Mahakama za 'Sharia' zianzishwe-Jaji Augustino
JAJI Augustino Ramadhani amesema, sheria za Kiislamu juu ya maisha binafsi na familia zinahitaji kuwepo mahakama maalum.

Jaji Ramadhani amesema, kama ambavyo kuna mahakama maalum za mambo ya biashara, kazi na kodi, sharia hizo za Kiislamu nazo zinahitaji mahakama pekee.

Jaji Augustino Ramadhani ameyasema hayo katika mada yake juu ya sheria ya Kiislamu (personal) katika Afrika akiangalia zaidi Tanzania.

Aliwasilisha mada hiyo katika semina iliyofanyika jijini Julai 21-23. Anuwani ya semina hiyo ilikuwa "Islamic Law in Africa Project".

Katika mada yake, Jaji Ramadhani alielezea umuhimu wa kutambua kuwepo kwa tofauti katika imani. Lakini pia akasisitiza uwepo wa vifungu vya sheria vitakavyowezesha utekelezaji wa imani hizo.

Amesema, tofauti na Ukristo, Uislamu una sheria maalum zenye maelezo na ufafanuzi wa kina. Hali hiyo amesema, inahitaji serikali kuchukua hatua maalum kuwezesha utekelezaji wa sheria hizo.

Katika mjadala wa mada yake, alisisitiza kuwa, hakimu katika kesi za Kiislamu ni lazima awe Muislamu. Amesema, sheria ya Kiislamu inatoka kwa Mungu na suala la kiimani. Kwa hiyo akasema, ni yule tu anayeamini anaweza kuhukumu. Jaji amesema, haki sio itekelezwe tu, lakini ionekane ikitendeka. Amesema, ni vigumu Muislamu kuona haki imetendeka iwapo hakimu si Muislamu.

Jaji Ramadhani amesema, katika kutekeleza sheria ya Kiislamu, wahusika ni lazima wachague moja kati ya mawili kuwa Waislamu wafungamane na sheria zake, au watoke wahukumiwe na sheria za nchi.

Ameyasema hayo akitoa ufafanuzi juu ya mgongano uliowahi kutokea. Mtu anakuwa Muislamu lakini katika mirathi anaikiuka sheria ya Kiislamu na kuishutumu kuwa inakiuka katiba ya nchi.

Hata hivyo, maelezo haya ya Jaji Ramadhani yanapingana na msimamo wake wa awali.

Katika kesi ya madai kati ya Anwar Z. Mohammed dhidi ya Said Selemani Masuka, alimshutumu Jaji Hamis Msumi kwa kuamua kesi hiyo kutumia sheria ya Kiislamu.

Katika kesi hiyo Jaji Msumi aliukataa wasia uliotoa mali yote ya mke kwa mume kwa hoja kwamba sheria ya Kiislamu hairuhusu wasia zaidi ya theluthi ya mali.

Shauri hili lilipofikishwa kwa Jaji Ramadhani kama rufaa alisema "udini" na "uzalendo" ulitumika kuliko sheria.

Semina juu ya 'Sheria katika Afrika' iliandaliwa na Chuo Kikuu cha Cape Town kitengo cha Uislamu (Centre for Contemporary Islam) na kufadhiliwa na The Ford Foundation ya Marekani.

Wajumbe kutoka Kenya, Uganda, Sudan, Afrika Kusini na kadhalika walihusika.

Hata hivyo, wakati nchi nyingine watoa mada walikuwa ama Waislamu wasomi au viongozi kutoka taasisi za Kiislamu. Waislamu Tanzania waliwakilishwa na Wakristo wawili.

Jaji Augustine S.L. Ramadhani na Bw. Robert V. Makaramba.

Dkt. Ahmed Sengendo kutoka Uganda akiongea na mwandishi wa habari hizi amesema, wajumbe wa semina hiyo walipohoji vipi semina yazungumzia sheria ya Kiislamu, lakini Waislamu wa Tanzania hawapo.

Amesema "waliowawakilisha" Waislamu walidai kuwa Waislamu walialikwa lakini hawakujitokeza.



Tanzania iko njia panda
Amani ya nchi mashakani


"NCHI ni huru, jitihada zetu hazikuruka patupu. Nyinyi vijana mna bahati kuzaliwa katika nchi huru. Ulindeni uhuru huu. Lakini muelewe kwa nini walioupigania walikuwa tayari kuyavumilia machungu".

Kauli hiyo ilitolewa na bibi Titi Mohammed alipokuwa akihojiwa na aliyekuwa mwandishi mashuhuri wa magazeti ya Daily News na Sunday News mwanzoni mwa miaka ya 90 bwana Reginald Mhango.

Hiyo ilikuwa katika kusherehekea miaka 30 ya uhuru wa Tanzania uliopatikana mwaka 1961 kutoka kwa wakoloni wa Kiingereza.

Bibi Titi alikuwa akihojiwa kama mmoja wa maveterani waliopigania uhuru wa nchi hii.

Kama alivyosema Bibi Titi ambaye hivi sasa amekuwa akionekana kushirikishwa katika kuwajenga baadhi ya wanasiasa, Watanzania hawana budi kuulinda uhuru.

Kuulinda uhuru ni pamoja na kuthamini michango ya watu mbali mbali walioshiriki katika mapambano ya kumng'oa mkoloni.

Aidha waliokabidhiwa madaraka hawanabudi kuongoza kwa mujibu wa katiba na sheria zilizowekwa.

Kadhalika kujali malalamiko na hisia za wananchi wote bila ya upendeleo wa aina yoyote sambamba na kuboresha maisha yao.

Mwezi Desemba mwaka huu nchi yetu itafikisha miaka 40 ya uhuru katika mazingira ambayo baadhi ya wananchi wake wamekuwa wakilalamika kubaguliwa kidini na kijamii.

Kwa miongo miwili sasa makundi ya Waislamu yamekuwa yakiirushia lawama serikali ya chama tawala kuwa imewapuuza na kuwakandamiza kipindi chote cha utawala wake.

Machapisho, vipeperushi na makongamano yanayojadili suala hilo mara kwa mara yamekuwa yakiikumbusha serikali hiyo irejee katika wajibu wake kwa mujibu wa katiba ya nchi.

Katika mlolongo wa malalamiko hayo Amir Sheikh Juma Mbukuzi alifikia kuitahadharisha serikali kuwa isipokuwa tayari kushughulikia malalamiko itawafanya Waislamu wapoteze imani yao kwa serikali.

"Hivi sasa Waislamu wa nchi hii hawana cha kupoteza ila unyonge wao iwapo vurugu itatokea", alihadharisha Sheikh huyo katika mkutano wake na Waandishi wa habari.

Kwa upande wake serikali haijaonekana kutaka kuchukua hatua yoyote kujibu hisia na malalamiko hayo ya Waislamu.

Uongozi wa awamu mbili za nyuma ulionekana kuwa na desturi ya kukaa kimya dhidi ya madai na malalamiko ya Waislamu wakati huo huo ukitekeleza kwa haraka kile ambacho kanisa na hasa Kanisa Katoliki ilichokihitaji.

Awamu ya tatu ilionesha dalili ya kutaka japo malalamiko hayo yafanyiwe utafiti wa kina kisha ushahidi wa kisayansi uyathibitishe.

Hata hivyo katika majibu ya Rais ilionekana kama kulikuwa na kukosea utaratibu uliozoeleka katika kuyapokea rasmi madai hayo.

Baada ya kimya cha miaka miwili baada ya kupokea madai ya Waislamu ghafla rais alitoa waraka uliodai kuwa matatizo ya Waislamu yanatokana na historia na kwamba serikali yake isingeweza kutekeleza hisia za kila mwananchi.

Hata hivyo pamoja na majibu hayo ya Rais baadhi wananchi wanaoitakia mema nchi yetu wameendelea kufanya kazi ya ziada kuandaa vitabu vinavyolichambua suala hilo kisomi kuthibitisha kile ambacho Waislamu wamekuwa wakikipigia kelele miaka yote.

Kitabu "Mwembechai Killings and the political future of Muslim in Tanzania" kilichozuiliwa uwanja wa ndege ambacho kinaelezea kwa kina tukio la mauaji ya Mwembechai na kukandamizwa kwa Waislamu katika Tanzania huru, wachambuzi kadhaa wa siasa za Tanzania wamekielezea kuwa ni miongoni mwa jitihada zenye uelekeo wa kuulinda uhuru wa nchi hii.

Kwa ajili hiyo wachambuzi hao wameonesha wasi wasi mkubwa juu ya hatima ya nchi hii iwapo serikali itakuwa na mwelekeo wa kukataa hata jitihada za kuonesha ushahidi wa madai ya ubaguzi na ukandimizaji.


Lipumba kufungua matawi 36 Tanga

MGOMBEA Urais kupitia Chama cha Wananchi (CUF) anatarajiwa kufungua matawi mapya 36 ya chama hicho katika maeneo ya kati ya Manispaa ya Tanga.

Taarifa ya chama hicho iliyotolewa mjini hapa imeeleza kuwa Prof. Lipumba atawasili mjini Tanga Julai 26 akitokea Dar es Salaam ambapo baada ya kufungua matawi hayo atafanya mkutano wa hadhara kwenye uwanja wa Tangamano.

Matawi yatakayofunguliwa na Prof. Lipumba yapo katika maeneo ya kata ya Mabawa matawi 9, Kata ya Makorora matawi 8, Mwakizaro pamoja na Duga matawi 12, Kata ya Bombo matawi 4 na kata ya Nguvumali matawi 3.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, Julai 26, Prof. Lipumba atakwenda kulala Muheza kwa ajili ya ufunguzi wa mkutano wa Baraza Kuu wa chama hicho utakaofanyika kuanzia Julai 27.

Tayari baadhi ya viongozi wa juu wa chama hicho pamoja na wajumbe mbalimbali wa mkutano huo wameanza kuwasili mjini Tanga.

Taarifa ya chama hicho imesema, Prof. Lipumba atapokewa kwenye eneo la Manga lililopo mpakani mwa Tanga na mkoa wa Pwani saa mbili asubuhi.

Wakati huo huo, gumzo la kuwasili kwa mgombea Urais kupitia Chama cha CUF Prof. Ibrahim Lipumba limetawala kila kona ya mji wa Tanga.

Mwenyekiti wa chama hicho wilaya ya Tanga Bw. Shekue Pashua amesema, watu mbalimbali wamejitokeza kutoa magari yao kwenda kumpokea Prof. Lipumba kwenye eneo la Manga Julai 26.


Mudir wa Ansaar Tanga asema kupiga kura ni kharamu


MUDIR wa Ansaar Sunna Tanga, Salim Barahiyan amerejea wito kwa wafuasi wake kuwa kupiga kura ni kharamu.

Kukaririwa kwa wito huo, kumejenga wasiwasi kuwa huenda kukaathiri idadi ya wafuasi wake watakaojiandikisha kupiga kura.

Akiongea Msikitini kwake Ijumaa iliyopita, Sheikh Salim ametoa changamoto kwa wenye kuhalalisha upigaji kura, waandae mdahalao waje na hoja zao.

Wito huo wa Mudir wa Ansaar kusisitiza ukharamu wa kupiga kura, umekuja wakati ambapo wanasiasa, jumuia na taasisi mbalimbali zisizo za kiserikali na viongozi wa kidini wamekuwa wakiwahimiza wananchi kufanya hima kujiandikisha na kupiga kura.

Baadhi ya wananchi waliosikiliza hotuba ya Mudir Salim, wamesema, wameshindwa kuona mantiki ya kuharamisha kuwachagua viongozi, lakini kuhalalisha kuwatii.

"Kama anaona kuchagua viongozi ni kharam, awe na ujasiri basi wa kutuambia tusiitii serikali. Vipi tuitii serikali ambayo tangu hapo ni haramu kuichagua?" amehoji Bw. Mbarouk.

Wakati huo huo, Mudir Salim amefafanua kuwa walilazimika kujenga ofisi ya CCM ili wapewe eneo la kupanua shule yao.

Katika toleo lililopita, gazeti hili lilieleza kuwa Ansaar Sunna ilijenga ofisi ya CCM Msambweni.

Habari hiyo ilifuatia maelezo ya diwani wa kata ya Msambweni mjini Tanga Bw. Kilo Rashid aliyoyatoa katika kikao cha upigaji kura ya maoni kilichofanyika hivi majuzi katika kata hiyo.

Katika kata hiyo Bw. Kilo alikuwa na wagombea wenzake wawili Bw. Mnyamisi na Bw. Mohamed Dhikri ambao walikuwa wakiwania kiti hicho cha udiwani.

Katika kujieleza kwa wapiga kura, Bw. Kilo pamoja na mambo mengine alieleza kazi aliyoifanyia kata hiyo kuwa ni pamoja na kufanikisha ujenzi wa ofisi ya CCM iliyojengwa na Ansaar Sunna.

--
JuuRUDI


Bonyeza hapa
kushriki mjadala au kutoa maoni juu ya habari hizi na masuala mengineyo ya Kiislamu kwenye Baraza ya Wasomaji

   Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu: Bonyeza hapa
Au
Andika barua  kwa: webmaster@islamtz.org
An-nuur Home | Ukurasa wa Mwanzo | Islam Tanzania
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook