Matumizi sahihi ya Kiswahili

LUGHA kama zao la jamii inahitaji maendeleo ili iweze kukua na kudumu. Kwa maneno mengine bila maendelezo lugha huweza kudumaa na pengine kufa.

Ipo mifano ya lugha mbalimbali katika nchi za Afrika ambazo zimetajwa kuwa zipo katika hatari ya kufa kwa sababu zimekosa maendeleo na hivyo kumezwa taratibu na lugha nyingine.

Kiswahili ni moja ya lugha iliyopata maendeleo makubwa katika Afrika. Kiswahili ndiyo lugha inayotegemewa kwa mawasiliano katika nchi za Afrika Mashariki ukiacha Kiingereza.

Kutokana na kutangaa kwa sifa ya Kiswahili watu wa nchi mbalimbali wamepata shauku ya kujifunza Kiswahili. Leo kuna vituo mbalimbali vya redio za nchi za kigeni ambazo zina vipindi vinavyotangazwa kwa Kiswahili.

Jambo kubwa na la kujivunia ni kwamba Kiswahili hivi sasa hufundishwa hata katika vyuo vilivyopo katika nchi za Ulaya na Marekani.

Mafanikio yaliyopatikana katika Kiswahili yamewezesha vitabu mbalimbali vya lugha za kigeni kutafsiriwa kwa Kiswahili.

Bila shaka ni mafanikio hayo hayo yaliyochochea kuibuka mjadala unaoendelea hadi sasa wa kutaka Kiswahili kitumike kufundishiwa katika shule za sekondari badala ya Kiingereza.

Moja ya vyanzo vinavyoendeleza lugha ni kuzungumza lugha kwa ufasaha. Tanzania ni moja ya nchi inayosifika kwa kuwa na watu wanaozungumza Kiswahili fasaha katika Afrika Mashariki.

Ufasaha wa lugha si kuzungumza kwa usahihi tu bali pia kutolazimika kuchanganya lugha mbili kwa wakati mmoja.

Imeonekana kwamba watu wengi wana tabia ya kuchanganya pamoja maneno ya Kiswahili na Kiingereza wanapozungumza. Baadhi ya watu wenye tabia hiyo hufaya hivyo kwa makusudi ya kujionesha kuwa wamesoma na wanakielewa Kiingereza. Kwa hiyo huona fahari wanapochanganya Kiingereza pamoja na Kiswahili.

Katika kuzungumza kwao Kiswahili na huku wakitumbukiza maneno ya Kiingereza huonesha kwamba Kiswahili si lugha iliyojitosheleza katika mawasiliano hata yale ya kawaida kati ya mtu na mtu hivyo hulazimika kuchanganya na Kiingereza.

Uchunguzi umeonesha kuwa watu wenye tabia hii wana udhaifu wa kumudu lugha zote mbili. Katika kuficha udhaifu wao hujikuta wakizungumza huku wakichanganya maneno ya lugha tofauti ili waweze kueleweka.

Jambo la kusikitisha ni kuwa wanaodhihirisha udhaifu huo ni wale wanaojiona kuwa wasomi.

Kwa bahati mbaya hata watu wengi wa kawaida wameathiriwa na tabia hii kwa kule kudhani kuwa ni tabia inayoendana na usomi, lakini kumbe bila kujua wanachangia kufifilisha juhudi ya kuendeleza Kiswahili, kwa sababu kwanza lugha wanayozungumza si fasaha, pili mchanganyo huo huharibu lugha na tatu kuna hatari kwa Kiingereza.

Athari ya tatizo hilo imejitokeza huko Kenya ambako Kiingereza kimeendelea kukimeza Kiswahili. Katika maeneo mengi ya Kenya isipokuwa sehemu za Pwani, Kiingereza kina nguvu zaidi kuliko Kiswahili. Na baya zaidi nikuwa Kiswahili kinachozungumzwa si fasaha.

Japokuwa Watanzania tumepiga hatua kubwa zaidi katika kuiendeleza lugha yetu ni muhimu tuilinde dhidi ya uharibifu wowote ule.

Tabia ya kuchanganya maneno ya Kiswahili na Kiingereza inaweza kulemaza ndimi zetu na ndimi zikadumaza lugha yetu.

Kazi ya kukiendeleza Kiswahili ni ya kila mmoja wetu. Hatuna budi tujivunie kwa kuwa na lugha moja iliyotuunganisha Watanzania na kukilinda Kiswahili ni kukizungumza kwa fasaha.

Kila kitu kina adabu zake na adabu ya lugha ni kutoichanganya na nyingine wakati wa kuzungumza.

--
JuuRUDI


Bonyeza hapa
kushriki mjadala au kutoa maoni juu ya habari hizi na masuala mengineyo ya Kiislamu kwenye Baraza ya Wasomaji

   Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu: Bonyeza hapa
Au
Andika barua  kwa: webmaster@islamtz.org


An-nuur Home | Ukurasa wa Mwanzo | Islam Tanzania
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook