Polisi wazingira msafara wa Lipumba
POLISI mjini Bukoba Ijumaa iliyopita nusura wazue balaa baada ya kutaka kuzuia msafara wa mapokezi ya mgombea wa Urais, Profesa Ibrahim Lipumba.

Maofisa wa jeshi hilo mkoani humo wakiongozwa na kamanda wao Bw. Lawrance Tarimo walivamia msafara wa Mwenyekiti huyo wa chama CUF wakidai yalikuwa ni maandamano ambayo hayakuwa na kibali.

Umati mkubwa wa watu uliokuwa katika msafara huo ulilipuka baada ya polisi hao kutaka kuzuia magari manne yaliyokuwa katika msafara huo likiwemo lililochukua vifaa vya Profesa Lipumba.

Hata hivyo baada ya majadiliano na Viongozi wa CUF makamanda hao walilazimika kuyaachia magari hayo hadi msafara huo ulipofika ofisi ya mkoa ya chama hicho.

Huku eneo zima la stand likiwa limezingirwa na utiriri wa FFU waliokuwa tayari kupokea amri ya kushambulia, wapenzi na wanachama wa vyama vya CUF na CHADEMA walikuwa wakizunguka huku na kule wakipiga mayowe na kuimba nyimbo maarufu ya ngangari.

Marushiano ya maneno baina ya polisi hao na umati mkubwa wa wananchi ulidumu kwa dakika kadhaa mpaka msafara huo uliporuhusiwa kuendelea na safari yake.

Wapita njia walioshushudia tukio hilo walilillaumu jeshi la polisi kwa kuwavamia wananchi waliokuwa wakitembea kwa amani baada ya kuwalaki viongozi wao.

Profesa Lipumba na ujumbe wake walifanya ziara ya kichama ya siku nne mkoani Bukoba iliyoanza mwishoni mwa wiki iliyopita wakitokea Jijini Dar es Salaam.

Viongozi hao wanatazamiwa kuingia mkoani Kigoma leo(jumanne) baada ya kumaliza ziara ya Bukoba.

Taarifa mkoani Kigoma zinafahamisha kuwa Katibu Mkuu wa CHADEMA Dk. Amani Kaborou na viongozi wengine wa chama hicho na CUF wako katika maandalizi makubwa ya ugeni huo ambao umeelezwa imekuwa ukisubiriwa kwa shauku kubwa na Wananchi wa mkoa huo.


Dar kujadili kushambuliwa Sheikh Ilunga Alhamisi

WAISLAMU Jijini Dar es Salaam, wanatazamiwa wiki hii kujadili tukio la kupigwa mapanga Sheikh Ilunga.

Taarifa ya Shura ya Maimamu iliyotolewa Jijini jana imesema, Waislamu watakusanyika katika msikiti wa Mtambani alasiri siku ya Alhamisi kutoa uamuzi juu ya tukio hilo na mengine yanayoendelea kutokea dhidi ya Waislamu.

Katika mkutano huo wa dharura Amir wa Shura ya Maimamu Sheikh Juma Mbukuzi atatoa Tamko rasmi dhidi ya unyama aliyofanyiwa Sheikh Ilunga.

Taarifa kutoka Mwanza zimeeleza kuwa, tangu kupatikana taarifa za unyama aliyofanyiwa Ustaadhi huyo, maelfu ya watu mjini humo wamekuwa wakimiminika Hospitali ya Rufaa ya Bugando ambako amelazwa kwa matibabu.

Siku ya Ijumaa misikiti yote ya Mwanza ilisomwa Khutba moja ya Ijumaa iliyoelezwa dhulma aliyofanyiwa Ustaadh huyo.

Imeripotiwa kuwa baada ya swala ya Ijumaa, waumini wa misikiti yote walikusanyika msikiti mkuu wa Ijumaa wa Almarhum Sheikh Amin Abdallah ambako baada ya nasaha za Viongozi wao kwa pamoja walielekea Hospitali ya Bugando.

Uwingi wa watu umeripotiwa kuzua wasi wasi mkubwa kwa maaskari waliokuwa wameweka ulinzi mkali Hospitalini hapo.

Askari hao walitoweka baada ya umati huo wa wananchi walioonekana kuwa na hasira kuzingira lango kuu la Hospitali hiyo huku wakirusha maneno yakushambulia vyombo vya Dola.

Hasira na shutuma hizo ziliibuka kufuatia madai ya polisi kwamba Sheikh Ilunga alikuwa amejificha porini kufuatia kutafutwa na polisi na kwamba eti mkasa huo wa kukatwa mapanga ulimfika akiwa msituni.

Polisi baada ya kuvamia wodi aliyolazwa Ilunga ilidai ilikuwa ikimsaka kwa muda wote mpaka ilipopata taarifa ya kuwa alifikishwa Hospitalini hapo baada ya kushambuliwa na mapanga.

Sheikh Ilunga alikatwa katwa mapanga na kundi watu waliokadiriwa kufikia 10 ambao hadi sasa hawajafahamika nyumbani kwake usiku wa manane kuamkia Alhamisi wiki iliyopita.


Serikali ipige marufuku dhulma sio kitabu

WANANCHI mbalimbali walioongea na gazeti hili wameitaka serikali ishughulike na kuondoa dhulma, sio kuficha ukweli.

"Mh. Rais alidai kuwa hakuna mwananchi anayeonewa wala kubaguliwa kutokana na dini yake, akataka apewe ushahidi kama upo. Mbona sasa anaukataa ushahidi hata kule kusomwa tu?" amehoji Bw. Abubakar wa Magomeni.

Akiongea na mwandishi wa habari hizi jana, Bw. Abubakar amesema, Waislamu wanaituhumu serikali kwa uonevu na dhulma. Na kwamba kitabu juu ya mauaji ya Mwembechai ni miongoni mwa vielelezo vya ushahidi.

"Tulirataji vielelezo hivyo viwafikie wananchi. Waviweke katika mizani. Rais anapopiga marufuku, je, ameona yaliyomo ni urongo mtupu au ni ukweli asiotaka ujulikane?" amehoji.

"Hali hii inatisha. Sijui hatma ya nchi hii itakuwa nini", amesema Bw. Salum Ally wa Magomeni.

Bw. Salum amesema, katika hali ya kawaida kitabu hicho kingeachwa watu wakisome na kukichambua. Aidha, amesema, alitaraji serikali ikikosoe kama kuna lolote la uongo.

"Kupiga marufuku kitabu hicho ni serikali yenyewe kukiri kufanya dhulma na uonevu kama ulivyoelezwa katika kitabu hicho", amesema.

Hata hivyo akasema, tatizo si serikali kukiri kufanya uonevu, lakini ule ujasiri wa kuonesha kutokujali na kudhihirisha dhamiri ya kudumu katika kudhulumu.

Mwananchi mwingine aliyejitambulisha kama Mama Salma wa Tandika amesema, huenda Rais hataki dhulma iliyofanywa Mwembechai na kuandikwa katika kitabu hicho itafahamike kwa Watanzania.

Naye Majid Ahmad wa Mburahati amesema, pamoja na Rais Mkapa kuzuia kitabu hicho, bado kanda za video za tukio hilo zipo na wataendelea kuziangalia.

Bw. Christopher wa Ubungo Kibo amesema, hadhani uamuzi huo ni wa busara. Amesema, serikali imeruhusu vitabu na majarida ambayo yanaonesha picha za uchi na kuharibu jamii. "Iweje leo izuie kitabu kinachoeleza tukio la Mwembechai, ukizingatia kuwa wengine hatulifahamu vizuri?" amehoji.

Kutokana na taarifa iliyotolewa na gazeti maalum la serikali, Rais Mkapa alipiga marufuku kitabu hicho Jumanne Agosti 1, 2000. Kwa mujibu wa gazeti hilo notisi namba 277, ni marufuku kwa mtu yeyote kuingiza ama kusambaza kitabu cha Mwembechai Killings and the political future of Tanzania.

--
JuuRUDI


Bonyeza hapa
kushriki mjadala au kutoa maoni juu ya habari hizi na masuala mengineyo ya Kiislamu kwenye Baraza ya Wasomaji

   Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu: Bonyeza hapa
Au
Andika barua  kwa: webmaster@islamtz.org


An-nuur Home | Ukurasa wa Mwanzo | Islam Tanzania
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook