MAONI YETU
Tusikubali uzuzu

MTU mmoja aliyejitambulisha kama msomi toka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam alifika Shinyanga hivi karibuni na kukutana na b'aadhi ya viongozi wa taasisi za Kiislamu.

Bwana huyo alidai kuwa kafika mkoani hapo kufanya utafiti. Utafiti gani? Kutaka kujua iwapo ipo dhulma dhidi ya Waislamu kama wenyewe wanavyodai.

Alipoulizwa lengo na matumizi ya utafiti, akadai kuwa utatumika kuishauri serikali.

Hata hivyo, makabrasha ya maswali dodoso aliyokuwa nayo yalichimba kutaka kujua undani zaidi wa Taasisi za Kiislamu kuliko utafiti aliotaja.

Pamoja na dosari hiyo wenyeji wake hawakukosa kumfanyia ukarimu. Walimpa maelekezo ambayo yangefanikisha zaidi utafiti wake tena kwa wepesi.

Kwanza walimuelekeza akasome kitabu "The Killings of Mwembechai" ambacho bado kimezuiliwa uwanja wa ndege. Kama atazuiliwa kukisoma basi aanzie hapo utafiti wake. Kwanini kitabu hicho kizuiliwe! Kina nini? Kwani hapakutokea mauaji Mwembechai?

Lakini la pili, walimtaka aende kwa Mwanasheria Mkuu wa serikali, Mwendesha Mashitaka Mkuu wa Serikali (DPP) na kwa Mkurugenzi wa Upelelezi (DCI) akaulize nini kimetokea katika sheria na katiba ya nchi mpaka leo wale walioua Waislamu pale Mwembechai hawajafikishwa mahakamani!

Awaulize pia ilikuwaje serikali ikachukua maamuzi mazito hadi kuua kwa shinikizo la uchochezi wa Paroko Lwambano.

Je, zile 'Balozi za nje' walizoziandama badala ya Paroko Lwambano washazichukulia hatua?

Kuhusu iwapo upo ubaguzi katika ajira au elimu walimtaka aende Wizara husika.

Huko ndiko kuna mafaili yatakayomuonesha Waislamu waliodumazwa wakasalia bila kupanda ngazi pamoja na elimu, na uzoefu wao.

Ni ushauri mwingi tu, walimpatia 'mtafiti' huyo, lakini kwa ujumla wake walimwambia data ziko serikalini.

Walioshikilia serikali wanajua kila kitu na hawana haja na data. Wakidai basi ni kutaka tu kuwapumbaza watu.

Haiwezi kuwa vinginevyo zaidi ya kuwalaghai watu, wajazane watu wa dini moja kwenye ofisi au chama halafu hao hao wajisifu kupiga vita udini na kuwakemea wengine.

Sisi tunadhani majibu na maelekezo yaliyotolewa na viongozi hawa wa Kiislamu Shinyanga 'swadakta'.

Yawezekana watu kama hawa wanazunguka sehemu nyingine nchini.

Hatuoni ni majibu gani munasibu wanayoweza kupewa zaidi ya haya waliyopewa huko Shinyanga.

Ukihisi ni fursa adhimu kuelezea madhila ukidhani wao hawajui. Wenzio wanakuona tu zuzu.

--
JuuRUDI


Bonyeza hapa
kushriki mjadala au kutoa maoni juu ya habari hizi na masuala mengineyo ya Kiislamu kwenye Baraza ya Wasomaji

   Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu: Bonyeza hapa
Au
Andika barua  kwa: webmaster@islamtz.org
 
An-nuur Home | Ukurasa wa Mwanzo | Islam Tanzania 
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook