MAKALA yetu ya leo imegawanyika katika mada mbili. Mada ya kwanza, inahusu maana ya lugha sanifu na katika mada ya pili, nitatoa ufafanuzi juu ya maneno yenye utatanishi katika Kiswahili.
Kabla sijaanza na mada yetu ya awali ni vizuri nieleze maana ya lugha kwa jumla. Lugha maana yake ni utaratibu mahsusi wa sauti, ishara na alama zinazotumika katika mawasiliano ya jamii.
Lugha hueleza hisia za watu katika harakati zao mbalimbali za kila siku katika siasa, uchumi, sayansi na kadhalika.
Kwa kawaida, mfumo wa lugha huambatana na maneno, maumbo yake na mpangilio wake, pia matamshi na matumizi ya maneno hayo. Lugha hukua hatua kwa hatua kulingana na maendeleo ya watu wanaoitumia na kurithiwa kutoka kizazi hadi kizazi.
Lugha huweza kuwa na lahaja mbalimbali. Lahaja ni tofauti za matamshi yanayotokea ndani ya lugha katika uzungumzaji wa watu wa sehemu moja na nyingine.
Kwa mfano katika Kiswahili kuna lahaja ya Kingozi, Kiamu, Kimvita, Kimtang'ata, Kimrima, Kiunguja na nyinginezo.
Lugha sanifu ni lahaja ambayo imeteulwa na kusanifiwa baada ya kukubalika iwe lugha rasmi ya mawasiliano kwa watumiaji wote wa lugha hiyo.
Lugha sanifu ndiyo inayotumika katika nyanja zote rasmi za mawasiliano.
Inaelezwa kuwa lahaja ya Kiunguja kwa upande wa Kiswahili ndiyo iliyoteuliwa kuwa lugha rasmi ya mawasiliano kwa vile imeenea sana katika pwani ya Afrika Mashariki.
Hata hivyo, kuteuliwa kwa lahaja moja kuwa lugha rasmi hakumaanishi kutotumika tena kwa lahaja nyingine ambazo zimetapakaa katika mwambao wa Afrika Mashariki. Lahaja hizo bado zinazugumzwa. Kwa mfano watu wa Mvita huongea Kimvita, watu wa Mtang'ata huongea Kimtang'ata na watu wa Mrima huongea Kimrima.
Sasa tuje katika mada yetu ya pili inayohusu maneno yanayotatanisha katika Kiswahili.
Ifuatayo ni orodha fupi ya maneno ambayo matumizi yake hutatanisha watu wengi na hivyo kuyatumia kwa makosa.
Maneno hayo ni mashaka na shaka. Onyesha na onesha, tokea na tukio, mazingara na mazingira, tegemea na egemea, yoyote na yeyote, tegemea na tarajia.
Si sahihi kusema "nina mashaka kuwa Omari hatafika".
Sahihi ni "Nina shaka kuwa Omari hatafika".
"Shaka" ni hali ya kuonesha wasiwasi, hali ya kutokuwa na yakini juu ya jambo fulani wakati "mashaka" ni hali ya taabu. Neno "mashaka" si wingi wa "shaka" kama wengi wanavyodhani. Shaka na mashaka ni maneno yenye maana tofauti.
Si sahihi kusema; "Juma alinionyesha nyumba aliyojenga".
Sahihi; "Juma alinionesha nyumba aliyojenga".
"Onyesha" ni kuonya kwa kitu kama kioo. Hutumika kwa kitu chochote kinachowezesha nuru ya macho kupenyeza upande wa pili wa kitu hicho. Kwa mfano "nguo hii naonyesha/inaonya haifai kuvaa". Maana ya pili ya kuonya ni kutahadharisha.
Si sahihi kusema "katika tokeo hilo mtu mmoja aliuawa".
Sahihi ni: "Katika tukio hilo mtu mmoja aliuawa.
"Tokeo" ni neno linalotokana na "toka" linaponyumbuliwa hubadilika na kuwa tokeo, tokeo, tokewa na kadhalika. "Tokeo" ni mustakbala wa "kutokea" wakati "tukio" ni neno linalotokana na "tuka" yaani kujiri kwa jambo.
Si sahihi kusema "wananchi tunatakiwa kuweka mazingara safi".
Sahihi ni "wananchi tunatakiwa kuweka mazingira safi". Mazingara na mazingira ni maneno yenye maana tofauti japokuwa watu wengi huyatumia kwa maana moja. Kwa kifupi "mazingira" maana yake ni mandhari au hali ya nchi au mahali wakati "mazingara" ni mambo yasiyo ya kawaida machoni kwa mtu. Huweza kuitwa mazingaombwe, kiini macho au uchawi.
Si sahihi kusema "Masudi alianguka baada ya kutegemea ukuta mbovu".
Sahihi ni "Masudi alianguka baada ya kuegemea ukuta mbovu". "Kutegemea" maana yake ni kuweka tumaini la kupata msaada fulani au pato fulani wakati "kuegemea" ni kuegesha mwili au sehemu ya mwili kwenye kitu kingine.
Si sahihi kusema "tulitegemea Faki angerudi leo".
Sahihi ni "tulitarajia Faki angerudi leo".
Si sahihi kusema "Hairuhusiwi kwa mtu yoyote kukaa hapa".
Sahihi ni "Hairuhusiwi kwa mtu yeyote kukaa hapa".
"Yoyote" inaweza kutumika kwa vitu mbalimbali kwa mfano: gari yoyote, nyumba yoyote na kadhalika. Kulingana na upatanisho wa kisarufi "yoyote" haiwezi kutumika kwanafsi ya mtu.
|
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook |