Wajibu wa mke kwa mumewe

"WEWE baba Sijali hiyo 'miharage' unayoileta saa hizi mkaa wenyewe unao! Kila siku maharage tukibadilisha dagaa na hao dagaa kila siku mwisho watutoboe matumbo, yamenifika mwenzenu kwa mme huyu", mama Sijali anasikika akilaumu hadharani mara tu mumewe alipomkabidhi kifurushi kidogo alichorudi nacho nyumbani.

"Chumba kimeshinda kikiwa kisafi umerudi wewe michanga mitupu, na unapotembea huangalii chini mpaka uzoe midongo hii kama trekta", hiyo ndiyo salamu ya mama Marijani wa Magomeni kwa mumewe ambaye ndiyo kwanza amefika na kujibwaga kwenye kochi akitokea matafututoni.

Bora ningekaa huko huko! Nimechoka nafikia kushutumiwa, mke gani huyu, analalamika kimoyo kimoyo Baba Marijani.

Hawa ni mifano ya wanawake wasiojua wajibu wao kwa waume zao na wako wengi wa namna hiyo katika tabaka zote za kimaisha.

Wanawake wanawajibika kisheria kwa waume zao kama tunavyojifunza katika aya ifuatayo:

"... Nao (wanawake) wanayo haki kwa sheria (kufanyiwa na waume zao) kama ile haki iliyo juu yao kuwafanyia waume zao. Na wanaume wana daraja zaidi kuliko wao. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye nguvu mwenye hikima". (2:228).

Ili nyumba iwe ya furaha na amani, mke anawajibika kwa kadri ya uwezo wake kumfanyia mumewe yafuatayo:

Kumtii mumewe katika mambo yote mema atakayomuelekeza

Ilivyo ni kwamba, Mwenyezi Mungu (s.w.), kwa Hekima yake isiyo mipaka, ametuumba na kututofautisha katika maumbile na vipaji ili tuweze kutegemeana na kusaidiana katika kuliendea lengo la kuwepo kwetu hapa ulimwenguni. Wanaume kulingana na umbile lao na jukumu lao la kuiangalia familia na kukidhi mahitaji yote muhimu ya maisha wamepewa wadhifa wa kuwa walinzi wa familia kama tunavyofahamishwa katika Qur'an:

Wanaume ni walinzi wa wanawake, kwa sababu Mwenyezi Mungu amewafadhilisha baadhi yao kuliko wengine na kwa sababu ya mali zao wanazozitoa (katika kukidhi haja zao). Basi wanawake wema ni wale wenye kutii, wanaojihifadhi (hata) wasipokuwepo (waume zao), kwa kuwa Mwenyezi Mungu amewaamrisha wajihifadhi... (4:34).

Mke kumtii mumewe katika mambo ya kheri, si kwa ajili ya kumfurahisha mumewe tu bali ni katika kumtii Mwenyezi Mungu (s.w.). Pia msisitizo wa mke kumtii mumewe unabainika katika hadithi ifuatayo:

Abu Hurairah ameeleza kuwa Mtume wa Mwenyezi Mungu aliulizwa: Ni nani mbora kuliko wote katika wanawake? Alijibu: Yule anayempa (mumewe) furaha wakati anapomuangalia, anayemtii wakati anapomuelekeza afanye jambo) na ambaye hampingi kuhusu yeye mwenyewe na mali yake kwa kuchelea, kutomfurahisha (kumuudhi). (Nisai).

Pia tunafahamishwa katika hadithi aliyosimulia Abu Sayid al-Khudri (r.a.) kuwa Mtume (s.a.w.) amesema: "... Hapana mwanamke atakayefunga (funga ya sunnah) bila ya ruhusa ya mumewe..." (Abu Daud, Ibn Majah).

Mwanamke aliye kasirikiwa na mumewe kwa sababu ya kutomtii katika jambo la kheri, laana ya Mwenyezi Mungu inakuwa juu yake. Pamoja na msisitizo huu, mke hatamtii mumewe katika mambo ya haramu. Katika hadithi aliyoisimulia Ali (r.a.), Mtume (s.a.w.) amesema:

Hapana ruhusa kumtii yeyote katika kumuasi Mwenyezi Mungu. Utii ni katika mambo ya kheri tu. (Bukhari, Muslim, Abu Daud, na Nisai).

Kumliwaza Mumewe

Mke hana budi kuifanya nyumba yake ni mahali pa furaha na utulivu wa mawazo kwa mumewe. Inatakiwa mwanaume anapotingwa na mambo magumu katika harakati mbali mbali za halali , apate maliwazo kutoka kwa mkewe arejeapo nyumbani.

Kazi nzuri na ya kuigwa aliyoifanya, Bibi Khadija katika kumliwaza na kumpa moyo Mtume (s.a.w.) katika mwanzo wa utume wake, haitasahauliwa katika historia.

Khadija ni mkewe Mtume (s.a.w.) wa kwanza ambaye ndiye mtu wa kwanza kumuamini Mtume. Hata kabla ya kupewa utume Muhammad (s.a.w.) alikuwa na ada ya kwenda kukaa peke yake katika Jabalil-Hiraa ili kupata wasaa na utulivu wa kutafakari juu ya Mwenyezi Mungu (s.w.).

Khadija hakumkataza wala hakulalamika. Badala yake alimtengenezea masurufu na kumpelekea, japokuwa wakati mwingine Mtume alikaa huko mwezi mzima. Alipojiwa na Jibril na kumpa wahyi wa kwanza Mtume (s.a.w.) aliogopa sana na akarejea nyumbani na kumueleza mkewe juu ya tukio hilo, na kumwambia kuwa a

Hapana shaka faraja hiyo ilimpa nguvu za kusubiri na kuhimili misukosuko iliyofuata. Bibi Khadija alishiriki kikamilifu katika misukosuko yote aliyoipata Mtume (s.a.w.). Mtume (s.a.w.) alibughudhiwa sana na makafiri wa Makka. Lakini kila aliporejea nyumbani alifarijika kutokana na moyo wa mapenzi na huruma na maneno ya kupewa moyo na faraja kutoka kwa Bibi Khadija. Hivyo Bibi Khadija alitimiza jukumu muhimu sana katika kipindi hicho kigumu.

Mtume naye alimpenda sana mkewe, na alikumbuka huduma zake na maliwazo yake katika maisha yake yote. Kila mara alikuwa akimkumbuka na kumsifia sana Khadija, hadi Bibi Aysha, mkewe, kibinaadamu alimuonea wivu na akasema: "Huishi kumtaja huyu Bibi Kizee Khadija, je Mwenyezi Mungu hajakupa badala yake mke bora kuliko yeye?" (Akimaanisha yeye mwenyewe, Aysha). Mtume (s.a.w.) alichukia na akasema: "La! Hajanipa badala yake mke bora kuliko yeye.

"Khadija aliukiri Uislamu wakati watu wengine waliukanusha, alinikiri wakati watu wengine walinikanusha, aliniunga mkono kwa mali yake na akaiweka mali yake chini yangu na chini ya Waislamu wakati watu wengine walikataa kutusaidia".

Kuhifadhi Nyumba

Mwanamke ni malkia wa nyumbani mwenye jukumu la kuhakikisha kuwa usalama na unadhifu unakuwepo nyumbani. Mwanamke hana haki ya kumkaribisha yoyote nyumbani kwake pasi na idhini ya mumewe. Kwa maana nyingine, mwanamke haruhusiwi katika sheria ya Kiislamu, kumkaribisha mtu yeyote ambaye mumewe hataki akakaribishwa nyumbani kwake, awe wa kike au wa kiume. Mtume (s.a.w.) katika hadithi iliyosimuliwa na Amr bin Al-As (r.a.) amewausia Waislamu kama ifuatavyo:

Jueni kuwa nyinyi mnahaki juu ya wake zenu, na wao wana haki juu yenu. Miongoni mwa haki zenu juu ya wake zenu ni kuwa wasimweke juu ya matandiko (viti) yenu msiyemtaka, wala wasimkaribishe katika majumba yenu msiyemtaka. (Tirmidh).

Mwanamke pia, ni wajibu wake kutunza mali yao na mumewe na asitoe kumpa yeyote pasina ruhusa kama tunavyojifunza katika hadithi ifuatayo:

Abu Umamah ameeleza: Nimemsikia Mtume wa Mwenyezi Mungu akisema katika khutuba yake katika Hija ya kuaga: "Hapana mwanamke yeyote atakayetumia kitu chochote kutoka kwenye nyumba ya mumewe, bila ya ruhusa yake. Aliulizwa: Ee Mtume wa Mwenyezi Mungu! Wala chakula? Alijibu: Hicho ndicho kitu chetu kilicho bora kuliko vyote. (Tirmidh).

Hadithi hii inasisitiza kuwa mke hatatoa mali ya mumewe kinyume na ridhaa yake. Lakini kama mke, kwa kumfahamu mumewe kuwa hatakuwa na neno, anaweza kutoa kitu sadaqa pasina na idhini yake lakini atapata nusu ya malipo atakayopata mumewe, kama tunavyojifunza katika hadithi ifuatayo:

Abu Hurairah ameeleza kuwa Mtume wa Mwenyezi Mungu amesema: Mwanamke akitumia (akitoa) kitu cha mumewe bila ya ruhusa yake, atapata nusu ya malipo ya mumewe. (Bukhari na Muslim).

Katika kutunza mali ya mume ni pamoja na kujizuia kufanya israfu. Ni jukumu la mke kuhakikisha kuwa hapana ubadhirifu wa chakula, nguo nakadhalika na kila kitu katika nyumba kinatunzwa vizuri. Mwenyezi Mungu (s.w.) hawapendi wenye kufanya ubadhirifu wala ubahili bali katika waja wake anaowapenda ni pamoja:

Na wale ambao wanapotumia hawatumii kwa fujo (hawafanyi ubadhirifu) wala hawafanyi ubahili, bali wanakuwa katikati baina ya hayo. (25:67).

Kuwa na Subira juu ya Mumewe

Mume na mke wote wanawajibika kuvumiliana na kusubiriana. Hakuna mwanaadamu aliyekamilika. Kama walivyo na udhaifu wanawake, vile vile wanaume wana udhaifu wao. Takriban kila mtu hakosi udhaifu ambao si wenye kumpendezesha mweziwe. Kama wanaume walivyosisitizwa kuwavumilia wake zao kwa udhaifu kama huu, na wanawake pia hawana budi kuwavumilia waume zao endapo watakuwa na udhaifu usiopendeza. Kufanyiana subira ni jambo linalopendeza mno mbele ya Mwenyezi Mungu (s.w.) na lina malipo makubwa kama tunavyojifunza katika aya mbali mbali za Qur'an:

Enyi mlioamini! Jisaidieni (katika mambo yenu) kwa kusubiri na kuswali. Bila shaka Mwenyezi Mungu yu pamoja na wanao subiri. (2:153).

Na anayesubiri na kusamehe (atalipwa malipo makubwa). Bila shaka hilo ni katika mambo makubwa ya kuazimiwa kufanywa (na kila Muislamu). (42:43).

Kutosheka na kile anachopewa na mumewe

Mwanamke hana budi kujizuilia na kumtaka mumewe ampatie matumizi ambayo hana uwezo nayo. Kwa upande wa mume, kama tulivyoona hana budi kwa kadiri ya uwezo wake kukidhi mahitaji muhimu ya mkewe na familia yake kwa ujumla. Pia ni vyema, kama mume anauwezo mkubwa, ampe mkewe ziada ya mahitaji muhimu na amzawadie mara kwa mara. Katika Qur'an tunajifunza kuwa:

Mwenye wasaa agharimu kwa kadri ya wasaa wake; na yule ambaye amepungukiwa riziki yake, atoe katika kile alichopewa na Mwenyezi Mungu; Mwenyezi Mungu hamkalifishi mtu yeyote ila kwa kadiri alichompa. Atajaalia Mwenyezi mungu baada ya dhiki faraja. (65:7).

Endapo mke atamdai mumewe hiki na kile na hali anaona kuwa uwezo wake ni mdogo, kwa vyovyote vile atamfanya mumewe aishi kwa wasi wasi. Atamuona mkewe kuwa hamtakii jema na hiyo itakuwa ni sababu tosha ya kuondoa upendo na huruma katika unyumba na kuvuruga amani katika familia.

Wanawake wa Kiislamu wanatakiwa wawasaidie waume zao kwa kila hali na wawaonee huruma na kuwatuliza na kuwaliwaza badala ya kuwakamua na kuwataka watoe hata kile wasicho na uwezo nacho. Katika historia tunajifunza kuwa wakeze Mtume (s.a.w.), kibinaadamu walighafilika na kumtaka Mtume (s.a.w.) awape matumizi yaliyokiuka uwezo wake. Tabia hii ilimuudhi sana Mwenyezi Mungu na Mtume wake. Kutokana na tabia yao hii Mtume (s.a.w.) aliwahama kwa kipindi cha mwezi mmoja (siku 29) kama tunavyojifunza katika hadithi ndefu iliyosimuliwa na Jabir (r.a.) na kukusanywa na Imam Muslim. Baada ya kipindi hiki, Mwenyezi Mungu (s.w.) alimshushia Mtume wake wahyi, ufuatao:

Ewe Mtume! Waambie wake zako: Ikiwa mnapenda maisha ya hii dunia na uzuri wake (mimi sinayo, na mimi siwezi kukulazimisheni kukaa na mimi katika hali ya ufakiri) njooni, nitakupeni kitoka nyumba, na kukuacheni muwachano mzuri. Na kama mnataka Mwenyezi Mungu na Mtume wake na nyumba ya Akhera, basi Mwenyezi Mungu amewaandalia wafanyao mema hayo, miongoni mwenu, malipo makubwa. (33:28-29).

Aya hizi hazikuwahusu wakeze Mtume (s.a.w.) tu, bali zinawahusu wanawake wote wa Kiislamu kuwa wakitosheka na kile kidogo wanachowapa waume zao kulingana na uwezo wako, Mwenyezi Mungu (s.w.) atakuwa radhi nao, na kuwapa furaha hapa ulimwenguni na ujira mkubwa huko Akhera. 
--
JuuRUDI


Bonyeza hapa
kushriki mjadala au kutoa maoni juu ya habari hizi na masuala mengineyo ya Kiislamu kwenye Baraza ya Wasomaji

   Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu: Bonyeza hapa
Au
Andika barua  kwa: webmaster@islamtz.org
 
An-nuur Home | Ukurasa wa Mwanzo | Islam Tanzania 
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook