Wapiganaji wa Kiislamu wakomboa mji wa Kurcheloy - Chechnya

CHECHNYA

WAPIGANAJI shupavu wa Kiislamu nchini Chechnya Jumatano ya wiki iliyopita (Juni 29, 2000) walifanikiwa kuving'oa vikosi vya Russia vilivyokuwa vimejichimbia katika mji wa Kurcheloy kusini ya Chechnya.

Vikosi hivyo ambavyo vimetajwa kuwa ni vya kutegemewa sana katika jeshi la Russia, kufuatia kunyukwa na Wachechen, vilikimbilia msitu ulio katika kijiji cha Marzomokh.

Wapiganaji wa Chechnya wameripotiwa kuvishambulia vikosi hivyo kwa siku mbili mfululizo kabla ya kuvisukuma nje ya mji huo.

Duru za wapiganaji hao zimethibitisha kuua askari 15 na kujeruhi 20 wa kikosi hicho hatari cha majeshi ya Russia katika shambulio la mwanzo.

"Walijaribu kuondoka kwa kujisinga nyasi wasionekane. 16 walikamatwa, wengine wanne walifanikiwa kuwaponyoka Mujahidiin", duru za Wachechen zimefahamisha.

Wakati mapambano yakiendelea Wachechen walifanikiwa kuingilia mtandao wa mawasiliano kati ya vikosi hivyo na Kamanda Mkuu wa jeshi la anga la Russia.

Serikali ya Russia imekiri kupoteza zaidi ya askari 30 katika mapigano na wengine kadhaa kujeruhiwa.

Kufuatia kipigo hicho, jeshi la Russia lilifanya mashambulizi ya anga eneo hilo lililodhibitiwa na Mujahidiin.

Katika mashambulizi hayo wapiganaji watano wa Chechnya waliuawa.

Majina ya mashahidi hao yametajwa kuwa ni pamoja na Abu Malik (raia wa Yemen), Abu Said Ash-Shimah na Abu Asim al Jiddawi (kutoka nchi moja ya Kiarabu) na Mchechen mmoja.

Muda mfupi kabla ya mashambulizi hayo ya anga ya Russia, Mujahidiin walifaulu kuangamiza magari matatu ya jeshi la Russia katika eneo hilo hilo la Kurcheloy.

Msemaji wa wapiganaji hao wa Kiislamu amesema operesheni hiyo ya Kurcheloy dhidi ya majeshi ya Russia yakisaidiwa na mawakala wao ni kampeni kamambe iliyoanzishwa na Wachechen kuyafukuza majeshi hayo kutoka Chechnya.

"Operesheni ya Kurcheloy imekata kauli zilizotolewa na kamanda wa majeshi ya Russia, Gennady Trushev na mnafiki Mufti Ahmad Qadirov kwamba vita Chechnya imekwisha na Russia ndiye mshindi", amesema msemaji huyo.

Wakati huo huo, vikosi vya wapiganaji wa Chechnya wiki iliyopita viliyashambulia majeshi ya Russia yaliyojichimbia mji mkuu wa nchi hiyo Grozny.

Katika eneo la viwanda la Zavodsky wapiganaji hao waliharibu ghala la silaha na kuua askari wawili wa Russia.

Katikati ya Grozny, Mujahidiin wakitumia maroketi na bunduki za rashasha (machine gun) walikishambulia kituo kimoja hata hivyo hazikupatikana taarifa za vifo wala majeruhi.

Katika eneo jingine la mji huo, mpiganaji mmoja wa Chechnya alifanikiwa kupenya na kulipua gari la kijeshi kwa kutumia kombora la RPG.

Askari watatu waliokuwemo ndani ya gari hilo waliuawa.

Wapiganaji wa Chechnya vile vile walishambulia eneo la viwanda vya vifaa vya eletroniki katika jiji la Grozny.

Askari wanane wa Russia waliuawa katika mashambulio hayo.

Taarifa kutoka Chechnya zimethibitisha kuenea kwa mapigano sehemu mbalimbali za nchi hiyo kati ya Wachechen na wavamizi wa Russia.

Miji ya Zhalka jirani na Argun, Masker Yurt, Zeken Yurt na Alkhan Yart ambako majeshi ya Russia yamepiga kambi, imeripotiwa kushambuliwa na wapiganaji wa Chechnya.
--
JuuRUDI


Bonyeza hapa
kushriki mjadala au kutoa maoni juu ya habari hizi na masuala mengineyo ya Kiislamu kwenye Baraza ya Wasomaji

   Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu: Bonyeza hapa
Au
Andika barua  kwa: webmaster@islamtz.org


An-nuur Home | Ukurasa wa Mwanzo | Islam Tanzania
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook