BARUA
Viongozi wa Zanzibar mjueni na muogopeni Allah

Ndugu Mhariri

IMEKUWA ni kawaida kwa viongozi wetu kumsahau Mwenyezi Mungu wanapokuwa madarakani hata kama walikuwa Masheikh hapo kabla, lao kubwa baada ya kupata madaraka ni kutafuta jina la Alhaj.

Baada ya hapo husahau kabisa , atakapotoka madarakani ndio hurudi tena, jee! nawauliza wamechukua dhamana kwa Mungu kuwa wakati wakiwa madarakani hatokufa? Je, hivi nyinyi mnafanyia khiyana Mungu na pia raia wenu?

Mwisho ni juu ya Salmin, Amani, Seif na wale wote wanaohusika kukaa pamoja na kuwatengenezea Wazanzibari mazingira mazuri ya uchaguzi na maisha yao kwa ujumla, kwani machafuko ya aina yoyote hayana faida na sisi na wao peke yao ndio wakataobeba masuulia mbele ya Mwenyezi Mungu siku hiyo na sisi tuko tunawashitaki.

Wajue dhulma zao kwetu hatutokwenda mahakama ya kimataifa bali siku hiyo mbele ya Mwenyezi Mungu ndio mahakama yetu na Yeye ndiye Hakimu wetu.

Mwisho kabisa, nawaomba Wazanzibari na Watanzania kwa jumla watuchagulie viongozi wenye nguvu, waaminifu na wanaojali hali za watu.

Nasoro Hamad,
Dar es Salaam.


Kiza kimetanda kweli

Ndugu Mhariri

TUMEJITOKEZA kwa mara ya kwanza kutoa maoni yetu. Kwanza tunampongeza Bw. Juma S.Kagoma kwa barua yake ya Julai 21, mwaka huu yenye kichwa cha habari kisomekacho: "Waliokuwa gizani wamekwishapata ushauri"?

Sisi tunasema bado kabisa. Kwanza wamekiri kuwa amani na upendo vimetoweka. Hilo limedhihiri hivi karibuni katika 'kula' za maoni za kupendekeza wagombea wa viti vya udiwani kwa tiketi ya CCM.

Ugomvi ulitawala nchi nzima. Hivyo imethibitisha wimbo ule usemao.Amani kwao imetoweka, kiza kwao kimetanda hawajui pakukamata. Hivyo inadhihirisha maneno ya hayati Kolimba kuwa CCM hawana dira wala muelekeo.

Omary H. Mbegu,
Yassin K. Sanda,
Dunia Maulid,
S.L.P. 15212,
Kigogo Darajani,
Dar es Salaam.


Kitabu cha Mwembechai Killings kwa Kiswahili

Ndugu Mhariri

KWA mara nyingine naomba unipe nafasi ili nichangie machache kupitia gazeti lako (letu) AN-NUUR. Napenda kutoa shukurani zangu za dhati kwa mtunzi wa kitabu "Mwembechai Killings" na InshaAllah malipo yake ni kwa Allah (s.w.) kwani kazi aliyoifanya ni mfano wa kuigwa japokuwa kitabu hicho kimezuiliwa uwanja wa ndege wa Dar es Salaam lakini kwa wenye kuweza kutumia wavu wa kimataifa (Internet) tayari wanakisoma vya kutosha na kwa uwezo wa Allah (s.w.) kitaruhusiwa tu muda si mrefu.

Sasa ombi langu ni kwamba kitabu hicho kifasiriwe kwa lugha ya Kiswahili kama kilivyofasiriwa kitabu kilichotungwa na Zainab Al Ghazal ili Waislamu wengi waweze kukisoma na kuelewa vya kutosha.

Rassanye Ally Saddiq,
Ilala,
Dar es Salaam. 
--
JuuRUDI


Bonyeza hapa
kushriki mjadala au kutoa maoni juu ya habari hizi na masuala mengineyo ya Kiislamu kwenye Baraza ya Wasomaji

   Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu: Bonyeza hapa
Au
Andika barua  kwa: webmaster@islamtz.org
 
An-nuur Home | Ukurasa wa Mwanzo | Islam Tanzania 
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook