Akiongea na mwandishi wa gazeti hili mwishoni mwa wiki katika moja ya tawi la TLP lililopo kati ya mtaa wa Mkunguni na Likoma Kariakoo, Bw. Seifu Said Mbelwa ameeleza kuwa katika tawi la kaskazini Kariakoo (TLP) limebakiwa na Katibu.
"Wanachama wote waliokuwa TLP wamehama na kujiunga na CUF, aliyebaki sasa ni Katibu tu wa tawi hilo", amesema Bw. Mbelwa.
Akiongelea sababu ya wanachama hao kukihama chama hicho (TLP) alieleza kuwa ni kutokana na Mwenyekiti wa chama hicho (TLP) Bw. Augustine Mrema kukataa Azimio la Muungano wa vyama vya upinzani.
Aidha, ameeleza kuwa sababu nyingine ni kutokana na kuonekana wazi kuwa CUF ndiyo yenye sera za kukomboa wananchi na hakina migogoro baina ya viongozi.
"Wameona chama cha Wananchi (CUF) ndiyo chenye matumaini na nguvu za kuweza kuleta mabadiliko katika nchi hii na hakina mvutano baina ya viongozi wa juu", amesema Mbelwa.
Bw. Seif Mbelwa ambaye pia ni mgombea Udiwani kwa tiketi ya chama cha CUF, jimbo la Ilala amesema kuwa tawi hilo lina zaidi ya vijana 120 ambao tayari wana kadi za CUF pia wameshapandisha bendera ya CUF pembeni mwa bendera ya TLP.
Diwani huyo mtarajiwa (Mbelwa) amesema, matawi mengine mawili ya TLP ambayo yamegeuka kuwa CUF yapo maeneo ya Ilala Kota jijini.
"Utaratibu wa kufungua rasmi matawi haya mapya ya CUF, unafanywa na Katibu wa jimbo Bw. Sheshe, na yanatarajia kufunguliwa na mmoja wa viongozi wa juu wa CUF", amesema.
Wakiongea kwa nyakati tofauti, baadhi ya wana CUF hao wapya wa mtaa wa Mkunguni na Likoma wamesema, wao walitaka umoja ili kuimarisha nguvu zaidi.
"Sisi tulitaka umoja, maana mpinzani wetu ni CCM, kitendo cha Mwenyekiti wetu (Mrema) kukataa umoja, tukaamua tukajiunga na CUF", amesema Bw. Musa Ramadhani.
Bw. Kisanga Ngoma amesema, "Mrema ni CCM 'B',
hana tofauti na CCM kwa hali hiyo anatudanganya wananchi, na tutarudisha
kadi za TLP rasmi siku ya ufunguzi wa tawi, nae abakie na jogoo lake".
OFISI ya Kadhi inayotarajiwa kuundwa imetajwa kuwa jinamizi jingine la kuwazuga Waislamu.
Hayo yameelezwa na Waislamu mbalimbali kufuatia kasi ya suala hilo kujadiliwa huku Waislamu wenyewe wakiwa hawashirikishwi.
"Nimesikia suala la ukadhi linajadiliwa na akina Augustino, Robert na Ford Foundation, wenyewe hatuna habari. Hili ni jinamizi lingine linaumuliwa", amesema Ustadh Juma wa Manzese.
"Ni kweli tunataka mahakama za Kiislamu, lakini ziwe kweli za Kiislamu na kwa ajili ya Uislamu", amesema Bw. Abdul Rahim.
Akiongea na Mwandishi wa habari hizi amesema, Unguja kuna ofisi ya Kadhi, Waislamu wa Bara kabla ya kuukubali ukadhi unaoelekea kuundwa na serikali wangeuliza kwa wenzao visiwani wajue ofisi hiyo imekuwa na faida gani.
Naye Sheikh Bassaleh akizungumzia suala hili ameitaka serikali kuwashirikisha waumini katika kuanzisha ofisi ya Kadhi Mkuu nchini.
Sheikh Ally Bassaleh alikuwa akiwahutubia Waislamu kwenye swala ya Ijumaa iliyoswaliwa katika Msikiti wa Sheikh Idrisa, Kariakoo mjini Dar es Salaam.
Alisema, ili kuweza kuunda ofisi ya Kadhi Mkuu ambaye atasimamia hukumu na sheria za Kiislamu hapana budi serikali kuwapa fursa Waislamu wenyewe wahusika badala ya kuwaundia kama BAKWATA.
"Ikiwa serikali imebaini umuhimu wa Waislamu kuwa na Kadhi wao basi watuachie wenyewe kuunda na kuendesha ofisi hiyo badala ya kutuundia kama ilivyofanya mwaka 1968 kwa kuunda BAKWATA ambalo kwa yakini si baraza la Kiislamu bali kundi fulani kwa masilahi ya serikali", alisema Sheikh Bassaleh.
Alisema, Waislamu ndio wenye haki ya kutafuta Kadhi wao kwa vile wanatambua yupi anayepaswa na sio kutafutiwa kama vile Waislamu vipofu.
Sheikh Bassaleh alieleza kuwa kwenye kongamano lililofanyika jijini na kushirikisha nchi za Uganda, Sudan, Afrika Kusini na wenyeji Tanzania, Waislamu wa nchi nyingine walituma wawakilishi wao, isipokuwa Tanzania iliyowakilishwa na Jaji Augustine Ramadhan na Robert Makaramba ambao si Waislamu.
Katika maelezo yake, Sheikh Bassaleh alihoji kuna umuhimu wa kuendelea kuwepo kwa Baraza hilo na ndipo waumini waliporipuka kwa kauli hatulitaki!
Sheikh huyo baada ya kupata jibu hilo, alisema,
upo umuhimu wa Waislamu kushirikishwa katika mambo yao ikiwemo kuundwa
na kuanzishwa kwa ofisi ya Kadhi Mkuu nchini na kuionya serikali kutotia
mkono wake kwa mara ya pili kama ilivyofanya kwa Baraza hilo.
--
![]()
|
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook |