Mkapa, Lipumba nao wawekwe 'kiti moto'

BAADHI ya wakazi wa jijini Dar es Salaam wametaka mdahao mwingine ufanyike kwa wagombea Urais kwa upande wa Jamhuri ya Muungano ya Tanzania kufuatia ule wa visiwani Zanzibar uliofanyika mwishoni mwa wiki.

Wamesema, ingekuwa vyema wananchi wakapata fursa kuwasikia Rais Mkapa na mgombea wa CUF, Prof. Lipumba.

"Tumewasikia Maalim Seif na Karume, vyema sasa tuisikie miamba kwa upande wa Jamhuri ya Muungano", amesema Bw. Juma wa Ubungo.

Wagombea Urais wa Zanzibar, Seif Sharif Hamad (CUF) na Amani Abeid Karume (CCM) Agosti 6, walichuana katika mdahalo ulioandaliwa na Idhaa ya Kiswahili ya Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC).

Wananchi hao kwa nyakati tofauti wakitoa maoni yao wameeleza kuwa, hiyo ni changamoto kwa wananchi kwa ujumla walio ndani na nje ya nchi ya Tanzania.

"Nimefurahishwa na mdahalo uliofanyika Zanzibar kwa utaratibu huo hata kwa wale wanaogombea katika Muungano nako BBC iandae mdahalo kama huo", alisema Bi. Magret wa Mbezi.

Mama Mboki wa Sinza ameeleza kuwa, mahojiano hayo yanasaidia Watanzania kuelewa ukweli wa mambo ufahamu na upeo wa wagombea.

Aidha, Bwana mmoja ambaye hakupenda kutajwa jina lake gazetini alieleza kuwa hiyo inasaidia kwa upande wa upinzani kwani hawapati nafasi ya kueleza sera ama mambo yao kupitia vyombo vya habari vya umma ukilinganisha na chama tawala.

"Upinzani hawapati nafasi katika vyombo vya habari vinavyoitwa vya Taifa (RTD, TVT), hivyo watu wengi ndani na nje ya Tanzania hawaelewi vyama vya upinzani vinasema nini", alisema Bwana huyo wa Kijitonyama.

Katika mdahalo uliofanyika mjini Zanzibar na kuongozwa na Bw. Tido Mhando Mkuu wa Idhaa ya Kiswahili (BBC), Maalim Seif akielezea juu ya sera ya kuimarisha uchumi katika Zanzibar alieleza kuwa tatizo la umaskini Zanzibar linatokana na serikali iliyopo madarakani.

"Naamini nchi yetu si masikini kiasi hicho. Mimi nadhani tunazo rasilimali za kutosha, la msingi ni kuhakikisha kwamba kila senti moja inayopatikana katika serikali inatumika kwa sababu ya maendeleo ya wananchi", alisema Maalim Seif.

Aidha, alieleza kuwa wananchi wa Zanzibar wanaupungufu wa ajira na kueleza kwamba serikali itakayoongozwa na CUF itahakikisha inatumia mapato yake vizuri na kuwapatia vijana ajira na kuwalipa vizuri.

Kwa upande wake Bw. Amani Karume (CCM), alieleza kwamba bila kupata uongozi mzuri na kupata misaada sio rahisi kufanikisha malengo ya kiuchumi yanayotakikana.

Aidha, alisisitiza juu ya ukusanyaji wa kodi ya serikali kwa hali ya juu na uwekaji sheria na taratibu zilizo wazi ili wawekezaji vitega uchumi kutoka nje wapate kuvutika kuweka vitega uchumi.


Kajiandikishe kupiga kura leo

LEO ni siku ya mwanzo ya kujiandikisha kupiga kura kwa ajili ya uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani unaotarajiwa kufanyika Oktoba 29, mwaka huu.

Kwa muda usiozidi wiki mbili mamilioni ya Watanzania watakuwa wamejiandikisha tayari kutumia haki yao ya kidemokrasia kuwachagua viongozi watakaowaongoza katika kipindi cha miaka mitano ijayo.

Tofauti na chaguzi nyingine za miaka ya nyuma, Watazania wengi wanatazamiwa kujiandikisha kupiga kura hasa baada ya viongozi wa baadhi ya vyama kupita sehemu mbali mbali kuwahimiza kutumia haki hiyo ya uraia kuweka uongozi wa nchi yao.

Taarifa kutoka sehemu kadhaa nchini zinafahamisha kuwa wananchi wengi wamekuwa wakisubiri kwa hamu kubwa kuwadia kwa hatua hiyo muhimu katika ushiriki wa uchaguzi mkuu ujao.

Baadhi ya Viongozi hao wamekuwa wakiwasisitiza wananchi hao kuchagua viongozi watakaowajibika kikamilifu katika kuijenga nchi ambayo hivi sasa inaelezwa ni ya tano kwa umasikini duniani.

Katika ziara yake hivi karibuni mjini Mwanza, Rais Benjamin Mkapa aliwataka wananchi kujiandikisha kupiga kura na wawaepuke wale wanaotoa Rushwa kujipatia uongozi.

Rais Mkapa ambaye ni Mwenyekiti wa CCM alitoa kauli hiyo kufuatia taarifa za kutawala kwa rushwa katika kura za maoni za Wabunge na Madiwani wa CCM.

Wakati akiwania Urais mwaka 1995, Rais Mkapa aliahidi kuwa mkali dhidi ya wala rushwa na kwamba kuchaguliwa kwake kungewezesha kukomeshwa kwa jinai hiyo.

Kwa upande wake, Profesa Ibarahim Lipumba ambaye ni Mwenyekiti wa CUF na mgombea wa Urais wa Vyama vya CUF na CHADEMA amewataka wananchi kujiandikisha kwa wingi na hatimaye kupiga kura ili kuwachagua viongozi watakaoliondoa Taifa hili katika lindi la umasikini ambalo wamedumu ndani yake kwa miaka 40 sasa.

Mbali ya viongozi wa kisiasa, viongozi wa taasisi na jumuiya mbali mbali wamekuwa wakiwahimiza wanachama na wafuasi wao kushiriki uchaguzi kuchagua viongozi watakaoliongoza Taifa la Tanzania kwa haki na usawa kwa raia wote.

Wamekuwa wakisisitiza hilo kwa kuwataka wananchi kujiandikisha kwa wingi katika uchaguzi huo ili wawachague viongozi wenye uwezo wa kuongoza.

Mchungaji Amani E. Lyimo wa kanisa la KKKT Kigogo akizungumza juzi katika kipindi kinachorushwa hewani na TVT kila Jumapili amesema, wananchi hawanabudi kushiriki uchaguzi mkuu ujao ili wanaofaa watakaotenda haki kwa wananchi wawachague.

Amesema ili kuwapata viongozi hao, wananchi wapime matendo ya viongozi na kwamba kiongozi asiyefaa ni yule anayeahidi bila ya kutekeleza kisha hurudia tena kuahidi uongo.

Amiri wa Shura ya Maimamu Sheikh Juma Mbukuzi amewataka Waislamu na wananchi kwa ujumla kujiandikisha kwa wingi kupiga kura ili wachague viongozi watakaoondosha vitendo vya kibaguzi na ukandamiza vinavyotishia amani na usalama wa Taifa.

Amesema kura ni njia ya amani itakayowawezesha watanzania kuondoa dhulma katika nchi yao.

Sheikh Juma Mbukuzi ni mmoja wa viongozi waliofikwa na misukosuko ya kuwekwa rumande mara kadhaa kwa msimamo wake wa kuitaka serikali iliyopo madarakani iache kuwabagua baadhi ya wananchi na kuwapendelea wengine.

Kampeni za Urais, Ubunge na Udiwani zitaanza rasmi katikati ya mwezi huu ambapo kila chama kitapata fursa ya kunadi sera zake kwa wananchi kupitia mikutano ya hadhara itakayofanywa maeneo mbali mbali nchini.

Aidha, wananchi watapata fursa ya kuwapima wagombea wa vyama vyote na kisha kutoa uamuzi wao juu ya nani atakaefaa kuwaongoza.

Baadhi ya Viongozi wa vyama na wataalamu wa mambo ya siasa wamevitaka vyombo vinavyohusika kusimamia uchaguzi kutoruhusu yale yaliyojitokeza katika uchaguzi wa mwaka 1995 ambapo baadhi ya maeneo yaliyoonekana kuwa na upinzani kwa chama tawala hayakupelekewa vifaa vya uchaguzi hali iliyosababisha kutokea vurugu.

Wameonya kuwa suala la uchaguzi ni zito na nyeti lisiposimamiwa kiadilifu huenda likasababisha kutokea machafuko makubwa na hatimaye maafa.

Aidha wamevitaka vyombo vya Dola kuacha mara moja mwenendo wao unaoashiria kukisaidia chama tawala dhidi ya vyama vya upinzani.

Wamesisitiza kuwa, vyombo vya Dola na polisi havina budi kuzingatia katiba ya nchi, kufuata sheria na kanuni katika kusimamia amani bila ya kuegemea upande fulani.

Wametahadharisha kuwa utendaji wa upendeleo ni wa hatari inayoweza kuzusha vurugu itakayopelekea kuvurugika kwa utaratibu mzima wa kupata au kubadilisha uongozi kwa njia za kidemokrasia na kulitumbukiza Taifa katika mapambano ya wenyewe kwa wenyewe.

"Tuwe na uzalendo, tujali maslahi ya nchi, tuache ubinafsi, tujifunze kutoka kwa wenzetu na tuache domokrasia ichukue mkondo wake kwa uhuru na haki", ameshauri mwanachuo mmoja anayechukua shahada ya uzamili katika katika fani ya siasa chuo kikuu cha Dar es Salaam.

Vyama vitakavyoshiriki katika uchaguzi mkuu wa mwaka huu ni pamoja na chama tawala (CCM), chama cha wananchi (CUF) kikishirikiana na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), UDP na TLP.

--
JuuRUDI


Bonyeza hapa
kushriki mjadala au kutoa maoni juu ya habari hizi na masuala mengineyo ya Kiislamu kwenye Baraza ya Wasomaji

   Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu: Bonyeza hapa
Au
Andika barua  kwa: webmaster@islamtz.org


An-nuur Home | Ukurasa wa Mwanzo | Islam Tanzania
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook