KATIKA matoleo ya nyuma ya gazeti hili tuliona kwa urefu mada ya ushirikina. Kwa mifano hai tulionesha upotofu huo ulivyoota mizizi katika jamii zetu.
Katika sehemu hii ya mfululizo huu tutaanza kuangalia namna tunavyopaswa kumpwekesha Mwenyezi Mungu katika maisha yetu. Sehemu itakuwa chini ya mada Tawhiid.
Kimaana Tawhiid ni umoja au upweke wa Mwenyezi Mungu (s.w.). Kiistilahi Tawhiid ni fikra ya kimapinduzi inayolenga kumkomboa mwanaadamu kutokana na aina zote za utumwa kwa nafsi yake, kwa wanaadamu wenzie na viumbe vyengine.
Kutokana na sifa za Mwenyezi Mungu (s.w.), tulizozipitia, tunaweza kuuangalia umoja na upweke wa Mwenyezi Mungu (s.w.) katika sifa tatu zifuatazo:
(a) Tawhiid Al-Uluuhiyya (Upweke wa Mwenyezi Mungu (s.w.) katika Uungu wake)
Kumpwekesha Mwenyezi Mungu (s.w.) katika uungu Wake ni kutokuwa na Mungu mwingine yeyote wa kumuelekea kwa ibada au maombi isipokuwa Mwenyezi Mungu (s.w.) peke yake. Muumini wa kweli katika kukabili maisha yake ya kila siku anatakiwa awe na yakini na msimamo thabiti juu ya Umoja na Upweke wa Mwenyezi Mungu (s.w.) katika Uungu wake. Aya zifuatazo zinatufundisha hilo:
"Na Mungu wenu ni Mungu Mmoja tu, hakuna Anayestahiki kuabudiwa ila Yeye, Ambaye ni Mwingi wa Rehma, Mwenye Kurehemu" (2:163).
"Kwa yakini haya ndiyo maelezo ya kweli (haki). Na hakuna anayestahiki kuabudiwa ila Mwenyezi Mungu (s.w.) na kwa hakika Mwenyezi Mungu Ndiye Mwenye nguvu na Mwenye Hekima." (3:62).
Sema: "Yeye ni Mwenyezi Mungu Aliye mmoja tu. Mwenyezi Mungu ndiye anayestahiki kukusudiwa (na viumbe vyake vyote kwa kumuabudu kumuomba na kumtegemea). Hakuzaa wala Hakuzaliwa. Wala hana anayefanana Naye hata Mmoja." (112:1-4).
Aya hizi zote zinatuhakikishia kuwa Mwenyezi Mungu (s.w.) ni Mungu Mmoja tu. Asiyefanana na chochote na Ndiye pekee anayestahiki kuabudiwa, kuombwa na kutegemewa.
Tawhiid katika sifa za Mwenyezi Mungu.
Kumpwekesha Mwenyezi Mungu (s.w.) katika Sifa Zake ni kutomsifu Mwenyezi Mungu (s.w.) kwa sifa zisizo zake kama zilivyobainishwa katika Qur'an na kutomsifu yeyote au kiumbe chochote kwa sifa anazostahiki kusifiwa kwazo Mwenyezi Mungu (s.w.). Tumeshaona sifa za Mwenyezi Mungu (s.w.) kama zilivyobainishwa katika Qur'an na hadithi. Katika hizo kuna nyingine ambazo hapana kiumbe yeyote anayeweza kuwa na hata chembe ya sifa hizo. Kwa mfano hapana kiumbe yeyote mwenye sifa ya kuumba, kufisha, kutokuwa na mwanzo wala mwisho (umilele), kujua yaliyofichikana katika nyoyo za watu, na nyingine nyingi kama hizi. Kuna baadhi ya sifa za Mwenyezi Mungu ambazo viumbe wanaweza kusifika kwazo lakini katika kiwango cha chini kabisa. Kwa mfano binaadamu huona, husikia, huhurumia na husamehe nakadhalika, lakini sifa hizi ni katika kiwango cha chini mno. Ieleweke wazi kuwa uoni, usikivu, huruma na usamehevu wa mwanaadamu sio sawa na ule wa Mwenyezi Mungu (s.w.) kwa sababu mbili kubwa. Kwanza, Sifa hizo anazosifika kwazo mwanaadamu ni za mipaka finyu mno wakati sifa zote anazosifika kwazo Mwenyezi Mungu (s.w.) hazina ukomo. Kwa mfano uoni na usikivu wa Mwenyezi Mungu hauna kikomo. Yeye Anaona na kusikia kila kitu na hakuna chochote kilichomo mbinguni na ardhini kinachofichikana Kwake.
Muumini wa kweli baada ya kuzijua fika sifa za Mwenyezi Mungu (s.w.) hamtukuzi au kumsifu yeyote pamoja au kinyume na Mwenyezi (s.w.) Daima humtegemea na kumtarajia Mwenyezi Mungu (s.w.) katika kila hali ya maisha yake na humtukuza na kumsifu Yeye Pekee kama vifanyavyo viumbe vingine vyote vilivyomo mbinguni na ardhini. Rejea tena sifa za Mwenyezi Mungu (s.w.) zilizoorodheshwa katika aya (57:1-6) na (59:22-24).
Muumini wa kweli akizingatia sifa za Mwenyezi Mungu kama zilivyojitokeza katika aya hizi, atayakinisha kuwa ni Mwenyezi Mungu pekee anayestahiki kusifiwa na kutukuzwa katika kiwango cha hali ya juu kabisa.
(c) Tawhiid Rabbuubiyya (Upweke wa Mwenyezi Mungu
"Rabb" ni neno la Kiarabu lenye maana pana Ar-Rabb ni sifa ya Mwenyezi Mungu (s.w.) inayoonesha utawala na Ulezi wake juu ya viumbe. Katika Suratul-Faatiha, Mwenyezi Mungu (s.w.) Ameitwa "Rabbil-'aalamiina"
Bwana au Mfalme wa walimwengu ambaye ni Mlezi, Mlinzi, Mhifadhi, Mstawishaji na Muendelezaji wa kila kitu alichokiumba kilichomo mbinguni na ardhini. Ndiye Mwangalizi au Mlezi pekee wa kila kiumbe katika kila hatua ya maisha yake na Ndiye mwenye haki pekee ya kukitawala kila kiumbe kwa sharia yake. Kwa hiyo kumpwekesha Mwenyezi Mungu (s.w.) katika Ubwana na Utawala wake ni kutofuata utaratibu mwingine wowote wa maisha unaokwenda kinyume na utaratibu aliouweka. Muumini wa kweli ni lazima afungamane na sharia na utaratibu aliouweka Mwenyezi Mungu (s.w.) katika kuendesha maisha yake ya kila siku. Muumini wakweli hatarajiwi kufuata sharia yoyote ile inayokwenda kinyume na sharia ya Mwenyezi Mungu (s.w.) na wala hatarajiwi kuhukumu kinyume na sharia Aliyoiweka Mwenyezi Mungu (s.w.). Pia Muumini wa kweli hastahiki kumtii yeyote kinyume na kumtii Mwenyezi Mungu (s.w.). Utii wake kwa yeyote hauna budi kuwa katika mipaka ya aya ifuatayo:
"Enyi mlioamini! Mtiini Mwenyezi Mungu na Mtiini Mtume na wenye mamlaka juu yenu, walio katika nyinyi (Waumini wezenu). Na kama mkihitalifiana juu ya jambo lolote basi lirudisheni kwa Mwenyezi Mungu na Mtume Wake, ikiwa mnamuamini Mwenyezi Mungu na Siku ya Mwisho. Hiyo ndio kheri, nayo inamatokeo bora kabisa". (4:59).
Aya hii inatufahamisha wazi kuwa wanaostahiki
kutiiwa moja kwa moja bila ya masharti
ni Mwenyezi Mungu (s.w.) na Mtume
Wake. Wengine wote, Waumini wawatii.
--
![]()
|
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook |