyah Bin Khalaf, mmoja wa mabwana wakubwa wa Kiquraysh, alipiga kelele kwa ukali na hasira akasema, "Hamna akili nyinyi kama huyu tuliyepoteza fedha zote kumkodi? Vipi mtu ataweza kupita katika pango lile pasina kuharibu utando wa mabuibui wale waliotanda pale, au vipi njiwa wataweza kukaa pale na kulalia mayao yao ikiwa pana mtu ndani ya pango lile? Wallah 'mabuibui wamelitanda pango hili hata kabla ya kuzaliwa mwenyewe Muhammad.Hajui chochote mfuataji huyu".Ukweli ni kwamba, buibui na njiwa wale hawajakuwepo zamani kama anavyodai Umayyah bali wote walikuja alfajiri ya siku ile ile ili wapate kuwaziba macho Maquraysh wasimwone Mtume na mwenzake. Buibui na njiwa walikuwa miongoni mwa askari wa jeshi la Allah katika kumnusuru Mtume wake na dini yake kama anavyotukumbusha katika Qur'an:
"Kama hamtamnusuru (Mtume) basi Mwenyezi Mungu alimnusuru walipomtoa wale waliokufuru, alipokuwa (mmoja tu na mwenziwe) wa pili wake (peke yao); walipokuwa wote wawili katika pango; (Mtume) alipomwambia sahibu yake:Usihuzunike, kwa yakini Mwenyezi Mungu yu pamoja nami.Akamteremshia utulivu wake na akamnusuru kwa majeshi msiyoyaona, na akafanya neno la wale waliokufuru kuwa chini, na neno la Mwenyezi Mungu ndilo la juu. Na Mwenyezi Mungu ndiyo anayeshinda na ndiye mwenye hikima." (9:40).
Maquraysh walipokata tamaa kuwa hawataweza kumuona Mtume katika viunga vya Makkah walitangaza kuwa atakayemleta Muhammad akiwa hai au amekufa atapata zawadi ya ngamia 100. Mtume na Abu Bakar walibaki mle pangoni kwa muda wa siku tatu kisha waliendelea na safari yao ya Yathrib na mambo yakaenda kama walivyopanga. Katika msafara wa kwenda Yathrib Mtume (s.a.w.) aliongozana na Abu Bakar, Mtumwa wa Abu Bakr, Bwana Amir bin Furayha, na yule Bedui aliyekodiwa kuwa mwongozaji wa msafara.
Huko Makkah shujaa alikwenda huku na kule kumtafuta Muhammad ili aweze kujipatia ile zawadi nono ya ngamia 100. Shujaa mmoja, Suraqah bin Malik alifanikiwa kuufuatia msafara wa Mtume lakini kabla hajakaribia farasi wake alijikwaa akaanguka.Alijaribu kumuinua na kuendelea kuufatilia, lakini farasi wake alianguka tena. Akamuinua tena na safari hii miguu yake ilizama ardhini akazuiliwa, hawezi kuchopoka. Ilipofika hali hivyho, Suraqah alipiga makelele ya kuomba amani na Mtume akampa. Pale pale akachopoka akasimama pembezoni mwa Mtume na kumwambia, mimi nina yakini kuwa jambo lako hili litaenea Bara Arabu yote. Basi naomba unipe barua yako ya amani na Allah atanisaidia." Mtume alimuamuru, Amiri bin Fuhayra amuandikie barua hiyho ya amani. Suraqahg alirejea Makkah na walipokutana na Abu Jahl alimpa habari juu ya yote yaliyomtokea na akamtaka Abu Jahl asilimu kama yeye alivyosilimu baada ya kuyakinisha kuwa kweli Muhammad ni Mtume wa kweli. Abu Jahl alimshangaa akamwambia; "Masikini Roho yako ndio kwanza sasa unajua kwamba Muhammad ni Mtume wa Haki? Mimi tangu zamani najua kuwa yeye Mtume wa Haki lakini sitaki kumfuata tu. Kwa nini kila utukufu wawe nao, Bani Hashim peke yao? Banu Hashim wanatoa watukufu na sisi Banu Makhzun tukatoa; wakatoa mashujaa na sisi tukatoa; wakalisha nasi tukalisha. Hata leo farasi wao na wetu wana gusana magoti kwa kukaribiana, anatokea kwao Mtume aliyeletwa na Allah sitamfuata' Tutapata wapi Mtume wa kumlinganisha na wao? Kwa hiyo, sitamuamini tukapata kuwapa cheo hiki Banu Hashim peke yao."
Kutokana na safari hii ya Mtume (s.a.w.) tunajifunza.
Kwanza tunaona uzito wa amana katika Uislamu. Mtume (s.a.w.) katika ile hali ya kuzingirwa na maadui kiasi kile kamwe hakusahau amana za watu alizokuwa nazo pamoja na kwamba amana hizo zilikuwa za hao maadui zake. Hivyo katika Uislamu hapana ruhusa ya kuhini amana ya mtu kwa kisingizio mwenye amana hiyo ni kafiri au adui wa Uislamu. Amana ni amana na ni lazima irejeshe kwa mwenyewe. Msisitizo wa kurejesha amana kwa wenyewe uko wazi katika Qur'an:
"..... Na atakayefanya khiana, atavileta siku ya kiyama alivyovifanyhia khiana, kisha kila mtu atalipwa kwa aliyoyachuma wala hawatadhulumiwa." (Rejea ........)
Pili, safari ya mtume inatufundisha umuhimu wa kuyapanga mambo yetu vizuri kabla ya utekelezaji. Safari ya Mtume ilipangiliwa vizuri mwanzo hadi mwisho kabla au kuianza safari yenyewe. Wakati wakuanza safari, mahali pa kujificha, namna ya kupata mahitaji muhimu, namna ya kupata habari kutoka kwa maadui, vipando vya kusafiria pamoja na mwongozaji wa msafara, vyote viliwekwa katika mpango na mwongozo mapema kabla ya siku ya safari. Pamoja na kumtegemea Allah (s.w.) kwa mafanikio yetu yote hatuna budi kufuata sheria za maumbile alizoziweka Allah (s.w.). Tunatakiwa katika uendeshaji wa mambo yetu tuweke mipango madhubuti yenye kuzingatia hali halisi ya mazingira yetu, kisha tujitahidi kuyatekeleza kwa kadri ya uwezo wetu huku tukitegemea mafanikio yetu kwa Allah (s.w.). Kawaida nusura ya Allah huja pale ambaypo mwanadamu hana uwezo napo. Mtume (s.a.w.) hakuwa na uwezo kupambana na maadui waliozingira nyumba yake, hivyo Allah (s.w.) alimnusuru kwa kuwalaza maadui zake akatoka na kwenda zake pasina kumwona. Pia pamoja na jitihada na tahadhari zote alizozichukua Mtume (s.a.w.) alileta nusura yake kwa kuwaamrisha buibui na njiwa wafanye vile walivyofanya. Vile vile Mtume (s.a.w.) alichukua kila hadhari ya kuchukua njia ya uficho isiyowahi kupitwa na ili wasije kufuatwa kwa urahisi, Allah (s.w.) akawaepusha na shari za Suraqah, baada ya wao kujitahidi kujihami kwa kadiri ya uwezo wao.
Mbinu ya Fitna.
Mbinu hii ilitumika pale Waislamu walipohamia Uhabeshi baada ya kuzidi kwa mateso. Maelezo kamili ya tukio hili ni kama ifuatavyo:
Waislamu kuhamia Uhabeshia (Abyssinia).
Mtume (s.a.w.) alipoona hali ya mateso kwa Waislamu imezidi kiasi cha kutoweza kuvumulika tena, hasa kwa wale waliokuwa wanyonge katika jamii, aliwapa Waislamu ruhusa ya kuhamia Uhabeshia (Abyssinia) kwa mfalme Negus aliyekuwa mwadilifu. Hivyo, mnamo mwishoni mwa mwaka wa tano baada ya utume (5 B.U.). Sawa na Oktoba, 615 A.D., kiasi cha watu 15 wanne miongoni mwao wakiwa wanawake, walihamia Uhabeshia. 'Uthman bin Affan na mkewe. Ruqayyah bint Muhammad (s.a.w.) walikuwa katika msafara huu 'Uthman alikuwa ndiye kiongozi wa msafara huu. Walipofika Uhabeshia walimuona mfalme Najash na kumuomba kukaa katika nchi yake naye akawakubalia kwa moyo mkunjufu. Baada ya Waislamu kukaa nchini humo kwa muda wa miezi mitatu kamili, ulikuja uvumi kuwa Maquraysh wote wa Makkah wamesilimu na hapana mateso tena dhidi ya Waislamu. Hivyo, wakaona hapana haja tena ya kuendelea kukaa katika nchi ya kigeni na wote wakaondoka kurudi Makkah. Walipofika Makkah waligundua kuwa ule ulikuwa ni uvumi tu na waliyokuta mambo ni mabaya zaidi kuliko walivyoyaacha. Walimuhadithia Mtume (s.a.w.) na Waislamu juu ya mapokezi mazuri na usalama waliopata huko Uhabeshia.Habari hizi ziliwavutia sana Waislamu na wengi wakawa na hamu kubwa ya kuhamia huko.
Kwa mara ya pili, likatoka kundi kubwa la Waislamu kuhamia Uhabeshi wengi wakiwemo wale waliokuwepo katika msafara wa kwanza. Katika msafara huu wa pili walihama Waislamu 83. Kiongozi wa msafara alikuwa Ja'far bin Abu Talib. 'Uthman safari hii alibakia Makkah. Msafara huu uliondoka kimya - kimya bila ya makafiri wa Kiquraysh kupata habari. Walipopata habari waliwafuata ili wawarudishe lakini hawakufanikiwa. Ndipo wakaamua watume ujumbe wa watu wawili ukiongizwa na Amr bin Al-As na wenzake 'Abdullah bin Abi Rabi'ah, kwa Mfalme Negus ili kumuomba asiwaruhusu Waislamu kukaa katika nchi yake na badala yake awaruhusu hao wajumbe wawachukue Waislamu na kurejea nao Makkah kwa shutuma kuwa wamegawanya watu kutokana na dini mpya wanayoifuata ilivyo kinyume na dini ya wazee wao na dini ya Kikristo anayoifuata mfalme.
Walimhadharisha wafalme ouvu miungu yao na mwaka unaofuatia tuabudu pamoja nao mungu wetu" au tumeafikiana nao kuwa tutafuata tu zile sharia za Allah ambazo haziiingiliani na sharia zao. Ni hivyo kwa sababu, haikugtokea katika historia mzima ya Uislamu kuanzia kwa Mtume Adamu (a.s.) mpaka kwa Mtume Muhammad (s.a.w.), makafiri na washirikina na wakaendesha mambo yao pamoja pasi na mgongano. Mgongano utaachaje kutokana na hali makafiri na washirikina wanachukia Uislamu mwisho wa kupindukia na daima wako mbioni kuuzuia Uislamu usisimame Waislamu wa kweli daima watakuwa wenye kupambana na makafiri na washirikina na ushindi utakuwa ni wao kwa Ahadi ya Allah (s.w.):
"Wanataka kuzima nuru ya Allah (nuru ya Uislamu) kwa vinywa vyao Mwenyezi Mungu atakamilisha nuru yake ijapokuwa makafiri watachukia. Yeye (Allah) ndiye aliyemtuma Mtume wake kwa uwongofu na kwa dini ya haki ili kuifanya ishinde dini zote ijapokuwa washirikina watachukia. (61:8-9).
Kwa kuwa ni lazima makafiri na washirikina wachukie Uislamu utakaposimama, Waislamu hawana namna ya kusimamisha ujumbe wa Uislamu katika jamii pasina kupambana nao. Wale wanaodhania kuwa wanaweza kuwa Waislamu pasina kupambana na wanadhani kuwa wanaweza kuwa Waislamu pasina kupambana na maadui wa Uislamu au pasina kuwa tayari kuteswa kama walivyoteswa akina Bilal, Allah (s.w.) anawakatisha tamaa kuwa Uislamu huo hautambuliki mbele yake kwa hiyo hauna malipo kutoka kwake kama tunavyojifunza katika aya zifuatazo:
"Mnadhani kuwa mtaingiza peponi, na hali hamjajiwa na mfano wa (yale yaliyowajia) wale walipita kabla yenu?
Yaliwapata mashaka na madhara na wakatetemeshwa sana hata mitume na walioamini pamoja nao wakasema:"Nusura ya Mwenyezi Mungu itafika lini?" Jueni kuwa nusura ya Mwenyezi Mungu iko karibu. (2:214).
Je, mnadhani mtaingia peponi, hali Mwenyezi Mungu hajawapambanua wale waliopigania dini ya Mwenyezi Mungu miongoni mwenu na kuwapambanua waliofanya subira? (3:142).
Je, mnadhani kuwa mtaachwa na hali Mwenyezi Mungu hakuwabainisha wale waliopigania dini miongoni mwenu na wasiwafanye rafiki wa moyo isipokuwa Mwenyezi Mungu na Mtume wake na Waislamu? Na Mwenyezi Mungu anazo habari za yote mnayoyafanya." (9:16).
Mfalme Negus kwa uadilifu wake mkubwa hakutosheka kusikiliza upande ule wa shutuma tu bali alitaka Waislamu nao wajieleze na akawauliza: "Dini yenu hii ni dini gani ambayo imewagawanya watu wenu na ambapo hamjajiunga na dini yangu au dini yoyote ile inayojulikana? Alijibu Jaffar (r.a.) kwa niaba ya Waislamu wenzake:
"Ewe mfalme, sisi tulikuwa waovu na majahili, tulikuwa tukiabudu masanamu na kula nyamafu hata mizoga ya wanyama waliokufa wenyewe. Tulifanya kila aina ya matendo machafu na ya aibu na hatukuwa waadilifu. Wenye nguvu miongoni mwetuwaliwakandamiza wanyonge. Kisha Allah akamleta Mtume miongoni mwetu ambaye tulimfahamu vema kwa nasabu yake, utukufu wake na uzuri wa tabia yake tukufu. Alituita tumuabudu Mungu mmoja tu na akatukataza kuabudu masanamu na mawe. Alitufundisha kusema ukweli, kutunza amana, kuwaangalia ndugu na jamaa na kuwafanyia wema majirani zetu. Alituamirhsa kufanya mema na kuacha maovu, alituamrisha kusimamisha swala na kutoa zakat.Alituamrisha kujiepusha na maovu na kujiepusha na umwagaji damu. Alitukataza zinaa, kusema uwongo kula mali ya yatima na kuwasingizia uovu wanawake watahirifu. Alitufundisha Qur'ani. Tulipomuamini na kuishi kulinganana mafundisho yake mazuri, watu wetu walianza kutupiga na kututesa wakidhania kuwa tutaiacha dini yetu na kurudia ibada ya masanamu, na ukatili wao kwetu ulipokithiri ndipo tukaja kujihami katika nchi yako kwa ruhusa ya Mtume wetu (s.a.w.)
Kisha mfalme Negus alimtaka Ja'ffar (r.a.) asome kutoka katika Qur'an. Alisoma aya chache katika Suratul Mariam (sura ya 19) zinazoeleza juu ya kuzaliwa kwa muujiza kwa Nabii Issa (a.s.) Kisomo cha Qur'an kilimgusa sana mfalme pamoja na viongozi wa Wakristo waliomzunguka kiasi cha kutiririkwa machozi. Mfalme aliikiri, "Naapa kwa jina la Allah kuwa maneno haya na ya yale ya Biblia ni mionzi ya mwanga inayotoka katika chanzo kimoja' aliufahamisha ujumbe wa Maquraysh kuwa kwa vyovyote iwavyo hawezi kuwatoa Waislamu na kwa upande mwingine aliwaambia Waislamu waishi kwa salama katika nchi yake. Wengi wa Waislamu waliishi mle mpaka mtume na Waislamu walipohamia Madinah.
Wengine walibakia mle mpaka 7 A.H. Mtume (s.a.w.) alipowaamuru wamfuate Madina.
Mafunzo yatokanayo na Hijira tutayapata katika kipengele cha Hijira au Madina. Ama funzo lingine kubwa tunalolipata katika kipengele hiki ni lile linalotokana na uongozi wa Ja'ffar (r.a.). Ja'ffar aliweza kuutetea Uislamu dhidi ya shutuma za makafiri na kuweza kumvuta mfalme muadilifu kuwa pamoja na Waislamu. Hii inatupa fundisho kuwa kila Muislamu wa wakweli hanabudi kuufahamu vema ujumbe wa Uislamu utokanao na Qur,an na sunnah ili aweze kuufikisha kwa watu vilivyo na ili aweze kuutetea ipasavyo.
Mbinu za kuwatenga
Makafiri wa Kiquraish baada ya kushindwa kuuzuia Uislamu kwa kila njia waliyoijaribu waliona kuwa hatua ya mwisho ilikuwa ni kumwuwa Mtume (s.a.w.) ili kung'oa kabisa mzizi wa fitina lakini pia walikuwa wakiwachelea jamaa zake, Banu Hashim. Hata hivyo katika mwaka wa 7 B.U. (Baada ya ya Utume) wakuu wa Makkah waliona wamwite Abu Talib wampe rai yao ya mwisho. Abu Talib aliitikia mwito na aliwaambia Banu Hashim nao waje kusikia rai hiyo. Wakuu hao walikuja na kiongozi wa Maquraysh Umarah bin Walid bin Mughira, aliyekuwa mshairi hodari mno kuliko Maquraysh wote. Wakamwambia Abu Talib "Umchukue huyu umfanye mwanao badala ya Muhammad, na sisi utupe Muhammad tumuulie mbali, tupumzike sisi na wewe pia "Abu Talib alikataa katakata rai ile na akaungwa mkono na Bani Hashim wote isipokuwa Abu Lahab. Banu Mutalib pia walijiunga na Banu Hashim katika kukataa rai ile. Makafiri wa Kiquraish walichukia kwa kukataliwa rai ile. Makafiri wa Kiquraysh walichukia sana na pale pale wakaandika mkataba wa kuwatenga (kuwasusia) Banu Hashim, Banu Muttalib na Waislamu wote. Mkataba uliwakataza Maquraysh kwamba hapona ruhusa kufanya matano yafuatayo:
(1). Kusema na Banu Hashim yoyote wala Banu Muttalib akiwa Muislamu au si Muislamu.
(2). Kuwauzia chochote wala kununua kitu kwao.
(3). Kuoana nao
(4). Kuwasaidia kwa njia yoyote ile.
(5). Kukaa pamoja nao.
Mkataba huu uliandikwa na Mansur bin Ikrimah na kutiwa sani na wakuu wote wa Makkah. Kisha mkataba huu ulibandikwa ukutani ndani ya Ka'bah. Baada ya mkataba Abu Talib alipendekeza kuwa Banu Hashim, Banu Muttalib na Waislamu watoke pamoja na wake zao na watoto zao wahamie nje ya mji wa Makkah katika bonde moja lililoitwa baada ya kuhamia kwao, Sib Abu Talib yaani makazi ya Abu Talib. Walikaa katika bonde hilo kwa muda wa miaka mitatu. Katika kipindi hicho walipata taabu sana ya njaa hadi kufikia kula majani ya porini. Maquraysh waliweka ulinzi mkali wa kuzuia wasiuziwe chochote. Baadhi ya wakuu wa Makkah Zuhayr bin Abi Umayyah Hisham bin Amr bin Harith, Mut'im bin Adiy bin Naufal, Abul Bakhatari bin Harith Al-Asady na Zania bin Al-Aswad ala-Asad - walipatwa na huruma na kulazimisha mkataba ule uvunjwe baada ya miaka mitatu. Walipoingia ndani ya Ka'bah ili kuubandua ule mkataba walikuta maneno yote ya mkataba yameshaliwa na mchwa na likabakia jina la Allah tu. Huu ulikuwa ni muujiza wa aina yake, lakini bado wakuu wa Maquraysh hawakuwa tayari kuamini.
Kuwatenga Waislamu na jamaa zao wa Banu Hahim na Banu Muttalib, ni mbinu nyingine ya makafiri wa Makkah waliyoibuni ili kuizima NURU ya Uislamu. Lakini hata hii haikufanikiwa.
|
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook |