VIONGOZI wa Msikiti wa Ubungo Darajani jijini wamedai kutishiwa kuuawa na mtu waliyemtaja kuwa ni mkereketwa wa CCM.
Katika barua ya julai 22, mwaka huu waliyomwandikia Amiri wa Shura ya Maimamu Jijini, ambayo gazeti hili lina nakala yake, viongozi hao wamemtaja mtu huyo kuwa ni Bwana Omar ambaye wamedai amekuwa akipita kueneza vitisho hivyo dhidi yao.
Sababu ya mtu huyo kutaka kuwafanyia uhalifu huo, viongozi hao wameeleza katika barua hiyo kuwa ni kutokana na wao kuunga mkono vyama vya upinzani na kwamba Msikiti wao umekuwa ukihubiri siasa.
"Sisi viongozi wa Msikiti huu wa Ubungo darajani tumetishiwa kuuawa na wakereketwa wa CCM. Vitisho hivyo vinaenezwa na mtu aitwae Omar ambae ni mkereketwa wa CCM, imeeleza sehemu ya barua hiyo.
Hata hivyo, uongozi huo haukueleza katika barua hiyo mahali anapoishi mtu huyo wala kuwataja wakereketwa wengine inaowatuhumu kuhusika na kadhia hiyo
Katika tukio jingine siku ya Jumamosi nyakati za asubuhi imeelezwa mtu aliyedhaniwa kuwa Afisa wa upelelezi alifika msikitini hapo na kutaka kuonana na Imamu, siku iliyofuatia (juzi asubuhi) Mwenyekiti wa Msikiti alihojiwa na vyombo vya dola kuhusiana na masuala kadhaa ya msikiti huo.
Katika matukio ya hivi karibuni yamekuwepo matukio ya Waislamu kukamatwa na kuwekwa rumande katika baadhi ya Misikiti. Madai yanayotolewa ni kuwa waumini hao wanafanya fujo misikitini.
Hata hivyo, waumini wamekuwa wakidai kuwa kukamatwa kwa wenzao hutokana na fitna zinazopelekwa katika vyombo vya dola na wakereketwa wa CCM.
Imeelezwa kuwa fitna hizo hupamba moto pale ambapo wakereketwa wa CCM huenguliwa katika uongozi wa Misikiti.
Hali hizo zimeikuta Misikiti ya Urafiki, Tegeta
na Uzuri.
Grozny, Chechnya
BATALIANI ya Wapiganaji wa Chechnya chini ya ukamanda wa ustaadh Ramadhan kilifanya shambulio la ghafla dhidi ya msafara wa kijeshi wa Russia katika vijiji vya Sheshan Aul katikati ya wiki iliyopita taarifa ya kijeshi ya wachechen imeeleza.
Katika mashambulizi hayo magari kadhaa yaliharibiwa na idadi kubwa ya askari wa Russia waliuliwa au kujeruhiwa.
Katika shambulio jingine lililofanyika eneo hilo siku hiyo hiyo, taarifa ya wachechen imethibitisha kuuawa kwa askari 20 wa Russia na silaha kadhaa kuharibiwa.
Aidha, katika mashambulizi yaliyofanyika kusini ya Grozny eneo 56 wapiganaji hao walifanikiwa kuangamiza askari 12 wa Kirusi na kuharibu kifaru kimoja.
Katika mapigano hayo yaliyodumu kwa masaa matano, Mujahidiin walipata neema ya ushahidi(walikufa mashahidi) na mmoja alijeruhiwa.
Katika tukio jingine linaloashiria kukata tamaa kwa wavamizi, imeripotiwa kuwa wanajeshi wa Kirusi walivamia soko kuu la mji wa Urus - Martan Jumanne iliyopita walipora na kuiba bidhaa mbali mbali pamoja na fedha.
Zaidi ya raia 180 walikamatwa katika uvamizi huo
na kisha kuachiwa baada ya mali zao kutaifishwa.
VYAMA vya upinzani vimeelezwa kuwa iwapo vitaendelea kuhujumiana kwa kupeana shutuma zisizo na ushahidi vitaendelea kuinufaisha CCM.
Hayo yameelezwa na wananchi mbalimbali walioongea na Mwandishi wa habari hizi mjini hapa kwa nyakati tofauti.
Wananchi hao wametoa mfano wa mkutano wa mgombea Urais kupitia chama cha TLP Bw. Augustine Mrema alioufanya mjini Tanga hivi majuzi ambapo alielekeza mashambulizi makali kwa mgombea Urais wa Chama cha CUF, Prof. Ibrahim Lipumba.
"Hali hii ya kupakana matope wenyewe kwa wenyewe itaidhoofisha kambi ya upinzani na hakuna tutakapofika", alidai mmoja wa wananchi hao aliyejtaja kwa jina la Mlemba.
Mwananchi mwingine aliyeeleza kukerwa na kauli ya Mwenyekiti wa chama cha UDP, Bw. John Cheyo aliyoitoa hivi majuzi kuwa anasikia harufu ya udini kwenye muungano wa CUF na CHADEMA, amesema, shutuma kama hizo ni za kupakana matope kwa sababu hazitolewi ushahidi wa kisayansi.
"Inaonekana vyama vya upinzani vinahujumiana wenyewe kwa wenyewe ili kuiachia CCM iendelee utawala", alidai.
Baadhi ya wananchi hao wameeleza wasiwasi wao kuwa baadhi ya vyama vya upinzani lengo lake si kuing'oa CCM kwenye mdaraka bali ni kujitafutia umaarufu tu wa kisiasa.
Wamedai kuwa chama kimoja kinapokiona kingine kinakubalika zaidi kwa waanchi huanza kukifanyia hujuma ilimradi tu kukiondolea matumaini ya kwenda Ikulu.
Wananchi hao wamevitaka vyama vya upinzani kutokubali
kugawanywa na CCM bali viimarishe nguvu zao kwa pamoja ili viweze kuing'oa
CCM kwenye madaraka.
--
![]()
|
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook |