Mafundisho ya Qur'an

Somo: Kujenga familia na jamii nzuri

"AMETUKUKA Mwenyezi Mungu aliyeumba dume na jike katika(vitu) vyote; katika vile ivioteshavyo ardhi, na katika nafsi zao(wanaadamu), na katika vile wasivyovijua".(36:36).

Jinsia moja ya kila kiumbe katika ardhi hii inaihitaji jinsia tofauti kuingiliana kimaumbile ili kuweza kuzaana na kujiendeleza kifamilia na kijamii.

Pasipo kuwepo maingiliano ya kimaumbile uhai kwa viumbe hivyo hapa duniani usingalikuwa wa kuendelea.

Kwa wanaadamu, kuzaliana kunatokea baada ya maingiliano ya kijinsia kati ya mwanaume na mwanamke ambayo kiustaarabu hufanyika baada ya makubaliano ya kindoa baina ya wawili hao ya kuishi pamoja kama mke na mume.

Mkataba wa ndoa hutiwa saini baada ya kutimizwa masharti kadhaa kwa mujibu wa mila, desturi au itikadi husika.

Ili kuleta mapenzi, furaha na maelewano ya wawili watarajiwa, ndoa haina budi kufuata sheria na ilenge kutimiza mahitaji maalum ya kimaisha na kuendeleza kizazi cha mwanaadamu.

"Na Mwenyezi Mungu amekuumbieni wake katika jinsi yenu, akakujaalieni kutoka kwa wake zenu watoto na wajukuu, na akakuruzukuni vitu vizuri vizuri. Basi je, wanaamini yasiyokuwa ya haki na kuzikataa neema za Mwenyezi Mungu"? (16:72).

Kwa mujibu wa mafundisho ya Qur'an, kuendelezwa uhai wa mwanaadamu lazima kufuate utaratibu maalum uliowekwa kisheria. Katika Uislamu ndoa hutoa familia na familia nyingi ndiyo msingi wa Taifa kwa hiyo ustawi wa Taifa hutegemea msingi mzuri wa mahusiano ya wanajamii ambayo huanzia katika ndoa kisha familia na baadaye jamii.

Jamii bora huandaa mazingira yatakayokiwezesha kizazi kipya cha jamii hiyo kuwa na ustawi na maendeleo zaidi. Kwa maana nyingine wazazi ndio wenye jukumu la kupigania kufa na kupona ustawi wa watoto wao. Iwapo mapambano hayo ya kimazingira yatahitaji kujitoa muhanga basi ni wajibu kwa wazazi kufanya hivyo.

Ule usemi usemao adui yako mzalie mwana, hauna nafasi katika Uislamu kwa kuwa umeficha woga unaotoa mwanya kwa mzazi kukwepa kujitoa muhanga dhidi ya adui kwa kumsukumia mwana jukumu hilo. Qur'an inatufundisha adui yako upambane naye "jino kwa jino" ili kuondoa bughdha kwako na wale wa baadaye. Kwa hiyo lazima utendaji ua uamuzi wa mzazi wa hivi sasa uzingatie athari kwa kizazi chake.

Kila familia lazima ielewe kuwa inawajibu wa kuchangia maendeleo ya jamii. Ni wajibu unaotokana na lengo la kuumbwa kwao kama makhalifa wa huu ulimwengu. Iwapo wanajamii hao wataishi bila ya kuwa na utaratibu ni wazi kutakuwa na migangano ambayo itaathiri maendeleo na ustawi kiasi ambacho rasilimali na nguvu kazi muhimu za jamii zitatumika kutatua matatizo.

Jukumu la kujenga familia yenye furaha halina budi kuchukuliwa kwa uzito wake. Uzito huo unaanzia pale jinsia mbili zinapoungana kama wanandoa. Na kabla ya hapo kila jinsia ikichungua kwa uangalifu mkubwa mwenza mtarajiwa.

Uislamu unahimiza wafuasi wake wa kiume na wa kike kuoana baina yao ili kuunda jamii ya wachaMungu ambayo itatumia mahusiano hayo kuendeleza kizazi na kuiletea maendeleo jamii hiyo.

Kwa ajili hiyo ndoa ni ibada katika Uislamu na ili iwe ibada kama zilivyo ibada nyingine lazima itimize masharti na kanuni zilizowekwa na Uislamu.

Nani wa kumuoa

Ndoa ni muungano wa roho baina ya wawili wapendanao. Mwenyezi Mungu huziunganisha roho za wawili hawa ili wawe na furaha na maelewano katika maisha yao. Ni muhimu sana kwa mwanaume kumchagua mwenza aliye na uelekeo wa uchaMungu. Hii ina maana kwamba kwa mfano mwanamke anayesimamisha swala upo uwezekano kuwa amejengeka kiroho. Vile vile mwanamke wa aina hiyo hutarajiwa kuwa mzingativu wa amri za Mwenyezi Mungu. Hii itajitokeza katika uvaaji wake na tabia yake kwa ujumla hadharani.

Mambo mengine ya kuzingatia ni moyo wa huruma, ukarimu na bashasha kwa ndugu na jamaa. Upelelezi wa kina ufanywe kabla ya kuamua binti fulani kuwa "mwenza" wako. Kufanya hivi kutasaidia kuifanya ndoa ifikie lengo lake.

Sifa nyingine nyingine ziwe ni pamoja na "uanawari" na umbali wa kinasaba. Vile vile ni vizuri mwanaume akamchagua yule anayempendeza kihaiba, utulivu wa kiakili na aliyelelewa vyema kitabia.

Kabla ya uchumba imesuniwa kwa mwanaume kumuona mchumba wake mtarajiwa. Kumuona huku si kama vile ifanyikavyo kwa majahili ambao kwanza hutangulia kuwekana ukimada au ubibi na ubwana wa uficho. Ukimada ni uzinifu na umeharamishwa katika mafundisho ya Uislamu. Vile vile ile tabia ya "kutoka out" au "kupimana tabia" kati ya wachumba wawili ni haramu kabisa katika Uislamu.

Uchumba ni hatua muhimu ambayo kijana wa kiislamu anayetaka kuoa hupaswa kuwa muangalifu sana. Mara nyingi katika jamii zetu Wanaume au familia za wanaotaka kuoa hushughulishwa zaidi na kuangalia kabila, koo, Taifa, rangi, urembo wa mwanamke na wakati mwingine uwezo wa kimali.

Kijana au mwanaume wa kiislamu anapotaka kuoa, lililo muhimu sana kwake ni kuangalia kwa muda mrefu tabia ya msichana hasa katika usimamishaji wa swala. Hata hivyo hili vile vile si kigezo kikuu kwani wapo "wakorofi" wa kimaadili baada ya kurukaruka huku na kule hujilazimisha "kuswali swali" au kuvaa Hijab na wengine mpaka Niqab wakilenga kupata waume wawaoe! Lakini kwa dhahiri yao hawaajaamua kikweli kikweli kuwa Waislamu. Hawa tabia zao halisi hudhihirika mara wanapoolewa!

Kumpata mke aliye mchaMungu kutachangia kwa kiasi kikubwa kuwalea vyema watoto, mama mwongofu atakazania wanawe wafuate mwenendo huo.

Nani wa kuolewa naye

Kama ilivyo kwa mwanaume anayetaka kuoa, mwanamke aliyepelekewa ombi la uchumba na kijana au mwanaume, lazima azingatie sifa ya uchaMungu kwa mtu huyo.

Kijana aliyeleta posa awe mwenye kuionea fahari dini yake na tabia yake ithibitishe uimara wa imani yake. Baba wa binti huyo apeleleze tabia na mwenendo wa kijana anayetaka "kufunga jengee". Atafiti kwa kina vikao, matembezi na marafiki wa mwanaume huyo.

Msichana asimkubali mwanaume mlevi au mzinifu hata kama atakuwa na uwezo kiasi gani wa kimali. Ndoa hudumu kwa mapenzi yatokanayo na haiba na maadili mazuri baina ya mke na mume wawili kati yao, ukipenda mali ni wazi itakapokauka ndoa nayo huvunjika!

Kwa kuwa Wanaume wengi hulazimika kuficha makucha yao wanapopeleka posa nyumba fulani, kwa hiyo ni wajibu wa mzazi kupeleleza kimya kimya maisha binafsi ya hivi sasa ya kijana anayetaka uchumba. Mzazi amsaidie binti yake kupata mume mzuri atakayeifanya ndoa kuwa na maana itakayokuwa na manufaa kwa dini yake na jamii kwa ujumla.

Ni katika mwenendo unaokubalika katika Uislamu binti kupendekeza fulani amuoe baada ya kupendezwa naye kihaiba na kimaadili baada ya kumchunguza kimya kimya kwa makini mwenendo na tabia yake .

Binti asikae akasubiri mpaka huyo aliyependezwa naye atoe pendekezo kwake, ingawa huonekana ni "fahari kubwa" kwa mwanamke katika jamii zetu hizi iwapo mwanaume atakuwa ndiye mpendekezaji.

Lakini katika Uislamu na kwakweli inapendeza kweli kwa binti mchaMungu atajasiri kutoa kupendekeza kijana mchaMungu amuoe!

Bibi Khadija mke wa kwanza wa Mtume(s.a.w) ndiye aliyependekeza aolewe na Mtume. Alimtuma rafiki yake Bi Nafisa kufikisha salaam hizo kwa Muhammad.

Wanawake wengi husita kupendekeza kwa kuchelea "fedheha" iwapo atakataliwa. Wakisahau mara nyingi hata wanaume hukataliwa wanapopeleka posa mahali.
--
JuuRUDI


Bonyeza hapa
kushriki mjadala au kutoa maoni juu ya habari hizi na masuala mengineyo ya Kiislamu kwenye Baraza ya Wasomaji

   Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu: Bonyeza hapa
Au
Andika barua  kwa: webmaster@islamtz.org


An-nuur Home | Ukurasa wa Mwanzo | Islam Tanzania
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook