Vijana CUF wanolewa

CHAMA cha CUF kimewataka vijana wake watakaokwenda sehemu mbalimbali nchini kwa ajili ya kampeni ya uchaguzi mkuu ujao, kutumia busara na unyenyekevu katika jamii.

Hayo yamesemwa na Naibu Katibu Mkuu Bara, Bw. Wilfred Lwakatare jana katika semina ya kuwaandaa vijana maalum kwa ajili ya kampeni ya kitaifa ndani ya ukumbi wa Starlight jijini.

"Mnatakiwa kuwa na mahusiano mazuri mbele ya jamii, kutumia busara kuliko jazba na tabia njema. Kwani wewe ni kioo cha chama", amesema Bw. Lwakatare.

Vijana hao wameelezwa kujenga mahusiano ya mtu na mtu, pamoja na kuwashawishi watu ili wakubali kujiunga na Chama chao (CUF) bila kutumia nguvu.

"Tunakaa na watu wengi, wazee, vijana wa aina tofauti tofauti, hawa tunahitaji kuwashawishi mtu anayeshawishi hatumii nguvu wala mabavu ni hoja tu", amesema Bw. Lwakatare.

Aidha, alieleza kuwa wao wana hoja nyingi za kushawishi jamii na wakaungwa mkono, amesema hoja ya vishawishi ni kuwa nchi hii ina matatizo mengi ya kijamii.

"Mambo kama ajira kwa vijana, viwanda kufa, barabara mbovu, hayo ni mambo ambayo serikali ya CCM imeshindwa kuyatatua kabisa", amesema na kuongeza, "CCM haiwezi kupinga hayo kwani ndiyo ipo madarakani na sasa hivi wanatumia fedha kwa kuwa vijana wengi wanashida ya fedha".

Pia aliwataka vijana hao kuwatoa woga wananchi wa vijijini na kuwaelimisha juu ya haki zao.

"Tuwaeleze jamii kwamba wakipewa pesa na wagombea wa CCM wapokee na kura ni siri yao wawanyime", amesisitiza.

Naye Bw. Ernest Lyanda akichangaia katika semina hiyo aliwaeleza vijana hao kuwa watakutana na mambo mengi haswa vitisho, pia aliwataka wakawafute ujinga wananchi wa vijijini, kwani CCM ndio wanatumia ujinga huo kuwadanganya.

"CCM wanatumia sana ujinga wa wananchi, endapo wataondokewa na ujinga ni wazi wanajua (CCM) watang'oka madarakani, hivyo muelewe kuwa mtatishwa ili msifikie lengo", amesema Bw. Lyanda.

Aliwaeleza kuwa CUF ni chama halali na kimesajiliwa kisheria.

"Tunatakiwa kuwa ngangari kwa kufuata sheria na taratibu zinavyosema, sisi ni wanachama halali tuliosajiliwa, hivyo tuna haki ya kutangaza, kuelimisha jamii", amesema Bw. Ernest Lyanda.


Japan kupunguza wimbi la Machinga


WIMBI la vijana kutoka mikoa ya Mtwara na Lindi, huenda likapungua kadiri upatikanaji ajira utakavyoimarika.

Kuelekea lengo hilo, serikali ya Japan imetoa msaada kuimarisha Chuo cha Ufundi Mtwara (Mtwara Vocational Training Centre).

Msaada huo ni vifaa vya kufundishia ufundi katika fani 11, vyenye thamani ya shilingi bilioni 2.5 (339,000,000 yen).

Kwa msaada huo, Chuo kitakuwa na uwezo wa kutoa mafunzo ya ufundi katika fani11. Mashuhuri katika fani hizo ikiwa ni Ufundi magari, umeme, useremala, uwashi, cherehani na utengenezaji vifaa kama majokofu na radio.

Aidha, Chuo kitakuwa na uwezo wa kuchukua wanafunzi wapatao 2350.

Mkuu wa mamlaka ya mafunzo ya ufundi nchini (VETA) Dkt. Adelhelm Meru amesema kuwa wanafunzi 2000 watakuwa ni wa kozi fupi za kila mara wakati 350 watakuwa wa kozi ndefu.

Akiongea na mwandishi wa habari hizi baada ya utiwaji saini msaada huo, Bw. Meru amesema, Chuo cha Ufundi Mtwara kitakuwa cha pili kwa ukubwa baada ya kile cha Chang'ombe Dar es Salaam. Amesema, Chuo hicho kimedhamiria kutoa vijana wenye ujuzi.



Masheikh upambe si kazi yenu

"Lengo letu si kutoa wasomi wenye nadharia nyingi vichwani. Bali ujuzi. Sisi hatutoi watu watafutao kazi bali tunazalisha kazi", amesema Bw. Meru.

Amesema, Chuo cha Ufundi Mtwara kilianza kujengwa mwaka 1997 kwa juhudi na michango ya wafanyakazi.

Dkt. Adelhelm Meru amesema, chuo kilianza kupokea wanafunzi mwaka jana. Kilianza na wanafunzi 80 katika fani 5 wakiwepo waalimu 10.

Hata hivyo, amesema, chuo kilianza kikiwa hakina vifaa ila vichache vya kuazima.

Dkt. Meru amesema msaada wa Japan utahusisha pia waalimu na wataalamu ambao watasadia ufungaji wa vifaa chuoni pamoja na utoaji wa mafunzo kwa waalimu kwa miezi mitatu juu ya namna ya kutumia vifaa hivyo.

Msaada mwingine uliotolewa na serikali ya Japan ni ule wa vifaa kwa Radio Tanzania.

Msaada huo ni wa sh. bilioni 10.5 (1,434,000,000 yen).

Msaada huo unajumuisha ujenzi wa Studio mpya na kituo cha kurushia matangazo Kunduchi.

Hafla ya kutiwa saini mkataba wa kutolewa msaada huo ilifanyika jana Wizara ya Fedha.

Balozi wa Japan nchini, Bw. Keitaro Sato aliweka sahihi kwa niaba ya nchi yake wakati Katibu wa kudumu Wizara ya Fedha Bw. Peter J. Ngumbulu aliiwakilisha serikali ya Tanzania.

Balozi wa Japan baada ya kusaini amesema, amefurahi kwani ahadi ya misaada hiyo iliyokuwa imetolewa na Waziri Mkuu wa zamani wa Japan Hayati Obuchi, imetekelezwa.


Kikundi cha wazee Moro chashutumiwa kufanya vurugu msikitini

KIKUNDI cha watu wanaodaiwa kutumiwa na baadhi ya viongozi wa chama tawala mjini morogoro ijumaa iliyopita kilivamia msikiti wa Mafiga mjini humo na kuvuruga swala ya Ijumaa.

Kikundi hicho kinachodaiwa kuwa ni cha wazee kilisababisha mtafaruku ambao ulipelekea baadhi ya watu kujeruhiwa.

Wazee hao wametajwa kuwa ni Salum Mdede, Mzee Lukwere, Abdul Waziri Koba na imamu Mohamed.

Akielezea mkasa huo mmoja waumini wa msikiti huo aliyejitambulisha kwa jina la Musa amesema watu hao wakiongozwa na kijana mmoja aliyemtaja kwa jina la Dadi Ramadhani Kambi kilivamia msikiti huo wakati Khatib akiwa mimbarini.

Kwa mujibu wa itikadi ya kiislamu Khatib wa swala ya Ijumaa awapo mimbarini imeelekezwa pasiwepo mazungumzo au shughuli nyingine na waumini hutakiwa kusikiliza kwa makini ujumbe huo wa ijumaa.

Hata hivyo pamoja na kulijua hilo, kikundi hicho kimedaiwa kuvuruga itifaki nzima ambapo inasemekana aliyeongoza operesheni hiyo aliingia msikitini na viatu na kwenda moja kwa moja kumnyang'anya Khatib Kipaza sauti.

"Wakati wazee hao wakifanya hayo, waumini waliendelea kutulia mpaka alipofikia kuanza kutoa maneno yasiyohusika ndipo mtafaruku wa kumtoa nje ulipotokea".

Imeelezwa hata hivyo vurugu hiyo haikuendelea na swala ya Ijumaa iliendelea kama ilivyopangwa.

Bwana Musa amesema vijana wawili kutoka kikundi hicho cha wazee walifika tena msikitini hapo siku ya jumapili julai 23, majira ya magharibi na kutaka kuvuruga darasa lililokuwa likiendelea.

"Bwana Dadi alifika akiongozana na mtu mwingine wakiwa wameshika nondo na mabomba, walizima taa ghafla na kuamuru watu waliokuwemo ndani watoke nje, waumini hao walikataa na kujaribu kuiwasha tena taa hiyo", alieleza kijana huyo na kuongoza, "Dadi akarusha nondo bahati nzuri haikumpta mtu, waumini hao walijaribu kumshika lakini aliendelea kuwashambulia kwa silaha hizo".

Imeelezwa kuwa kijana huyo alifika msikitini hapo akionekana mwenye kujiamini na alijiandaa kimapambano dhidi ya waumini wa msikiti huo.

Wakati purukushani ya kumdhibiti asiendelee kuleta madhara kwa waumini hao ikiendelea, imedaiwa baadhi ya watu walikwenda kutoa taarifa polisi ambako hata hivyo inasemekana maelezo yao hayakupewa uzito.

"Wakati tunaandikisha 'statementi' ya kuvamiwa msikitini, walifika wazee akina Salum Mdede waliomtuma Dadi kuleta vurugu msikitini na mmoja wa maafisa wa kituo hicho alimuamuru afisa aliyekuwa akichukuwa maelezo yetu aache kwa madai kwamba sisi ndio watu wa vurugu na wazee kama hao hawawezi kufanya mambo hayo ya kihuni", ameeleza bwana Musa.

Inasemekana afisa huyo aliamuru waumini waliotangulia kutoa maelezo polisi wawekwe mahabusu na ifunguliwe kesi dhidi yao ya kusababisha vurugu msikitini na kutaka kuteka nyara uongozi wa msikiti.

Imeelezwa kufuatia amri ya kamanda huyo waumini hao waliofanyiwa vurugu msikitini kwao na wengine waliokamatwa katika msako waliwekwa mahabusu kwa muda wa siku tatu kabla ya kufikishwa rumande.

Majina ya waliofikishwa mahakamani ni Ramadhani Sanze(34), Mbarara Abdallah Maharagande(29) na Shaaban Vigulo(40).

Wengine ni Juma Mohammed Sultan "Kijoka" (32) Munawwar Mussa Rubajuma(22) na Hussein Bashir.

Watuhumiwa wote wako nje kwa dhamana hadi kesi yao itakapotajwa tena mahakamani hapo.

Katika siku za hivi karibuni kumezuka hali inayotuhumiwa kuchochewa na viongozi wa CCM au vyombo vya dola ambapo Misikiti huvamiwa na waumini kukamatwa wakidaiwa kufanya vurugu au kuzungumza siasa za upinzani.

Mara kadhaa polisi imeonekana kusaidia watu walio dhidi ya waumini ili kujenga mazingira ya kutekeleza kile kinachoonekana "mpango maalum" wa kudhibiti waumini wa dini ya Kiislamu.

--
JuuRUDI


Bonyeza hapa
kushriki mjadala au kutoa maoni juu ya habari hizi na masuala mengineyo ya Kiislamu kwenye Baraza ya Wasomaji

   Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu: Bonyeza hapa
Au
Andika barua  kwa: webmaster@islamtz.org
An-nuur Home | Ukurasa wa Mwanzo | Islam Tanzania
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook