Malima aonya
MIZANI, Feb. 24, 1995
WAZIRI wa Viwanda na Biashara, Profesa Kighoma Ali Malima amekatisha ukimiya wake dhidi ya shutuma mbalimbali ambazo zimekuwa zikielekezwa kwake na kusema kuwa tuhuma hizo zilikuwa ni njama za kulichafua jina lake.
Profesa Malima ambaye ni mchapakazi na mkimya asiyependa siasa za magazetini amefafanua ukweli juu ya mambo mazito aliyobebeshwa yeye binafsi wakati alipokuwa Waziri wa Hazina wiki mbili zilizopita wakati alipofanya mahojiano na gazeti litolewalo kila wiki mara moja kwa lugha ya Kiswahili.
Akizungumzia shutuma kuwa yeye alitoa msamaha wa kodi kwa kampuni ya Merchant Vintmers iliyoagiza pombe ya Stella Artois na kuikosesha serikal mabilioni ya fedha, Profesa Malima alisema hajawahi hata mara moja kutoa msamaha huo na kwamba "huo ni uzushi mtupu".
Akifafanua Profesa Malima alisema, kinyume na kutoa msamaha, walichofanyiwa Stella huko nyuma ni kupewa kibali cha kulipa ushuru wa forodha kwa awamu mbili, tatu au zaidi, mradi tu kipindi hicho cha malipo hakizidi miezi tisa.
Amesema, utaratibu wa kutoa vibali kwa wafanyabiashara na makampuni kulipa kodi kwa awamu ulianzishwa 1986 wakati ambapo kulikuwepo upungufu mkubwa wa bidhaa muhimu kwa wananchi na ulilenga kuwapa motisha wafanyabiashara wanaotaka kuagiza kwa wingi bidhaa kutoka nje.
Profesa Malima amesema, utaratibu huo hakuuanzisha, lakini ulianzishwa wakati Bw. Cleopa Msuya akiwa Waziri wa Fedha na hayati Kibona aliurithi na hata yeye alipoingia Hazina aliukuta utaratibu huo hadi alipoufuta Novemba 1993.
Profesa Malima ameeleza kusikitishwa kwake na hatua ya magazeti kuendesha kampeni ya uongo na uzushi dhidi yake na katika hali ambayo inaonesha chuki hata magazeti ya CCM yaliingia katika njama hizo ambazo Profesa anasema, hazikutangazwa kwa bahati mbaya, hizi ni njama za makusudi zenye lengo la kuchafua jina langu".
Aidha, Profesa Malima anaamini kuwa kampeni inayoendeshwa na magazeti yote dhidi yake haihusiani na kazi: "Kampeni hii inaelekea kuwa na agenda maalum, wameazimia kuchafua jina langu ili kufanikisha malengo fulani fulani", alisema.
Amehoji kuwa ikiwa kila wizara mambo yanapokwenda vibaya lazima alaumiwe Waziri kwa kuwa kiongozi basi mfano huo lazima uzingatiwe sana. Kwa kuwa alipokuwa Waziri wa Fedha lawama zote alipewa yeye japokuwa hazikuwa na ukweli wowote.
Profesa Malima amesisitiza lazima ionekane wazi kuwa kuna mwelekeo maalum katika kampeni hiyo kwani, "Wizara ya Mambo ya Nje, kiongozi anayeshughulikiwa ni Katibu Mkuu, Dk. Ibrahim Msabaha. Wizara ya Elimu ya Juu, mkorofi ni Katibu Mkuu Dk. Mohamed Bilali. Wizara ya Kazi mkorofi ni Katibu Mkuu Kenya Hassan na vile vile Wizara ya Elimu anayeshughulikiwa ni Katibu Mkuu Ali Mansour Vuai, alitoa mfano na kuongeza "Sasa angalia wote hawa wana sifa moja inayowaunganisha na Profesa Malima (akimaanisha Uislamu).
"Tunaipeleka wapi nchi yetu?" Aliuliza Profesa
Malima na kusema, kama Wizara ya Fedha aliyekuwa akiandamwa ni Waziri kwa
nini Wizara nyingine wanaoandamwa si Mawaziri? Amesema, magazeti yenye
mtindo huo hayana budi kurekebisha mitazamo na mienendo yao "vinginevyo
tunakabiliwa na hatari kubwa ya Disquised Apartheid (aina mbaya
sana ya ubaguzi) alionya.
Haki, Mei 10-16, 1996
Na Ramadhani Mkumbukwa
WAKATI Mchungaji Christopher Mtikila ameahidi kufanya mkutano katika viwanja vya Jangwani Jumamosi ijayo na "kummaliza Bwana Augustine Mrema na chama chake cha NCCR - Mageuzi kisiasa, naye Rais wa PODEMO, Balozi Christopher Kassanga Tumbo amedai kwamba Nyerere, Mwinyi na Mrema ni kitu kimoja na kwamba kinachofanyika ni kujaribu kuwahadaa tu wananchi.
Balozi Tumbo ameyatamka hayo mwishoni mwa wiki alipokuwa akiongea na waandishi wa habari katika makao makuu ya PODEMO yaliyoko Magomeni Mapipa Jijini baada ya kuirejea historia ya mahusiano ya nafasi za uongozi za Rais Mwinyi na Bwana Mrema wakati mauaji ya Mwanza na Shinyanga, jinsi Nyerere alivyolizima suala hilo la mauaji bila kuwachukulia hatua Mrema na Mwinyi na jinsi watu hao walivyolindana, kupeana madaraka na kupandishana vyeo.
Wakati Mchungaji Mtikila ameahidi kuyaweka hadharani anayodai makosa ya Bwana Mrema siku hiyo (Mei 15) na kuwa tayari kutoa ushahidi wa yote atakayoyasema dhidi yake, Kassanga Tumbo yeye amedai kwamba Rais Mwinyi na Mrema bado wanastahili kuulizwa na kubebeshwa lawama ya mauaji ya Shinyanga ya watu 35 ambapo Mrema alikuwa Afisa Usalama wa Wilaya na Mwinyi alikuwa Waziri wa Mambo ya Ndani.
Amedai kwamba katika mauaji hayo, vyombo vya dola ndivyo vilivyohusika katika kuwatesa wananchi waliokuwa wakidai haki zao za kutetea chama chao cha ushirika kwa kuwafungia watu 36 katika kidogo kinachotosha watu sita (6) tu hali ambayo iliwafanya wakose hewa na 35 kufa.
Amesema Tumbo kwamba, serikali ya Tanzania tukio hilo la kusikitisha liliishangaza dunia pale ambapo Mwalimu Julius K. Nyerere akiwa Rais ilifanyika mbinu ya kuwahadaa wananchi kwa kumtaka Mwinyi ajiuzulu Uwaziri wa Mambo ya Ndani na baadaye Nyerere akamerejesha tena Mwinyi kwenye uongozi wa nchi alipompeleka kuwa balozi wa Tanzania huko Cairo, Misri.
Baada ya hapo, ameendelea kusema Kasanga Tumbo kwamba, Mwalimu Nyerere aliendelea kumkumbatia Mwinyi kwa kumpa nafasi mbalimbali ikiwa ni pamoja na ubalozi wa Tanzania nchini Canada, kisha Urais wa Zanzibar hatimaye kumpendekeza kwa kumlundikia sifa chungu nzima achaguliwe kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Akifafanua zaidi madai yake, Balozi Tumbo amesema, mzunguko kamili wa uhusiano wa Nyerere, Mwinyi na Mrema ulibanika pale ambapo Mwinyi aliposhika Urais akamkumbuka waliyekuwa naye kwenye lawama ya mauaji hayo ya Mwanza na (Bwana Augustine Mrema) na kumpa Uwaziri wa Mambo ya Ndani na pia Unaibu Waziri Mkuu licha ya kwamba walikuwepo mawaziri wengine (senior) wasio na doa ambao wangestahili kupewa Unaibu Waziri Mkuu.
"Mwinyi na Mrema walitakiwa kushitakiwa kutokana na yale ya Mwanza na Shinyanga lakini badala yake ilitumika hadaa tu ya serikali kwa kutumia magazeti yake ya serikali na CCM ili wananchi waridhike na kitendo cha Mwinyi kujiuzulu", amesema Balozi Tumbo huku akionesha kusikitika.
Akionesha jinsi watu hawa watatu walivyo na uhusiano uliofichika, Balozi Tumbo amesema kwamba, hivi sasa Bwana Mrema katika kampeni zake za kuwania Urais amekuwa akitumia kitabu cha Mwalimu Nyerere alichokitunga ili akubalike na wananchi.
Kutokana na historia hiyo ya mzunguko wa uhusiano uliofichika wa Nyerere, Mwinyi na Mrema, Balozi Tumbo amesema, endapo juhudi za kumkweza Mrema kwenye kiti cha Urais zitafanikiwa, basi ni bayana kwamba serikali ya Mrema itakuwa ni ile ya Nyerere na pia ya Mwinyi.
Alipoulizwa ni kwa nini basi watu hao watatu wamekuwa wanapondana katika mikutano wanayofaya, Balozi Tumbo amejibu kwamba: "Hawa watu wa CCM ni wajanja sana, wasomea saikolojia na wanajua jinsi ya kuwahadaa watu... wanatumia ujanja wa kichuguu wa kuwa na milango mitatu kumbe chumba chao ni kimoja".
Ameendelea kusema kwamba CCM haina 'nguvu tena, wameamua kumtumia Mrema ili akubalike na kuwekwa madarakani kisha aendeleze sera za CM na pia atimize matakwa ya Nyerere ya kuyarejsha baadhi ya mambo kama vile Azimio la Arusha ambalo wanaona yamefanyika makosa sana kulidhoofisha.
Amesema Balozi Tumbo kwamba ndiyo maana Mrema amekuwa akishambulia serikali kwa mambo mengine tu lakini hajawahi kuzikosoa kwa kina sera za CCM. "Achotaka ni kulirudisha Azimio la Arusha ambalo liliwanyang'anya wananchi mali zao, mashamba yao, viwanda vyao, na vitu vingine vingi kwa njia ya dhulma.
Balozi Tumbo ametoa mfano wa Mwamwindi alivyonyang'anywa shamba lake na jinsi ambavyo kifo chake hakikuwekwa waziwazi kwa wananchi. "Shamba la marehemu Mwamwindi sasa limekuwa ni shamba la kijiji cha Mfumaki cha CCM", amedai Balozi Tumbo.
Hata hivyo, Balozi Tumbo amesema, anamuunga mkono Bwana Mrema kwa kutamka hadharani makosa ya serikali aliyokuwa akiitumikia kwa kuwa hiyo inasaidia kuwathibitishia wananchi kwamba kauli za wapinzani dhidi ya serikali ni za kweli.
Lakini, amesisitiza Balozi huyo kwamba kutokana na staili yake ya uongozi pamoja na dhamira yake ya kuyarejesha mambo ya Mwalimu Nyerere, hafai kuwa kiongozi wa nchi.
Ameshutumu uongozi wa Bwana Mrema wa kutumia "udikteta" na ubaguzi katika kuwashughulikia wakosaji. Mrema alikuwa akiwakamata watu wengi wakiwemo wazawa na wageni, lakini ni 'gabachori' gani aliyeko jela" Ameuliza.
Aidha, amesema Balozi Tumbo kwamba kitendo cha Bwana Mrema kuwa anatumia ofisi yake kuigeuza mahaama ya kuamulia kesi siyo utaratibu na kwamba kitendo hicho kinaonyesha kwamba huenda Mrema alikuwa akiitumia ofisi hiyo ya serikali kwa manufaa yake binafsi.
Amehoji suala la Bwana Mrema kuwasumbua wakulima wa korosho kwa kuwaita wamfuate ofisini kwake na pia kupatikana kwa mamilioni ya fedha ndani ya ofisi yake.
"Itakuwaje Waziri wa serikali awe na mamilioni ya fedha za umma ofisini kwake badala ya kuziweka kwenye vyombo vinavyohusika na utunzaji wa fedha? Ameuliza kwa mshangao Balozi Tumbo.
Mawazo haya ya Balozi Tumbo kwamba Bwana Mrema bado ana dhamira ya kuyaendeleza mambo ya Nyerere na CCM yanalingana na yale aliyowahi kutamka Mchungaji Christopher Mtikila mara tu aliporejea nchini kutoka Ulaya na Marekani kwamba, pilikapilika za Bwana Mrema ni mbinu za CCM za kuwahadaa wapinzani ili CCM ije ishinde uchaguzi kirahisi.
Mtikila alifafanua madai yake kwa kumfananisha
Bwana Mrema na kiongozi mmoja wa KANU aitwaye John Kin ambaye alikihama
chama hicho na kuzoa maelfu ya watu waliomfuata kwenda FORD lakini baadaye
aliwaacha FORD kwenye mataa aliporejea kwenye chama cha KANU.
--
![]()
|
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook |