KUTOKA MAGAZETI YA ZAMANI
Wahindi toka Msumbiji walia kuporwa na Mreno
Mwafrika, Agosti 28, 1962

UNYANG'ANYI wa nguvu uliofanyiwa Wahindi kadhaa waliotoka Msumbuji hivi majuzi waliueleza Mombasa kama wa "kikatili sana". Walieleza kwamba mali zao walizozitolea jasho kwa muda wa miaka mingi zote wamenyang'anywa na serikali ya Kireno huko Msumbiji.

Ukatili huu ulielezwa na Wahindi hao waliotoka huko, ambao walikataliwa kupewa idhini ya kuchukua mali zao pia vyombo vya nyumbani, na baada ya hapo mali zao zikafilisiwa kabisa na kufanywa mali ya serikali ya Ureno katika Msumbiji.

Kundi hili la watu wapatao ishirini waliomba majina yao yahifadhiwe ili uvumi huo usije ukamfikia Mreno na akazidi kuwakatili ndugu zetu waliobaki huko. Mzee mmoja na bibi yake walieleza kwa masikitiko makubwa kwamba sisi tumeishi kule kwa muda wa miaka arobaini na sasa tunarudishwa India kwa nguvu. Yule bibi kizee yakimtoka machozi kwa wingi alisema "tunarudi kama maskini na tumepoteza mali yetu yote tuliochuma kwa muda wa miaka arobaini".

Waliendelea kuniambia kwamba wote hao waliotolewa huko walilazimishwa kutia sahihi mkataba usemao "wanatoka huko kwa hiari yao na sio kama wanafukuzwa".


Waislamu wazidi kujitoa CCM
Mizani, Julai 2, 1993

MAELFU ya waumni wa dini ya Kiislamu wanazidi kukikimbia Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwa kukusanya kadi za chama hicho ili hatimaye zikabidhiwe kwa viongozi wa ngazi za juu ikiw ani kuonesha kukasirishwa kwao na matamshi ya Waziri wa Mambo ya Ndani wakati wa kuwasaka wale serikali iliyowaita jina "Waislamu wenye siasa kali" ambapo alinukuliwa mara kadhaa akidai kuwa viongozi hao walikuwa ni "wahuni", "majambazi" na wenye kutumia madawa ya kulevya.

Muumini mmoja kutoka Bagamoyo ambaye alikuwa na furushi la kadi za CCM zipatazo 700 alizikusanya kutoka kwa waumini wa wilaya hiyo, alimwambia mwandishi wa habari hizi kuwa, watu waliokamatwa kwa madai ya kuvunja mabucha ya nyama ya nguruwe huko Manzese, Dar es Salaam ni Masheikh, Maimamu na wahadhiri lakini "hili kuwa hawa ni majambazi tumelisikia kwa Bw. Mrema" alisema muumini huyo ambaye hakutaka jina lake litajwe.

Muumini huyo alisema, CCM ndiyo inayostahili lawama kwa kuwa ndiyo iliyompa madaraka Waziri Mrema ya kuweza kuwadhalilisha viongozi wa dini ya Kiislamu na kuwaita wahuni. Na inapofikia hatua viongozi wa serikali kuwakashifu Masheikh ambao wanaaminiwa na jumuiya ya Waislamu ni wazi kuwa wakati huo ni serikali yenyewe imejitoea hadharani kupambana na imani ya raia zake, alifafanua.

"Tunajitoa CCM ili kukiacha chama hicho katika usafi bila ya wanachama wahuni na wavuta bangi ambao ni sisi Waislamu", alisema muumini huyo na kuongeza "kama viongozi wa CCM wanaweza kumwita mtu kama Sheikh Kassim, Sheikh Yahya, Maimamu na wahadhir kadhaa waliokamatwa kuwasingizia bila ushahidi wowote kuwa ni wala madawa ya kulevya, wahaini, majambazi, vidudunjia, wavuta bangi, vichwa maji, basi na sisi tunaoongozwa nao tutakuwa ni wendawazimu kabisa na sidhani kama CCM wana haja na wanachama kama hao".

Hata hivyo, waumini wengi wanaamini kuwa kampeni ya Waziri Mrema ya kupambana na Waislamu ilikuwa ni njama za kuwahujumu viongozi wa Kiislamu kutokana na baadhi ya kauli zake alizokuwa akitoa na kama vile kudai kuwa yeye mwenyewe (Mrema) angemvua Joho la kidini Sheikh Kassim na kisha kumpiga ngumi. "Kama kupambana naye kwa masumbwi kama hiyo ni chuki tu na udini" Aliuliza Sheikh Shaaban mmoja wa wakereketwa wa Kiislamu.

Wakati akiamuru Sheikh Kassim bin Jumaa akamatwe, Waziri Mrema alimtaja kiongozi huyo mwenye wafuasi wengi Waislamu kuwa "Ni mzizi wa fitina... ni mfuasi wa kikundi kinachojiita cha Waislamu wenye msimamo mkali... Hawa ni vidudunjia wachumia tumbo ambao wamenunuliwa na mabwana zao huko nje kusudi wavuruge amani ya Tanzania kwa manufaa yao binafsi".Lakini Waziri huyo mpaka sasa hajafafanua hao mabwana waliomnunua Sheikh Kassim ni kutoka wapi na ni kwa kiasi gani cha fedha walizomnunua.

Mpaka sasa zaidi ya kadi 46103 zimekwishakusanywa na kuna taarifa mikoa kadhaa imeitikia na zoezi hilo linaendelea vizuri. Mikoa ambayo kadi zinaendelea kukusanywa kimya kimya ni Arusha, Mwanza, Tabora, Kigoma, Morogoro, Dar es Salaam, Mbeya, Kilimanjaro, Tanga na katika wilaya za Handeni na Bagamoyo.

Pamoja na Waislamu kukusanya kadi za CCM kwa wingi mkubwa kutokana na kuwapa Waislamu majina mabaya ya uhaini na ulevi kulikofanywa na Waziri Mrema, mpaka sasa bado hakuna tetesi yoyote kuwa waumini hao watajiunga na chama gani cha kisiasa katika vyama kadhaa vilivyopo. Lakini kuna minong'ono kuwa wanajiondoa katika CCM ili kuepusha kuchanganya dini na siasa, na pia wengine wanadai kuwa Waziri Mrema ajiuzulu kutokana na kuwakashifu Waislamu na viongozi wao.

Wakati huo huo, maelfu ya waumini wamemchagua Sheikh Kassim bin Juma bin Khamis kuwa Imam wao na wameahidi kumtii na kujitoa mhanga pamoja naye katika kuuhami Uislamu na kutetea maslahi ya Waislamu. Kuanzia sasa Sheikh Kassim atatambulika miongoni mwa wafuasi wake kama "Imam". 
--
JuuRUDI


Bonyeza hapa
kushriki mjadala au kutoa maoni juu ya habari hizi na masuala mengineyo ya Kiislamu kwenye Baraza ya Wasomaji

   Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu: Bonyeza hapa
Au
Andika barua  kwa: webmaster@islamtz.org
 
An-nuur Home | Ukurasa wa Mwanzo | Islam Tanzania 
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook