NAANZA makala hii kwa kuwauliza akina dada na mama Waislamu (Ma-Ustadhat) swali, Je, mpo? Kwa sababu maeneo yenu yanaguswa lakini kimya! Au ndio mpo katika kufanya tathmini ya kura zenu ili msijechagua watu wasiofaa? Kama hivyo ndivyo, basi nawatakia tathmini njema, lakini punguzeni ukimya, nasema tathmini njema.
Mwezi uliopita nilikuwa nasoma kitabu kimoja kiitwacho Beyond Inequality Women in Tanzania katika ukurasa wa 39 nilikutana na maneno yafuatayo na hapa sina budi kunukuu:
"Talaka pia imezoeleka miongoni mwa Waislamu, ambao wanaweza kupata talaka na kufanya ukewenza! Talaka imerahisishwa chini ya mwenendo wa 'Talaka" ambao unamruhusu mmojawapo kuoa na kuacha kwa urahisi. Hata hivyo, mfumo huu ni wa kinyanyasaji dhidi ya wanawake". (tafsiri ni yangu)
Baada ya kusoma maneno haya nilijiuliza maswali mbalimbali, lakini kujiuliza kwangu maswali hakukuweza kunishawishi nikubali kwamba wahusika waliandika kitabu hicho pasipo kufahamu nini wanaandika.
Mara baada ya Salman Rushdie kuandika kitabu chake, mwandishi Roald Dahl alimuelezea Salman Rushdie na kusema: Clearly he has profound knowledge of the Muslim religion and Its people, and he must have been totally aware of the deep and violet feelings his book would stir up among devout Muslims, in other words he knew exactly what he was doing and he can not plead otherwise.
Rushdie alifahamu fika nini alikuwa anaandika, na hivyo ndivyo ilivyo kwa waandishi wengi ambao hujifanya kuelezea Uislamu. Hivyo hivyo, ndivyo wahusika wa kitabu nilichokitaja hapo juu walivyofanya.
Sasa tutizame ulemavu wa maelezo yao na sio kuwapa lawama tu. Maelezo yangu yatakuwa chini ya maswali yafuatayo:
Je, talaka imezoeleka miongoni mwa Waislamu?
Je, talaka katika Uislamu imerahisishwa chini ya utaratibu wa talaka?
Je, Uislamu unaruhusu kuoa na kuacha kwa urahisi?
Je, ukewenza ni udhalilishaji kwa wanawake?
Talaka ni ruhusa katika Uislamu iwapo zipo sababu za msingi ambazo zinaweza kupelekea ndoa kuvunjika. Miongoni mwa mambo yaliyoruhusiwa ambayo Mwenyezi Mungu anayachukia ni suala la mume na mke kuachana.
Pamoja na hayo, Uislamu haujarahisisha talaka kiasi cha kumfanya mtu aoe na kuacha kwa urahisi.
Ni kweli usiopingika kama ilivyoelezwa hapo juu kwamba talaka imeruhusiwa katika Uislamu, lakini kuruhusiwa huku hakumaanishi kuwa Muislamu anaweza kuacha kwa urahisi au hovyo hovyo tu.
Uislamu umeweka taratibu za kisayansi pale panapotokea kutoelewana kati ya mume na mke kabla ya talaka hio kutolewa. Kwa sababu talaka ni halali inayomchukiza Mwenyezi Mungu. Wahusika mume na mke wanapaswa kukaa chini na kutatua tatizo hilo mapema iwezekanavyo. Pili kama pasipofikiwa muwafaka ndugu wahusishwe, wote wa upande wa mume na mke. Na kama hii pia ikishindikana talaka hutolewa, kwa sababu watu hawa hawawezi kukaa kwa amani na furaha ndani ya ndoa yao. (4:35)
Pindi talaka inapotolewa mwanaume haruhusiwi kumfukuza mkewe katika nyumba waishio (isipokuwa kama amefanya kosa kubwa sana), vivyo hivyo mwanamke pia hatakiwi kuondoka sehemu hiyo. Ni wajibu wa mwanaume kumhudumia mwanamke huyo kama vile talaka haijatolewa. Mwanamke atakuwepo katika kipindi cha kusubiri probationary period cha miezi mitatu na kama ni mja mzito mpaka pale atakapojifungua. Lengo la kukaa kipindi hicho ni kuangalia kama muwafaka unaweza kupatikana. (65:4), (65:1)
Ifahamike katika Uislamu ipo ruhusa kwa mwanamke kuomba talaka kwa mumewe ikiwa zipo sababu za msingi, Mtume Muhammad (s.a.w.) amesema kama mwanamke yeyote ataomba mumewe talaka pasipo sababu za msingi pepo itakuwa ngumu sana kwake kuingia. (Abu Daud, Ibn Majah). Vivyo hivyo kwa mwanaume kutoa talaka pasipo sababu za msingi.
Ni kutokana na maelezo hayo, Uislamu haujarahisisha suala la talaka kiasi ambavyo wahusika na watu wengineo wangependa kufikiri kama talaka ingekuwa imerahisishwa katika Uislamu kiasi cha kuacha kwa urahisi 'Divorce easily', talaka isingekuwa ni halali inayochukiwa na Mwenyezi Mungu. Uislamu pia usingeweka kipindi cha kusubiri kama lengo ni kuacha kwa urahisi, Mtume Muhammad (s.a.w.) asingeyasema hayo maneno ambayo nimeyanukuu hapo juu iwapo talaka ni suala lililorahisishwa katika mfumo wa maisha ya Kiislamu.
Uislamu unatufundisha kama hakuna maelewano tuachene kwa amani na upendo. (2:229, 65:2)
Katika mazingira kama haya talaka pia haijazoeleka miongoni mwa Waislamu. Tukirejea aya yetu tunakutana na neno 'Common'. Divorce is also more common among Muslims...'. Neno 'common' limeelezewa hivi: Ni kawaida, kuzoeleka, kutokea mara kwa mara na sehemu nyingi. Hivyo, talaka ni suala lililozoeleka na kutokea mara kwa mara ndani ya jamii ya Waislamu.
Katika kitabu hicho sikuwahi kuona takwimu ya orodha ya ndoa zinazoonesha kwamba Waislamu Tanzania wanavunja ndoa zao sana ukilinganisha labda na wasio Waislamu, hivyo hivyo kwa Afrika na duniani kwa ujumla. Hivyo suala la kuzoeleka bado linautata. Uislamu hata hivyo umeruhusu talaka lakini Ukristo unapinga suala hili, pamoja na ukweli kwamba limeruhusiwa (rejea (Mathayo 19:9).
Msomi mmoja wa Kimagharibi Rebecca West aliwahi kuandika na hapa ni busara kunukuu maneno yake:
Though I have the kind of Temperament that hates to break a marriage I had made, I regard divorce laws a necessary part of the arrangements in a civilized state.
Mwandishi huyo pamoja na kutopenda kuvunja ndoa yake lakini anachukulia sheria za talaka kama ni sehemu ya msingi katika nchi iliyostarabika. Anaamini zipo sababu za msingi za kuvunjika kwa ndoa, na kama zipo hakuna budi kuwepo utaratibu unaozungumzia suala hili la talaka.
Jarida moja la Kikristo liitwalo The Watchtower la Februari 15 ukurasa wa tatu kuna maelezo yafuatayo:
"Kama tutalinganisha suala la uvunjikaji wa ndoa dunia na tetemeko la ardhi, Marekani itakuwa katika 'epicentre' (sehemu ambapo ni kiini cha tetemeko la ardhi). Hivi karibuni ndoa zaidi ya milioni moja zilivunjika - wastani wa ndoa mbili kwa dakika moja..."
Kutokana na kukosekana kwa takwimu kama hizi maelezo ya kwamba talaka imezoeleka miongoni mwa Waislamu hayana msingi na ni hoja mbovu.
Mwisho ninapenda kumaliza kwa kutizama suala la ukewenza . Suala hili limekuwa likionekana kama ni udhalilishaji kwa wanawake, lakini je hii ni kweli?
Ukewenza kama ilivyo talaka ni suala lililoruhusiwa na ruhusa hiyo ni hadi wanawake wanne. Na wanawake watakaoolewa yaani wapili, tatu na nne wanayo haki sawa na yule wa kwanza. Na sharti la msingi ni kutenda haki kwa wote.
Nisingependa kurudia sababu za ukewenza ambazo zimekuwa zikitolewa hapo nyuma, lakini nizungumzie sababu moja tu, mwanamke mwenye akili timamu hupenda kuwa na mtu atakayemjali na kuishi naye kwa furaha. Sasa je ikitokea idadi ya wanawake ni kubwa ukilinganisha na ya wanaume, wanawake hawa waende wapi? Je ni wanawake wangapi wanaoweza kuishi kipindi chao chote bila ya ndoa?
Idadi hiyo kubwa ya wanawake huwaweka katika hali kubwa tatu. Mosi, wakubali kuwafurahisha wanaume wenye uchu katika kipindi chao chote cha maisha na kubakia wakiitwa majina mabaya na ya kejeli, pili, wavumilie kuishi hivyo hivyo katika kipindi chao cha maisha, tatu, wakubali waolewe na wanaume ambao tayari wanawake na ambao watatenda uadilifu.
Ninaamini kwamba suluhisho namba tatu ndio muafaka kwa binadamu yeyote mwenye akili timamu.
Hivyo, katika mazingira haya ukewenza haumdhalilishi
mwanamke, isipokuwa humuhifadhi na kumpa hadhi anayostahili. Na sidhani
kama wapo wanawake wenye busara ambao wako tayari kufanywa vyombo vya starehe
tu. Ninaamini hupenda waheshimiwe na kupewa haki zao na si kudhalilishwa.
Ni kutokana na ukweli huu wanawake wa nje 'vimada' hutumia mbinu zote ili
kuvunja ndoa za watu ili wao nao waolewe, hawapendi kuwa 'vimada'.
--
![]()
|
|