SIKU ya Ijumaa Julai 14, mwaka huu Rais wa serikali ya awamu ya tatu na Mwenyekiti wa Chama tawala cha CCM, Mheshimiwa Benjamin Mkapa alilihutubia Bunge la Muungano na kutangazwa moja kwa moja na vyombo vya habari.
Hotuba ya Mheshimiwa Rais pamoja na mambo mengine ilitawaliwa na majisifu ya mafanikio ya serikali ya awamu ya tatu na kupambwa na nasaha kadhaa kwa watendaji ndani ya serikali, taasisi zisizo kuwa a serikali, vyama vya siasa na Watanzania wote kwa ujumla.
Pamoja na uzuri huo, hotuba hiyo ilikosa ile silika ya kujishusha, kwani haikuthubutu hata kidogo kugusia maeneo ambayo serikali yake ilishindwa kutenda vyema kwa jamii. Kwa ujumla wake haikuwa na kujikosoa katika utendaji wake.
Na hii ni hatari sana kwa watendaji katika chama chake pia kwamba watendaji wote ndani ya serikali na taasisi zake. Ninasema hivyo kwa sababu, hotuba yake inajaribu kujenga dhana kwamba Watanzania kwa watendaji wake katika nafasi mbalimbali hawakuwa na makosa na hivyo WOTE wanastahiki kuendelea na wajibu wao kwa miaka mingine mitano ijayo.
Si hivyo tu bali kushindwa kuonesha mapungufu katika utendaji kunawafanya watendaji hao kubweteka kuwa ni "perfect" wasiohitaji kushauriwa hivyo kukanusha ukweli kuwa mkamilifu katika utendaji ni Mwenyezi Mungu tu.
Lakini labda lingine nililobaini katika hotuba hiyo ni kuwa Wabunge wengi uwezo wao wa kuchambua mambo ni mdogo sana, hivyo kushabikia taarifa ambayo inastahiki kupewa maswali kadhaa. Kwa mfano katika kuusifu utendaji wa serikali yake ya awamu ya tatu, Mheshimiwa Rais Benjamin Mkapa alisikika akitaja uwingi wa uongezeko la shule za msingi, sekondari, vituo vya elimu ya watu wazima na nyumba za kuishi waalimu na kadhalika.
Wakati Rais akiyasema haya Wabunge wengi walionekana wakipiga meza zao kwa nguvu zote kuashiria kuridhika na kauli hizo na mafanikio hayo. Nionavyo mimi kwa Mbunge yeyote yule awaye anaetembelea jamii yake husika hivi sasa asingefurahia taarifa hiyo lazima angeuliza maswali yafuatayo:
Je, shule hizi zina wanafunzi, zina zana za kutosha za kufundishia, zina waalimu wenye sifa inayotakiwa? Kweli zina madawati? Si hayo tu bali kubwa zaidi ni kuwa kwa nini leo hii si jambo la kushangaza kuona watoto wengi hasa katika jiji la Dar es Salaam na miji mingi nchini wenye uwezo wa kwenda shule mpaka umri wa miaka kumi hata kumi na moja hawajafanya hivyo?
Kama hilo halitoshi kwa nini leo hii haishangazi kuona mtoto wa ngazi kuanzia chekechea hadi kidato cha sita anadai kupewa masomo ya ziada kwa maana ya "tuition"?
Kwa Mbunge muungwana na muadilifu mwenye kubeba dhamana ya uwakilishi wa wapiga kura wake, haya ndiyo maswali ya msingi yaliyotarajiwa vinginevyo tutabakia kuamini kuwa wabunge wengi wapo bungeni kwa kukumbatia maslahi binafsi tu.
Mwisho kushindwa kuonyesha mapungufu katika utendaji katika maeneo kadhaa ya serikali ya awamu ya tatu tunapoelekea uchaguzi kunaonesha dhamira ya chama husika kutokuwa tayari kujisahihisha katika safu ya utendaji kama itapata fursa ya kuongoza nchi kwa mara nyingine.
|
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook |