KATIKA toleo lililopita tulianza kuangalia dawa ya ushirikina. Tukasema Tawhiid ndio dawa sahihi ya ugonjwa huo unaothiri maisha ya mwanaadamu hapa ulimwenguni. Tuliona maana ya neno Tawhiid na vile vile baadhi ya vigawanyo vyake. Hata hivyo ili twende tukiwa na mtazamo na imani moja tumelazimika kurejea nyuma kidogo, tumjue vyema Mungu Muumba kabla ya kuendelea kuchambua vile inavyotakiwa apwekeshwe katika maisha ya kila siku.
Wanaoyazingatia kwa makini mazingira yaliyowazunguka hufikishwa kubaini kuwa kila kitu cha ulimwengu huu chenye uhai na kisicho na uhai lazima kiwe kimeumbwa. Pengine swali lao la msingi litabaki katika kumjua ni nani huyo Muumba mweledi wa huu ulimwengu.
Ushahidi wa kimaumbile unaudhihirisha ulimwengu si zao la ulimwengu wenyewe. Kwa mfano isingewezekana kunguni kujiumba mwenyewe, hali kadhalika mfumo wa jua usingeweza kujitengeneza na kujiweka wenyewe vile ulivyo. Mimea, wanaadamu, vijidudu vidogo visivyoonekana, vipepeo nakadhalika, havina uwezo wa kujiumba vyenyewe.
Kwa hiyo tunalazimika kufikia hitimisho kwamba hakuna katika vile tunavyoviona au tusivyoviona ambacho awali kilikuwa na uwezo wa kujiumba chenyewe.
Wala haliingii akilini dai la kuwa viumbe hivi vimetokea kwa bahati nasibu, bali lazima awepo Muumba asieshabihiani na chochote katika vile alivyoviumba.
Lazima Muumba huyo asiwe mwenye kudirikiwa na milango dhaifu ya fahamu ya yule aliyemuumba, uwezo wake uwe mkuu isivyokadirika, lakini wakati huo huo kuwepo kwake na sifa zake zidhihirike katika kila kilichopo ambacho milango ya fahamu ya mwanaadamu yaweza kukidiriki.
Kosa la msingi walifanyalo wale wamkanao Muumba linashabihiana lile la wale wanaokiri kuwepo kwake lakini kwa mtazamo potofu.
Tumeona kule nyuma kwa urefu washirikina wanavyoabudu na madubwasha mbali mbali walivyoyapa uwezo wa kiungu.
Watu hawa hawakani kuwepo uumbwaji wa maumbile lakini wana imani za kishirikina ya wanavyomtazama Muumba wa maumbile hayo. Watu wengi wanaitakidi kuwa Mwenyezi Mungu yuko juu mbinguni. Wanamtazama Mwenyezi Mungu kana kwamba yuko juu ya Mbingu akiziutazama ulimwengu kutokea juu na mara moja moja au nyakati fulani fulani ndiyo hujitokeza kuingilia mambo ya kiulimwengu.
Wengine huitakidi kwamba Mwenyezi Mungu baada ya kuumba ulimwengu alimaliza shughuli zake na tangu wakati huo akawa hana shughuli nao. Amewaumba watu akawaachia wajiendeshee mambo yao wenyewe.
Watu wengine walio waumini wameshindwa kuyafahamu sawa sawa mafundisho ya Qur'an ambayo yanamueleza Mwenyezi kuwa yuko kila mahali.
Wanadhani Mwenyezi Mungu kukizunguka kila kitu ni inafanana na hewa au mawimbi ya radio. Dhana hiyo si sahihi kwa sababu inamdunisha Mwenyezi Mungu na kumuweka sawa na viumbe vyake. Hivyo sivyo alivyo Mwenyezi Mungu.
Mwenyezi Mungu hafanani na chochote katika vile tunavyoweza kuvifikiria. Mwenyezi Mungu hafanani na wala hana uhusiano katika uungu wake na wale tunaowaitakidi kuwa ni washirika wake.
Vibwengo, makangila, Mahepe, Mahaka, Vipwerezo,
Migigila, Vimbweho, Subiani, Mizuka, Sauta, Lata, Uza, Manata na vyote
vile vinavyodhaniwa au kupewa uwezo na ushirika na Mwenyezi Mungu, havina
ushirika wala uwezo wa kumdhuru au kumnufaisha mtu katika maisha ya kila
siku kinyume na Muumba Mwenyezi Mungu(s.w).
--
![]()
|
|