MTU mmoja ajulikanaye kwa jina la Alhaj
Swedi Mchombe amekufa mikononi mwa askari Magereza katika mazingira ya
kutatanisha.
Kibali cha mazishi No. 0826033 kutoka Hospitali ya Mawenzi kilichotolewa Julai 8, kimedai sababu za kifo ni kifua kikuu na ukimwi (TB na CD4).
Hata hivyo, maiti ya marehemu Swedi inaonyesha alipigwa sana kichwani na kunyongwa shingo.
Viongozi wa Msikiti wa Riadha wameeleza kuwa maiti ya Alhaj Swedi Mchombe ilikabidhiwa kwa Waislamu wa Msikiti wa Riadha Moshi Julai 14, ikiwa imetapakaa damu na majereha mengi kichwani.
Wamesema, askari Magereza walikabidhi maiti hiyo kwa Waislamu wakidai kuwa ndugu zake hawatambuliki.
Kabla ya kumkosha na kumkafini, Waislamu waliamua kumfunua maiti wampige picha ili watoe matangazo kwa matarajio ya kufikisha habari kwa wanaomfahamu.
"La haula, kumfunua maiti ametapakaa damu na majeraha mengi. Mishipa ya shingo imevunjwa. Ilibidi tumwekee jiwe ili kuzuia shingo isizunguke na ndipo tukampiga picha", ameeleza muumini mmoja aliyeshiriki kumuosha maiti.
Taarifa za uchunguzi wa gazeti hili zinaonesha kuwa, Alhaj Swedi Mchombe alikamatwa Mwanga mkoani hapo.
Baadaye alipelekwa Kituo Kikuu cha polisi Moshi, na kisha gereza la Karanga.
Julai 6, 2000 alipelekwa Mawenzi kwa matibabu na kufariki hospitali hapo Julai 8.
Uchunguzi zaidi umeonesha kuwa Julai 12, mwaka huu, askari kanzu wa kike aliyejitambulisha kwa jina moja na Marry alifika Msikiti wa Riadha na kumueleza Imam kuwa kuna Muislamu amefariki hana ndugu.
Magereza walitoa kibali cha kukabidhi maiti kwa Imam, Sheikh Athumani Uhenga Julai 13, mwaka huu.
Kabla ya mazishi Julai 14, Imam alionana na daktari Mawenzi na akaelezwa "ndugu yenu kafa kwa ukimwi na TB".
Uchunguzi zaidi wa gazeti hili umeonesha kuwa baada ya kukamatwa Alhaj Swedi alitoa maelezo binafsi polisi ikiwa ni pamoja na kuwataja ndugu zake na namba zao za simu.
Hata hivyo, juhudi za gazeti hili kuzipata hazikufanikiwa.
Inasemekana kuwa baada ya kifo chake askari walitaka azikwe haraka haraka na Manispaa. Hata hivyo baadhi ya Waislamu waliopo Manispaa na hospitali ya Mawenzi walipinga na kuhoji:
"Waislamu wote wasio na ndugu huwa wanazikwa na Waislamu wa Msikiti wa Riadha, inakuwaje huyu azikwe kibudu?"
Baadhi ya polisi waliohojiwa juu ya Alhaj Swedi walikiri kumfahamu na kudai kuwa ilishatolewa amri aachiwe kwani alikuwa hana kosa.
Hata hivyo, walipooneshwa picha ya marehemu walishtuka na kudai wasihusishwe kwa kauli yoyote ila aulizwe Mkuu wa Kituo au RCO.
Hadi tunakwenda mitamboni jana juhudi za kumpata yeyote kati yao hazikuweza kufanikiwa.
Habari zimeeleza kuwa Waislamu mjini Moshi wanaunda kamati kufungua Inquest ya kifo cha Alhaj Swed Mchombe huku wakiwaomba Waislamu kote nchini kushirikiana nao.
Aidha, wameomba iwapo yupo anayemfahamu marehemu afikishe habari kwa ndugu zake.
MZEE Suleiman Saleh Digaru ameeleza alivyoshambuliwa na polisi katika tukio la mzozo wa makaburi Manzese.
Amesema, alipigwa na kuumizwa hali iliyomfanya hadi leo ashindwe kufanya shughuli zake.
Akitoa maelezo nyumbani kwake maeneo ya Manzese Uzuri jana, Bw. Suleiman alisema; "Mimi nilikuwa napita njia, kilichoniponza ni kofia niliyokuwa nimevaa. Nilipigwa mpaka kuzirai", alisema Bw. Suleiman.
Alieleza kuwa alikuwa akielekea nyumbani kwake. "Nilisikia sauti kutoka kwa askari aliyevalia kiraia ikieleza kuwa hao wanaovaa kofia ndio wenyewe. Hapo nilipigwa rungu la kichwani na polisi mmoja", amesema.
Amesema kuwa baada ya hapo waliongezeka askari na kuwa watatu na kuanza kumshambulia.
Ameeleza kuwa polisi hao walimuacha hapo baada ya kuzirai mpaka alipopata fahamu na kujikongoja hadi nyumbani kwake na kupelekwa hospitali.
Bw. Suleiman aliyekuwa anaongea na gazeti hili jana anaeleza kuwa mpaka sasa anasumbuliwa na mkono wa kulia, mbavu, magoti pamoja na jeraha aliloshonwa mguuni.
Amesema, shughuli zake za kilimo huko Ruvu Kitongani (mkoa wa Pwani) zimesimama kwani hajiwezi toka apigwe na polisi.
KASI ya kupepea bendera za Chama cha CUF wilayani Mwanga, imeelezwa kumstua Mbunge mkongwe wa Jimbo hilo, Bw. Cleopa Msuya.
Katika tukio moja imeelezwa Msuya akiwa katika safari zake alilazimika kusimamisha gari na kuwahoji vijana waliokuwa katika tawi lao jipya la CUF.
"Kwanini mmeweka bendera ya CUF hapa kwani CCM imekunyimeni nini hata mnaikataa?" alihoji Msuya.
Vijana hao imeelezwa wakiizunguka bendera yao ya CUF wakawa wanaibusu.
Katika tukio jingine imeelezwa kuwa viongozi wa CCM na wale wa BAKWATA wamekuwa wakiwabughudhi watu waliotoa nyumba zao kufungua ofisi za CUF au hata kutundika bendera mbele yake.
Katika eneo la Mombasa Stoo wilayani humo, mwananchi mmoja aliamriwa ama ashushe bendera au akahe na biashara yake.
Taarifa kutoka Mwanga zimeeleza kuwa shinikizo lilikuwa kubwa ikabidi ofisi na bendera yake ihamie jengo lililokuwa Juhudi Hotel zamani.
Kufuatia sakata hilo, bendera nyingine mbili zilizopandishwa kwa mtu mmoja aliyetambulika kama Bw. Chenonana katika eneo la Ndanda palipokuwa na kijiwe maarufu cha CCM.
Katika eneo la Mwanga mjini habari zinasema 'vijiwe' vilivyokuwa vya CCM vimekuwa vikipepea bendera za CUF, jambo ambalo linaleta sura ya upinzani kupata nguvu wilayani humo.
|
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook |