AKINA mama wa Kiislamu wamehimizwa kuwalea watoto wao katika maadili mazuri ya Kiislamu tangu wakiwa wachanga.
Hayo yamesemwa na Mwenyekiti wa kundi la Da'awah la kina mama wa Kiislamu katika Msikiti wa External jijini Dar es Salaam.
Akitoa mada ya malezi ya watoto katika mikutano yao ya kila wiki iliyofanyika Msikitini hapo, Bi Zulfa aliwakumbusha wanawake kuwa wao ndio walezi wa karibu sana kwa watoto wao hivyo yafaa kuzitambua na kuzifuata taratibu za malezi ya watoto tangia wakiwa wachanga.
Bi Zulfa aliongeza kusema, pamoja na kwamba malezi ya mtoto ni ya wazazi wawili, lakini mama anachukua nafasi kubwa kulingana na majukumu ya wanaume waliyonayo juu ya familia pamoja na jamii kwa ujumla.
"Jukumu la kuihudumia familia ni la Baba, pia viongozi wa kijamii kwa ujumla na wa kina baba, hivyo wakati haya yanafanywa mwanamke anakuwa yeye ni mtu wa nyumbani pamoja na watoto", alisema Bi Zulfa.
Katika darsa hilo ambalo lilihudhuriwa na wakina mama toka Tabata, Sinza na Temeke, wakinamama walitahadharishwa na propaganda zinazoenezwa kuwa mwanamke hana haki wala usawa katika jamii.
"Kamwe Uislamu haujambagua mwanamke kijinsia na Muislamu yeyote atakayesimamia msimamo huo basi amejitenga na Uislamu", alisema Bi Amina ambaye aliwasilisha mada ya msimamo wa Uislamu juu ya propaganda za kitwaghuti.
Awali akifungua darasa hilo, Mwenyekiti wa kinamama
wa External aliwataka viongozi wa Misikiti kuwapa fursa wanawake kuendesha
darasa zao na kwamba pale wanapowaomba msaada wa kielimu wasisite kuwasaidia.
WAAJIRI wa waandishi wa vyombo vya habari nchini wametakiwa kuwajengea mazingira mazuri wafanyakazi wao kwa kuwapatia vifaa vya kutendea kazi, mawasiliano ya uhakika pamoja na fedha za kutosha ili waweze kufanya kazi zao vizuri wakati wa uchaguzi mkuu.
Hayo yameelezwa na Bw. Lawrance Kilimwiko wakati akitoa muongozo kwa waandishi wa habari juu ya kuandika habari za uchaguzi katika semina ya siku mbili iliyofanyika Ijumaa na Jumamosi iliyopita katika ukumbi wa Madini mjini hapa.
Alisema, ni wajibu wa wamiliki wa vyombo hivyo kuwacha kuwalipa waandishi wao hususan wa mikoani malipo kulingana na habari alizozituma katika vyombo hivyo na badala yake wathamini muda, pamoja na mizunguko ya kufuatilia habari.
"Tabia ya wamiliki kuwalipa waandishi kulingana na habari aliyoitoa tena kwa kuipima kwa rula watawafanya wafanyakazi hao kujiingiza katika vitendo vya rushwa na kupelekea kupotosha habari za uchaguzi, jambo ambalo linaweza kuleta madhara katika jamii", alisema mkufunzi huyo kutoka AJM.
Aidha, alivitaka vyombo vya habari na waandishi
kutorudia makosa yaliyofanyika wakati wa uchaguzi mkuu wa mwaka 1995 ambapo
baadhi ya vyama vya siasa na wagombea wake hawakuweza kupata hata nafasi
ya kutangazwa katika vyombo hivyo.
AMIRI, Sheikh Juma Mbukuzi Salim ametoa wito, wale wanaowania nafasi za uongozi kwa njia ya rushwa wasichaguliwe.
Amesema, rushwa ni adui mkubwa wa haki miongoni mwa maadui wa haki.
"Kwa kuwachagua watoa rushwa kushika nafasi za uongozi jamii itapata madhara makubwa", amesema.
Kwa kufafanua Sheikh Mbukuzi amesema, wale wote wanaowania nafasi za kutaka kuiongoza jamii kwa kutoa rushwa ni wazi kuwa hawana sera nzuri zitakazoleta maendeleo katika nchi zitakazokubalika kwa wananchi zaidi ya kuwadanganya.
"Kitakachofuatia baada ya kufanikiwa kushika uongozi kwa njia ya rushwa ni kudhulumu haki za wananchi bila huruma", amesema.
Kwa hali hiyo, Sheikh Mbukuzi amesema, kutokuwachagua watoa rushwa ni kulinda haki na kinyume cha hivyo ni kuuza haki.
Aidha, Sheikh Mbukuzi amesema, Uislamu umekataza kutoa rushwa, kupokea au kusaidia vitendo vya rushwa. Kuthibitisha hili Sheikh Mbukuzi alinukuu maelezo ya Mtume (s.a.w.) kwamba: "Wana laana ya Mwenyezi Mungu mtoa rushwa, mpojeaji na mwenye kusaidia hayo".
Sheikh Mbukuzi amesema, muda ambao watakuwa madarakani
viongozi waliochaguliwa kwa rushwa, wananchi wasitarajie chochote zaidi
ya madhara makubwa yanayotokana na rushwa.
TOFAUTI na mikutano ya vyama vingine, polisi walionekana kuwa wengi katika mkutano wa CUF uliofanyika juzi Julai 26, katika uwanja wa Tangamano.
Mkutano huo uliohutubiwa na Mwenyekiti wa Chama hicho, Prof. Ibrahim Lipumba ulihudhuriwa na umati wa watu ambao haujaonekana uwanjani hapo kwa masiku ya karibuni.
Haikuweza kufahamika ni kwa nini polisi walikuwa wengi sana wakati ulikuwa mkutano wa kawaida.
Katika mkutano huo, Prof. Lipumba amesema, kuongeza ufanisi katika uchumi ni kuongeza ajira na sio kupunguza wafanyakazi.
Lipumba ameikosoa sera ya serikali ya kuunguza wafanyakazi kuwa inaongeza umaskini.
Amesema, usahidi wa sera za CCM zinavyoongeza umaskini ni zoezi la serikali inaloendelea la kupunguza wafanyakazi.
Aidha, amesema, adui maradhi hawezi kuondoka nchini wakati hospitali hazina dawa.
Prof. Lipumba amesema, kutokana na wagonjwa kuagiwa vifaa hata watoto wadogo sasa wanajua vifaa vya kujifungulia.
Hata hivyo amesema, wakati hospitali hazina vifaa wala madawa, viongozi wa serikali wamekuwa wakienda Ulaya kujitizamia afya zao.
Amesema, licha ya CCM kuahidi kuwa kuondoa umasikini, maradhi na ujinga mara tu baada ya uhuru, sera za chama hicho zimeendelea kuwajenga maadui hao.
|
|