BARUA YA WAZI KWA WAGOMBEA URAIS WA ZANZIBAR

Wapendwa Ndugu Seif na Amani,

KWANZA napenda kukupongezeni kwa vyama vyenu kukuteuweni kuwa wagombea wa kiti cha Rais wa Zanzibar. Hii ni imani kubwa ambayo wanachama wenzenu wameonyesha kwenu na heshima ambayo lazima muienzi. Matumaini ya Wazanzibari wenzenu sasa yako kwenu. Lakini kabla hatujafika siku ya uchaguzi, ambapo wananchi wenzetu wataamua nani kati yenu aliongoze taifa letu katika kipindi cha miaka mitano ijayo, kuna mambo ningeomba mkayafikiria na kuyasimamia.

Sina haja ya kukuelezeeni vipi umoja na mashikamano wa visiwa vyetu umeparaganyika. Hakuna haja ya kuonyesheana vidole juu ya nani amesababisha hali hii, ijapokuwa tuna wajibu wa kujua chimbo lake. Tulianza kubaguwana kikabila, kimkoa, kimajimbo, kichama na sasa hata kiukoo. Naliposikia hata uraia wa mzee Abeid Karume unatiliwa mashakani na kizazi kile kile ambacho leo kinanufaika na matunda ya ujasiri na uongozi wake, najiuliza: Sasa tunakwenda wapi? Sidhani kwamba kati yenu, au yeyote kati ya viongozi wa juu wa vyama vyenu Zanzibar, alikuwepo pale jengo la Rahaleo mwaka 1957 wakati mzee Karume alipokuja kujiandikisha kupiga kura kwenye uchaguzi wa mwaka ule. Mimi nalikuwepo, nikichungulia dirishani. Sheikh Ali Ahmed alimpinga mzee Karume kwamba hakuzaliwa Zanzibar, lakini pingamizi hili ilishindwa, na mahakama kuthibitisha kwamba mzee Karume ni mzaliwa wa Zanzibar. Leo, miaka 43 baadaye, suala hili kuletwa tena ni kuthibitisha tumerejea nyuma kiasi gani.

Kwa hivyo, suala la kwanza ni kurejesha imani ya Wazanzibari katika umoja na uzalendo wao. Njia ambayo nyinyi mnaweza kusaidia ni katika kampeni zenu kuhimiza wajibu, haki na heshima ya kila Mzanzibari bila ya kujali rangi, kabila au sehemu atokayo mtu. Tukubali na tukiri kwamba historia ya visiwa vyetu imejaalia mchanganyiko wa makabila na tamaduni mbalimbali, na hata tukisema kwamba kitovu cha uzawa ni Kizimkazi au Tumbatu, tujue kwamba hata sehemu hizo zilikuwa zimeingiliwa na watu kutoka nje karne nyingi hata kabla ya kuzaliwa Nabii Issa. Yeyote ataekwenda Kizimkazi, Unguja Ukuu, Tumbatu na Pemba ataona ushahidi wa haya. Kwa hivyo huyo Mmakunduchi, Mtumbatu au Mpemba wa leo akitafuta sana nasaba yake asishangae akaona kwamba katika mishipa yake ya damu kuna mchanganyiko wa aina mbalimbali.

Katika historia yetu maovu mengi yametokea mnamo karne za nyuma na hata katika miaka hii hamsini iliyopita kikiwemo pia kipindi cha tangu mapinduzi. Lakini kuna haja ya kukumbushana hayo? Kwanini tufungike na historia hiyo iliyopita badala ya kusonga mbele na kukabiliana na ya leo na ya kesho? Njia ya kuhakikisha kwamba maovu hayatatokea tena ni kuwatia wananchi imani kwamba hakutokuwepo na siasa za ubabe na kutojali, kwamba misingi ya demokrasia na haki za binadamu itawekwa na kuimarishwa, haki muhimu za wananchi zitalindwa, kutakuwa na jitihada za makusudi za kuondosha ufukara na kwamba kila mwananchi atahakikishiwa elimu, matibabu, chakula, mahali pa kuishi, maji safi na atafunguliwa njia za kuendeleza maisha na kipaji chake, na kwamba kila mmoja atawajibika, kutakuwa na uwazi, vyombo imara vitawekwa kusimamia yote hayo, na hakuna hata mmoja atayekuwa juu ya sheria.

Katika kampeni zenu, muwatake wananchi wayasamehe yaliyopita. Naambiwa kwamba wakati Amani anaingia kwenye boti kutoka Dar es Salaam akirejea Zanzibar baada ya mkutano mkuu maalumu wa CCM kule Dodoma, alishindikizwa huku akiwa amekamatwa mkono na Bimkubwa Said Hanga na Ashura Babu. Bila ya kutaka kutonesha makovu, lakini tukio hili lilituonesha haja ya kusameheana: Bimkubwa ni mjane wa Abdallah Kassim Hanga ambaye 'alipotea' wakati wa awamu ya kwanza ya SMZ iliyoongozwa na baba wa Amani, wakati Ashura alikuwa mke wa Abdulrahman Babu ambaye alishitakiwa na kuwekwa kizuizini kwa miaka saba kwa kutuhumiwa kwamba alihusika na kuuawa kwa Mzee Karume. Lakini leo akina mama wote hao wawili wanamuona Amani kuwa ni 'mtoto' wao.

Kuna njia mbalimbali ambazo nchi zilizofikwa na misukosuko kama yetu zimefanya ili kuleta suluhu na amani katika jamii, na zaidi kuhakikisha kwamba misukosuko kama hiyo hairejei tena. Baada ya vita kuu vya pili vya dunia, kulikuwa na Mahakama ya Nuremburg ambayo iliwahukumu wale wakuu wa kifeshisti walioleta maafa duniani, na Afrika ya Kusini walianzisha tume ya ukweli na mapatano ambapo kila mmoja anakwenda kukiri makosa yake na kuomba msamaha. Katika Afrika ya Magharibi, miongoni mwa makabila mengi, kuna desturi kwamba ukimkosea mtu, bila ya kujali ukubwa wa kosa lenyewe, ukaenda tu na kumpigia magoti na kumkamata mguu, basi hana budi ila kukusamehe.

Ilipendekezwa mara baada ya kuchaguliwa Sheikh Idrisa Abdulwakili kama Rais wa Zanzibar, kwamba Rais aitishe mkutano wa hadhara ambapo atawataka radhi wananchi kwa makosa na maovu yote yaliyotokea huko nyuma na kuwataka wayasamehe. Na baada ya hapo aombe zisomwe khitma katika misikiti yote ya Zanzibar na duwa kwenye makanisa na nyumba nyingine za ibada kuwaombea wote wale ambao wamefariki kwa sababu za kisiasa. Na hapo kufungua ukurasa mpya. Wazo hilo lilipuuzwa.

Tumeona katika miaka hii ya karibuni Rais Bill Clinton wa Marekani alipotembelea Senegal alitaka msamaha kwa maovu yaliyotendeka wakati wa biashara ya utumwa; Papa aliomba msamaha kwa makosa ambayo Kanisa Katoliki imeyafanya; na hivi karibuni alipokwenda Israel, Papa ameomba msamaha kwa Mayahudi kwa Kanisa Katoliki kukaa kimya wakati wa mateso yaliyofanywa na Hitler na wafuasi wake dhidi ya Mayahudi kule nchi za Ulaya; serikali ya Marekani imewataka msamaha Wahindi Wekundu (Red Indians) kule Marekani; na serikali ya Australia imewataka msamaha Aborigins wa nchi hiyo; Wairish wanapatana ili wawe na taifa moja; Korea ya kaskazini na ya kusini zimesahau chuki na uhasama wao wa zaidi ya miaka 50 na sasa zinazungumzia juu ya kuungana na kusahau tofauti zao; na Wapalestina na Mayahudi wamo katika jitihada za kutafuta mapatano katika migogoro yao iliyokuwepo tangu mwaka 1948. Tusistaajabu wakati bado tukiwa hai tukashuhudia muungano wa Palestina, Israel, Jordan na Lebanon. Huo ndio mkondo wa historia ya sasa ya ulimwengu.

Ningekuombeni mkalifanya suala hili la kuomba msamaha na kuwataka wananchi kuyasemehe yaliyopita kuwa ni kitu cha kwanza katika kampeni zenu. Na yeyote kati yenu atayeshinda katika uchaguzi ujao kuliweka hilo kuwa ni jambo lake la kwanza katika ajenda yake ya kazi. Vinginevyo, awamu itayoongozwa na yeyote kati yenu itakumbwa na hili 'jinamizi' la historia yetu.

Najuwa kwamba kila mmoja wenu ana matumaini ya ushindi mkubwa. Na hata ikiwa chama kimoja kitapata asilimia thamanini ya kura na kushinda viti 40 kati ya viti 50 vinavyowaniwa, bado chama hicho hakitoweza kuendesha nchi peke yake. Hii ni kwa sababu ya mgawanyiko ndani ya jamii yetu ambao nimeuelezea hapo juu. Mapendekezo mengi ya maana na yenye busara yalitolewa kabla na baada ya uchaguzi mkuu wa mwaka 1995, lakini yalipuuzwa na hata kufanyiwa kejeli. Ni busara kwamba chama chochote kitachoshinda kikikaribishe chama kingine na hata wananchi wengine wasiokuwa na chama kujiunga katika serikali. Madhumuni ni kwamba kila chama, jumuiya na kikundi kihisi kuwa kimeshirikishwa na kwamba kina hisa katika utawala mpya. Hiyo inaweza kuitwa serikali ya mseto (coalition), ya umoja wa kitaifa (national unity) au ya mapatano (reconciliation), lakini la umuhimu ni kwamba itamjumuisha kila mmoja (inclusive). Sera za serikali hiyo bila ya shaka zitatokana na ilani za uchaguzi ya chama kitachoshinda, lakini wengine pia watakuwa wanachangia katika kufanikisha sera nzuri na zenye manufaa kwa taifa.

Naweza kukupeni mfano wa Liberia ambako naishi sasa. Sisemi kuwa hii ni nchi ya demokrasia halisi au kwamba ni mfano wa kuigwa katika utawala bora, lakini kuna kitu kimoja kimenivutia. Katika uchaguzi mkuu wa waka 1997, chama cha NPP kinachoongozwa na Rais Charles Taylor kilishinda asilimia 80 ya kura, na kina viti 49 kati ya viti 64 kwenye Baraza la Wawakilishi na viti 21 kati ya viti 26 ndani ya Baraza la Seneti. Rais Taylor angeweza kuunda serikali bila ya kuwashirikisha wapinzani wake. Lakini kwenye Baraza la Mawaziri kuna Mawaziri 3 kati ya 21, akiwemo waziri wa usalama wa taifa, kutoka vyama vya upinzani, kati ya manaibu waziri 55 basi 29 wanatoka ama vyama vya upinzani au hawana vyama, mkurugenzi mkuu wa baraza la mawaziri (sawa na Katibu Mkuu wa Ikulu huko kwetu) ni kiongozi kutoka moja ya vyama vya upinzani; na kuna watendaji wakuu wa idara za serikali ambao ama ni washabiki wa vyama vya upinzani au hawana vyama. Hivi karibuni kulikuwa na jitihada kutoka chama tawala za kuwaondowa baadhi ya watendaji wa serikali ambao wanajulikana ni wapenzi wa vyama vya upinzani na kuwaweka badala yake wakereketwa wa chama tawala katika nafasi hizo kwa kisingizio kwamba kinataka watendaji wenye kuaminika na chama, lakini jaribio hili lilipingwa na kila kikundi na jumuiya zinazopigania haki za binadamu. Chama tawala kimebidi kiliwache wazo hilo. Kwa hakika katika mkutano wake mkuu uliofanyika miezi michache iliyopita, chama tawala kimebidi kuwataka wanachama wake wanaoshika nafasi za utendaji katika chama na ambao pia ni watendaji wakuu wa serikali, wajiuzulu moja ya nafasi hizo.

Miongoni wa wananchi wenzetu kumekuwepo na hisia tofauti kuhusu muungano. Najuwa pia kwamba vyama vyenu vina mitizamo tofauti juu ya jambo hili. Na mimi sibishi kwamba kuna matatizo mengi ndani ya muungano wenu. Hili ni jambo ambalo ingefaa lijadiliwe kwa uwazi, na mna haki ya kulizungumzia katika kampeni zenu. Lakini ningeshauri kuwa mjadala wenyewe ungefaa uwe unaambatana na ukweli halisi wa mambo, ukitiliwa nguvu na takwimu na nyaraka, na uzito wa hoja, na usivutiwe na jazba na kutaka 'ushindi' wa ufasaha wa kuzunguma. Mkumbuke kwamba kubomowa ni rahisi, kujenga kunataka ujasiri, subira na ustahamilivu.

Kwa yeyote kati yenu ataechaguliwa kutakuwa na haja ya kuangalia upya sera za kiuchumi na kijamii. Nimekuwa nikiwaambia wenzangu kwamba inaonesha nchi yetu ina uwezo mkubwa wa kuwavutia matapeli. Kila mwekezaji tunaeambiwa anakuja amekuwa ni 'bomu'. Ahadi za kuwepo na hoteli ya Holiday Inn pale uwanja wa Maisara; Sun City kule kijiji cha Fumba, hoteli ya kisasa na uwanja wa kuchezea 'golf' kule Mangapwani; hoteli na bandari ya kisasa, benki za nje ya ufukwe wa bahari pamoja na Chuo Kikuu kule Nungwi, na bustani ya viumbe vya baharini kutoka Mzingani mpaka Mambomsiige, yote haya tumeyasikia! Badala yake nchi yetu imekuwa ndio njia kuu ya kupitishia 'unga' huku vijana wetu wakitumbukia katika utumiaji wa madawa ya kulevya na umalaya, wakiwa hawaoni mustakabali wa maisha yao ya baaadaye. Bila ya kuwa na mawazo mapya na kutekeleza sera za kujitegemea na kuwapa wananchi uwezo wa kiuchumi, basi nchi itazidi kudidimia. Na bila kuhifadhi, kuendeleza na kudumisha utamaduni wetu, na kusita kuendekeza huu 'utamaduni wa coca-cola', basi fundisha chuo kikuu cha Middlessex Uingereza. Bahati mbaya kwamba alipokuja Zanzibar miaka miwili iliyopita, hakuna hata mmoja aliyemdhukuru. Kuna pia wafanyabiashara wa Kizanzibari waliofanikiwa katika nchi za nje: huduma za vyakula zinazotolewa pale uwanja wa ndege wa Harare kwa wasafiri na ndege zinazotuwa hapo zinatolewa na kampuni inayomilikiwa na Mzanzibari. Sio wote walioondoka Zanzibar wameondoka kwa sababu za kisiasa, na baada ya Jamshid kupewa msamaha na kukaribishwa arejee, sioni tena hata hao walioondoka kwa sababu za kisiasa wasiweze nao kukaribishwa. La muhimu ni kuwaona hawa ndugu zetu waliopo nchi za nje kuwa ni raslimali kubwa ambayo pindi ikihamasishwa na kuelekezwa, na kutotiliwa mashaka na wasiwasi, basi inaweza kusaidia sana katika maendeleo yetu.

Wenzetu wa Jamhuri ya China wanawatumia vizuri Machina wanaoishi ncih za nje kwa kuwavutia waweke rasilimali zao China, watowe ujuzi wao na hata kuwapeleka watoto wao kusoma China katika baadhi ya fani. Mayahudi kokote walipo wanasaidia Israel; na chama cha PLO kwa miaka mingi kimeendeleza mipango yake ya elimu na huduma za jamii kwa kutegemea michango ya Wapalestina wanaoishi katika nchi mbalimbali.

Msimamo wa Seif na chama cha CUF juu ya Tume ya Uchaguzi unajulikana. Sijui mawazo ya Amani kuhusu Tume hiyo; na CCM, tangu baada ya uchaguzi mkuu wa 1995, haikutamka kitu juu ya Tume, ijapokuwa tunakumbuka ile barua iliyopelekwa kwa Tume na Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar kabla ya kutangazwa matokeo ya uchaguzi wa mwaka 1995,

Lakini kama washindani wakuu katika uchaguzi ujao itabidi muafikiane juu ya huyu msimamizi mkuu wa uchaguzi huo. Ikiwa nyote au m moja wenu hana imani na Tume hiyo, basi si ajabu tukaingia kwenye mgogoro ule ule tunaojaribu kuuepuka safari hii.

Kwa katiba na sheria ya uchaguzi zilivyo, hakuna mwenye madaraka ya kuwabadili wajumbe wa Tume mara wateuliwapo na Mheshimiwa Rais. Lakini kwa kuitakia salama Zanzibar (na Tanzania) na kuepusha malumbano ambayo yatazidi kuleta chuki na uhasama na kuirejesha nyuma zaidi nchi yetu, ningeshaurini kwamba nyote kwa pamoja mngewaomba wajumbe wa sasa wa Tume wakajiuzulu kwa hiari yao na kumuomba Mheshimiwa Rais kuteua wajumbe wengine ambao wataonekana na jamii kwamba si washabiki wa upande wowote ule.

Hili linawezekana kwani mtakumbuka kwamba mwaka 1995 Maalim Mwinshiwesa Idarous aliombwa kujiuzulu kama Mwenyekiti wa Tume kwa kuhisiwa kwamba kwa sababu ya mahusiano yake ya karibu na chama tawala, huenda akapendelea upande mmoja, na alifanya hivyo. Ni vizuri ikiwa nyinyi na vyama vyenu mkaingia katika mashindano haya mkiwa na imani na Tume kwamba itatenda na kusimamia haki.

La mwisho ni kukuombeni kuwataka wanachama wenu na wananchi wenzetu kwa ujumla kuhakikisha kwamba tunakuwa na uchaguzi wa amani na salama. Tafadhalini msiwaachie jazba na hamasa kutawala, badala yake muhubiri busara, hekima na upandeo ambazo ndizo nguzo za mila na maadili yetu.

Hayo yote ninayokwambieni ni kutoka moyoni mwangu kwa kuwa, kama usemi wa Kiswahili usemavyo, kuishi kwingi ni kuona mengi. Wajibu wangu kama msomi ni kushauri na kutanabaisha pale nnapoona kuna kasoro au njia tuifuatayo itatupeleka pabaya. Ni hairi yenu kama wanasiasa kuukubali au kuukataa ushauri mnaopewa. Lakini ni wajibu wa wananchi kuhakikisha kwamba hawaongozwi kwenye giza na ukosefu wa matumaini.

Bahati mbaya kwamba safari hii sitoweza kupiga kura kwani nitakaporejea nchini muda wa kujiandikisha kama mpiga kura utakuwa umemalizika. Lakini nakutakieni kila la kheri. Yeyote kati yenu atayeshinda kwenye uchaguzi ambao utaonekana na kuthibitishwa kwamba ni huru na wa haki awe na uhakika wa kupata ushirikiano wangu (pindipo atauihitaji).

Wasalaam,

Profesa Haroub Othman
Monrovia, Liberia
Tel & Fax 231 - 226636
Mobile 231 - 227103 dial tone 282033
E-Mail: namtho@hotmail.com
Haroub.Othman@undp.org
 
--
JuuRUDI


Bonyeza hapa
kushriki mjadala au kutoa maoni juu ya habari hizi na masuala mengineyo ya Kiislamu kwenye Baraza ya Wasomaji

   Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu: Bonyeza hapa
Au
Andika barua  kwa: webmaster@islamtz.org
 
An-nuur Home | Ukurasa wa Mwanzo | Islam Tanzania 
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook