Ukristo ndio unaomjali mwanamke
Ndugu Mhariri
KATIKA gazeti la AN-NUUR toleo la tarehe 21-23, 2000 Bw. Iddi Mbwana ameandika makala kuhusu utukufu wa mwanamke katika Uislamu. Ameongea mengi ambayo mimi siwezi kuyaingilia kwa kuwa ni mafundisho ya Kiislamu, isipokuwa ni pale alipouliza swali kuwa "Je, ni dini gani duniani inayomtambua, kumjali na kumpa hadhi mwanamke zaidi ya Uislamu?
Hakuishia hapo, akaitaja dini ya Kikristo kuwa inamdhalilisha mwanamke na kumhesabu kuwa ndiye chanzo cha dhambi, hapa bila shaka mwandishi anataka jibu.
Biblia imemnukuu Adamu akijitetea kuwa mwanamke uliyenipa ndiye aliyempa tunda akala. (Mw. 3:12) Lakini huo ulikuwa utetezi wake binafsi kwani wote waliadhibiwa sawa, hivyo mwanamke hakudharauliwa.
Hata hivyo, swali la Bwana Idd Mbwana kuwa ni dini gani inayomtambua, kumjali na kumpa hadhi mwanamke ni dini ya Kikristo kwa sababu zifuatazo:
Mungu Yehova amewajalia ufunuo wa unabiii na uongozi wanawake sawa na wanaume. Mariamu alikuwa Nabii (Kut. 15:20), Debora alikuwa Nabii (Waamuzi 4:4), Anna alikuwa Nabii (Luka 2:36).
Lakini Qur'an 21:7 mwanamke amenyimwa ufunuo (wahyi) huo. Je usawa uko wapi? Katika 1 Pet. 3:7 Wakristo wanaamriwa wawaheshimu wake zao kwani ni warithi wa pamoja wa neema ya uzima. Lakini katika Qur'an 4:34 Waislamu wameamriwa wawatenge vitandani wanawake pia wawapige! Je, usawa uko wapi?
Katika Mat. 19:5, Wakristo mke na mume wanapooana wanakuwa mwili mmoja; lakini wanawake wengi katika Uislamu wanagawana mume mmoja! Je usawa uko wapi?
Mwisho wanaume na wanawake katika Ukristo husali pamoja kuonyesha kuwa wako sawa, lakini wanawake Waislamu hutengwa uchochoroni kwa madai kuwa wataleta matamanio na kusababisha dhambi. Kwa hali hiyo mwanamke katika Uislamu ndiye anayedhalilishwa na kuhesabika kuwa anasababisha dhambi na siyo Ukristo.
Mathias Lazila,
S.L.B. 9043,
Dar es Salaam.
Ndugu Mhariri
NAOMBA nitoe maoni yangu katika gazeti la AN-NUUR, nimesoma katika gazeti moja hivi karibuni habari iliyochukua nafasi zaidi ambayo ina kichwa cha habari kinachosema "Waraka hatari wasambazwa Zanzibar" pia waraka huo umeandikwa ukurasa watatu wa gazeti hilo.
Napenda nimfahamishe Mhariri wa gazeti hilo na yeyote mwenye mawazo kama hayo, kuwa kutuhukumu kwa matakwa ya Muumba sio hatari bali ni wajibu wa viumbe waliopo katika muda huu ambao dini, uongozi au sharia kutoka kwa Allah (s.w.) iliyo motomoto imetimia kama ilivyotabiriwa (Kumbukumbu la Torati 33:1-2).
Kwa hiyo iwapo kuna chama ambacho kitakubaliana na madokezo nambari 4, 7, 9 mpaka 14 ya waraka huo itakuwa ni wajibu kwa wanaofuata maelekezo ya Muumba kushirikiana nao kwa hali na mali ili watukaribishe kwa Allah (s.w.). Nashangazwa na kauli ya Mhariri kwa Waislamu kama ilivyo Zanzibar ambayo asilimia 99 na zaidi iwe ni hari kuhukumiwa kwa hukumu za Mungu tunayemwamini.
Namshauri asisimamie mambo asiyokuwa na elimu nayo.
I.J. Mohamed,
S.L.P. 340,
Mtwara.
Ndugu Mhariri
NAOMBA kujibu barua ya Ndugu Bukile Labunja (Rai Julai 6-12,2000) kuwa swali la mwanamke kuvaa mavazi ya kumstiri (hijabu) si jambo la hiari, bali ni amri ya Mungu, tena si kwa Waislamu tu, bali hata kwa Wakristo pia!
Mwenyezi Mungu amemwagiza Mtume (s.a.w.) awaamrishe wakeze na wanawake wa Kiislamu wavae hijabu (Kuran 33:59). Na Biblia, halikadhalika inawaagiza wanawake wa Kikristo nao wavae mavazi yanayositiri miili yao, yaani hijabu. Biblia inasema: "Vivyo hivyo, wanawake wajipambe kwa mavazi ya kujistiri (Timotheo 2:9). Ndiyo maana tukaona masista, makanisani wanavaa hijabu kufunika miili na vichwa vyao.
Sasa ndugu Lubunja anayefurahikia wanawake wanaovaa bikini na kujitandaza bichi, pamoja na wale wanaoshiriki mashindano ya urembo wakiwa nusu uchi, anafuata mafundisho ya dini gani?
Waislamu hawaongozwi na "News Week", "Rai" au gazeti jingine lolote, wanaongozwa na Kurani tukufu na Sunnah ya Mtume (s.a.w.). Basi Malkia Rania, mke wa Mfalme wa Jordan, hata kama mumewe anatokana na kizazi cha Mtume (s.a.w.), lakini akitenda kinyume na mafundisho ya Uislamu wote wawili , yeye na huyo Mumewe, watapata dhambi. Ule uhusiano wa damu wa mumewe na Mtume (s.a.w.) hautawasaidia kitu.
Nabii Nuhu alimwomba Mungu amwokoe mwanae, kafiri, kutokana na gharika, akamkatalia. Akamjibu kuwa huyo mwanawe si katika watu wake kwa sababu matendo yake hayakuwa mema (Kuran 11:42). Na Abu Lahab, ingawa ni Baba mdogo wa Mtume (s.a.w.) lakini kwa ukafiri wake, ataingia motoni yeye pamoja na mkewe (Kur'an 111:1-5).
Mwisho, Ndugu Lubunja amedai kuwa wenyeji wa Ghuba ni Wamanga, na Washihili, Waarabu. Kwake yeye, Waarabu ni wakazi wa Misri, Jordan, Palestina, Moroco, Syria na Tunisia. Inaonekana Ndugu Lubunja si mbumbumbu wa Kur'an tukufu na Biblia tu, bali hata wa Jiografia na Historia.
Inafaa aelewe kuwa Waarabu wa asili ni wenyeji wa Yemen na Ghuba ambao yeye amewaita Wamanga na Washihiri. Ama wenyeji wa Misri asili yao ni Makibti (Copts), watu wa Jordan na Palestina ni Waafilisti (Philistine) na hata huyo Malkia Rania ni Mfilisti. Wenyeji wa Syria ni Wakaladayo (Chaldeans). Na watu wa Moroco na Tunisia ni Waberber na Watuareg, sio Waarabu.
Chuki na jazba hazitamsaidia kitu ndugu Lubunja. Asome ataujua ukweli.
Ali Said Bassaleh,
S.L.P. 15653,
Dar es Salaam.
Ndugu Mhariri
SHUKRANI zangu za dhati kwako kwa kunipa fursa hii ili nami nitoe malalamiko yangu kwa niaba ya Waislamu wenzangu wapenda haki hapa Chunya.
Malalamiko yanakuja kufuatia uongozi wa BAKWATA wa wilaya ya hapa Chunya mkoani Mbeya kufuatia utaratibu wao wa uendeshaji wa shughuli za Uislamu unaofanywa na viongozi hao kwa kile wanachokiita kutimiza maagizo ya uongozi wa juu ya Baraza.
Mimi nijuavyo na kusikia Masheikh wengi wakitueleza ni kwamba sisi ni umma bora kwani tunaamrishana mema na kukatazana maovu na pia Mwenyezi Mungu ametuamrisha kuwa tuwe na vikundi vinavyofanya kazi hiyo ya kuamrisha mema na kukataza mabaya. Na hii ndiyo maana sehemu zingine utawaona maamiri au Tabligh wanapita kila Misikiti ili kuwazindua Waislamu wafuate maamrisho ya Mola wao.
Lakini chakushangaza hapa Chunya Masheikh wa BAKWATA hawataki kuona wageni hao wa Tabligh na wala haitaki wapokelewe hapa wilayani eti kwa sababu walipokea taarifa kutoka BAKWATA Makao Makuu ikiagiza kuwa vikundi vya Tabligh visipokelewe na hili limethibitika zaidi ya mara mbili tukishuhudia hawa Maamiri wakifukuzwa tena chini ya amri ya Polisi eti kwa sababu BAKWATA haiwatambui kama Waislamu.
Pia kuna kijana mmoja yeye ni mhamiaji alikuja hapa Chunya (jina tunalihifadhi) muda wa miaka mitano iliyopita yeye alianzisha utaratibu wa kuunda vikundi tukawa tunazunguka naye vijijini kuwazindua Waislamu lakini hivi sasa BAKWATA wilaya hasa Sheikh wa Wilaya na viongozi wenzake wamempa amri tena kwa barua maalum kuwa asifanye kazi yoyote ya dini eti kwa sababu watu wa Tabligh wakifika Chunya yeye anawapokea hali ya kuwa BAKWATA imetoa amri wasipokelewe hata kupewa msaada wowote hata chakula.
Sasa matokeo yake Uislamu hapa wilayani Chunya unazidi kudidimia siku hadi siku. Leo hapa Chunya kama unataka kuzungumza na Waislamu, sharti uje na barua maalum (kibali) ndio utapewa kibali maalum au uwe mtu wa BAKWATA.
Je, hivi ndio sifa ya sisi umati Muhammad kuitwa umma bora? Au huu ndio mshikamano ambao Mwenyezi Mungu katuambia tushikamane.
Mwisho ninayo mengi ya kuongea kuhusu Uislamu wa Chunya lakini kwa leo nitawachia wenzangu nafasi.
Ni katika kilio cha Uislamu Chunya.
Ally A. Ally,
S.L.P. 32,
Chunya.
|
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook |