KUUJUA Uislamu ni elimu na kila Muislamu anatakiwa aujue Uislamu wake. Kwa kweli muumini mjinga asiyejua dini anakuwa sawa na bendera inayofuata upepo.
Katika hadithi nyingi za Mtume (s.a.w.) muumini wa aina hii ametolewa kasoro nyingi.
Kwa sababu ya kuuelewa umuhimu wa elimu, Uislamu umehimiza Waislamu kuitafuta na kujifunza elimu.
Mfumo wa maisha ya Muislamu umetawaliwa na sheria maalum ambapo ili mtu aishi kama Muislamu wa kweli inambidi awe na elimu.
Elimu huanza tangu utoto. Ni utaratibu uliopo tangu kutangaza kwa Uislamu kwa watoto wa Kiislamu kupelekwa katika madrasa kusoma elimu.
Hapo zamani wazazi walikuwa wakichukua jukumu la kuwasomesha wenyewe watoto wao ambapo kwa siku hizi hutegemea zaidi madrasa.
Kwa sababu hii miji yenye Waislamu wengi madrasa za watoto huonekana katika kila kona ya mji.
Uislamu haukubagui elimu itakayomletea manufaa binadamu katika dunia na akhera hivyo Uislamu haukuhimiza elimu ya dini tu bali hata ya dunia.
Kama wasemavyo wahenga kuwa elimu haina mwisho binadamu hujifunza kila siku hivyo Muislamu hujifunza elimu katika utoto na utu uzima kwa kadiri na kwa kiwango atakachoweza au kutosheka nacho.
Hata hivyo kiwango ambacho Muislamu anatakiwa afikirie ni kuijua misingi ya Uislamu wake kama vile nguzo za Uislamu na imani.
Jambo ambalo kwa kweli hivi sasa linasikitisha ni kwamba wazazi wengi wamesahau ule wajibu wao wa kuwapa elimu watoto wao.
Wazazi wengi huwahimiza watoto wao kwenda sahule ili kupata elimu ya dunia na kuisahau elimu ya dini.
Hii leo Waislamu tunakutwa na mitihani mingi kwa sababu ya kukosa elimu ya dini miongoni mwetu.
Vitendo vya Waislamu kushindwa kuutetea Uislamu wao pale inapolazimika na kufikia kudhalilishwa au kujifanyia mambo kinyume na misingi ya Uislamu ni matokeo ya ukosefu wa elimu ya dini.
Uchunguzi uliofanywa na mwandishi wa gazeti hili katika mji wa Tanga ambao hadi katika miaka ya 1980 ulikuwa umetapakaa madrasa nyingi za watoto, hivi sasa una madrasa chache za watoto baada ya baadhi ya madrasa hizo kufa kwa kukosa watoto.
Nyingi ya zile madrasa zilizobaki zina idadi ndogo ya watoto ikilinganishwa na miaka ya nyuma.
Ustadh Salim Rashid Mazrui mmiliki wa madrasa Taalimu iliopo barabara 19 mjini Tanga na ambayo ni moja ya madrasa maarufu na ya miaka mingi mjini Tanga anasema sababu kubwa iliyofanya baadhi ya madrasa hizo kukosa watoto ni tatizo la wazazi wenyewe kutowajibika na watoto wao.
Anasema wazazi hawawahimizi watoto wao kwenda kusoma hasa pale wanapoonesha uvivu kama vile wanavyowahimiza kwenda shule.
"Mzazi anaridhika akimuona mtoto wake anaenda shule, lakini hamuulizi mbona hukwenda madrasa leo", anasema Ustadh Mazrui.
"Jambo hili linawapa dhana watoto kuona kuwa shule ni muhimu kuliko madrasa na hivyo kuendelea kukwepa masomo ya dini", anabainisha.
Anasema, matokeo yake ni mtoto kuacha kabisa masomo ya dini.
Ustadh Mazrui anaeleza sababu nyingine ya upungufu wa watoto kwenye madrasa kuwa ni baadhi ya watoto kuachishwa kusoma na wazazi wao baada ya watoto hao kuwashitakia kuwa wamechapwa na walimu wao.
"Jambo la ajabu ni kuwa hata shule watoto huchapwa wanapokosa lakini wazazi hawawaachiehi masomo ya shule", anadai.
Anabainisha kuwa jambo hili hutokea na kuendelea kwa vile hakuna sheria ya kumlazimisha mzazi kulepeleka mtoto kusoma madrasa kama ilivyo kwa shule za serikali.
Katika mazungumzo yake na mwandishi wa gazeti hili Ustadh Mazrui anawashauri Masheikh kuwaelimisha Waislamu umuhimu wa elimu ya dini na wajibu walionao wazazi kuwapa elimu watoto wao.
"Masheikh wana wajibu mkubwa wa kuwaelimisha Waislamu kwamba elimu ni faradhi kwa Waislamu hivyo ni lazima watoto wa Kiislamu wahimizwe kusoma", anasisitiza Ustadh Mazrui.
|
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook |