SI laana ya Mwenyezi Mungu, kuwa enzi za akina Maulana, Saleh Zimbwe, Kinanda na Yanga Fadhili Bwanga zimetoweka. Prof. Ibrahim Lipumba amewaeleza hayo wananchi wa Tanga juzi.
Amesema, mikoa ya Tanga, Morogoro na Tabora ilikuwa ndiyo ikitamba katika mpira wa miguu. Lakini akasema hivi sasa michezo imedidimia kila pembe ya nchi.
Aidha, alisema, mikoa hiyo ilitamba katika muziki vikiwemo vikundi vya taarabu, Moro Jaz, Jamhuri Jazz, Kikokids, Nyanyembe na Wazee wa Kazi Segere matata. Prof. Lipumba amesema, mafanikio hayo yote yameporomoka.
Katika eneo la uchumi, Prof. Lipumba amesema, katika miaka ya sitini na sabini maelfu ya Watanzania walikuwa wakimiminika Tanga kufuata ajira.
Ajira hizo zilijaa katika shirika la Reli, Bandari, mashamba ya mkonge na viwanda.
Hata hivyo, akasema, leo sio tu kuwa Tanga haitoi ajira kwa wageni toka mikoa mingine bali hata wa-Tanga wenyewe hawana ajira.
Amesema, vijana wa Tanga wamekuwa ndio wanaoongoza kwa kudandia meli.
Prof. Lipumba amwaambia wananchi wa Tanga kuwa kuporomoka kwa uchumi na michezo hakutokani na laana ya Mwenyezi Mungu. Bali ni matokeo ya sera zisizotekelezeka za CCM na usimamizi mbovu wa sera hizo.
Amewataka wananchi hao kuhakikisha wanajiandikisha na kupiga kura.
Prof. Lipumba alikuwa akihutubia wananchi wa Tanga katika uwanja wa Tangamno Julai 26.
Awali, Manispaa ya Tanga ilitikiswa kwa kishindo cha Chama cha Wananchi (CUF) kufuatia ufunguzi wa matawi ya chama hicho uliofanywa na Mwenyekiti wake Prof. Ibrahim Lipumba.
Wakati wa ufunguzi wa matawi, Prof. Lipumba akiwa amefuatana na mgombea mwenza wake Bw. Nassor Hamis na Katibu Mkuu Maalim Seif, walitembea kwa miguu kutoka tawi moja hadi jingine huku wakifuatiwa na umati wa wananchi.
Msafara wa ufunguzi huo wa matawi ulianzia barabara ya ishirini yalipo makao makuu ya wilaya ya chama hicho na kupitia barabara za Ngamiani ambapo matawi manne yalifunguliwa, likiwamo la Ibrahim Lipumba na Boom. Aidha, ofisi za Kata za Ngamiani Kaskazini na Usagara zilifunguliwa rasmi. Baada ya ufunguzi wa matawi ya Ngamiani msafara huo ulikwenda Makorora ambako matawi kadhaa yalifunguliwa.
Msafara wa Prof. Lipumba ulipata mapokezi makubwa ya wananchi katika kitongoji cha Segera na kuingia Tanga juzi majira ya saa saba mchana. Huku viongozi wa kitaifa wa chama hicho wakiwa kwenye magari ya wazi, waliwapungia wananchi ambao walijitokeza kuupokea msafara huo.
Gari yao iliongozwa na mapikipiki na kufuatiwa na msururu wa magari ishirini na nane yakiwemo malori ya matawi maarufu ya jijini Dar es Salaam ya Chechnya, Kossovo, Mashujaa wa Mwembechai, Ukanda wa Gaza na mengineyo.
Ili kuhakikisha usalama palikuwepo pia gari ya polisi ikifuatilia msafara
huo wa mgombea huyo wa Urais.
WAKATI Rais wa awamu ya tatu akiahidi kuingia karne ya ishirini na moja ya sayansi na teknolojia kwa mbwembwe, wilaya nzima ya Handeni haina mawasiliano ya Fax wala mawasiliano ya Kompyuta (E-mail) isipokuwa kwenye ofisi moja tu ya mradi wa misitu unaofadhiliwa na serikali ya Ujerumani.
Haya yaligunduliwa kufuatia mwandishi wa habari hizi kuhangaika mji wote wa Handeni akitafuta mawasiliano ya Fax ambapo hata kituo cha TTCL mjini hakuna huduma hizo.
Mwandishi wa habari hizi alielekezwa kwenye ofisi ya mradi wa misitu (HIAP) ambapo ndio sehemu pekee angeweza kupata huduma hizo, lakini alikataliwa kupewa huduma hizo, hazitolewi mpaka awe na kibali kutoka Ofisi ya Mkuu wa Wilaya, kwa mujibu wa maelezo ya Afisa mmoja wa mradi huo amabye tunalihifadhi jina lake.
Aidha, kuna kituo kimoja tu kinachotoa huduma ya simu za ndani na nje kiitwacho Handeni Travelers Telephone Service ambacho kinadaiwa kuwa kinamilikiwa na Waziri wa Nishati na Madini ambaye pia ni Mbunge wa jimbo hilo la uchaguzi, Mhe. Abdallah Kigoda.
Mhudumu wa kituo hicho, Bi Asha alisema kuwa walikuwa wamefunga mashine ya Fax lakini baada ya kuona hakuna wateja wakaamua kuacha kutoa huduma hiyo.
"Miezi miwili baada ya kufunga Fax hakukuwa na mteja yeyote hivyo tuliirudisha. Hata hii biashara ya simu nayo haina wateja wengi", alisema mhudumu huyo na kuongeza kuwa watu wengi wanaotumia simu kwenye kituo chake ni wageni kutoka nje ya wilaya hiyo.
Kuwapo nyuma katika huduma za mawasiliano ya kisasa na watumiaji wachache
wa huduma za simu inaonesha ni kwa kiasi gani wilaya hii iko nyuma kimaendeleo
na imekithiri kwa umaskini. Aidha, ni kielelezo kuwa katika wilaya hii
hakuna shughuli zozote nzito za kiuchumi zenye kuhitaji mawasiliano ya
haraka.
MWENYEKITI wa chama cha upinzani cha Tanzania Labour Party (TLP) Bw. Augustine Lyatonga Mrema amewaambia wananchi mjini hapa kuwa japokuwa CCM ni chama cha udini wa Kikristo lakini udini wake umezoeleka.
Bw. Mrema aliyasema hayo hivi karibuni wakati akihutubia mkutano wa hadhara katika uwanja wa mpira uliopo Manundu hapa Korogwe, akiwa ameongozana na Makamu Mwenyekiti wake Ali Iddi Hamisi.
Akiuchambua udini uliopo CCM, Bw. Mrema alidai kuwa viongozi wote wa juu wa CCM na baadhi ya Mawaziri waandamizi ukimuondoa Makamu wa Rais ni Wakristo na kwamba hata uteuzi wake wa Wakuu wa Mikoa na Wilaya huzingatia zaidi udini ambapo Wakristo huwa ni wengi kuliko dini zingine. Aidha, Mwenyekiti huyo wa TLP alisema, CUF nayo ina udini wa Kiislamu kwa kuwa viongozi wa juu ni Waislamu.
Kwa udini huo, Bw. Mrema akawataka wananchi hao kuhakikisha kuwa wanaipigia kura TLP kwani chama hicho hakina nguvu ya udini bali siasa. Lakini akatoa tahadhari kuwa kama wananchi wataamua kutoipigia kura TLP basi bora waipigie kura CCM kwani udini wake umezoeleka.
Wakiongea na gazeti hili wananchi wa hapa Korogwe wameonesha mshangao kwa kauli hiyo ya Bw. Mrema. Wakahoji iweje Bw. Mrema aseme udini wa CCM una nafuu na umezoeleka kama sio kuipigia kampeni CCM irejee madarakani.
Wakiongeza wananchi hao walisema, wanaungana na uchambuzi wa udini uliopo
CCM kama ulifanywa na Bw. Mrema kuhusu nafasi za kuteuliwa katika utendaji
wa CCM yenyewe, serikali na mashirika yake kufanywa kwa upendeleo wa Wakristo
dhidi ya dini nyingine. Lakini wakatofautiana naye kuhusu ombi lake la
kutaka CCM ipigiwe kura za kuirudisha madarakani.
--
![]()
|
|