Ujasusi wa zama za KGB- 6:
KGB ndani ya idara ya usalama ya Misri

ILI kuwa karibu zaidi na Soviet na kujitenga na nchi za magharibi Bwana Sharraf alichochea maandamano yaliyofanyika Mwezi Novemba 1967 Jijini Cairo ambayo yalimalizika kwa kuchomwa moto maktaba ya Marekani.

Kwa "uchapa kazi mzuri" wa Bwana Sharraf, KGB uliufanya mji wa Cairo kuwa kituo kikuu cha operesheni za kijasusi. Endelea.

Mnamo mwezi mei mwaka 1970, aliyekuwa balozi wa Soviet nchini Misri, Sergei Vinogradov kwa maelekezo ya pesoneli kuu kutoka mjini Moscow, alimwita Jijini Cairo bwana Sakharov aliyekuwa afisa wake mjini Alexandria.

Wito huo ilikuwa ni kumfahamisha majukumu na wadhifa mpya aliopewa ikiwa ni pamoja na kuhamishwa kituo cha kazi kutoka Alexandria kuja Cairo.

Promosheni hiyo ilifuatia kuridhishwa kwa makao makuu ya shirika hilo na utendaji kazi wa afisa huyo wa kirusi ambaye kwa muda mrefu aliendeshea shughuli zake za ujasusi nje ya Cairo.

Ufanisi wa majasusi wa Soviet mjini Cairo, mahusiano ya kijeshi kati ya Soviet na Misri yaliyotiwa saini na ajenti wake Bwana Sharraf kwa upande Misri, yaliiwezesha KGB kwa kushirikiana na GRU(Soviet Military Intelligence), kujipenyeza kwa wapiganaji wa msituni wa kipalestina waliokuwa wakiendesha mapambano dhidi ya utawala wa Israel.

"Lengo la kujipenyeza huku ilikuwa kuondoa ushawishi wa China kwa Wapalestina mpango ambao ungeiwezesha Soviet kuzitia mkononi nchi za kiarabu kupitia mapambano yao na Taifa la Israil", ilieleza taarifa moja ya kijasusi iliyochapishwa katika jarida la New York Times la septemba 18, 1972.

Baadaye KGB ikiendesha harakati za msituni za wapalestina, ilidaiwa kuwa iliziamuru balozi zote Soviet kutoendesha shughuli zozote na wapalestina bila ya malekezo ya makao makuu.

"Agizo hilo lilitolewa mei 10, 1971 ambapo mawasiliano na wapalestina iliamriwa yafanywe na maafisa wa KGB, GRU, au kamati ya Soviet ya mahusiano na nchi Afrika na Asia", zilidai taarifa za kijasusi zilizochapishwa na baadhi ya mashirika ya habari ya nchi za magharibi.

Pamoja na kujipenyeza kikamilifu nchini Misri mpango KGB "kuiteka Misri" ulivurugika baada ya kifo cha Nasser.

Aliyemrithi Rais huyo, Bwana Anwar Saadat alionekana kutaka kuwa huru kimaamuzi, kutokana msimamo huo Soviet ilipanga kumng'oa madarakani mnamo mwaka 1971. Hata hivyo jaribio hilo lilishindwa.

Inaelezwa njama hizo ziliandaliwa mjini Moscow ambako baada ya ujumbe wa maafisa wa ngazi za juu wa Misri ukiongozwa na bwana Sharraf kualikwa kuwa wasikilizaji katika mkutano wa 24 chama tawala cha Soviet, KGB ilitumia fursa hiyo kufanya mazungumzo ya siri na bwana Sharraf kuhusiana na mpango wa mapinduzi iliyokusudia kuufanya nchini Misri.

Kufuatia mazungumzo hayo, bwana Sharraf alilazimika kubaki Moscow wakati wajumbe wengine wakirejea Misri. Sababu aliyoitoa juu ya kubakia huko ilikuwa ni ya kuangaliwa afya yake.

Ukielezea tukio hilo, mtandao wa kijasusi wa nchi za magharibi ulidai Soviet ilikusudia kuweka serikali mpya ambayo viongozi wake wangekuwa wapokezi wa maagizo na malekezo kutoka Moscow, hata hivyo ilidaiwa serikali ya Saadat iligundua njama hizo.

Bwana Sami Sharraf na maofisa wenziwe katika idara ya usalama ya Misri wapatao 90 waliotuhumiwa kuhusika na njama hizo kwa kushirikiana na KGB na GRU walikamatwa.

Sharraf alihukumiwa adhabu ya kifo kwa kosa la uhaini ambayo hata hivyo, baadaye ilibadilishwa ikawa kifungo cha maisha jela.

--
JuuRUDI


Bonyeza hapa
kushriki mjadala au kutoa maoni juu ya habari hizi na masuala mengineyo ya Kiislamu kwenye Baraza ya Wasomaji

   Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu: Bonyeza hapa
Au
Andika barua  kwa: webmaster@islamtz.org
An-nuur Home | Ukurasa wa Mwanzo | Islam Tanzania
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook