RIWAYA

Joka la Mdimu - 8

SEGA

IDADI kubwa ya wakazi wa Sega walikuwa Islamu. Mwezi mtukufu wa Ramadhani ulitarajiwa kuandama juma moja baadaye na dalili za maandalizi ya kufunga zikaonekana. Mazungumzo yalionesha hofu ya kupata mchele wa daku kwani Ramadhani ya mwaka uliopita wafungaji walikula ugali wa mahindi ya njano badala ya mchele kama ambavyo walizowea.

Tino alikuwa Islamu ambaye alithamini sana kufunga sababu hiyo ndiyo nguzo pekee ya dini yake aliyoweza kuitekeleza vyema. Ila yeye, hakusumbuliwa na fikra za mchele wa daku maana angenunua wa kulanguliwa kama alivyokuwa akifanya. Badala yake mawazo yake yalikuwa katika fainali kugombea ubingwa wa daraja la pili baina ya timu yake ya Sega Warriors na City Devils iliyokuwa ichezwe Jumamosi iliyofuatia katika uwanja maarufu wa Wembley pale pale Sega. Fikra hizo zilitosha kumtikisa moyo wake maana katika michezo yote miwili iliyopita baina yao walichapwa bao mbili kwa moja na baadaye moja kwa bila. City Devils kama jina lenyewe, ilitia hofu miongoni mwa timu zote za daraja la pili jijini Mindule.

Mazoezi makali yalifanywa asubuhi na jioni kama maandalizi ya fainali hiyo. Saa kumi kila jioni Tino alivaa bukta na fulana yake ya mazoezi akachukua viatu vya mpira hadi katika klabu yao. Kutoka hapo waliandamana na wenzake hadi uwanja wa mazoezi. Baada ya kuvaa viatu vyao waliamua kufanya mazoezi na mwalimu maalum. Waliruka kichura, kukimbia na mpira, kupiga danadana na kadhalika. Haja ilikuwa ni kuongeza pumzi, nguvu za mwili na kumiliki mpira vizuri pamoja na kufunga magoli hasa kupiga mipira ya adhabu, jambo ambalo liliwanyima ushindi mara zote walipokutana na City Devils.

Na kila saa kumi na moja wachezaji wote walikwenda moja kwa moja wakakutana kiwanjani ambako walikimbia kwa muda mrefu. Baadaye waligawana timu mbili na kucheza kwa kasi mno.

Mazoezi ya safari hii yalikuwa tofauti na mengi ambayo Tino alipata kuyafanya. Wanachama na washambiki wengi walihudhuria jioni na hata asubuhi kuwapa moyo.

"Shetani lazima wauawe safari hii", alipania shabiki mmoja ambaye hakukosa kuhudhuria mazoezi yote kila siku.

Kwa Tino, mazoezi haya yalikuwa na upekee maana umri wake ulisonga na hii ilikuwa ndiyo mechi yake muhimu ya mwisho kabla "hajaning'iniza viatu". Sega nzima mazungumzo yalihusu mechi hiyo. Na uongo uongo mwisho ukawa kweli.

Jumamosi ya mechi hakukuwa na mazoezi asubuhi lakini wachezaji wote walitakiwa kukutana klabuni saa mbili kamili kijumba kidogo ambacho kilikuwa ndiyo klabu ya Sega Warriors kilianza kujaa wachezaji. Waliingia mmoja mmoja, wawili wawili, watatu watatu. Hivyo hivyo hadi kufikia saa mbili na nusu nafasi haikutosha. Baadhi yao wakasimama nje. Hakuna aliyehisi kuketi. Walisalimiana kwa usuluba mkubwa na kuzungumzia mechi hiyo tu. Tino alizungumza pole pole mara moja moja na wachezaji wenzake. Ile hofu ya mbali bado ilikuwa imemtawala. Lakini haikuwa mara yake ya kwanza. Hali hiyo ilimpata kabla ya mechi zote kubwa, lakini ilitoweka mara tu alipougusa mpira baada ya kuanza.

Mzee mmoja wa makamu alipiga kofi ndani ya kile kijumba. Wale mashabiki waliokuwa nje walisogea na kujipenyenza ndani na waliokosa nafasi wakachuchumaa kuchungulia ndani, na walioshindwa kufanya hivyo wakatega viganja masikioni kusikiliza.

"Sega oyee," aliita.

"Oyee!", kibanda kilitetema mara tatu kabla hajaendelea.

"Kazi yetu nini?"

"Shinda! Shinda! Shinda!" kibanda kikatetema tena. Yule mzee alipeleka kichwa mbele, akatabasamu na kutazama huku na kule. Alipunga mkono wake kwa ridhaa. Akaendelea, "Tunataka wachezaji wetu wawe askari halisi, leo chezeni kufa na kupona. Tunataka mpira wa ufundi, wa kazi hapana kupiga viatu. Tunataka nini? aliuliza tena.

"Lindanda", wanachama walirindima.

"Naam! Lakini ngoma chini", alisema huku akiinama na kutandaza viganja vyake chini chini na kusimama ghafla akitazama juu na kusisitiza "Hapana kupiga minazi".

"Daima kumbukeni, mpira ni spoti! Sio vita", alikazia macho pale aliposimama Tino na wachezaji wenzake ambao walitikisa vichwa.

"na kwetu sisi wanachama lazima kufika uwanjani mapema kwa wingi. Hapana kubaki mtu nyumbani. Kikosi cha ngoma Sega kipo?"

"Tupo!" sauti ziliitikia kutoka nje.

Akaanza kuimbisha, "Sega! Sega! Sega, usiogope!" huku akipiga kofi.

"Segaaa, Sega! washabiki wote wakaitikia.

"Hakuna kupumzika. Ngoma mtindo mmoja, akasisitiza.

Akageukia upande mwingine na kuendelea "Na kumbukeni neno kuu la kushangilia ! Nini?"

"Funga, shinda! Funga, shinda! Funga, shinda!" sauti za mashabiki zikarindima tena.

Sina zaidi", akamalizia.

Robo saa tu kupita watu wote walitoka isipokuwa wachezaji na viongozi wa timu. Kulikuwa na maelekezo ya mwisho ya namna ya kufanya na kutiana moyo.

Mwisho kabisa alibakia yule kiongozi na mzee mwingine mmoja wakizungumza taratibu kisha wakatoka hadi kwa mganga, maarufu kwa jina la mtaalamu. Walipofika, walivua viatu mlangoni na kuingia ndani. Walikaribishwa na mtaalamu, mtu mzima, kavaa fulana na kikoi. "Ndiyo mmefuatia ile shughuli yenu?" akauliza.

"Naam", aliitikia yule kiongozi.

Mganga aliinuka na kwenda kwenye sehemu ya kando ya chumba chake kilichojaa vitabu na tunguri. Alichomoa kitabu kimoja kikuu kuu akakipulizia kama kufuta vumbi. Alirejea kuketi pale chini kwenye mkeka kama walivyoketi wale wageni wake. Alikifungua kile kitabu kwa makini. Alichukua miwani yake na kuipachika machoni juu ya pua. Ndipo alipoinua macho makavu kuwatazama wale viongozi wa Sega Warriors akasema bila tabasamu, "Mchezo mgumu lakini msihofu. Shika hii!" Alitoa kitu kutoka kwenye koti na kumkabidhi yule kiongozi ambaye alivipokea kwa makini na hofu kiasi. Kisha wote wakatazamana kwa macho baridi mithili ya jogoo wanaotangaza vita.

"Nimekueleza miiko yake", yule mganga alikumbusha.

"Labda kuna mengine zaidi".

"Ni ile ile! Lakini muhimu mno. Moja avae golikipa na nyingine avae mchezaji unayemwamini kwa ustadi na usafi". Kimya kidogo kilipita, na yule mganga akasisitiza. "Hala hala usafi! Atadhurika mtu bure! Maneno yale yalimtia hofu yule mzee. Waama alikwisha waeleza wachezaji wote wasinywe pombe, kuvuta bangi wala kujamialiana na wanawake kwa siku tatu nzima kabla ya mechi. Lakini vipi angehakikisha utii wa amri hiyo!

"Vijana wa siku hizi wakorofi mtaalamu. Nimewaeleza wote. Basi sijui tena!" Kauli hiyo haikumridhisha kabisa mtaalamu akatikisa kichwa huku na kule akasema, "Labda labda, ndiyo huleta maafa".

"Tuombe Mungu", alisema mwenzake yule kiongozi. Mganga alimtupia jicho akatabasamu kidogo na kusema "Mungu ndiyo tumeshamuomba". Akaagana nao. Akatoka na mchanganyiko wa hofu na furaha.

Uwanja wa Wembley ulikuwa katikati ya Sega. Kutokana na michezo mingi iliyofanyika hapo ulikuwa na majani machache na sehemu kubwa ilikuwa mchanga mtupu. Karibu na hapo palikuwa na shule ya msingi na magenge ya wafanyabiashara na maduka ya nyama ya ng'ombe na samaki wakavu na wabichi. Miembe miwili mikubwa iliota kila upande wa kiwanja hicho.

Saa kumi kamili kukizunguka kiwanja chote kilijaa unasi, wake kwa waume, wazee kwa vijana. Lakini timu zilikuwa bado kufika isipokuwa washabiki wa City Devils walikwishawasili. City Devils ilisifika kwa kucheza kwa nguvu na mashabiki wao walikuwa washari. Hii leo kikosi kamili cha mashabiki hao kilishawasili na kusimama upande wa kulia wa uwanja huo wakipunga bendera yao ya njano na weupe. Walikuja na mbwa na ngedere. Walikaa kimya kusubiri timu yao ambayo iliwasili punde na basi ndogo aina ya Isuzu Journey. Kelele za hoi hoi za washabiki ziliongezeka. Ngedere na mbwa walibweka na kuwatishia watu wengine kuwasogelea. Muda huo huo walianza kupiga manyanga na kuimba "Shetani! oyee! Shetani oyee!" Shetani chinja" kwa muda wote kukasikika. "Chinja Chinja!"

Katika klabu ya Sega Warriors wachezaji wote walianza kuvaa jezi zao. Zitto alivaa namba sita na Tino nambari tisa. Kwa siri kabisa yule kiongozi wao alimwita golikipa na Tino na kuwakabidhi vile vitu walivyopewa na mganga kila mmoja chake.

"Vaeni hizi!" aliwaeleza na amri ikafuatwa. Teksi ya Amani, aliyefunga kitambaa chekundu kichwani na kuvaa joho jekundu liliandikwa Sega, na nyingine tatu ziliwachukua baadhi ya wachezaji maarufu.

Baada ya nusu saa, ngoma ya Sega ikiwa mbele yao Sega Warriors waliingia katika uwanja wa Wembley huku mashabiki wao wakipiga kelele mno. Haja yao kubwa ilikuwa ni kulipiza kisasi cha kufungwa mara mbili na City Devils kuliko hata ule ushindi wenyewe wa kombe la Daraja la Pili. Na tumaini lao liliongezwa na kuchezea katika uwanja wa nyumbani.

"Funga! Funga! funga! shinda!", ikatangaa kote.

Mchanganyiko wa kelele za mashabiki wa timu zote mbili ulikifanya kiwanja kipambe moto, vumbi likatimka huku na kule.

Hatimaye kote kulikuwa kimya. Halafu ghafla tena, mzee mmoja mrefu mweusi ana mapengo mengi akaguta, "Mioto na mioto nakwisha kutana! Taungua nani"?

"Shetani!" Sauti moja ilijibu kwa mbali, kisha kukafuatia, "Chinja, chinja", kutokea upande wa City Devils.

"Acheni kelele shetani nyiye!" ilipaa sauti ya shabiki mmoja wa Sega Warriors.

Filimbi kali ya mwamuzi ilikata fujo yote na ghafla kote kukawa kimya. Mashabiki waliokuwa wakirukaruka katikati ya uwanja walitoka kukaa pembeni tayari kuangalia pambano hilo. Muda huohuo City Devils waliingia uwanjani kwa mashamu shamu yote, na 'minjonjo' ya kila aina huku wakisindikizwa na ngedere na mbwa. Manyanga yalivuma na kuchanganyika na mibweko ya mbwa na hoi hoi za mashabiki.

Punde si punde Sega Warriors nao wakiwa wamevalia jezi nyekundu tupu walijitoma uwanjani kwa madaha wakisindikizwa na ngoma ya Sega na nyimbo maarufu, "Sega Sega! Segaa Segaa! Sega usiogope!"

Firimbi kulia tu, mpira ulianza kwa kasi na timu zikacheza kwa nguvu. Nje ngoma ziliendelea kulia, kelele kusikika, manyanga kuvuma. Vyote vikazifanya timu kushambuliana zaidi na zaidi.

Itaendelea Ijumaa
--
JuuRUDI


Bonyeza hapa
kushriki mjadala au kutoa maoni juu ya habari hizi na masuala mengineyo ya Kiislamu kwenye Baraza ya Wasomaji

   Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu: Bonyeza hapa
Au
Andika barua  kwa: webmaster@islamtz.org


An-nuur Home | Ukurasa wa Mwanzo | Islam Tanzania
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook