Kitendawili kimeteguliwa

KILE kitendawili cha hafai huyu ana udini sasa kimeteguliwa. Hivyo kila kitu kiko wazi mwenye akili na aelewe. Ni muda mrefu sana tumekuwa tunasikia suala la watu fulani hawafai kuchaguliwa kwa sababu watatulea udini nchini mwetu, na hivyo kutuletea ghasia na machafuko yatakayopelekea kuvuruga amani tuliyoizoea kwa muda mrefu sana.

Tumekuwa tikihimizwa kuchaguwa viongozi wacha Mungu lakini sio wenye udini kwa usalama wa amani na utulivu. Tumeimbiwa nyimbo nyingi na kutolewa hotuba nyingi toka kwa viongozi mbalimbali toka wa ngazi ya kitaifa mpaka chini.

Wakati tukiambiwa hivi wengi tulielewa kuwa mwenye udini ni mtu yeyote mwenye kuwa na tabia ya kufanya mambo ya uongozi kwa upendeleo dhidi ya dini nyingine iliyotofauti na yake. Hivyo basi anaweza kuwa Muislamu au Mkristo. Huo wimbo tuliuona ni mzuri kwani ulionesha kweli una nia ya kulinda amani yetu katika nchi. Tuliitikia sote wimbo huo tena kwa mkazo sana na kuanza kuufanyia kazi.

Waislamu tulianza kusema sehemu au maeneo tuliyoona yana walakini huo ili kutekeleza sera hiyo kwa faida ya nchi yetu. Kwenye elimu tukaeleza wapi tunaona mambo hayaendi sawa. Kwenye maofisi tukaeleza vipi tunaona haki haitendeki na nini kifanyike ili kuleta usawa wa wafanyakazi wote wa ofisini.Kuhusu uteuzi wa viongozi mbalimbali kuanzia ngazi ya kata mpaka taifa, tukaonesha pale tulipoona haki haikutendeka ili parekebishwe kwa sababu sote tunajua kuwa tunapigana vita juu ya udini ambayo ni mbaya na ina athari mbaya na ya muda mrefu ikiachiwa iwepo.

Ingawa wimbo huo unaimbwa mpaka sasa, lakini kile kilichosemwa na Waislamu kilitupwa chini na kupata majibu kuwa hatuwezi kugawa vyeo kwa upendeleo, mkitaka vyeo someni kwanza ndipo mtapata. Zaidi ya hayo vyeo havigawiwi kwa kuangalia dini, tunagawa tu kwa kufuata uwezo wa watu hivyo hapa suala la udini halipo.

Sasa umefika wakati wa uchaguzi mkuu wa Urais, Wabunge na madiwani. Uteuzi wa wagombea mbalimbali umeanza kwa wenye kutaka kugombea kuchukua fomu. Pia mikakati mbalimbali kuhusu uchaguzi imeanza kuandaliwa na vyama mbalimbali. pamoja na jitihada zilizoanzwa kufanywa na hivyo vyama, kama kutafuta ushirikiano katika uteuzi wa wagombea wao, kumeibuka pia lawama kuhusu uteuzi huo kutoka kwa viongozi na watu mbalimbali kutoa malalamiko yao na hata kejeli kwa hao wagombea.

La ajabu sasa wanadai wagombea wa vyama kama CUF na CHADEMA wana sera za udini kwa sababu tu wagombea wao wa Urais ni Waislamu, hivyo wataifanya nchi iwe na viongozi wa juu wote Waislamu na hiyo ni hatari kwa nchi kutawaliwa na watu wa dini moja tu wakati nchi hii ina dini nyingine. Napata mashaka kutoamini kama mwaka 1995 katika uchaguzi mkuu sera hii haikutumika. Kwani kuna sababu nyingi zisizo za msingi zilizotolewa kwa baadhi ya wagombea ambao walikuwa Waislamu ili wasichaguliwe kwenye kinyang'anyiro cha Urais.

Hiyo hoja sasa imetudhihirishia ukweli kuwa ukisikia udini jua ni Uislamu. Kwa msingi huo haitakaa hata mwaka mmoja kwa Muislamu wa Bara akawa Rais wa Tanzania, kwani mgombea mwenza kwa sheria lazima atoke Zanzibar na kwa hali hiyo atakuwa Muislamu na mgombea wa Zanzibar atakuwa Muslamu kutokana na hali hiyo italazimu Muislamu asigombee ili kuepuka hali kama hiyo kujitokeza hata kama Muislamu huyo ana uwezo au anapendwa na wananchi kwa kiasi gani.

Lakini inatubidi tuhoji hivyo kosa hilo au ubaya huo ni kwa Waislamu tu? Au hata kwa upande wa dini nyingine? Mbona ukiangalia mfumo uliopo sasa umehodhiwa na viongozi wa Kikristo kwa zaidi ya asilimia 80 hapo hakuna ubaya au hofu yoyote kwa nchi yetu?

Hata hiyo miaka ya uongozi wa Mwalimu tulipokuwa na yeye Mwalimu kama Rais, Marehemu Sokoine Waziri Mkuu, Mkuu wa majeshi, Mwanasheria Mkuu, Gavana wa Benki Kuuu, wakurugenzi wa mashirika mbalimbali ya umma, wakuu ya idara za serikali, wakuu wa mikoa na wilaya, wakuu wa shule na vyuo, na sehemu nyingine mbalimbali, wote hao walikuwa Wakristo, mbona akina Cheyo hamkukemea hatari hiyo kwa nchi?

Katika kipindi au vipindi vyote hivyo sisi Waislamu tulijua kuwa hao viongozi waliwekwa tu kwa sababu ndio wenye uwezo wa kufanya hiyo kazi, lakini hatukufikiria kabisa kama dini zao zilikuwa ndiyo kigezo cha kuchaguliwa kwao na hivyo hatukuwa na wala hatukuona kama kuna hatari yoyote kwa nchi yetu kama wanaonavyo hivi sasa ndugu zetu akina Cheyo na wenzake.

Kama Waislamu tulikubali kuwa hii nchi ni yetu sote na sote tuna haki ya kuiendeleza kwa njia mbalimbali pamoja na kutoa mchango wa uongozi kwa mwenye kuweza iweje ninyi wenzetu msikubali ukweli huo na kutoa nafasi kwa kila mwenye uwezo wa kuongoza aongoze kwa faida yetu na vizazi vyetu vijavyo?

Suala la hatima ya nchi ni letu sote, si la baadhi ya watu wa dini fulani hivyo basi nyie wote wenye mtazamo finyu wa kimawazo tunawaomba muepukane na ubinafsi na muanze kuipenda nchi yenu kwa kukubali kuwa hamko peke yenu katika hii nchi ila pia na watu wengine wapo na wana haki sawa na nyie bila kujali ni Muislamu au Mkristo au mpagani cha msingi ni je anao uwezo wa kuwa kiongozi? Masuala ya vigezo vya dini zao ni misikitini au makanisani au mizimuni sio katika uongozi wa hii nchi.

Watanzania tusipoangalia hawa watu kama Bwana Cheyo na wenzie watatufikisha kule waliko Warundi na Wanyarwanda kwa kupenda kubaguana mwisho wakaishia kwenye kuuana.

Napenda kuwaomba wale viongozi wote wenye tabia ya kupenda kuhutubia na kujitia kusema kuwa chama fulai hakifai kina udini kwa sababu tu viongozi au wagombea wa chama hicho ni Waislamu, umefika wakati sasa wa kuacha mahubiri hayo kwani hatupendi wananchi kulishwa sumu mbaya kwa huo mchezo wa ubinafsi wa hivi sasa usije ukatuletea mauti ya baadaye. Tuseme lilo la kweli. Kiongozi kama hafai aelezwe matatizo yake asisingiziwe vitu visivyoendana na uongozi. Tunachohitaji ni sera na kama chama kweli kina viongozi wanaojali wananchi wake na siyo mambo binafsi ya dini zao.

--
JuuRUDI


Bonyeza hapa
kushriki mjadala au kutoa maoni juu ya habari hizi na masuala mengineyo ya Kiislamu kwenye Baraza ya Wasomaji

   Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu: Bonyeza hapa
Au
Andika barua  kwa: webmaster@islamtz.org
An-nuur Home | Ukurasa wa Mwanzo | Islam Tanzania
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook