KILA jamii ya watu ina mila, desturi na maadili yake, na kila mtu wa jamii hiyo anatakiwa aendane na maadili hayo na anapoenda kinyume na hivyo inavyotakiwa huonekana kama muovu.
Mila, desturi na maadili ya watu wa Kiafrika hutofautiana na watu wa Magharibi (Ulaya) kama tofauti iliyopo kati ya maadili mema ya Kiislamu na dini nyingine, mfano Kiislamu ni haramu kunywa pombe lakini Kikristo yasemekana ipo ruhusa kunywa ati lakini usilewe.
Mila, desturi na maadili ya jamii fulani ikitumiwa katika jamii ya watu wengine huonekana ni kinyume na kupotosha watu wa jamii hiyo.
Kwa hakika mtoto hufunzwa desturi, maadili na mila za jamii yake na pia anaishi kwa kufuatana nazo.
Sio mzazi au mlezi pekee anapaswa kumfunza mtoto maadili mema bali pia jamii nzima kwa ujumla ikiwemo Taasisi za elimu na dini, vyombo vya habari na kadhalika.
Je, watoto hao watafunza vipi? Sio taabu wala shida na pia si kwa njia ngumu ila mtoto anaweza kufundishwa kupitia michezo ya kuigiza, majarida, hadithi, nyimbo au kuwepo darasani.
Njia hizo zinaweza kumfundisha mtoto akaelewa na kufuata maadili ya jamii yake tu na si maadili na desturi za jamii nyingine.
Hapa Tanzania, mambo yamekuwa kinyume, njia zinazotakiwa kumfundisha mtoto maadili mazuri ili asipotee ndio zimekuwa za kumpotosha, kama televisheni zetu zinaonesha michezo na nyimbo mbalimbali ambazo zinawapotosha watoto wetu.
Kubwa na baya zaidi ni kwa sasa majarida mengi ya hadithi yanayosambazwa nchini yanalenga mambo ya mapenzi (ngono) yanayooneshwa wazi wazi kwa michoro.
Majarida hayo huwekwa kwenye meza na kusambazwa kama mpunga ulioanikwa ili ukauke, tena maganda ya majarida hayo yamechorwa picha za wanawake nusu uchi na mwanaume ambayo kwa kweli hayastahili kuoneshwa wazi.
Majarida hayo huuzwa sehemu zenye msongamano wa watu kama sokoni na kwenye vituo vya mabasi ambapo kila mtu huweza kuona na kusoma bila hata kununua.
Katika vituo vya mabasi kuna makundi ya wanafunzi ambao hupoteza muda mwinig kusoma na kuangalia majarida hayo.
Wanafunzi hao ni watoto na hawapotezi muda tu kuangalia ila pia hupoteza hizo pesa kidogo anazopewa na wazazi wake kwa kununua majarida hayo.
Waziri wa Habari wa zamani Zanzibar, Mohamed Seif Khatib aliwahi kukataza majarida yanayolenga ngono, lakini inavyoonesha serikali haifuatilii kwani serikali yenyewe ndio inayotoa vibali kwa majarida hayo.
Wanaomiliki na kusambaza majarida hayo wanafaidika na kupata faida kubwa kwani soko la majarida hayo linazidi kuwa kubwa kadri siku zinavyozidi kusonga mbele. Kwa maana hiyo maadili ya Kitanzania na Kiislamu yanaporomoka kwa kasi sana.
Akili ya mtoto ni rahisi kushika chochote kiwe kizuri, kiwe kibaya ni lazima tu kitakaa akilini mwake.
Watoto ndio wanaotegemewa kuwa wazazi wa kesho, je, tunavyozidi kuruhusu majarida hayo yaendelee kupanua soko lake, wazazi wa kesho upeo wao wa akili utakuwaje?
Suala hili ni lazima tulifikirie kwa undani zaidi na athari zinazoendelea kujitokeza na hasa kwa miaka ijayo.
Ikiwa majarida hayo yataendelea kuruhusiwa kuuzwa,
basi kuna hatari ya mila, desturi na maadili ya Kiislamu na Kitanzania
hupotea kabisa na watu kuishi kama wanyama.
--
![]()
|
|