Mrema adai angependekezwa yeye kuwania Urais

MGOMBEA Urais kupitia Chama cha TLP, Bw. Augustine Lyatonga Mrema amemshutumu Prof. Ibrahim Lipumba kwa kile alichodai kuwa ni yeye mwenye sifa za kugombea Urais Lipumba hakustahili kugombea.

Bw. Mrema alikuwa akihutubia wakazi wa Manispaa ya Tanga katika mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye uwanja wa Tangamano mwishoni mwa wiki iliyopita.

Alisema, katika muungano huo wa vyama vya upinzani yeye Mrema ndiye aliyekuwa akistahili asimamishwe kugombea Urais kwa vile anakubalika zaidi na wananchi kuliko Prof. Lipumba.

Alisema, aliukacha muungano huo baada ya kuona Prof. Lipumba ndiye atakayegombea Urais katika muungano wao.

Katika mkutano huo ambao chama cha CUF kilialikwa, Mrema alitumia vigezo vya kura ya maoni kwenye magazeti na uchaguzi uliopita kuonesha kuwa yeye anakubalika zaidi kuliko Prof. Lipumba.

Akifafanua alisema, katika kura ya maoni iliyoendeshwa na gazeti moja mwezi Juni mwaka huu alimshinda Prof. Lipumba kwa asilimia kubwa na hata katika uchaguzi wa mwaka 1995 alipata kura milioni moja na laki nane wakati Prof. alipata kura laki nne tu.

Katika mkutano huo ambao ulijaa wafuasi wengi wa CUF, Mrema aliwashangaza watu kwa kutumia muda mwingi kumshutumu Prof. Lipumba na kuwataka wana CUF wamchague mtu anayekubalika na watu wengi.

"Lipumba alipokwenda Arusha na Moshi hakupata watu, lakini mimi lipokwenda Tabora mahali alikozaliwa Lipumba mkutano wangu ulijaa watu", Mrema alijitapa.

Aliongeza kuwa kigezo kuwa Prof. Lipumba anamzidi kwa elimu hakina maana hata CCM walimpitisha Karume mwenye elimu ya kidato cha sita na kumuacha Bilal mwenye PhD.

Watu wengi walianza kuondoka mapema kwenye mkutano huo baada ya kuona Mrema anaelekeza shutuma kwa wapinzani wenzie badala ya kueleza sera za chama chake au kukosoa uongozi wa chama tawala.

"Hivi mgomvi wa Mrema ni CCM au ni CUF?" alihoji mmoja wa wafuasi hao wakati akiondoka kwenye uwanja huo.

Hata hivyo, baadhi ya wafuasi hao walisikika wakiikejeli hotuba ya Mrema na kudai kuwa kushinda katika kura ya maoni iliyoendeshwa na magazeti hakumaanishi kukubalika na Watanzania walio wengi.

Vile vile walisikika wakidai kuwa katika uchaguzi wa mwaka 1995 Prof. Lipumba alikuwa hafahamiki zaidi kuliko ilivyo sasa ambapo Watanzania wengi wameshamtambua.

Wamesema, elimu hasa ya uchumi aliyonayo Prof. Lipumba ni kigezo muhimu cha kukubalika kwa wananchi kwa vile matatizo makubwa ya nchi yetu ni ya kiuchumi.

"Hatutaki Rais mwenye cheti cha propaganda na ushushushu", walidai watu hao bila ya kufafanua.


Wazee Mwanza watakiwa kuwaunga mkono vijana

WAZEE Waislamu wametakiwa kuwa bega kwa bega na vijana wao katika harakati za kuleta mageuzi nchini.

Wametakiwa wakumbuke walikotoka ambako historia inaonesha ni wao walisimama kidete wakawango'a wakoloni weupe walioitawala nchi hii.

Aidha wameaswa kuutupilia mbali woga ambao imeelezwa ni moja wa maadui wa haki.

Sheikh Rajab Cherehani alitoa nasaha hizo katika hafla ya uzawa wa mtume iliyofanyika katika msikiti wa Safina eneo la Nyakato mjini Mwanza.

Sheikh Rajab amesema kumuiga mtume ni kufuata nyayo zake katika kuiendea kila hatua ya maisha.

Amesema mtume alikuwa mwanasiasa mahiri aliyeweza kuwaongoza watu kupigania na kuchukua haki zao kutoka kwa madhalimu.

Kwa hiyo Sheikh huyo aliwaonya masheikh na maimamu wasiochanganya dini na siasa kuwa kwakufanya hivyo wanakuwa wamemkhalifu mtume(s.a.w).

"Waislamu ndio wanasiasa hasa kwa kuwa wana muongozo usiobadilika na unaosimamia uadilifu kwa wote", Sheikh Rajab aliuambia umati wa Waislamu uliofurika katika shughuli hiyo.

Akitoa mfano wa ushirikiano alioujenga marehemu Sheikh Al Amin Abdallah kati ya wazee na vijana mjini humo, alikemea tabia iliyozuka hivi karibuni ambapo vyombo vya dola huwatumia baadhi ya wazee wa kiislamu kujenga mazingira ya kukamatwa ovyo Waislamu, kuwekwa rumande na kufunguliwa mashitaka hewa.

Sheikh Cherehani alisisitiza kuwa ili nchi iweze kuwa na amani na utulivu wa kweli hapana budi kuwepo uongozi utakaotoa haki sawa kwa raia wote.

Alisema hilo ni jukumu la Waislamu kwa umoja wao kuwachagua na kuwaweka madarakani viongozi wasio na upendeleo wala chuki dhidi ya baadhi ya raia.

--
JuuRUDI


Bonyeza hapa
kushriki mjadala au kutoa maoni juu ya habari hizi na masuala mengineyo ya Kiislamu kwenye Baraza ya Wasomaji

   Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu: Bonyeza hapa
Au
Andika barua  kwa: webmaster@islamtz.org


An-nuur Home | Ukurasa wa Mwanzo | Islam Tanzania
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook