MNAMO Julai 25, wiki hii mazungumzo ya kutafuta amani ya Mashariki ya Kati huko Camp David, Marekani yalimalizika bila ya maafikiano.Kikwazo kikubwa kikiwa ni hadhi ya mji wa Jerusalem. Makala hii inauelezea zaidi mji huo na hali ya mahusiano ya wakazi wake. Kama ilivyotafsiriwa kutoka gazeti la News Week la Julai 24, mwaka huu.
Kwenye ncha ya uchochoro uliogiza unaotokea mtaa wa maduka ya chini kwa chini, ndipo nyumbani kwa Issa Muhammad al Sharawnesh na mkewe Sabha. Nyumba yao imeelekezana na nyumba ya Mungu.
Mawe yake yamekuwa nyororo kutokana na kuguswa kiutii kwa karne na karne. Pangekuwa pahala pazuri pa kuishi lakini wakina Sharawneh ni Waislamu na Mungu aliyetajwa ni wa Kiyahudi. Ukuta huo ni sehemu ndogo ya magofu ya Kiyahudi ya enzi za Heroda ambapo jumba hilo liliharibiwa na Warumi mnamo mwaka 70 B.K.
Kwa miaka mingi sasa, kikundi cha Wayahudi wenye msimamo mkali kimekuwa kikija hapa kusali na kuimba kwa mbwembwe. Wanaamini kuwa upande wa pili wa ukuta huo ndio katikati ya ulimwengu wote. Kufuatana na imani ya Kiyadi hapo ndipo Mungu alipokusanya vumbi la kumuumba Adam (a.s.) ambapo Cain alimuua Abel na hapo ndipo Ibrahim (a.s.) alipomtoa sadaka mwanawe ( .
Uwepo Mungu hapo ni mkubwa kiasi ambacho kwa sheria ya Kiyahudi ya halacha binadamu hana utohara wa kupita juu ya jengo takatifu (Templement) lililopo hapo, mpaka iwe siku hiyo ndiyo ujio wa Messiah.
"Wana makelele mno, na hawana staha kwa maisha yetu ya faragha", analalamika bwana Issa Muhammad mwenye umri wa miaka 52, ambaye familia yake imeishia hapo kwenye mji mkongwe kwa vizazi na vizazi. Mke wake ndiye mkali zaidi, anasisitiza. "Mayahudi hawana pao hapa, hii ni sehemu takatifu ya Uislamu".
Hivyo hivyo ndivyo ilivyo, eneo la "Templemount" kwa karne 14 limekuwa ni takatifu kwa Waislamu na ndipo penye Msikiti mtakatifu wa Alaqsa. Waislamu wanalichukulia eneo hili kuwa ni la tatu kwa utakatifu baada ya Makka na Madina. Mtume Muhammad (s.a.w.) ndipo alipotua katika safari yake ya Israa na ndipo alipoondokea katika safari yake ya Miiraji kwenda mbinguni. (Ufafanuzi wa Israa na Miiraj ni wangu).
"Imani ya Kiislamu hapa ni upuuzi mtupu", anasema Rabbi Joseph Laiper, ambaye amekuja kusali chini ya dirisha la akina Sharawneh. "Hili ni eneo la Mayahudi". Eneo hilo dogo lina sehemu tu ya ushahidi wa mizozo katika mji wa Jerusalem, baina ya Waislamu na Mayahudi na Waarabu na Waisrael kwa upande mwingine. Na yako mengine mengi.
Tembelea baadhi ya mitaa na utaona mengi. Utasikia milio ya kengele za kanisa, adhana za Waislamu, midundo ya magoma moto na kwa siku yenye mkosi utanusa harufu ya moshi wa bomu la kutoa machozi.
Wiki iliyopita Waisrael na Wapalestina walianza juhudi ya hali ya juu kufikia suluhisho la mwisho. Waziri Mkuu Ehud Baraka na Rais Yasser Araf waliungana na Rais Bill Clinton. Wasuluhishi wamekuwa wakijiwina kuhusiana na mipaka ya taifa la Wapalestina ardhi inayokaliwa na Waisraeli tangu baada ya vita vya 1967, ambayo inajumuisha nusu ya mashariki ya Jerusalem.
Barak amewaahidi watu wake "Yerusalayim" utabaki mji mkuu wa Waisrail na usiogawanywa". Arafat anye amemwambia Clinton ya kuwa anahofia kuuawa ikiwa ataugeuka mji mtakatifu wa Waislamu na Al-Qudus yake. Anataka mji mkuu wa Wapalestina uwe hapo hapo.
Arafat alitishia kujitoa katika mazungumzo wiki iliyopita pale Clinton alipotoa pendekezo lililoashiria kuwapendelea Waisrael.
Kwanini Jerusalem umekuwa mji wenye kuchemka kiasi hicho? Hapa mikusanyiko ya watu inapigana kupata kazi na elimu bora kwa watoto wao. Viongozi wakuu wa Kikristo wanapigana vikumbo kama watoto wa shule ili kupata nafasi ya angalau kufyagia vingazi katika Kanisa takatifu la Sepulcha ambapo wanaamini ndipo Yesu (a.s.) aliposulubiwa na baadaye kufufuliwa.
Waisrael wengi wanaona mji wa Jerusalem ni kipenzi sana kwao kiasi kwamba wanataka sehemu yoyote iwayo isiachiliwe. Tsvi Rogim amekuja Jerusalem akitokea Los Angeles miaka mitano iliyopita ili kufanya makazi yaliyoadimu ya juu ya kilima kitakatifu.
Rogim ameshughulika mno na matayarisho ya kuijenga upya jengo muhimu la Wayahudi lililopo hapo. Hashughulishwi kabisa na kuwepo kwa Misikiti miwili ya Waislamu eneo hilo. Kwa namna moja au nyingine mipango itafifia. Kwa miaka kadhaa mayahudi wa msimamo mkali wamekuwa wakipanga kama hivyo na hatimaye serikali ya Israel kuwavurugia.
Kila asubuhi Rogim hufanya josho la utakaso. Ikifika saa 1.20, yeye huwa ni wa mwanzo katika foleni kwenye lango la kuingilia kilima hicho, ambapo hupekuliwa na askari. Mienendo ya kiitikadi ya Rogim ni sehemu ya mapambano hatari kati ya Waislamu na Mayahudi kwenye mji huo mkongwe.
Wakati Israel ilipouteka mji huu mwaka 1967, bendera ya Israel ilipachikwa juu ya Msikiti wa Al'aqsa, lakini Moshe Dayan, Waziri wa ulinzi wakati huo na msanii wa ushindi wa Israel aliamrisha bendera iteremshwe mara moja, pengine kwa kuheshimu sehemu takatifu za kidini au kwa kuelewa tu jambo hilo lilikuwa hatari. Dayan baadae alirejesha uendeshaji wa sehemu hiyo kwa mamlaka ya Kiislamu, Waqf.
Waislamu wengi wanaamini kuwa moja ya mipango ya kuihujumu Misikiti ya eneo hilo itafanikiwa. Mamlaka ya Waqf inakataza Mayahudi kusali eneo hilo. "Mayahudi watakuwa wanataka mwisho ikiwa wataugusa tu Msikiti wangu", anasema AbuAli (49) ambaye anauza manukato na kanda za kidini kwenye mji huo mkongwe. "Itakuwa ni vita ... kuwauwa wachokozi ni jambo la maana sana".
Huku akiukaribia Msikiti Rogim anasema hatosali hapo. Lakini mwaka uliopita alifurushwa kwa kufanya hilo hilo. Kwa hivyo sasa anafuatana na askari wa Kiizrael mwenye fulana isiyopenya risasi, na kwa upande wa pili na afisa wa Waqf mwenye redio ya kuitiana. Anaposita tu maafisa wawili wanaingiwa na shaka na kumtaka asonge mbele.
Mizozano baina ya Waarabu na Waisrael, nyakati nyingne hupunguza mivutano baina ya Wayahudi wa msimamo na wale wenzao wa kisekula. Wenye msimamo mkali walikuwa ni karibu theluthi moja ya wakazi wote wa Jerusalem mwaka 1996. Kwa vile wanawake wa Kiharedi (wenye msimamo mkali) wana watoto mara tatu zaidi ya wale wa Kisekula, inatarajiwa ikifika mwaka 2010, idadi yao itakuwa imefikia asilimia 40.
Udhibiti wa kisiasa wa Waharedi unaongezeka sana, tayari wameshika nafasi zote muhimu katika mji wa Jerusalem na wanausemi. Hivi karibuni vyama vyao viwili vya kisiasa viliingia kwenye safa za kisiasa za Barak ili kupinga mwenendo wa amani wa mashariki ya kati.
Baadhi ya Waisrael wa kisekula wanawaona wenzao wenye msimamo mkali kuwa ni hatari na hakuna tofauti na Waislamu wenye msimamo kama huo, Meir Shalev ansema "mwishowe hawa watauwana tu". Anaona ni vyema eneo hilo likabidhiwe kwa umoja wa Mataifa au taasisi nyingine yoyote ya kimataifa.
Israel iliiteka Jerusalem ya Mashariki mwaka 1967, na haraka ikaanza kujenga makazi ya Wayahudi, ikaongeza mipaka na ikadhibiti idadi ya Wapelestina kwa kuwanyima vibali vya kujenga. Wengi wa Waisrael wanauchukulia mji wa Jerusalem kama ni alama ya imani yao.
Suluhisho wanalolipendelea zaidi ni kuupanua zaidi mji huo kuliko kuugawanya. Upanuzi huo utakuwa ni kuingiza Jerusalem ya Magharibi ambayo ni makazi ya Wayahudi. Na hatimaye kuviingiza vijiji vya Waarabu ambavyo vinatarajiwa kuwa sehemu ya mji mkuu wa Wapalestina, Al Quds.
Kutokana na ramani iliyochorwa na Pundak, sehemu za kweli takatifu za Kiyahudi ndani ya Jerusalem ni chache mno, ambazo karibu zote zimo kwenye mji mkongwe ambayo ni chini ya asilimia moja ya eneo lote la Jerusalem. Pamoja na hivyo Waisrael wengi akiwemo Meya wao Ehud Olmert wanalikataa wao la udhibiti pamoja. "Ama ni Jerusalem iliyogawanywa au moja".
Wapelestina wanalalamika kwamba waumini wa Kiyahudi
huwa wanawacha kwa makusudi chupa za soda na vikombe vya plastiki tele
juu ya ardhi "ili waonyeshe kuwa ni eneo lao", anasema Sabha Al Sharawneh.
WAPIGANAJI wa uhuru wa Zimbabwe wa zamani wamevamia mashamba ya wazungu. Wamefahamisha walimwengu kwamba wamechukua hatua hii isiyo ya kawaida baada ya serikali ya Zimbabwe, inayoongozwa na Rais Robert Mugabe kushindwa kuwapataia ardhi baada ya miaka kumi na nane ya uhuru wa hiyo. Hili wamelitumia kama shindikizo kwa serikali hiyo hiyo na wakati huo huo ikiandaa kwa uchaguzi wa Wabunge.
Rais Robert Mugabe hajakemea uvamizi huo ila upo ushahidi wa kutosha kuwa yeye pamoja na serikali yake wanawaunga mkono wapiganaji hao wa zamani. Hali hii inatoa picha kamili kuwa sasa serikali yake haiangalii tena sheria za ardhi, bali amechagua kuzingatia maslahi yake ya kisiasa na umaarufu tu.
Viongozi wa Afrika ya Kusini walikutana kujadili uvamizi huo na hali nzima ya Zimbabwe, lakini wapi hawakuweza kufaulu. Pia chama cha wakulima wakubwa wa nchi hiyo kilifanya mazungumzo na Rais Robert Mugabe, lakini mazungumzo yao hayakusaidia kitu. Sasa Rais Robert Mugambe amekuwa Bwana Haambiliki.
Mazao ya kilimo yanayopatikana humo ni tumbaku, mahindi, maziwa, ngano, nikitaja yaliyo makuu tu kwa biashara ya kimataifa. Kilimo kinaiingizia karibu asilimia arobaini ya fedha za kigeni. Upo uwezekano mkubwa kuwa Zimbabwe karibuni itaipoteza nafasi hii.
Kwa mfano, hivi sasa Tumbaku inaoza, bado haijavunwa kutokana na uvamizi huo. Pia hakuna uwezekano wa kupanda tena mazao mbalimbali ya kilimo. Kwa sababu wenye mashamba hawana salama wala imani na serikali ya Rais Mugabe.
Hali ya Zimbabwe imekwisha waambukiza matajiri wengi na sasa wamesitisha mipango yao ya uwekezaji wa vitega uchumi ndani ya nchi hiyo kwa mfano uliyokaribu Mary and Robert ya Afrika Kusini imesitisha kuwekeza vitega uchumi Zimbabwe.
Bunge la Zimbabwe ambalo limechaguliwa na wananchi hivi karibuni, ndilo lina nguvu za kikatiba na kisheria kuondoa mgogoro huu, ambao tayari umeipatia nchi hiyo hasara.
Wananchi pia wawe tayari kushirikiana na Bunge kwa suala hili ili limalizike salama bila ya kutoa nafasi kwa jamii moja au nyingine ya kusema kuwa imefanyika dhulma au jamii fulani imependelewa.
Bila ya kufuata katiba na sheria zilizowekwa, basi ni bayana kuwa uchumi wa nchi hiyo utaporomoka. Hivyo kuifanya nchi hiyo kukosa mengi ya manufaa kutoka nchi tajiri. Hapa ndipo umaskini utakapoanza na kuifanya Zimbabwe muflisi. Hii itaifanya Jamhuri ya Afrika Kusini na Jamhuri nyingine jirani kuyumba, pia, kiuchumi.
Athari za kupuuzia katiba na sheria zinafika mbali na ni hatari kwa kizazi chetu cha kesho. Njia ya mafanikio ni kujisahihisha na kujenga ustaarabu mpya wa kisiasa.
Ustaarabu wa kwanza wa kila zuri duniani ulipatikana Misri. Wakati ni huu wa kuiga ustaarabu huu kama tunakubali kukiri madhaifu tuliyonayo na kuyawacha. Hili linawezekana, hivyo tujaribu.
|
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook |