BARUA

Udini tuliousikia bungeni ni babu kubwa!

Ndugu Mhariri

WEWE Mheshimiwa Rais (Benjamin William Mkapa) unaongoza serikali, mimi (Pius Msekwa) naongoza Bunge na Jaji Barnabasi Samata anaongoza Mahakama.

Hayo yalikuwa maneno ya Spika wa Bunge kabla ya kumkaribisha Rais kuliaga Bunge.

Kimsingi taasisi hizo tatu ndizo zinazounda Dola. Kwa maana hiyo Dola nzima ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imeshikwa na Wakrsito watupu. Hata kiongozi Mkuu wa shughuli za serikali na zile za Bunge yani Waziri Mkuu ni Mkristo.

Kana kwamba hao hawatoshi, Naibu Spika wa Bunge na Katibu wa Bunge nao pia Wakristo Sijui Mheshimiwa John Cheyo na wenziwe wanaivumilia vipi harufu hii kali ya udini?

Si hivyo tu, uongozi wa serikali katika wizara na idara nyeti umeshikwa na Wakristo watupu, Rais Mkristo, Waziri Mkuu Mkristo, Waziri wa Fedha Mkristo, Mwanasheria Mkuu Mkristo, Kurugenzi kadhaa za idara nyeti zimeshikwa na Wakristo watupu!

Na sijui wale wenzangu na mimi tunaoimbishwa propaganda za udini mmeliona hilo? Na kama mmeng'amua, mna maoni gani juu ya wale wanaokituhumu chama fulani kuwa ni cha kidini?

Je, sasa mmetanabahi kuwa udini ni Uislamu? Wakati watu wakipiga kelele za kutobaguana kwa misingi ya dini, kumbe dola nzima imegubikwa joho la udini!

Kama vile hilo halitoshi, Tume ya Uchaguzi ambayo, kimsingi ndio inayoratibu na kusimamia zoezi la kura, nayo imevishwa joho la udini! Inaongozwa na Wakristo watupu.

Wasimamizi wa uchaguzi na waratibu nao vile vile ni wakristo watupu. Huu bwana Cheyo ndio udini wa wazi ambao ungepaswa kuulalamikia.

Nikiwa raia mwenye kulitakia mema taifa langu naiasa serikali na baadhi ya wanasiasa kuwa waache tabia ya mtoto kikojozi ambaye baada ya kumwaga kojo kitandani hugeuka na kumsingizia mwenzie.

Na ukweli uliowazi kuwa CCM na serikali yake vimebomoa msingi muhimu wa utaifa uliojengwa na wazee wa TANU ambao walikuwa Waislamu watupu.

Wazee hao walimkaribisha Julius Nyerere Mkristo na kumpa uongozi.

Kwa bahati mbaya au nzuri, Waislamu, kwa miaka mingi walipumbazwa na moyo wa uzalendo na labda pia usingizi ulichangia. Lakini sasa wameamka. Mwamko huo ndio unaotafsiriwa kuwa ni hatari inayotishia umoja wa kitaifa.

Kwa hali ilivyo sasa propaganda hazitafaa chochote. Jambo muhimu ni kurekebisha mambo haya. Na kwa kuanzia serikali kama kweli hailengi kujenga mfumo kristo nchi hii basi ibadili muundo wa Tume. Tume iwe na uwiano sawia wa watu wa dini zote.

Wananchi wema Waislamu na Wakristo hasa walalahoi wenzetu Waprotestant tuikemee hali hii kabla "mfumo katoliki" unaopewa baraka na hawa viongozi wetu walio madarakani haujatufikisha pabaya.

Mama Akili,
S.L.P. 1876,
Morogoro.



Cheyo na Mrema wakereketwa wa mfumo Kristo

Ndugu Mhariri

NIPE nafasi kidogo ili nitoe maoni yangu kuhusu ubaguzi wa kidini uliojengwa hapa nchini ambao kwa jina la ubatizo huitwa "Mfumo Kristo", yaani kila jambo kutazamwa au kupimwa kwa jicho la Ukristo.

Mfumo huo hatari kwa umoja wa kitaifa unatoa fursa kwa Ukristo hususan Ukatoliki kuhodhi serikali na sekta zake zote.

Chini ya mfumo huo uongozi wa nchi hii umefanywa kuwa milki ya Wakristo hasa Wakatoliki ndiyo maana hata Waprotestant nao huwekwa kundi moja na Waislamu kuwa ni watu "wasiofaa" kushika nyadhifa muhimu.

Mazingira yaliyojengwa na mfumo huo yameifanya ikulu iwe mali ya Mkatoliki au yule aliyepata ridhaa ya Wakatoliki kama ilivyojitokeza katika awamu ya pili.

Ndio maana hata wale tunaowaona ni wapinzani nao wanaimba na kuushabikia mfumo huo mpaka wengine kwenda 'kugaragara' kwa akina Pengo.

Kauli za akina Cheyo na Mrema zimewaweka wazi Watanzania kuwa ni aina ipi ya uongozi inayotakiwa na mfumo Kristo.

Wale walio nyuma ya viongozi hao wakidhani wanakusudia kuleta mageuzi ya kweli ya kiuchumi baada ya CCM kushindwa, watazame upya mwelekeo wao wa kisiasa.

Bwana Cheyo ametamka bayana kuwa amejitoa kwenye muungano wa wapinzani kwa kuwa umemsimamisha Profesa Lipumba kuwa mgombea Urais, kwa kuwa Lipumba ni Muislamu basi bwana Cheyo anasema huo ni udini.

Bwana Mrema amedai huko Tanga hivi karibuni kuwa ameukataa muungano wa wapinzani eti kwa kuwa hakuitwa (yeye hakuwa na mpango wa muungano) na amegundua udini ndani ya muungano huo, udini wenyewe ni kule kusimamishwa Lipumba kuwa mgombea!

Labda swali dogo tu l kwa wafuasi hawa wa mfumo Kristo ni hili: Hivi kwa mfano wapinzani wangemsimamisha Mrema au Cheyo , huku CCM ikiwa tayari imemsimamisha Benjamin William Mkapa. Hapa hakuna udini?

Au hivi sasa walivyojitenga ambapo Cheyo atagombea kwa UDP - Mkristo, Mrema TLP - Mkristo na Benjamin William Mkapa CCM - Mkristo. Huu si udini!

Kwa mtazamo wa mfumo Kristo wa akina Cheyo na Mrema, udini ni Lipumba Muislamu kugombea Urais.

Kwa ukereketwa wenu wa mfumo Kristo Mrema, Cheyo na CCM yenu hamuitakii maendeleo nchi hii.

Shaban Almas,
Temeke,
Dar es Salaam.


Mwembechai 'Killings' ni chetu

Ndugu Mhariri

WASOMI Waislamu tunayodhima kubwa kuinusuru nchi hii na matokeo ya ubaguzi uliodumu nchini kwa miongo kadhaa.

Lakini dhima kubwa zaidi ipo kwa sisi ambao tumebahatika kuwa watumishi wa serikali katika ngazi mbalimbali.

Mengi ya kuwabagua na kuwakandamiza Waislamu tuliyashuhudia. Lakini tulizingirwa. Naomba kwa masikitiko makubwa nikiri kuwa wengi tulikuwa waoga. Hatukuthubutu kusema.

Waliyosema Mzee Lila ni madogo yapo mengi.

Lakini niseme tu kuwa: Kitabu - Mwembechai Killings si cha Dkt. Njozi ni chetu. Na ndio maana tumeki - down load tunacho wakati serikali inazuia kilichopo uwanja wa ndege.

Ni chetu kwa maana ya kwamba yaliyomo ni yetu na tunawajibika sote kwa umoja wetu Waislamu. Si kitabu cha Njozi ni Chetu.

Naamini sote tulioko kwenye mtandao tunafanya kazi kubwa kusambaza kurasa na kufasiri kwa Kiswahili kwa wenzetu wasioelewa vyema Kiingereza.

Mstaafu serikalini,
Abu Hussein,
Morogoro.


Waliokuwa gizani wameshapata mshauri?

Ndugu Mhariri

KWA mara ya kwanza napenda kulitumia gazeti lako kutoa dukuduku langu.

Hakuna asiyejua ya kuwa Watanzania tumepata pigo kali sana la kuondokewa na Mwalimu Nyerere. Nyimbo nyingi za maombolezo ziliimbwa nami nilifanikiwa kudokoa machache kati ya maudhui yake.

Kwanza, amani na upendo vimetoweka, kiza kimetanda, hatujui pa pakukamata. Sasa twende wapi tukapate ushauri?

Shaka yangu pasipo na amani na upendo pana vurugu. Penye kiza kilichotanda watu hawaoni ndiyo maana hawajui pakushika. Tena watu hawa hawana mshauri.

Swali je, watu hawa washapata mshauri mwingine au bado? Kama wamempata mbona hawatuarifu na kama hawana je watu wasio na amani wala upendo, kiza kimetanda hawajui pa kushika tukiwachagua watuongoze watatuelekeza wapi?

Wito kwa Watanzania waepukane na mabishano ya itikadi. Bali tuangalie hoja za msingi. Kodi za mapato na kodi za maendeleo zinakusanywa, huduma za afya hospitali za serikali hazina dawa, bali madawa yanapatikana kwenye maduka ya watu binafsi. Vipi hapa?

Ada ya shule za serikali ni shilingi 60,000 kima cha chini kwa mwaka. Mkulima wa matunda hana soko la matunda yake. Atasomeshaje mtoto. Sasa naomba jibu tulipoambiwa ili tuendelee twahitaji vitu vinne yaani watu, ardhi, siasa safi na uongozi bora. Nini hakipo na tutakipata wapi?

Jumanne S. Kagoma,
Dar es Salaam.
--
JuuRUDI


Bonyeza hapa
kushriki mjadala au kutoa maoni juu ya habari hizi na masuala mengineyo ya Kiislamu kwenye Baraza ya Wasomaji

   Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu: Bonyeza hapa
Au
Andika barua  kwa: webmaster@islamtz.org


An-nuur Home | Ukurasa wa Mwanzo | Islam Tanzania
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook