Mashairi

Nalia

Nalia nasikitika, mambo nikikumbukia,
Machozi yanidondoka, mambo nikifikiria,
Waja tunadhalilika, hapa kwetu Tanzania,
Nalia twadhulumiwa, nasi tunafurahia.

Nalia twadhulumiwa, twashindwa kujitetea,
Dhalimu aneemeka, na huku afurahia,
Na sisi tumetosheka, hatuchukui hatua,
Nalia twadhulumiwa, nasi tunafurahia.

Kila ninapokumbuka, machungu hunizidia,
Nyoyoni ninanyongeka, raha inaniishia,
Hata nikisononeka, hiyo si njema hatua,
Nalia twadhulumiwa, nasi tunafurahia.

Wajibu wetu hakika, dhulma kuindoa,
Ameagiza Rabuka, kudhulumu ni hatia,
Tutajitia mashaka, kikubali dhulumiwa,
Nalia twadhulumiwa, nasi tunafurahia.

Yapaswa kuzikumbuka, amri zake Jalia,
Kisasi kinalipika, pindi tutakapoamua,
Dhalimu ataondoka, hapa petu Tanzania,
Nalia twadhulumiwa, nasi tunafurahia.

Kiasi tulo teseka, chatosha nawaambia,
Azma tusipoweka, kweli tutaangamia,
Tazidi kudhalilika, waja tutaangamia,
Nalia twadhulumiwa, nasi tunafurahia.

Wakati umeshafika, yatosha yalotokea,
Mikono ikitumika, dhalimu tamuondoa,
Fursa imeshafika, nini tunachongojea,
Nalia twadhulumiwa, nasi tunafurahia.

‘Mchechnya’ F.M.
Dar es Salaam.


Mashujaa wa CUF

Tipwiri mtipwiriko, wana CUF waingia,
Ngangari lao tamko, mashujaa waingia,
Shangwe hoi na chereko, mkombozi kaingia,
Hao hao mashujaa, wana CUF waingia.

Mwaona hayo magari, haki sawa waingia,
Yamewabeba ngangari, Kosovo na Chechinia,
Mashujaa majasiri, haki wanopigania,
Hao hao mashujaa, wana CUF waingia.

CUF chama cha umoja, usawa na haki pia,
Mashujaa kwa pamoja, haki wameshapania,
Kutetea umoja, na uchumi Tanzania,
Hao hao mashujaa, wana CUF waingia.

Mwamuona Profesa, wa CUF anaingia,
Lipumba sio mapesa, hilo ndugu zingatia,
Mashujaa nao sasa, na Swaibu waingia,
Hao hao mashujaa, wana CUF waingia.

CUF hao waingia, Jangwani wanaingia,
Magari yao mamia, watu wawashangilia,
Haki sawa waimbia, kwa ndugu Watanzania,
Hao hao mashujaa, wana CUF waingia.

Matawi nayo mamia, kwa magari waingia,
Ukombozi yao nia, wana CUF wavutia,
Wenzenu twashudia, mikoani nawambia,
Hao hao mashujaa, wana CUF waingia.

Igeni haya jamani, mikoani nawambia,
Mijini na vijijini, wote CUF kuingia,
Jama mnangoja nini, nusura imefikia,
Hao hao mashujaa, wana CUF waingia.

Wana waso na papara, ni ngangari barabara,
CUF twawapenda bara, visiwani ngome bora,
Wana CUF ni imara, visiwani pia bara,
Hao hao mashujaa, wana CUF waingia.

Wapinzani kweli kweli, tena ngangari kabisa,
CUF ni jibu la kweli, ndugu nawaasa,
Wengine sio wa kweli, ni vibaraka naasa,
Hao hao mashujaa, wana CUF waingia.

Wacheni tutipwirike, ndani ya mtipwiriko,
Ilihaki ipatike, CUF ndo letu tamko,
Wacheni tufurahike, kwa Lipu ndiko tuliko,
Hao hao mashujaa, wana CUF waingia.

Ni kumi na moja beti, na hapa ni hitimisho,
Na wito tujidhatiti, tusifungwe goli mwisho,
Goli baya la penati, lindeni naasa mwisho,
Hao hao mashujaa, wana CUF waingia.

Almasi H. Shemdoe,
“Tunda la Matumaini”,
Dar es Salaam.
--
JuuRUDI


Bonyeza hapa
kushriki mjadala au kutoa maoni juu ya habari hizi na masuala mengineyo ya Kiislamu kwenye Baraza ya Wasomaji

   Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu: Bonyeza hapa
Au
Andika barua  kwa: webmaster@islamtz.org


An-nuur Home | Ukurasa wa Mwanzo | Islam Tanzania
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook