KURA ni kitendo cha kumchagua kiongozi ambaye wewe binafsi unaona atafaa kuongoza jamii katika ngazi fulani. Kitendo hicho hufanyika mara moja baada ya muda fulani kufuatana na jinsi mlivyojipangia wenyewe kisheria. Inaweza kuwa kila baada ya miaka mitatu au mitano kutegemeana na matashi yenu.
Nchini mwetu hivi sasa wakati wa kupiga kura umekaribia. Apendapo Mola ifikapo Oktoba 29, 2000 itakuwa ni siku ya uchaguzi wa kitaifa kwani tutachagua Madiwani, Wabunge na Rais wa nchi yetu. Hawa tutakaowachagua ndiyo tutakuwa tumewapa dhamana ya kuendesha na kuiongoza hii nchi kwa miaka mitano mfululizo. Miongoni mwao tutakuwa na Rais na Mawaziri wake, Wabunge na Madiwani. Kwa msingi huo basi huu uchaguzi ni wa muhimu sana kwetu sote kwani hapa ndipo tutapata serikali yetu na hatima ya nchi utawakabidhi wao tutakaowachagua.
Ndugu mwananchi, hii ni nafasi muhimu katika maisha yako wewe, familia yako na nchi yako. Kwa mustakabali mwema na maendeleo ya nchi yetu ni vyema kukitumia kipindi hiki vizuri na bila kukosa. Hatima ya nchi yetu iko mikononi mwetu wananchi. Tunavyotaka nchi yetu iwe ni jukumu letu kupanga iweje. Huku kunawezekana tu kwa sisi wananchi kuitumai fursa hii ya kupiga kura vyema bila kukosa. Hapo ndipo tutaweza kuweka viongozi tunaowataka na kuwaondoa wale tunaoona ni wabovu na wenye ubinafsi. Ili tusije kuwa ni watu wenye kujuta baadaye ni vyema kufanya uchaguzi kwa makini kwa kuwapima wagombea wetu kwa umakini bila kufuata au kusikiliza propaganda au vitisho vyovyote kutoka kwa wale wenye tamaa na ubinafsi katika uongozi.
Katika kupiga kura kuna hatua ya mwanzo ambayo ni kujiandikisha kwanza katika wakati uliopangwa na vyombo vinavyohusika. Hiki ni kipindi muhimu, kwani bila kujiandikisha huwezi kupiga kura. Wakati ukiwadia ni lazima kuwahi kujiandikisha ili uweze kupiga kura yako ifikapo Oktoba 29.
Baada ya kujiandikisha, kunafuatia kipindi cha kampeni. Hapa ndipo wagombea wote huanza kujieleza sera na malengo yao pindi watakapopata uongozi. Kawaida katika kipindi hiki wagombea wote huwa ni watu wenye ahadi nyingi na nzuri ingawa wengi wao hutoa ahadi za uwongo ili kutudanganya wakishapata hizo kura hawana cha kutufanyia zaidi ya kujali nafsi zao tu. Kipindi hiki wengi pia huanza kudiriki kutoa zawadi na pesa ili kuwarubuni wapiga kura wawape kura.
Utoaji na upokeaji wa zawadi na pesa hizo ni rushwa iliyodhahiri. Wananchi hatunabudi tuelewe kuwa kura zetu ni gharama kubwa mno kwako mpokeaji, kwa familia yako na kwa taifa zima kwa ujumla. Muda wa kupiga kura tena ni baada ya miaka mitano, kama umechaguwa kiongozi mbovu ina maana tumekula hasara ya kusubiri mpaka muda huo wote uishe. Hapo tutakuwa tumejikwamisha kwa zaidi ya miaka hiyo mitano kwani kama ilikuwa tupige hatua mbele tutakuwa tumesimama hapo hapo au kurudi nyuma, kwani dunia inasonga mbele na teknolojia zinaenda zikibadilika hivyo sisi tutaendelea kusota.
Kwa faida ya kura yako hakikisha haumchaguwi anayetoa zawadi au pesa kwani huyo ni bomu ambalo litakupasukia akisha shika madaraka. Hatajali wananchi wala nchi yake, kazi yake itakuwa ni kurudisha pesa zake kwa faida kwani alikuwa anafanya biashara ya kura. Hakuna biashara bila faida. Nchi yetu sote tunaijua ilipofikia na nani kaifikisha hapa na nini kimetufikisha hapa, hivyo basi tusifanye tena mchezo na hizo wanatamka kuwa wanaipinga, na wataipiga vita rushwa. Lakini kimatendo wao wenyewe ndiyo nambari wani kwa kuomba na kupokea rushwa la sivyo wasingenunua kura kwa rushwa za vizawadi na pesa.
Ombi maalum kwa kina mama, eleweni kuwa kura yako ni mali yenye thamani kuliko lulu, almasi au dhahabu. Mwanao, mjukuu wako utawainua kwa kura yako au utawakandamiza kwa kura yako. Uongozi mbovu maana yake ni kwamba serikai mbovu na ndiyo kurudi nyuma au kukwama au kudidimia kwa kila kitu. Je na wewe hutaki elimu, afya, matibabu kwa mtoto wako? Je wewe hutaki urahisi wa maisha yako kwa kuwa na barabara nzuri wepesi wa kufanya biashara zako? Je, wewe hutaki kodi zinazokuletea maendeleo yako ya jamii? Je, wewe hutaki ustawi wa jamii? Je, wewe hutaki haki sawa kwa kila raia bila ubaguzi wa rangi, dini, kabila, utajiri au umaskini? Je, wewe hutaki haki zako za uraia zilizowazi? Kama majibu unahitaji, basi usikubali kurubuniwa na vizawadi vya khanga na kilo mbili za sukari na mikopo uchwara ya shilingi 20,000 eti uondoe umaskini kwa mtaji wa shilingi 20,000 ili uwape kura yako.
Hakuna anayeweza kutukomboa au kutuletea kiongozi bora ila ni sisi wenyewe kwa kutumia kipindi cha kupiga kura vizuri kwa kumchagua kiongozi anayejali watu na matatizo yao anayetambua shida na matatizo ya watu na mwenye nia ya kutatua shida zao na mpenda maendeleo ya watu wote sio wale wenye kujipendelea wao wenyewe na jamaa zao bila kujali wala kuwafikiria wengine. Sio wale wenye kugawa keki yetu ya taifa kwa baadhi ya watu au sehemu na hali wengine wakibaki kukodolea macho wenzao wanavyoneemeka wakati wao wakibaki hoi.
Pia tuwachague wale kweli wenye uchungu na nchi hii sio wale wenye kukodisha viwanja vyetu vya ndege kwa kodi ya Dola 1000 kwa mwaka au wenye kutoza kodi za migodi ya dhahabu kwa dola 3 katika kila dola 100. Tuchaguwe wale kweli wenye uwezo wa kutufanya tuweze kuutumia utajiri wetu wa nchi aliotujalia Mwenyezi Mungu.
Wananchi imefika wakati wagombea uongozi watambue kuwa kura zetu ni ghali mno kwao kuweza kuzinunua hivyo wasipoteze muda na pesa zao bure. Tunachotaka kutoka kwao ni kazi na matendo ya maendeleo sio maneno na ahadi za pwagu.
|
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook |