RIWAYA
Joka la Mdimu -15

KWA miaka mingi Gray Kwacha alikereketwa na azma ya kujenga nyumba itakayovunja kiburi cha wenzake. Kwanza alitafakari namna ya kupata kiwanja. Viwanja vilitolewa kwa mgugumbaro: nipe nikupe. Kashfa kadha wa kadha zilifichuliwa kuhusiana na Halmashauri ya Jiji la Mindule kwa namna yao ya kutoa viwanja. Watu walisota, nenda rudi miaka zaidi ya kumi bila ya viwanja. Waliojiweza walicheza mchezo utakiwao wakakabidhiwa muradi wao. Walio wengi walikata tamaa, ghadhabu zikawapanda na kuwatuma kujenga Sega na sehemu nyingine kama hizo: kwenye maporomoko na hata mitaro ya maji machafu.

Lakini Gray Kwacha alikuwa mtu wa nyendo,akajua karata gani aicheze na ipi aibakishe. Alisema kwa kiburi, suala sio kupata kiwanja ila mahali panapofaa kuporomosha jumba la kifahari. Basi kwa muda wa juma, kila jioni aliendesha gari lake sehemu mbalimbali za ufuko wa bahari kutafuta mahali pa kumfaa. Hatimaye alipata sehemu mbili ikawa aamue achague ipi. Bali uamuzi huo ulimuwia vigumu. Alirejea nyumbani kutafakari bila ya kumuhusisha mke wake. Zaidi ya miaka sita sasa alikuwa hamshirikishi mkewe katika maamuzi yake yoyote. Hakumtaka la kheri wala la shari. Baada ya kuwaza sana akapata wazo la kuvichukua viwanja vyote. Atajenga kimoja baada ya kimoja. Fedha sio tatizo.

Na kweli, juma lililofuatia uamuzi wake huo alikwenda kuonana na Mkuregenzi wa Jiji. Mwenyekiti wa Kamati ya Uwagaji Viwanja aliitwa na kutakiwa aweke jina la Gray Kwacha katika orodha ya wanaopendekezwa kupatiwa viwanja.

Basi, juma lililofuatia Gray Kwacha akawasilishiwa hati mbili za kumiliki viwanja, tena vile alivyovitaka. Zikabaki hatua nyingine tatu: Kutafuta michoro ya nyumba yenyewe, kontrakta wa kuzijenga na kisingizio cha mkopo wa kuzijenga. Azma ya kuvunja kiburi cha 'wenzake' ilimfanya apagawe na shauku ya ajabu.

Jijini pale palikuwa na kampuni kadha za wasanii majengo na kontrakta. Maarufu kati ya hizo ilimilikiwa na serikali. Nyingine chache zilikuwa za Kimarekani, Kijerumani, Kifaransa, Kiingereza na Kitaliani. Gray Kwacha alizitembelea kampuni hizo akaoneshwa sampuli mbalimbali za michoro ya nyumba za fahari. Alizinunua sampuli hizo na kwenda nazo ofisini ambako alibaki baada ya saa za kazi kuzipitia huku ametumbua macho. Katika uchaguzi huo mkali hatimaye ilibakia michoro minne ya kampuni za Kimarekani, Kijerumani, Kifaransa na Kitaliani. Kila mchoro ulimvutia kwa aina yake. Mwisho alivutiwa na michoro miwili: ule wa Kifaransa uliokuwa na ghorofa moja, na ule wa Kijerumani uliokuwa na paa la mfuto. Michoro yote ilionesha kwa undani kila kitu, hadi sehemu za kuegesha gari, miti, mabwawa ya kuogelea na wigo kuzizunguka nyumba zenyewe.

Aliketi tena kwa mwezi mmoja akiziachia fikra zake ziyumbe hivi na vile. Katika kipindi hicho alitembelewa kwanza na kontrakta mkuu wa Kitaliani, baadaye wa Kimarekani, halafu wa Kiingeleza na mwisho wa Kifaransa kumchombeza atie mkataba wa kujengewa nyumba nao. Majadiliano hayo yalifanyika ofisini, na kuendelea hadi nje hotelini ambako maakuli yalifuatiliwa na vinywaji. Mameneja walitoa makadirio ya gharama za ujenzi, vifaa vitakavyotumika pamoja na muda wenyewe. Kwa ujumla ile kampuni ya Kitaliani na Kiingereza zilikuwa na masharti nafuu ya ujenzi, ila Kwacha hakuvutiwa na michoro ya nyumba zao. Na hakutaka kampuni hizo zijenge nyumba zile kwa michoro ya kampuni nyingine. Vizuri, nitaamua, aliwajibu mameneja wote kwa kiungwana maana biashara haigombi.

Kimya tena kilipita, ndipo ghafla akaenda ofisini kwa meneja wa ile kampuni ya Kifaransa na baadaye ile ya Kijerumani. Gharama ya nyumba iliyokuwa ijengwe na Wafaransa ilikuwa shilingi milioni mia mbili na nusu na ile nyingine milioni mia tatu. Vifaa vyote, isipokuwa mbao na saruji vilikuwa vitoke nje.

Hatimaye Gray Kwacha alichagua michoro ya Kijerumani na Kifaransa akatia saini mikataba ya ujenzi na kulipa nusu ya fedha zote za ujenzi.

Sasa ikabakia kisingizio. Alikwenda katika Benki ya Backlays na kuchukua mkopo wa shilingi milioni ishirini, ndipo roho ikamchelea kidogo.

Siku baada ya siku ujenzi uliendelea. Mafundi walipeana zamu kuanzia asubuhi lama machweo ya jua. Kila jioni, isipokuwa kwa siku alizosafiri, Kwacha alivitembelea viwanja vyake kuona namna ujenzi ulivyoendelea. Matembezi hayo yalizua mashindano ya ndani baina ya makampuni yale mawili ya ujenzi.

Nyumba ya kwanza kumalizika ilikuwa ile iliyojengwa na kampuni ya Kijerumani. Ilikuwa nyumba kubwa ya vyumba vinne vya kulala na veranda kubwa sana yenye madirisha ya vioo vitupu kuanzia juu hadi chini. Bila kushusha mapazia mtu aliye ndani angejiona kama yuko nje. Nyumba hii ilikuwa na paa la mfuto. Ilizungukwa na eka mbili za bustani ya mawaridi na maua mengine ya kuvutia macho. Kati ya maua hayo mlipandwa ukoka ambao kutokana na kunyunyuziwa maji asubuhi na jioni ulimea na kuwa mithili ya zuria la kijani. Hatua chache Kaskazini mwa nyumba hiyo lilitua bwawa la wastani la kuogelea. Fenicha za nyumba hii ziliagizwa kutoka Sweden na baadhi kutoka pale pale hasa zile za mbao. Kontrakta alimwingiza Kwacha ndani ya nyumba yake kuikagua baadaye alimkabidhi funguo za milango yote na kila sehemu iliyostahili kufungwa na kufunguliwa. Naye, kimya kimya, alizipokea funguo hizo, bila ya kumueleza mkewe.

Afanye nini na nyumba ile? Tangu hapo mwanzo alikwishaamua kuwa yeye si mtu wa kulala chini bali ghorofani. Isitoshe usalama wa nyumba ile yenye vioo vitupu ulihitaji ulinzi mkubwa mno. Mwisho kimya kimya alitiliana saini mkataba na ubalozi wa nchi moja ya nje kuipangisha nyumba hiyo kwa msharti ya kulipia kodi ya miaka mitano yote kwa pamoja, kwa dola za Kimarekani.

Nyumba ya pili ilimalizika miezi mitatu baadaye. Ilikuwa nyumba ya kipekee. Ilisimama na kuzibeza nyumba zote jirani na hapo kwa haiba yake, na bwana lake la kuogelea. Kwacha alimtafuta mtaalamu wa Korea na kumtengenezea bustani kuizunguka nyumba hiyo. Halafu akamtafuta mtunza bustani maarufu kupita wote pale jijini, akamuajiri aitunze bustani yake kila Jumamosi. Hatimaye Gray Kwacha alimfahamisha mkewe kukamilika kwa nyumba hii na mipango yake ya kuhamia kule.

Kuhamia kwenyewe kuliadhimishwa kwa sherehe iliyojaa furaha na karaha. Viti vilipangwa kando ya bwawa la kuogelea, muziki ukapigwa na vileo vikanywewa. Waalikwa walikuwa wastahiki, wazee kwa vijana, wake kwa waume, kuanzia mawaziri, makatibu wakuu, viongozi wa chama kimoja cha siasa kilichokuwa kinatawala na wengine kadha wa kadha.

Nyama ya kukaangwa ya mbuzi, kuku, nguruwe ilipitishwa miongoni mwa watu waliokuwa wamesimama kwa kunogewa na mazungumzo, na wengine waliokuwa wameketi katika maongezi au kuangalia maji ya bluu ya bwawa lile jipya la kuogelea.

Sherehe hiyo ilianzia saa moja na kufikia saa tatu mambo yaliuma. Vijana walijimwaga kucheza muziki.

Karibu na ile sehemu iliyokuwa inachezwa muziki aliketi Katibu Mkuu wa Wizara ya Mila na Utamaduni, hapungui miaka hamsini na ushei. Kumtazama umoja tu, alionekana kuwepo pale kiwiliwili tu. Alipitisha macho yake huku na kule kuwadeku wachezaji taratibu akinywa brandy yake. Mara moja moja alisimama kwenda kwenye bwawa kuangalia maji yakimetameta kuitikia miali ya taa za mviringo zilizokuwa pembeni mwa bwawa hilo. Baadaye alirejea alipoketi awali akakaza macho kuitazama mbingu ambako nyota zilikuwa zikimetameta juu ya blanketi zito la mbingu nyeusi. Lakini yote hayo yalikuwa si kitu si chochote. Katibu Mkuu yule alitawaliwa na fikra za kumkosa kimada wake. Ni kweli kuwa hakumpa taarifa ya kutoka naye nje, lakini aliwaza hiyo haikuwa sababu ya kutomkuta nyumbani kwake.

Nyumba alimpangia, kivazi alimkatia, chakula alimnunulia na haja nyingine za mwilini kumtoshelezea, sasa nini tena? Muziki wa taratibu ulishamiri kuwatumbuiza waalikwa ila mawazo ya bwana yule yaliruka mbali mno, yalipotua naye akapumua kwa kite. Mwili ulimzizima kwa simanzi. Saa hizi angekuwa naye akisakata muziki. Sasa yiko wapi saa hivi? Lahaula! Kushuka macho macho mbele hakuamini! Kwani mbele yake alisimama kijana mrefu jamali mkono wake wa kushoto umeshuka hadi juu kidogo tu ya makalio. Wote, wasichana na mwanaume wale walitopea katika dunia yao kwa wao, maana ndege kwenye mti lala, haruki hendi mahala.

Moyo ulimpapa yule bwana, akatukana, na kusema. Leo nimemfeli. Lakini ndiye au siye? Uso wa yule msichana ulikuwa umelala mno kifuani pa yule kijana ikawa vigumu kuutambua wajihi wake. Lakini mbona miguu kama yake? Viatu vile sivyo alivyomletea juzi kutoka Paris? Na hata lile gauni alilovaa si alimnunulia London. Shenzi! Ghafla akavundumka na kuweka glasi ya kinywaji chini kwa nguvu hadi ikaalika na kuvunjika. Akapiga hatua moja, mbili tatu, akawa mkabala na yule kijana aliyekuwa anacheza na yule msichana wake.

"Nini mzee"? yule kijana aliuliza kwa mshangao, akaendelea, "Ndiyo mapishi yamekubali nini?"

"Wee Esther?" yule Katibu alifoka kama faru aliyejeruhiwa. Pata shika ikaanza kwa mzee na kijana kutupiana makonde makali. Wakaanza kuserereka ukingoni mwa bwawa.Hata kaumu ya waalikwa ilipotaharuki Katibu Mkuu na kijana waliteleza na kutumbukia bwawani kwa kishindo pwacha? Zogo likahanikiza pote.

*****

Saa tatu kamili usiku watoto wa Gray Kwacha wote mabinti, walimaliza kuangalia video wakaenda chumbani kwa mama yao kumuaga.

"Mama lala salama", walisema kwa mpigo. Mama yao aliyekuwa anafuma vitambaa, kama kupitisha muda tu, aliinua macho kuwaangalia binti zake.

"Mmechoka kuangalia video?"

"Aa! Tumeshaziona mara nyingi. Tunataka nyingine".

"Na baba yenu mwaogopa kumwambia".

Walibaki kimya kama walioshtushwa na kauli ile.

Kimya kilipita na hatimaye binti wale wakaondoka kuelekea vitandani mwao wakitafakari kauli ile. Walipania mno lau na kungekuwa na maelewano na upendo mkubwa baina ya baba na mama yao. Licha ya ukosefu huo, baba yao alikuwa mkali na isipokuwa alipokuwa na wageni, au kuumwa, hakurejea nyumbani lama saa nne au tano usiku. Na hakutaka maongezi na binti zake, hata yule mdogo kabisa. Walikula wakashiba, wakapelekwa shule kwa gari, wakafuliwa nguo na mtumishi, wakanunuliwa kila kitu walichohitaji, ila walikosa raha.

Mke wa Gray Kwacha hakuwa na kitu mahsusi kilichomfanya avutie. Alikuwa na umbo la simba, mpana kifuani mwembamba kiunoni. Utovu wa kazi, chakula kizuri na nafasi vilimfanya afure na kuwa kufi la mama. Binti zake wale watatu aliwazaa katika kipindi cha miaka mitano mfululizo, mmoja baada ya mwingine. Wa mwisho alikuwa na miaka minne akisoma darasa la pili katika shule ya kimataifa, pamoja na dada zake.

Huko kwao wanawake wenzake waliyalilia ngoa maisha yake ya ndoa na mumewe Gray Kwacha pasi kumaizi kuwa sumu hufichwa kwenye vikombe vya dhahabu. Baina yake na mumewe palikuwa na mkato mithili ya wembe; mgumu kuonekana kwa macho ila kwa madhara yake. Alikonda akajipa moyo, akarudisha hali yake, akakonda tena. Hivyo hivyo! Mara nyingine aliwashawishi binti zake kwenda nao likizo ili akajiliwaze na kuliwazwa. Gray Kwacha alifurahia mno kila wasaa wa namna hiyo ambao ulimpa uhuru wa kuranda na kuwanda. Lakini wala sio, kwani kuna siku ambayo mkewe alimnyima uhuru wake? Mara ya mwisho mkewe alimpiga hawara yake alitishia kumfukuza nyumbani. Wazazi, ndugu na jamaa wakamueleza vumilia, atatulia. Asumbuliwa na ujana walimnasihi. Mwache afanye yake nawe jali yako, wengine walimshauri. Lakini akawajibu na kusisitiza, siwezi kwenda kinyume na ndoa, alijikaza.
--
JuuRUDI


Bonyeza hapa
kushriki mjadala au kutoa maoni juu ya habari hizi na masuala mengineyo ya Kiislamu kwenye Baraza ya Wasomaji

   Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu: Bonyeza hapa
Au
Andika barua  kwa: webmaster@islamtz.org
 
An-nuur Home | Ukurasa wa Mwanzo | Islam Tanzania 
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook