Bunge lote lasinzia
Raia wa Tanzania, Bara visiwani pia,
Hivi kweli mnajua, kuwa bunge lasinzia,
Posho wanajichotea, na ‘mishangingi’ sawia,
Bunge lote lasinzia, ndoto ni posho na gari.
Aibu inatokea, picha zinapotwaliwa,
Wabunge wa Tanzania, bungeni wanasinzia,
Wageni wanadhania, ni utani si sheria,
Bunge lote lasinzia, ndoto ni posho na gari.
Spika kawaambia, ruksa kujilalia,
Ila amewausia, mkoromo kuto-toa,
Walale kwa kusinzia, na ute kujitolea,
Bunge lote lasinzia, ndoto ni posho na gari.
Chaguzi imewajia, wa Tanzania raia,
Mbio watawajilia, kura mtawapigia,
Wabunge tawaambia, mema tutawatendea,
Bunge lote lasinzia, ndoto ni posho na gari.
Muswada ukijilia, kwa kura kupitishia,
Kwa wingi wamezidia, wapinzani wanalia,
Vijembe tawapigia, na kedi tawafanyia,
Bunge lote lasinzia, ndoto ni posho na gari.
Vema mkijiandaa, kura kuzikazania,
Kuchagua wanofaa, wenye na haki sawia,
Bunge - enda likafaa, miswada kujadilia,
Bunge lote lasinzia, ndoto ni posho na gari.
Beti nane natulia, nazidi sisitizia,
Haki kuikazania, viongozi kuchagua,
Bungeni wende kukaa, macho-pasi kusinzia,
Bunge lote lasinzia, ndoto ni posho na gari.
Bakari K.M.,
Morogoro.
Kila kitu duniani, kinapo mahala pake,
Kama hakikosekani, hunoga utamu wake,
Watu huwa furahani, hawatamani kitoke,
Huwa na kubwa thamani, isiyo mfano wake.
Somo liweze kufana, na pia lisomesheke,
Lazima kupatikana, alie mjuzi wake,
Ndipo hapo utaona, mazuri matunda yake,
Tena yaliyo mwanan, bayana kipimo chake.
Operesheni kutimu, hadi ikafanikiwa,
Lazima mataalamu, daktari maridhawa,
Bingwa aliehitimu, ndiye mkasi tapewa,
Taweza kustakimu, na mgonjwa akapowa.
Na gari ili liende, salama barabarani,
Abiria walipande, kwa vile waliamini,
Ni lile liso na mbinde, lenye dereva makini,
Mjuzi mlimbwende, kazi anoithamini.
Na chakula kivutie, kiite apetaiti,
Kwanza budi kinukie, harufu njema si shoti,
Na viungo vikolee, mazuri mahanjumati,
Mpishi abobeae, ndiye ataethibiti,
Kila kitu kwa ujuzi, ndipo tutendeka vyema,
Kwa anothamini, kwa ari anojituma,
Akifanya kwa mapenzi, taleta tijara njema,
Na watu kimpa enzi, atazijaza neema.
Tanzania nchi yetu, bado inasaga lami,
Imemaliza viatu, safari haisimami,
Kila siku ni papatu, kwa tatizo la uchumi,
Mebaki haina kitu, haiwezi kujihami.
Mjuzi ametokea, uchumi anauweza,
Fani ameizoea, aona kama kucheza,
Ataka tusaidia, tatizo kulimaliza,
Huruma atuonea, mambo yanatutatiza,
Kwanini simchague, safari ifike mwisho?
Mzigo situlemee, tumeshapata fundisho,
Mkanda tuufungue, watutia huzunisho,
Maisha tufurahie, tufaidi stawisho.
Tushajifunga yatosha, hakuna kujivunia,
Lazima kubadilisha, tusije kuangamia,
Hali zetu zimeisha, wao matumbo yakua,
Wanajistarehesha, sisi tumenyong’nyea.
Sihaba,
Dar es Salaam.
|
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook |