Na Dkt. Abdallah Saffari
HUKU na huko Tino aliangalia nyika zilizo na ukame akizimithilisha na ugumba. Hakukuwa na nyumba za maana isipokuwa kila baada ya mwendo wa nusu saa walitokea kwenye vijumba viwili, vitatu au vinne vilivyojengwa kwa suti za nyasi au udogo mwekundu na kuezekwa kwa nyasi. Nje yake, watoto walio uchi au kuvaa vibwende vya shuka za kishingoshingo, suruali au vishati, waliliangalia gari likipita. Walifinya macho kuzuia vumbi lisiingie machoni. Lakini haikuwa rahisi. Vumbi lote jekundu lilitua juu ya mauongo yao na kufanya tabaka jekundu lililobadilisha rangi zao pamoja na zile za nywele zao kuwaachia kikohozi na matongo. Mikononi au shingoni walikuwa wameshika au kuning'iniza manati za kuwindia ndege.
Pale mbele Tino alikaa akiangaza macho huku na huko, akimwangalia dereva, sasa kifua wazi, akisumbuka kukanyaga klachi, kubadili gea, kuongeza mafuta na kukwepa makorongo.
"Shenzi, hii sio barabara ila shamba. Kodi twatoa barabara hazitengenezwi".
Lakini hakuna aliyejibu. Na safari iliendelea taratibu mno kiasi cha maili ishirini au thelathini kwa saa, tena kwa zile sehemu zilizo afadhali.
Saa kumi na mbili walitokeza kunako mashamba ya mkonge. Tofauti na zamani ambapo miraba ya mashamba hayo ilikuwa safi hata kumuona panya aliyekatiza, sasa ilikuwa magugu matupu. Majani ya mikonge yaliyokomaa yalibaki ndani ya machaka huku malingoti makavu yakisimama twe! Na mengine baada ya kupigwa na mvua na kuoza. Yalisenuka na kuangukiana ovyo ovyo. Kwa hali hiyo idadi ya majani ya mkonge yaliyokatwa ilipungua mno pamoja na ubora wake. Badala ya kuwa marefu, mapana na mazito, sasa yalikuwa vifyefye vilivyotoa singa fupi duni zilizo katika mithili ya kipilipili.
"Mkonge si mali tena", alisema yule utingo.
"Umefanywa si mali", alijibu Tino akiendelea kuangaza macho katika machaka yale yaliyokuwa vigumu kuyaita mkonge au minokoa.
Saa kumi na mbili na nusu Tino alishuka Manga akalipa nauli na kumshukuru dereva na utingo wake, akaanza kujiandaa kwa safari ya Boko.
Pale aliposhushwa hapakuwa mbali na kituo kikubwa cha mabasi yaliyokwenda kijijini kwao. Alitembea kwa hatua za haraka hadi kituoni hapo ambapo alipakuta peupe isipokuwa kwa wasafiri wachache walioketi hapa na pale. Badala ya kuketi alistahabu kusimama kunyoosha viungo. Makalio yote na kiuno vilikuwa vyampwita kwa mtindio alioupata njiani.
Magharibi jua jekundu lilishuka taratibu likitupa mionzi yake dhaifu. Muda mfupi lilizibwa na mwembe mkubwa baadaye kutoweka kabisa. Upeka ukatua juu ya uso wa dunia. Tino akajiwa na hofu ya usiku. Haraka alipapasa mfuko wake. Alipokuwa hakukiona alichokitafuta aliuweka mfuko huo juu ya goti la mguu wa kulia aliloliinua na kufungua zipu. Akatia mkono mfukoni kupapasa mpaka pale aliporidhika kuishika ala ya kisu chake. Alihema na kupiga plani ya upesi upesi.
Dhahiri saa zilikuwa zinayoyoma. Karibuni mabasi yote yalikuwa yameondoka. Isitoshe maongezi aliyoyasikia juu juu njiani na hapa mjini yalihusu uhaba mkubwa wa dizeli. Alikuwa na mawili ya kufanya: alale pale mjini ambapo alikuwa na rafiki wengi pamoja na uwezo wa kupanga nyumba ya kulala, au auchape wa rondo hadi Boko.
Tino alishauriana na watu wawili waliosimama jirani naye kwa mintarafu ya wazo lake la kwenda kwa miguu bila ya mafanikio.
"Basi naomba Mungu", aliwaaga na kuondoka kwa mwendo wa kawaida.
Alitembea kuelekea Kaskazini hadi karibu na mwisho wa mji ambapo aliingia kunywa chai na maandazi matatu katika kijimkahawa kidogo kando ya barabara. Ghafla njaa yote ilimtoka maana maandazi yenyewe yalikauka kwa kukosa wanunuzi na hayakuwa na sukari. Vikombe vyenyewe vilikuwa na madoa ya uchafu kana kwamba sehemu hiyo ilikuwa na ngambi ya maji. Kikombe kilinata kwa uchafu huo. Chai yenyewe iliyosemwa ya maziwa ilikuwa bure ghali mithili ya maji ya mkurumuzi. Ilikuwa kushikiza tumbo kwa vile msafiri kafiri.
Kutoka hapo Tino alitembea hadi nyumba za mwisho wa mji. Na kiza nacho kilianza kutamalaki kote. Aliangalia mbinguni, akihofu kuwa mvua na safari hatari. Anga yote ilikuwa nyeusi kuashiria mwezi mpevu na nyota moja moja zilimetameta.
Kutoka mjini hapo hadi kijiji ilikuwa maili thelathini, mwendo wa saa nne au zaidi kwa miguu kutegemea na kasi ya mtembeaji. Maili tano za mwanzo barabara ilikuwa ya lami, baada ya hapo ilikuwa ya kokoto au kama wajenzi wa barabara walivyoiita ; murram. Sehemu hii ya barabara ilijengwa kabla ya uhuru wa nchi hii na kampuni ya Kibelgiji iliyomiliki shamba moja la mkonge zama hizo, ili kurahisisha usafiri wa malori yao yaliyokuwa yakisomba marobota ya mkonge kutoka huko hadi bandarini Manga. Zama hizo kila changarawe ziliposombwa na mvua ya masika au udongo kupeperushwa na upepo vifusi vilimiminwa upya. Madereva wote wa magari na wapanda baiskeli wakaburudika kupita barabara hiyo. Lakini sasa ilikuwa si kitu si chochote. Mambo yalianza kuwa mabaya zaidi miaka kumi iliyopita wakati serikali ilipodai kuchukua hisa ya asilimia sabini kwenye kampuni ile ya Mkonge ya Wabelgiji iliyomiliki shamba hilo na Matumbi. Wazo hilo lilikataliwa moja kwa moja na utawala wa kampuni hiyo, wakafunga virago vyao na kugura. Waliondoka na zana zote za maana za kazi kuanzia viberenge, reli zake, matrekta na korona. Vifaa vingine kama vile magari ya zamani na nyumba ama waliviuza kwa watu binafsi au kuziachia serikali kwa maya. Kampuni hiyo ambayo ilikuwa na mashamba mengine ya mkonge katika mikoa mingine nchini ilifunga mashamba hayo na kuhamia nchi ya jirani na baadhi ya wafanyakazi wao stadi hasa mafundi. Huko waliendelea na mashamba yao mengine yaliyokuwepo.
Baada ya uamuzi huo serikali ilijipiga kifua na kuunda kampuni yake kuliendesha shamba hilo. Maana mkonge lilikuwa ndilo zao kubwa la biashara kupita yote lililoipatia nchi hii asilimia tisini ya fedha za kigeni. Dhahiri basi, dhamira hiyo ilipiga chini, maana mashambani hapo mambo yakawa shafuu shafuu tu!
Tino alitembea kwa kasi ili afike mapema aendako, pili kwa ajili ya hofu iliyoambatana na upeka na kiza kinene cha usiku. Hadithi mbalimbali za mikasa iliyowafika wasafiri wa usiku zilimjia: wanyama, majambazi na mumiani. Waana wanyama sio sana maana tangu utoto wake hakusikia mtu kuraruliwa na chui au simba katika barabara ile. Labda nyoka, lakini hiyo aliihesabu kama kudra ya Mungu tu. Sema mumiani! Hapo mwili ulimsisimka.
Hadithi za mumiani zilikuwa nyingi japo serikali ya kikoloni na hata ile ya uhuru ilizikana. Lakini yeye binafsi alisikia watu wakisimulia walivyovamiwa na 'machinjachinja' yaani mumiani waliokuwa na machupa ya damu. Waliona magari yaliyokuwa na watu hao ambao walidai kuua mbu kumbe walifanya shughuli ya kukusanya damu kwa nguvu. Alionyeshwa hata kovu za mapambano nao. Hivyo aliridhika na ushahidi huo. Chambilecho aliamini hakuna siri, akaona basi mumiani jambo dhahiri.
Alitembea akiangalia huku na huku, mpaka akasikia pumzi na hatua zake za haraka. Vichaka vya michakari, migunga na vibamba viliizingira mikonge na kuongeza kiza ambacho macho yake yalishindwa kukipenya. Sauti za nyenze na vinyama mwitu vingine zikasikika huko na huko.
Baada ya mwendo wa zaidi ya saa moja na nusu alikaribia darajani, ambapo palivuma kwa mumiani. Hapa palichanganyika na sauti za nyenze na vyura ambazo zilinyamaza kutoka na vishindo vya hatua zake. Huku kisu chake mkononi, mara kwa mara akageuka nyuma kuangalia vichakani kwa matu kama tahadhari. Bila ya kujijua akajikuta yumo katika kukimbia. Hakupunguza kasi hiyo mpaka alipolipita lile daraja, akapandisha kilima na kuanza kutembea kama pale awali, kinywa wazi kupapia hewa. Hakukutana na gari wala mtu njiani.
Lakini alipokaribia kambi ya zamani ya shamba la mkonge alipunguza kasi. Sasa alikutana na mtu mmoja mmoja ambao aliwasalimu, "usiku".
"Mchana", walijibu kuashiria amani. Jibu la "usiku" lingeashiria kondo.
Baada ya kulipita shamba lile la Matumbi aliingia katika mapori mengine yaliyochanganyika na mashamba ya minazi, mihogo na migomba. Humo aliweza hata kusikia sauti za komba wakitafuta pombe kwenye virenge vya minazi au kula ndizi mbivu. Komba walikuwa na tabia ya kukwangua ndizi mbichi kuzifanya ziive upesi kwa jua. Baadaye waliipitia mikungu hiyo ya ndizi kukagua kama ilikuwa tayari kuliwa. Aidha, walivuma kwa ulevi kupita kiasi. Kwa jumla sauti hizi za komba zilikuwa faraja kwa Tino kwa vile alihusisha na wanadamu, sio simba.
Tino aliingia wilayani saa nne kasoro robo, shati lote limetota, miguu mizito kama imefungwa nanga. Kwa mara ya kwanza alisikia njaa kali. Alitembea pole pole akitafuta mkahawa ulio wazi. Baada ya jitihada ya nusu saa nzima alikata tamaa.
|
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook |