Tujifunze kutoka kusadikika

KATIKA makala haya tunajaribu kwa tawfiq ya Allah (s.w.) kuonesha namna ambavyo mwanadamu amekuwa kwa zama zote mpinzani mkuu wa haki, usawa na ukweli. Kadhalika tunakumbusha harakati za mwanadamu kuzuia haki isitendeke na njia alizozitumia. Pamoja na hayo ipo pia haja ya kubainisha mbinu zilizotumika zama zilizopita zinavyotumika leo na hivyo kuthibitisha kujirudia kwa historia.

Watu wanaoisoma historia ya mwanadamu na ambao wana tabia ya kuukubali ukweli unapodhihiri, hawataona tabu kukubali kuwa, tukio kuu lililotokea karne ya 7 A.D. ni moja ya alama kuu za historia ya mwanadamu.

Hilo si geni kwa wanahistoria kuwa mwaka 610 A.D. karne ya saba Mwenyezi Mungu alimuinua kijana wa Kiarabu miongoni mwa jamii iliyoparaganyika kwa kiza cha ujinga, dhulma na ukandamizaji wa wanadamu wenyewe kwa wenyewe.

Tukio hilo ni kule kuletewa Muhammad (s.a.w.) wahyi. Katika ufunuo huo, aliagizwa awe ni rehema kwa walimwengu wote kwa kuwatoa katika lindi la ujinga na kuwaelimisha juu ya haki zao kwa kuwafudisha njia sahihi ya maisha. "Na hatukukutuma ila uwe rehma kwa walimwengu wote". (21:107)

Historia inatuonesha kuwa, wanadamu wamekuwa wakitawaliwa tangu zamani. Kwa kawaida watu waliobobea katika utawala wa ukandamizaji na uonevu, hawatoi fursa kwa yeyote kujaribu kuwaonesha watawaliwa haki zao wanazostahili katika jamii yao.

Baya zaidi ni pale ambapo mmoja au kundi litajitokeza bayana kwa nia ya kuwaongoza watu katika kujikomboa kutokana na dhulma na ukandamizaji. Atakayethubutu atapambana na nguvu za watawala. Hiyo ndiyo hali iliyomkuta Mtume (s.a.w.) pamoja na mitume wote. Historia inatukumbusha dharau na kejeli alizofanyiwa Mtume (s.a.w.) na ami yake Abu Lahab kama ilivyobainishwa katika Qur'an 111:1-5.

Kadhalika historia inatufundisha kuwa, pamoja na dharau, makeo na kejeli alizofanywa Mtume, haikuwa sababu ya kuficha ukweli. Basi akawa amejipinda katika kuwalingania watu juu ya ujumbe wa haki hali iliyopelekea wakuu wa jamii hiyo nao kubuni mbinu zaidi za kuzuia haki kwa njia ya mafundisho ya viumbe wao.

Njia kuu zilizotumika katika kuzima wimbi la kuelimika jamii ni pamoja na kuwadhalilisha kwa maneno ya kashfa wale wanaoiongoza jamii kufikia haki. Mfano ni ile hali iliyojitokeza kutokana na Abu Lahab. Lakini baada ya kubaini kuwa njia ya kumdhalilisha haikufua dafu, na ujumbe ukawa unaenea kama moto nyikani, zilibuniwa njia nyingine, zikiwa ni kuzungumza sifa za uongo juu yake. Kuweka wajumbe kila kona ya mji ili kuwatahadharisha waingiao wasimsikilize Mtume.

Walidanganywa kuwa yeye mwendawazimu, muimba mashairi na mdanganyifu wa jamii. Waliambiwa pia wakimuona anasema lolote wazibe masikio yao ili wasisikie maneno yake kwani yanatia sumu katika vichwa vya watu. Hatimaye walioona haya hayakuwa dawa, basi walimsihi aachane na sera zake, kama ni mali anataka wampe marundo ya dhahabu au kama ni mke anahitaji wamchagulie binti mzuri kuliko wote wamuoze. Hayo yote yakaruka patupu. Haki na dhulma ni mfano wa giza na mwanga. Havikai pamoja. Haki ikitendeka lazima dhulma itakoma kama vile ambavyo mwanga ukiingia lazima giza litoweke.

Sasa na tuyaangalij yanayotokea katika dunia hivi sasa tunapoingia karne ya 21 A.D. Na tujihusishe na eneo dogo la dunia kwa kuitazama jamii ya Tanzania. Tutakafari kwa fikra za uhakika ni jinsi gani yaliyotokea karne ya saba yanavyojiakisi leo.

Baada ya nchi yetu kutawaliwa kwa mfumo wa ukiritimba wa chama kimoja tangu 1961 hadi 1995, takriban miaka thelathini na tano, kundi ndogo, lililokuwa likitawala kwa muda wote huo, limejikuta likiwa wao ndio taifa na taifa ni wao. Hawa wamejijengea himaya (vanguard) ambapo watakaloamua wao huwa ndilo. Wakisema tuhamishe makao makuu Dodoma lakini tukae Dar es Salaam, basi huwa hivyo.

Utawala wa aina hii hauna tofauti na tawala za kifalme ambazo mara zote kunakuwa pengo kubwa kati ya familia ya kifalme na raia wengine. Na kanuni ya tawala hizi ni aina ya kifalme kupata huduma zote tena kwa israfu ya kutisha na kuwaacha raia wengine wakiishi kwa kubahatisha hata kwa zile huduma za lazima.

Kutokana na hali hiyo, wimbi la mabadiliko ya tawala kutoka ukiritimba wa chama kimoja na falme kudhahiri duniani, ilibidi nchi zote zilizokuwa na tawala za aina hiyo zikubali mabadiliko ikiwa ni pamoja na Tanzania japo kwa shingo upande.

Kwa hakika mabadiliko haya hayakufurahiwa kwani yalimaanisha jamii kuwa na sauti juu ya mambo yao na kwa maana hiyo kupunguza eneo la ukandamizaji wa jamii.

Katika mfumo huu mpya, hapa Tanzania kulijitokeza watu ambao walijijasirisha kukosoa ukiritimba na kuwaandaa wananchi kujitafutia haki zao kwa njia ya makubaliano ya kiutawala. Taaluma za kuwaandaa watu katika kujiandaa kujikomboa kisiasa, kiuchumi na kiustawi wa jamii zikaanza kutolewa na waliokuwa wakikereketwa na hali ilivyokuwa.

Kutokana na hali hiyo, wale wenye kutazama kwa jicho la tafakuri na kuyajadili macho katika vichwa vyao vya akili za uhakika, hapana shaka wanashuhudia kutoka katika lile kundi lililobobea katika utawala, maneno na matendo yanayotoa taswira kamili ya yale ya karne ya saba. Kauli kama "Hao ni Maprofesa wachovu".

Tunaamini bado watu wanayo kumbukizi ya mkutano wa wanahabari ulioandaliwa na chama tawala CCM kwa uongozi wa katibu Mkuu Mhe. Philip Mangula.

Mkutano huo ambao ulishereheshwa kwa kanda ya video, ulikusudiwa uwadanganye watu kwa kuwatumia wanahabari na kanda ya video, wakubali kile ambacho wao wanadai ni ubaya wa chama cha wananchi CUF.

Ilidhaniwa watu wangepokea maelezo ya mkutano huo na kanda hiyo kama vile wapokeavyo sakarament au dua na waseme tumekubali tumesadiki au waitikie Amina. Ni vizuri kukumbusha tu kuwa, mkutano huo uliandaliwa baada ya kutokea tafrani katika mkutano wa CUF wa ndani ambao ulivurugwa na polisi.

Katika hali ya purukushani hizo, polisi mmoja kuumia. Lakini pia raia mmoja alipigwa risasi na polisi na kutelekezwa mferejini. Ilibidi asaidiwe na raia wema kumpeleka hospitali. Kilichofuatia ni vyombo vya habari kutangaza kwa mapana na marefu juu ya polisi aliyeumia. Yule raia aliyepigwa risasi ilibidi watu wapate habari kutoka vyombo vya habari vya nje.

Lengo CUF ionake mbaya, lakini vyombo vya watawala visiumbuliwe. Hali hii haikuishia hapo tu bali ilipelekea Chama tawala CCM kuandaa mkutano maalum na kuandaa kanda ya kuonesha tukio hilo ili wananchi waone hicho wanachokita wao.

La ajabu na la kusaidia kuwatanabaisha watu ni jinsi kanda ile ilivyokosa uadilifu, kwa kuonesha polisi aliyeanguka na kuumia lakini ikaficha raia aliyepigwa risasi na polisi hao hao. Tabia ile ile ya Makuraishi ya kuwaambia watu wazibe masikio na macho ili wasimuone wala kumsikia mtoa habari njema juu yao.

Kabla hilo halijasahaulika, Mhe. Jaji Makame wa Tume ya Uchaguzi akaibuka na mkutano wa Maaskofu. Mkutano huo ulikuwa wa kuikosoa Tume kutokana na malalamiko ya wananchi juu ya vitendo vinavyoashiria kuipendelea CCM na kuachiwa kufanya kampeni na kutumia vyombo vya dola kabla ya wakati wa kujinadi haujatangazwa na tume hiyo, na kutumia fursa hiyo chama na serikali yake kuvipiga vijembe vyama vingine. Kwanini mkutano huo uwe wa Maaskofu bila kuwashrikisha Maimamu na Masheikh, hilo tunamuachia Mhe. Jaji mwenyewe.

Hata hivyo, tuna maswali ambayo tunadhani yeye Jaji ndiye mwenye majibu sadifu. Tumeelezwa kuwa katika kutetea tume na vyombo vya dola, Mhe. Jaji alikanusha katakata kuwa Tume yake inaipendelea CCM wala kuvinyamazia vyombo vya dola katika kuibeba CCM kwa kuvipuuza vyama vingine. Hivi Mtanzania wa kijiji kipi ambaye kwa kusikia redio na kusoma magazeti haoni kuwa CCM kwa kutumia vyombo vya dola imeshaanza kampeni miezi kadhaa iliyopita.

Ni hadhira mbovu kiasi gani ambayo haiwezi kuelewa kuwa kipindi cha radio ya Taifa (RTD) cha "Maneno Hayoo!" kinafanya kampeni za CCM kwa njia ya redio na kuvikejeli vyama vingine? Kama CCM haitumii vyombo vya dola kwa kampeni zisizo rasmi nini kilipelekea radio ya taifa RTD kulazimika kubadili ratibu ya vipindi vyake na kuitangaza mikutano ya uteuzi ya CCM kwa siku mbili mtawalio, wakati mikutano ya vyama vingine haitangazwi hata kwenye kipindi cha majira wacha taarifa za habari? Huu ni ule ule mtindo wa karne ya saba wa kuwaonya watu wazibe masikio ili wasisikie sera za yule jamaa yao wasije wakatanabahi.

Kutokana na ufahamu wa mageuzi unavyoenea kwa kasi, tayari wale walioshikilia mpini wameingiwa na kiwewe. Kama sio sio kiwewe kwanini kauli ya CUF ya 'jino kwa jino' kauli safi tena shurutia, ipewe tafsiri mbaya, ibatizwe kuwa ndiyo sera ya CUF na kufanywa kigezo cha kuichafua CUF? Kama sio kiwewe kuna ubaya gani jirani yako akikuambia: "Bwana ee! Leo ukipika biriani na mimi nitapika biriani". "Ukiamua kusafiri kwa ndege na mimi pia nitasafiri kwa ndege", "Ukining'ata na mimi nitakung'ata". "Jino kwa jino". Hizo zote ni kauli shurutia. Msemaji hatafanya mpaka afanyiwe yeye kwanza. Hivi wanaotoa tafsiri potofu ni wajinga wa lugha au wamedhamiria?

Lakini pia jambo la kulitia akilini zaidi na kulitumia kama kigezo cha kuutambua ukweli ni kuwa, chama tawala kimeshatoa kauli za mfano huo na pia nyingine zenye maana mbaya hasa katika hali halisi. Bado tunakumbuka mwaka 1995 wakati Makamu wa Mwenyekiti wa CCM Zanzibar ambaye pia ni Rais, alipokuwa akishauriwa kuunda serikali ya kitaifa alivyodai kuwa hawezi kuchanganya mchele na kokoto. Kauli hii haikuwa na maana nyingine ila kuwagawa Wazanzibari katika daraja mbili. Moja lenye hadhi ya mchele na nyingine yenye hadhi ya kokoto.

Iko wapi tofauti ya wazo kama hilo na lile la kina Botha wa Afrika Kusini la kusema watu wa aina hii hawaruhusiwi kuingia hoteli au treni fulani. Kauli za Mwenyekiti wa CCM Tanzania Bara za "kofi kwa makofi", "ngumi kwa ngumi", "mtu kwa mtu" zimefikishwa hadi bungeni kutaka itolewe tofauti ya hizo na ile ya CUF.

Mtu ambaye hakusikia mwenyewe wakati Waziri katika ofisi ya Waziri Mkuu, kwa maana ya serikali, akijibu, hawezi kuamini kuwa Waziri alithubutu kuwaambia Watanzania maneno yafuatayo: "Kwa kuwa CCM haina Makamu wa Rais basi kauli kama hizo hazipo! Jibu hilo lilitolewa na serikali katika ukumbi wa chombo cha sheria; kwa sababu tu muuliza sawali alitumia wadhifa wa "Makamu wa Rais wa CCM badala ya Makamu Mwenyekiti wa CCM. Lakini Mhe. Malecela yupo! Kauli kazitoa! Na radio na magazeti tulisikia na kusoma! Tunaloweza kusema hapa tu ni kuwa na sisi tumewasikia! Tumewaelewa!.

Bunge hilo hilo ambalo ofisi ya Waziri Mkuu inathubutu kuwaambia Watanzania kuwa CCM ikisema sikieni na wengine wakisema zibeni masikio linatudhihirishia kuwa mshituko sio mdogo. Lakini la kusikitisha zaidi ni kuwa kila Waziri aliyepata fursa ya kuzungumza kuhitimisha mjadala wa bajeti yake badala ya kujibu hoja za wabunge alitumia nafasi hiyo kukejeli vyama vya upinzani na kutoa matamshi ambayo kwa kweli baadhi hayakuonesha uungwana hata chembe.

Tunakumbuka zaidi hotuba ya Waziri Mkuu ambayo ilijaa kejeli nyingi hasa kwa CUF na UDP. Kwa CUF aliwasakama zaidi kwa madai kuwa jino kwa jino ni hatari na kuwa walihusika katika kumuumiza polisi na kumnyang'a nya silaha. Lakini ni vyema Waziri Mkuu akumbushwe kuwa hatujasahau kuwa aliwapongeza wauaji wa raia wasiokuwa na hatia pale Mwembechai.

Marehemu Shaaban Robert katika riwaya yake ya 'kusadikika' anatufunza kuwa nchi ya kusadikika ambayo ilikuwa imezama katika ukandamizaji na kutojali elimu za fikra za wasadikika wema, hatimaye ilifaidika kwa kumsikiliza kijana Ikibali ambaye alidhaniwa kuwa mtu mbaya kabla hajapatiwa wasaa wa kuikosoa ngome ya watawala na kutoa nasaha na mipango yake ya kuikomboa nchi kiuchumi na kijamii. Hatujifunzi tu kutoka kwa hao?

--
JuuRUDI


Bonyeza hapa
kushriki mjadala au kutoa maoni juu ya habari hizi na masuala mengineyo ya Kiislamu kwenye Baraza ya Wasomaji

   Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu: Bonyeza hapa
Au
Andika barua  kwa: webmaster@islamtz.org
 
An-nuur Home | Ukurasa wa Mwanzo | Islam Tanzania 
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook