BARUA

Msituletee mchezo wa 'karata tatu'

Ndugu Mhariri

KWA muda mrefu sasa Waislamu tumeilalamikia serikali ya Tanzania kwa kule kuwapendelea Wakristo kwa kuwapa nafasi za juu katika serikali na kuwaacha Waislamu.

Tulijibiwa kuwa Wakristo wamepewa nafasi za juu serikalini sio kwa ajili ya upendeleo wa kidini, bali ni kwa sababu Wakristo wamesoma na wana elimu kubwa kuwashinda Waislamu.

Tulifikiwa kuambiwa: "Nyinyi Waislamu hamkusoma halafu mnataka kuongoza nchi. Nyinyi mmesoma Qur'an, huwezi kuongoza nchi au kupewa nafasi ya juu serikalini kwa kisomo cha Qur'an. Someni kama wenzenu Wakristo".

Baada ya kejeli hizo, amejitokeza Muislamu (Prof. Ibrahim Lipumba) ambaye ni msomi kuwashnda kina John Cheyo, Mkapa na Augustine Mrema. Wameanza kutuletea mchezo wa "karata tatu". Elimu si kigezo tena.

Julai 14, mwaka huu katika uwanja wa Tangamano hapa Tanga, mgombea Urais kwa tiketi ya TLP Bw. Augustine Mrema alisema: "Rais sio lazima we msomi bali ni yule anayekubalika na wananchi".

Haya si maneno ya Mrema ni bali ni maneno ya watalaamu wa Kikristo - Tanzania. Katika kitabu chao kiitwacho "Uchaguzi wa Kisiasa kwa nini tujali? wanasema: "Sifa ya kiongozi si kuwa msomi wa Diploma na anayejua mengi..." Uk. 17.

Nyinyi hamna haya? Mara mnasema mnapewa uongozi kwa sababu ya usomi wenu, mara kiongozi sio lazima we msomi. Sasa tushike lipi? Hivi Lipumba angekuwa Mkristo mngelithubutu kutamka maneno haya? Acheni ujanja ujanja kama ule wa "karata tatu".

Wapo Waislamu wengi ambao wana elimu ya Chuo Kikuu lakini wameishia kuuaza nyanya na kukodisha baiskeli.

Akina Dk. Msabaha pamoja na visomo na Ubunge wao wametelekezwa.

Ninatoa changamoto nielezwe elimu za Mawaziri kuanzia Waziri Mkuu.

Basi itoeni CV (Curriculum Vitae) zao hadharani.

Ibn Rashid,
Tanga.
Kaima Mwanjia,
S.L.P. 2084,
Tanga.



Mrema mpinzani wa upinzani

Ndugu Mhariri

Niweke japo pembeni ya gazeti lako tukufu niwazindue wananchi wa Tanga na Tanzania nzima kuhusu huyo Mrema.

Kwanza, Mrema si mpinzani wa kweli, hili limedhihirika kwenye mkutano wake wa hadhara alioufanya Tangamano ameigeukia kambi ya upinzani ambayo yeye mwenyewe yumo na kukishambulia chama fulani cha upinzani pamoja na kiongozi wake wa kitaifa.

Sasa yeye Mrema ni mpinzani wa chama tawala (CCM) au ni mpinzani wa upinzani? Ndio nikasema huyu Mrema ni CCM B tena ni muuaji wa upinzani.



Vyombo vya habari si vya Taifa bali vya CCM

Ndugu Mhariri

SERIKALI inatudanganya pale inaposema kuwa RTD na TVT ni mali ya Taifa. Haiwezekani mali ya taifa lote la Tanzania aitumie mtu mmoja.

CUF, TLP, CHADEMA, NCCR na kadhalika wanaruhusiwa kuvitumia vyombo hivyo?

Maana sisi tulio huku mikoani na vijijini hatusikii habari ya vyama vingine ila CCM.

Sisi tulio mikoani tukitaka kujua habari ya vyama vingine hadi ufungulie sauti ya Ujerumani au BBC London, kinyume cha hapo, ziro. Hivyo ndio usawa huo?

Leo mjumbe wa shida wa CCM hata kama ana shughuli ya ngoma ya kutoa wanawe, RTD na TVT vitatangaza na kutuonyesha mpaka shughuli inaisha.

Rashid A. Lioche,
S.L.P. 4,
Kilwa Kiwawa.


Jeshi litazame upya agizo hili

Ndugu Mhariri

VIONGOZI mbalimbali serikalini wamekuwa na tabia ya kuwasema Waislamu mara kwa mara kuwa wana udini. Tukashindwa kuelewa udini maana yake ni nini.

Baadaye tukagundua kuwa udini maana yake ni Uislamu. Hili linadhihirika katika hoja zifuatazo:

Julai mwaka 1999, Prof. Kapuya alipozungumza bungeni kuwa wanafunzi wa Kiislamu waruhusiwe kuvaa Hijab na kuswali swala ya Ijumaa, Wabunge wenzake walimjibu kuwa huo ni udini.

CUF ina udini kwa sababu Mwenyekiti, Makamu wake na Katibu Mkuu ni Waislamu. Lakini CCM haina udini hata kama Mwenyekiti, Makamu wake na Katibu wote ni Wakristo.

Siku hizi bondia Mike Tyson ana udini anapoingia ulingoni kwa ajili ya mapambano, yaani analeta Uislamu.

Watanzania hasa Wakristo wanamsifu Nyerere kuwa alifanikiwa kuondoa udini, yaani Uislamu ndani ya chama cha TANU.

Ni kweli kwa sababu Machi 1963 Nyerere alivunja Baraza la Wazee la TANU lililoongozwa na Sheikh Idd Tulio.

Baraza hili lilikuwa na wajumbe 173 na wote walikuwa ni Waislamu.

Nyerere alilivunja hili na akaanza kujenga himaya ya Wakristo katika TANU na kisha CCM.

Hi ndio tafsiri na taarifa ya neno udini.

Bin Liguo,
S.L.P. 2318,
Tanga.


Jeshi litazame upya agizo hili

Ndugu Mhariri,

Limetolewa agizo kwetu wanajeshi kwamba hairuhusiwi kwa mwananjeshi kuingia katika jengo la ibada kwa ajili ya kufanya ibada akiwa amavaa sare ya kijeshi.

Sababu iliyotolewa ni kwamba uvaaji huo umekuwa ukileta hisia mbaya kwa raia.

Kufuatia uamuzi huo Sisi maafisa wadogo, maafisa wakubwa na wapiganaji wengine wa jeshi la wananchi wa Tanzania tunaofuatilia imani zetu za dini tumechanganyikiwa.

Tumechanganyikiwa kwa kuwa huku kambini hakuna majengo wala maeneo yliyotengwa kwa ajili ya ibada ambayo yangetuwezesha kufanya ibada tukiwa na sare zetu bila ya kuchanganyika na raia wa nje ya kambi.

Na tuliochanganyikiwa zaidi ni sisi tulio Waislamu ambao tunatakiwa tuabudu kutwa mara tano. Zaidi ya hivyo kuna swala ya Ijumaa ambayo imepewa msisitizo wa pekee kwa muislamu kuhudhuria msikitini. Ni wazi agizo hilo limetuweka njia panda ya ama kubeba nguo za kiraia tuendapo maofini, ambayo ni hali inayoweza kuibua hisia nyingine baadaye, ili muda wa swala za adhudhuri au alasiri tuhudhurie ibada, au tuvikose kabisa vipindi hivyo ambako ni kupingana na imani ya dini yetu.

Kwa mujibu wa mafundisho ya Uislamu swala ni nguzo kuu katika nguzo zinazosimamisha itikadi ya kiislamu, kutoitekeleza nguzo hiyo ni sawa na kuiangusha dini ambao ni uasi unaomuelekeza mtu motoni kwa mujibu wa mafundisho haya.

Kwa hiyo Wanajeshi tulio Waislamu tunaona agizo hili litatuathiri zaidi kuliko wenzetu wakristo kwa sababu wao huabudu jumapili na kwa mujibu wa utaratibu wa kinchi siku hiyo ni ya mapumziko.

Jeshi letu kama lilivyo jina lake ni jeshi la wananchi wa Tanzania ambao wana mila, desturi na imani zao ambazo katiba ya nchi imezitambua na kuziheshimu na zaidi ndizo chimbuko la katiba yenyewe, ispokuwa zile zinazokwenda kinyume na utu au maslahi ya wanajamii wote.

Hata aliyekuwa Amiri jeshi mkuu wa kwanza hayati mwalimu Nyerere alipata kusema katika hotuba zake ya kuwa yeye anafurahi sana anapowaona watanzania wanaabudu katika dini zao.

Kwa hiyo ningependa kuwasilisha ombi rasmi kwenu viongozi wetu wa juu wa jeshi kuwa agizo hili linaathari kubwa sana kiimani na kidini hivyo kwa hekima na busara zenu na kwa kutumia uwezo mlionao naomba mpitie tena uamuzi huu ili nasi Wanajeshi kama ilivyo kwa wananchi wengine wa nchi hii tupate fursa ya kutekeleza maamrisho ya dini zetu kwa mujibu wa katiba ya nchi.

Mwanajeshi muathirika
Tabora
--
JuuRUDI


Bonyeza hapa
kushriki mjadala au kutoa maoni juu ya habari hizi na masuala mengineyo ya Kiislamu kwenye Baraza ya Wasomaji

   Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu: Bonyeza hapa
Au
Andika barua  kwa: webmaster@islamtz.org
An-nuur Home | Ukurasa wa Mwanzo | Islam Tanzania
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook