RIWAYA

Joka la Mdimu - 16

KWALE

GRAY KWACHA alitoa udhuru wa kutokuwepo kazini kwa siku tatu. Akaanza maandalizi ya safari ya kwenda Kwale. Safari hii ilikuwa kwa minajili miwili, mosi kutimiza miadi ya kuonana na maashuki wake Leila. Pili, kwenda kuonana na wawindaji wake ili kupata vipusa alivyomuahidi Shiraz Bhanj.

Lakini maandalizi yenyewe hasa yalikuwa kulipeleka gari lake, Range Rover gereji kufanyiwa matengenezo ya lazima. Alilipeleka gari hilo katika kampuni ya Cooper Motor ambako aliliacha hadi siku ya pili alipokwenda kulichukua na kuhakikishiwa kwamba lingeweza kwenda zaidi ya maili elfu moja bila ya matengenezo.

Vituo vyote vya petroli njiani vilikuwa vimefungwa, magari yakasafiri na vitangi vya plastiki au mapipa makubwa ya dizeli na petroli ya kutosha safari nzima. Naye ilibidi afanye hivyo. Jioni alikwenda kituo cha Caltex alikokuwa maarufu, akajaza mafuta ndani ya tangi hadi likajaa. Kisha akajaza vitangi vitatu vya plastiki.

Safari ilikuwa ianze alfajiri kuepuka jua. Usiku ule alifanya shughuli nyingine kidogo muhimu. Ana kwa ana na mlango wa chumba chao cha kulalia kulikuwa na chumba kidogo mitihili ya stoo.

Ndani ya chumba hicho kulikuwa na kasha jeusi la chuma la urefu wa futi tano kwa futi mbili. Aliwasha taa na kuingia ndani ya chumba hicho akajifungia kwa ndani. Pole pole alichomoa funguo na kuzichomeka ndani ya kufuli zito la shaba. Alizungusha funguo hizo mara mbili kabla halijafunguka. Kumaliza hivyo aliuinua mfuniko mzito wa kasha lile kwa mikono miwili, huku bawabu zake zikilia kwa kukosa mafuta na kufunguliwa mara chache. Ndani mlikuwa na pembe mbili za faru ambazo hazikumpotezea muda. Badala yake aliiangalia mifuko miwili mirefu ya kinvasi. Kwa kutumia mkono wa kulia aliuchukua mfuko ule wa juu. Sehemu yake ya juu ilikuwa nyembamba kuliko chini. Alivuta zipu kutoka juu hadi chini ya mfuko huo. Ndani yake alichomoa bunduki kubwa, akaiangalia kwa mkaini. Upesi aliirejesha ndani ya mfuko wake na kuuchukua ule mfuko mwingine, akafanya hivyo hivyo.

Baada ya kuirejesha bunduki ile ndani ya mfuko wake aliiweka ndani ya lile kasha la chuma. Akachuchumaa kando yake akafikiri kidogo kabla ya kuchukua mfuko mwingne wa nguo kando kando ya kasha hilo hilo. Kutoka humo alichomoa darubini mbili za kuwindia. Nazo aliziangalia kwa muda kisha akazirejesha zilipokuwa. Bunduki zile mbili pamoja na darubini zake alizinunua Ubelgiji miezi mitatu iliyopita ili awapelekee wawindaji wake Kwale. Kuridhika na aliyoyaona mle chumbani alilifunga vyema kasha, akatoka kwenda kulala.

Gray Kwacha aliamka alfajiri kabisa. Baada ya kunawa na kuvaa alitia sanduku lake la nguo ndani ya gari. Baadaye akaingia tena mle ndani ya chumba kilicho na lile kasha la bunduki. Kutoka humo alichukua bunduki moja na darubini yake akaviweka chini ya kiti cha nyuma cha gari. Kumaliza hayo akanywa kikombe kimoja cha kahawa tupu, akamuaga mkewe na binti zake, akatoka tena nje ambako aliingia ndani na kulipiga moto gari lake. Aliliachia liungurume kwa muda, akaondoka taratibu huku mkewe na binti zake wamesimama wakimkodolea macho. Kwa pamoja waliliangalia gari zuri likondoka kwa madaha. Binti zake walitamani sana kusafiri na baba yao. Lakini licha ya safari zake nyingi mno, hawakupata fursa hiyo. Walibaki wametuwaa pale nje kwa zaidi ya dakika tano hata baada ya lile gari jeupe kutoweka kuangalia kisichokuwepo. Mama yao aliwatazama, akasema kwa sauti kali, "sasa mwangoja nini?" Kama vile waliotahayari, walirejea ndani vichwa chini.

******

Kwale ni jimbo na mji maarufu mno ndani na nje ya mipaka ya nchi hii. Iko katika nyanda za juu Kaskazini kiasi cha maili mia nne kutoka jijini Mindule.

Pamoja na mambo mengine ya kuvutia, kama vile hali ya hewa baridi na mandhari ya nchi, hifadhi ya Kwale kulikuwa na hoteli nyingi mno imeongezea sana haiba na umaarufu wa jimbo hili. Na kwa vile aliye kando ya waridi kunukia hana budi, mji wa Kwale nao ukapata umaarufu ulioandamana na hifadhi ile ya Kwale. Kulikuwa na hoteli nyingi mno kuliko mji mwingine wowote nchini mle, ambazo mwaka mzima zilipokea na kuwakirimu watalii kutoka dahari mbalimbali. Katika jitihada ya kuwaridhia watalii hao pamoja na kuinua kipato chake cha fedha za kigeni, serikali ilikopeshwa fedha na Benki ya Dunia kujenga uwanja wa ndege wa kimataifa. Kiasi cha maili ishirini kusini ya mji wa Kwale, kuna uwanda wa mbuga ulioranda kwa masafa marefu kushinda upeo wa macho. Hapo ndipo palijengwa uwanja huo. Ndege ya kwanza ya kimataifa kutua ilikuwa ya Shirika la Ndege la Udachi, KLM. Ukiachilia mbali ndege chache za kimataifa zinazotua hapo, na wakati wa msimu wa watalii, wafanyakazi wa uwanja huo walipumzika muda mrefu mno bila shughuli. Shirika la Ndege la nchi ile zilikuwa na ndege nne tu ambazo hutua hapo mara mbili kwa siku.

********

Saa mbili na robo Boeing 767 ya Shirika la Ndege la Ethiopia ilikuwa inakaribia kutua katika uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kwale. Rubani aliyekuwa akiiongoza ndege ile pamoja na wenzake wenzake wawili na wafanyakazi wengine sita alikaza macho yake mbele. Taa nyingi zilijipanga pembeni mwa barabara kuu ya kushukia, zikaendelea hivyo hadi kukutana na nyingine mbele zilizoelekea kunako majengo ya uwanja huo. Kando yake ulionekana weusi wa nyasi fupi ambazo zilifichwa na kiza cha usiku.

Leila alikuwa ameketi kitini pake karibu na dirisha. Muda mfupi uliopita alifunga riwaya ya mapenzi aliyokuwa anaisoma. Akaona kheri aangaze nje. Katika safari zake za angani akiwa kazini hakupata muda mrefu mno wa kupumzika. Hakuacha kustaajabia vile Mungu alivyompa binadamu maarifa ya kuunda 'dude' kama hili lililoweza kupaa kasi na uzito mkubwa likakata masafa marefu kama si kitu chochote. Alisikia na kusoma habari za ajali na mikasa ya angani, lakini aliona vyema zaidi kuitelekeza kuliko kuipatiliza. Na hasa pale manufaa yanapozidi balaa. Isitoshe, ajali haina kinga sini!

Katika jitihada yake ya kuangaza nje hakufurahishwa sana na kile alichomudu kukiona. Kiza kitupu na vimulimuli vya taa za uwanjani. Majengo ya uwanja wenyewe hayakuweza kuonekana maana yalikuwa upande mwingine. Hivyo usiku ukamkosesha kile alichomudu kukiona mara moja tu ndege yao ilipotua uwanjani pale mchana. Wakati ule ndege yao iliyakata mawingu taratibu kutokea kwenye anga safi ambako aliona mbuga ikisambaa kote kama shuka kubwa ya kijani.

Sasa ndege iligusa chini kwa kishindo kidogo mno ikakimbia kasi kabisa kabla ya kupunguza mwendo wake. Kwa mbali alisikia mvumo mkali wa injini zile nne zenye nguvu. Alipokuwa akijiandaa hakuacha kumfikiria Gray Kwacha. Je, asipokuwepo?

Swali hilo lilifungua upya somo lile la mapenzi. Nini maana na aina zake? Nani apewe na asipewe na kwa jinsi gani. Mapenzi sawa na maudhi, alitongoa msanii mmoja, kwamba nyingi kwake ni hatari! Leila alikumbuka wanaume aliokutana nao, akapendana nao. Hivi yupi alimpenda zaidi. Alijaribu kukumbuka, akapata shida maana msururu ulikuwa mrefu: Waasia, Waafrika, Wazungu. Akajaribu kulipata jina au busubusu tu (maana majina nayo asingeweza kuyakumbuka) ya mtu ambaye labda alimpenda kikweli, asipate jawabu. Akajiuliza zaidi, kama ni hivyo basi, mapenzi yana maana gani kwake?

Maswali hayo yalimtafiri mno akili. Badala ya kumfikiria zaidi Gray Kwacha, akatarajia zaidi faraja katika kuangalia wanyama kwenye Hifadhi ya Kwale.

Itaendelea Ijumaa
--
JuuRUDI


Bonyeza hapa
kushriki mjadala au kutoa maoni juu ya habari hizi na masuala mengineyo ya Kiislamu kwenye Baraza ya Wasomaji

   Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu: Bonyeza hapa
Au
Andika barua  kwa: webmaster@islamtz.org

 
An-nuur Home | Ukurasa wa Mwanzo | Islam Tanzania
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook