Sara Dumba uana habari gani huo ?
Ndugu Mhariri
MIMI kitaaluma ni mwalimu, ninafundisha shule moja ya sekondari Jijini.
Naelewa kitaaluma ni mwiko wanataaluma moja kufedheheshana. Kwa mfano, mimi siwezi kuingia darasani nikaanza kumshambulia au kueleza udhaifu wa mwalimu mwenzangu kwa wanafunzi, kwa sababu kufanya hivyo ni kinyume na taaluma. Kama kuna dosari zipo njia za kurekebishana sisi wenyewe.
Pamoja na hivyo, mwiko huo huvunjika pale inapoonekana upotoshaji au uharibifu wa makusudi unafanyika.
Nadhani hata ninyi wana habari, taaluma yenu ina maadili kama hayo, ndio maana sijasoma hata gazeti moja, radio au TV ikishambulia nyingine kwa wazi au kukitaja chombo husika.
Hata hivyo, nimelazimika kuandika barua hii na naomba Mhariri uitoe kufuatia upungufu wa kihabari uliojitokeza katika taarifa ya mwakilishi wa RTD kanda ya mashariki katika kipindi cha majira iliyohusu mgogoro wa mirathi morogoro.
Katika kipindi hicho mwakilishi huyo bibi Sara Dumba aliyeko Morogoro aliripoti mgogoro wa mirathi unaoendelea mjini humo baina ya familia ya marehemu Mohamed Mbegu na mtoto wa kuapanga(Yatima) bi Zawadi aliyekuwa akilelewa na mzee huyo katika familia hiyo.
Bibi Sara Dumba kwa jinsi alivyoonekena kushabikia upande mmoja alionekana kusahau hata maadili ya kazi yake.
Taarifa aliyoitoa juu ya mzozo huo haikuwa kamilifu na alionekana wazi kutoa maelezo ya upande mmoja akiunga mkono hukumu ya mahakama na kilichoendelea baada ya hukumu hiyo.
Mimi nadhani kitaaluma alipaswa kupata maelezo ya pande zote mbili kabla ya kuirusha hewani taarifa yake. Kwa kufanya hivyo angewasaidia wasikiliza kuelewa kiini cha mgogoro na usahihi wa hiyo hukumu ya mahakama.
Kwa jinsi alivyoliripoti suala hilo ametuacha wasikilizaji tukiwa na maswali mengi hasa tulio waumini wa dini ya kiislamu.
Nadhani hata mwanahabari mwenziwe bwana Swedi Mwinyi aliyekuwa akiwasiliana naye hakuweza kulielewa sawa sawa suala hilo.
Kwa ufahamu wangu ulionifanya nichanganyikiwe na taarifa ya bibi Sara, mirathi ya Waislamu hairuhusu mtu asiye wa nasaba husika kurithi mali ya marehemu hata kama utakuwepo wasia unaoelekeza hivyo ulioachwa na marehemu, nadhani sababu hii ndiyo iliyowasukuma watoto wa marehemu Mbegu kupinga hukumu ya mahakama.
Inavyofahamika katika mirathi ya Waislamu hata kama Marehemu atakuwa na mapenzi ya namna gani na mtu asiye wa nasaba naye kidamu, hana ruksa ya kumshirikisha katika mirathi.
Bali atakachofanya ni kuandika wasia kuwaomba warithi wake wamkumbuke mtu huyo katika mgawanyo wa mirathi. Wasia kwa mujibu wa sheria ya kiislamu hauzidi theluthi moja(1/3).
Kwa hiyo hukumu ya mahakama kama ilivyoripotiwa na bibi Sara Dumba kwa mujibu wa sheria ya kiislamu ni BATILI na inayotakiwa itupiliwe mbali.
Kwa sababu katika sheria ya kiislamu marehemu hana ruhusu wala uwezo wa kumrithisha mali yake mtu asiye na nasaba naye kidamu.
Katika sheria hiyo marehemu kama hana ndugu wa kumrithi mali inakuwa wakfu kwa Uislamu na Waislamu.
Kwa hiyo nawaomba ninyi waandishi wa habari mnaotangaza na kuandika habari muwe
makini na mzingatie athari ya hayo mnayorusha hewani kwa ajili ya jamii.
Mwisho namuomba bibi Sara Dumba afuatilie tena taarifa hiyo, ili aweze kuitoa kama inavyopasa na atuache wasikilizaji tuchambue wenyewe.
Vyovyote itakavyokuwa, hata kama hao watoto husika walikuwa hawana mapenzi au mahusiano mazuri na marehemu bado haki ya mirathi inabaki kwao labda wawe wameritadi(wametoka Uislamu). Na kama ni hivyo mali hiyo bado haitakuwa ya huyo bibi
Zawadi, itakuwa wakfu kwa Waislamu na Uislamu. Bi Zawadi atazingatiwa katika Wakfu huo kwa namna wasia ulivyopendekeza.
Ndugu Mhariri
NINA wasiwasi na mabadiliko katika sheria ya uchaguzi yaliyofanywa hivi karibuni.
Mabadiliko hayo yanafanya kufungwa sanduku la kura kwa kufuli isiwe lazima na pili msimamizi awe na uhuru wa kuamua pa kuhesabia kura.
Vyovyote itakavyokuwa mabadiliko hayo hayana nia njema.
Kwanini sanduku lisiwe na kufuli? Kama ni lakiri hiyo yaweza kuyeyushwa ikawekwa nyingine. Na kwanini wananchi wanyimwe fursa ya kuhesabu kura zao pale walipopigia?
Nini dhamira ya mabadiliko haya? Wanachi kuweni macho.
Malik Abeid,
Moshi.
Mwalimu Said Ali
D'Salaam.
|
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook |