KATIKA mazuri ya Uislamu na katika uliyokuja nayo yenye kuwasahilishia watu yao ni kuwa hakukuharimisha jambo ila umeweka badala yake jambo lililo bora zaidi lichukuwe mahali pake na kutosheleza kujiepusha na lile baya, kama alivyobainisha haya Ibn Qayiim (Mungu amrehemu).
Mwenyezi Mungu amewaharimishia kutazamia kwa mishale akawapa badala yake dua ya Istikhara.
Akawaharimishia riba na kuwapa badala yake biashara yenye kuleta faida.
Akawaharimishia kamari na kuwapa badala yake ruhusa ya kula mali kwa mashindano yenye manufaa katika dini, kwa mafarasi na ngamia na kutupa mishale.
Akawaharimishia hariri na kuwapa badala yake aina mbalimbali za kivazi chesma cha sufi na katani na pamba.
Akawaharimishia zinaa na liwati na kuwapa badala yake ndoa ya halali.
Akawaharimishia kunywa vileo na kuwapa badala yake vinywaji vitamu vyenye manufaa kwa roho na kiwiliwili. Akawaharimishia vyakula vibaya na kuwapa badala yake vyakula vizuri.
Vivyo hivyo, tukichungua hukumu za Kiislamu zote, tutakuta kuwa Mwenyezi Mungu hakuwadhiki waja wake katika jambo ila huwapa wasaa na nafasi katika jambo jengine linalolingana na lile, kwani yeye Mola aliyetukuka hawatakii waja wake la shida, wala mashaka wala taabu, bali anawatakia wepesi na kheri na hidaya na rehema kama alivyosema:
Mwenyezi Mungu anataka kukubainishieni na kukuongozeni katika mwendo wa wale waliokutangulieni, na anapenda kukukhofishieni . Na Mwenyezi Mungu ni Mjuzi na mwenye hekima. Mwenyezi Mungu anataka kukukhafishieni, lakini wanaofuata matamanio yao wanataka mpotoke upotofu mkubwa (uliokhalifu haki). Mwenyezi Mungu anataka kukukhafifishieni maana mwanadamu ameumbwa dhaifu (hana nguvu kubwa za kiwiliwili wala nguvu kubwa za kupigana na moyo na shetani). (An-Nisaa: 26-28)
Linalosababisha haramu ni haramu
Katika misingi iliyowekwa na Uislamu katika masuala ya halali na haramu ni kuwa jambo likiharimishwa basi huharimishwa na kila njia ambayo itamwasilisha mtu katika jambo lile, na husimama Uislamu kutazama kila uchochoro unaofikisha kwenye jambo hilo ukauziba na kuuwekea vikwazo.
Kwa hivyo, ukiwa umeharimisha zinaa kwa mfano, basi huharimisha kila lenye kuanzisha na kusababisha ovu hilo, kama kutojistiri Kiislamu au kupatikana faragha baina ya watoto wa kike na kiume, au kuchanganyika wavulana na wasichana katika mahali pamoja bila ya stara wala sitaha, au kuwepo mapicha ya uchi yenye kusisimua matamanio ya vijana, au nyimbo chafu na kadhalika.
Kwa ajili ya mambo haya, Maulamaa wa Fikihi wameweka kanuni ya kuzuia mambo kama haya: Kila lenye kusababisha ya haramu ni haramu. Nayo inashabihiana na kawaida iliyowekwa na Uislamu ya kuwa dhambi za jambo la haramu, hupata siyo tu mwenye kufanya peke yake bali humfikia kila aliyeshiriki katika kulifanya ikiwa kwa vitendo au maneno, na kila mmoja wao hupata dhambi kwa kiasi alivyoshiriki.
Na ndio maana tunamuona Mtume (s.a.w.) katika masuala ya ulevi, amemlaani mwenye kunywa, mwenye kugema na kufanya, mwenye kuchukua na mwenye kupelekewa na mwenye kuuza kama tutakavyoeleza baadaye. Halikadhalika, katika riba, amemlaani mwenye kula na mwenye kupewa na mwenye kuandika na mwenye kushuhudia.
Na kama hivyo, kila chenye kusaidia haramu huwa haramu na kila mwenye kusaidia katika haramu huwa mshirika katika madhambi.
Kutumia hila katika kuhalalisha ya haramu ni haramu
Kama ulivyoharimisha Uislamu kila njia za dhahiri zinazopelekea kwenye haramu, halikadhalika umeharimisha kutumia hila katika kutenda ya haramu kwa njia za ujanja za kishetani na uliwalaumu sana Mayahudi kwa yale waliyoyafanya katika kuhalalisha aliyoyaharimisha Mungu kwa kutumia hila. Akasema Mtume (s.a.w.): (Msifanye waliyoyafanya Mahayudi na kuhalalisha yale yaliyoharimishwa na Mwenyezi Mungu kwa chembe ya hila).
Haya ni kwa kuwa Mwenyezi Mungu aliwaharimishia Mahayudi kuvua samaki siku ya Jumamosi, wakataka kumhadaa Mola wao, wakawa wanachimba mahandaki siku ya Ijumaa ili watumbukie humo samaki siku ya Jumamosi wapate kuja kuwachukuwa siku ya Jumapili, na hila kama hizi katika Uislamu ni haramu kwani makusudio ni kujizuiya na kuvua moja kwa moja siku ile ikiwa kwa njia ya hila au ya sawa sawa.
Na katika hila chafu zinazotumika ni kukiita kitu kilichoharimishwa kwa jina lisilokuwa lake na kubadilisha umbo lake ilhali hakika yake ni ile ile, na bila ya shaka ya kuwa hapana faida ya kubadilisha jina na kugeuza umbo ikiwa hakika ya kitu iko pale pale.
Basi ikiwa watu wamevumbua njia za kula riba kwa kutumia hila au wameleta majina mapya ya ulevi wanayatumia kwa kuhalalisha kunywa kwake, madhambi ya riba na ulevi yako pale pale hayaondoki, na mambo kama haya yameelezwa na Mtume (s.a.w.) tokea zama zake, akasema:
(Kikundi cha watu katika umma wangu kitahalalisha ulevi watakaouita kwa majina mengine yasiyokuwa yake).
(Itawajia watu zama, watahalalisha riba kwa jina la biashara).
Haya yote yamedhihiri katika zama zetu hizi, na yaliyo ya ajabu mengine ya wakati wetu huu ni huitwa michezo ya ngoma za kihuni (ustadi) na ulevi (vinywaji vya kuburudisha) na riba (faida) na mengineyo chungu zima yanayohalalishwa kwa kutumia hila hizi na hizi.
Nia njema haiwi sababu ya kufanya ya haramu
Uislamu unakadiri na kukisia sababu za kheri, kusudi jema na nia nzuri katika sharia zake zote na maelekezo yake yote, hata Mtume (s.a.w.) amesema: )Hakika vitendo ni kwa mujibu wa nia ya mtu, na kila mtu atalipwa kwa mujibu wa nia yake).
Aidha, nia njema huvifanya hata vitendo vya desturi vya halali kuwa ni njia ya kuonesha utiifu na kujikurubisha kwa Mwenyezi Mungu maadamu ni kwa ajili yake Yeye.
Kwani kila mwenye kula chakula chake cha halali kwa nia ya kuhifadhi uhai wake na kukipa nguvu kiwiliwili chake ili aweze kufanya wajibu wake kwa Mola wake na umma wake, huwa chakula chake na kinywaji chake ni ibada na njia ya kujikurubisha kwa Mola wake.
Vile vile, mwenye kuyaendea matamanio yake kwa mkewe kwa nia ya kupata mtoto wa kheri au kujikinga na machafu yeye na mkewe, jambo hili la starehe huwa ni ibada inayostahiki thawabu. Na haya yamethibiti kwa maneno yake Mtume (s.a.w.) wakati siku moja aliposema: (Na katika kulala kwenu na wake zenu ni sadaka). Wakamuuliza: (Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu, katika kuyaendea mmoja wetu katika matamanio yake hupata thawabu pia?) Akajibu: (Jee, angekuwa ameyaweka matamanio yake katika haramu, si angepata madhambi? Basi kadhalika akiyaweka katika halali hupata thawabu).
Vivyo hivyo, kila kitendo cha halali afanyacho Muislamu akatia nia njema hugeuka kuwa ibada. Ama haramu, hubakia kuwa haramu hata ikiwa itafanywa kwa madhumuni mema na makusudio matakatifu namna gani, wala Uislamu hauradhi kamwe kufanywa haramu ndio njia ya kufikia kwenye shabaha yake, kwani Uislamu unajibidiisha kupatikana lengo jema lakini hufikiwa kwa njia yoyote ile) Au (kuifikia haki kwa namna yoyote ile hata kwa kutumbukia katika batili). Bali inatuwajibikia katika Uislamu kuifikia haki kwa njia ya haki peke yake.
Basi mwenye kukusanya mali kwa njia za riba au za haramu kama kuuza ulevi au kucheza kamari au kitendo kilichokatazwa ili ajenge Msikiti au afanye lolote la heri, nia yake hiyo njema haitoweza kumsaidia kwa kumshufaiya au kumuombea msamaha na kumuondolea madhambi yake ya kufanya haramu hizo, kwani katika Uislamu nia njema haigeuzi la haramu kuwa halali.
Haya ndiyo aliyotufundisha Mtume (s.a.w.) aliposema: (Hakika Mwenyezi Mungu ni mzuri. Naye hakubali ila zuri na Mwenyezi Mungu amewaamrisha wale walioamini yale aliyowaamrisha Mitume wake). Kisha akasoma:
Enyi Mitume! Kuleni vyakula vizuri na fanyeni mema. Hakika mimi ni Mjuzi wa (yote) mnayoyatenda. (Al-Muuminun: 51)
Enyi mlioamini! Kuleni vizuri tulivyokuruzukuni. (Al-Baqaarah: 172)
Kisha akamtaja: (Mtu anakwenda safari ndefu, nywele matimutimu, amejaa vumbi - anakwenda kufanya hija au umra na kadhalika anainua mikono yake mbinguni akiomba "Ewe Mola, Ewe Mola" na huku chakula chake ni haramu na kinywaji chake ni haramu na kivazi chake ni haramu na kulisha kwake analisha kwa haramu, basi vipi mtu huyo atajibiwa dua yake?)
Vile vile akasema: (Hapati mja mali ya haramu kisha akayatoa sadaka akakubaliwa, wala akawapa watu wake akabarikiwa katika mali hayo, wala akayawacha nyuma ya mgongo wake (baada ya kufa kwake) ila huwa akiba yake ya kumtia motoni. Hakika Mwenyezi Mungu aliyetukuka hafuti baya kwa baya, walakini hufuta baya kwa zuri, hakika ovu haliwezi kufuta ovu.
|
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook |